Highlander
JF-Expert Member
- Feb 12, 2012
- 3,093
- 1,077
Wadau wa hapa Great Thinkers ninalo ombi maalumu kwenu kuhusu tatizo la kuugawa mkoa wa Mbeya. Kuna kambi tatu zimezuka kule Mbeya kuhusu suala hili, kwa mujibu wa taarifa ambazo ninazo leo, na ni kambi zenye sura ya Ukabila. Ninaamini jamvi hili linao uwezo kuisaidia serikali yetu kufanya uamuzi ambao ni sahihi kufuta hii sura ya ukabila badala ya kustawisha taswira hiyo. Kambi moja inataka Rungwe kuwa ndo Mkoa mpya, Kambi ya pili inataka Chunya, na sasa Mbozi wanataka Kwao ndiyo kuwe Mkoa Mpya na makao makuu yawe Mlowo! Na kwamba wazo hili 'eti' linaungwa mkono ya WanaIleje.
BACKGROUND:
Miaka ya 1980 Mkoa wa Mbeya ulikuwa na Chama Kikuu cha Ushirika kikiitwa MBECU: Mbeya Co-operative Union. Wanambeya wanaotoka Kyela na Rungwe Waliomba wapewe uhuru kuunda chama chao. Walipewa idhini hiyo wakajitenga na kuunda chama chao kilichoitwa KYERUCU: Kyela-Rungwe Co-operative Union. Lakini baadaye wakazi wa Wilaya za Kyela na Rungwe walishindwa kukaa pamoja katika Chama hiki Kyerucu ikavunjika na kuunda vyama viwili tofauti zikazaliwa KYECU ya Kyela na RUCU ya Rungwe.
Angalizo ni kwamba Kusambaratika kwa mshikamano wa WanaMbeya kupitia MBECU ulianzia kwenye Ukanda wa Unyakyusa kutafuta kujitenga. MBECU bila Wanyakyusa ilichechemea kwa Muda fulani ikajifia taratibu baada ya Watu wa Mbozi, ambako makabila makubwa ni Wanyiha na Wanyamwanga walipoamua nao kujitenga na kuunda Vyama vyao vya Ushirika, kikiwepo chama kilichoitwa ISAYULA: Isansa-Iyula Co-operative Union.
HOJA YA KUIGAWA MBEYA ILIYOPO LEO
Taarifa nilizo nazo ni kwamba Wilaya ya Rungwe ndio waasisi wa wazo la Kuigawa Mbeya. Rungwe waliomba wapewe idhini kuwa mkoa. Katika Mtizamo huo, ilieleweka wazi kwamba mazingira ya ki-jiografia ya Mkoa huo yangelazimisha Wilaya za Rungwe na Kyela kuingia katika Mkoa huo wa Rungwe. Lakini Pia Ileje Ingeweza kuingia bila shida, na pengine sehemu fulani-fulani za Iringa ya Zamani kwenye maeneo ambayo pengine sasa ni Njombe. Wazo la Rungwe ndilo hasa msingi wa mgororo uliopo leo, ambao umeanzia kwenye msimamo wa Serikali kukataa Rungwe kuwa Mkoa: ambapo mimi pia nikiwa MwanaMbeya mwenye kutetea umoja na mshikamano wa Mkoa wetu nasita kukubali ombi hilo la Rungwe haraka-haraka kwa sababu ya historia niliyoiweka hapo juu.
MBOZI, MOMBA, ILEJE NA CHUNYA
Leo nimepewa taarifa ifuatayo: kwamba katika siku mbili tatu zilizopita, Full council ya wilaya ya Mbozi imepitisha Azimio kukataa Chunya kuwa Makao Makuu ya Mkoa Mpya dada wa Mbeya ambao unatakiwa kuitwa Mkoa wa Songwe. WanaMbozi wamepitisha azimio Mkoa Mpya Uwe Mbozi na Makao Makuu yawe Mlowo. Kwa mujibu wa taarifa hizo, wanaCCM wa wilaya za Ileje na Momba wanaafiki wazo hili kuweka makao makuu ya Mkoa Mpya kuwa Mlowo, Mbozi. Tatizo linalozuka ni hili: Chunya watapata shida sana kuja Mlowo.
My Take: Mkoa ubakie ulivyo!
Naomba mawazo yenu wadau tuisaidie Serikali yetu kufanya maamuzi sahihi.
-------------------
HITIMISHO
-------------------
Mjadala umeelekeza haja ya kuchukua hatua: Kwamba next week tuhamie Phase Two ya mjadala--ACTION. Wenzetu waliopo on the ground kule Mbozi na Ileje wameanza kuchukua hatua kwa mujibu wa taarifa ambazo ninazo.WanaIleje na Mbozi wamekataa kupelekwa Chunya, wakitaka Mkoa mpya uwe Mbozi kama kuna ulazima wa kuugawa Mkoa. Sisi katika intelligentsia ya Mkoa wa Mbeya tulioko katika Diaspora ya Mkoa tunapiga wazo zima la kuugawa mkoa kwa sababu hatuoni haja, umuhimu wala sababu ya kuridhisha ya kuugawa mkoa.
Mjadala unaelekeza sasa tuhamie kwenye vitendo, nionavyo mimi: Tunatakiwa sasa kuwaunga mkono wenzetu walioko on the ground kwa kuchukua hatua kuzuwia upuuzi huu. Tusiishie kupost-post tu maneno humu JF. Jaza Vocha kwenye laini yako, hamasisha madiwani, hamasisha wajumbe wa nyumba kumi, hamasisha Walimu wa shule za Msingi na Sekondari, hamasisha Mabibi shamba na Mabwana shamba, Manesi na Medical assistant wataopata shida sana kusafiri kutoka Itumba, Msia, Idunda na kwingineko, eti kwenda Mkwajuni kufuata huduma za Mkoa wapinge upuuzi huu. Wapatie maelezo yanayojitosheleza: Waelekeze kwenye petittion ambayo inaandaliwa kama hawa wenzetu chini ya RC Abbas Kandoro watajaribu kutekeleza upuuzi huu.
Wadau wa mjadala huu kama kuna mahala nimekosea katika hitimisho hili naomba marekebisho tafadhali.