Kuelekea uchaguzi wafanyakazi tujikumbushe ile hadithi ya mbayuwayu na Mwanakijiji | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kuelekea uchaguzi wafanyakazi tujikumbushe ile hadithi ya mbayuwayu na Mwanakijiji

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by SHUPAZA, Oct 30, 2010.

 1. SHUPAZA

  SHUPAZA JF-Expert Member

  #1
  Oct 30, 2010
  Joined: Aug 4, 2009
  Messages: 548
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 35
  Na. M. M. Mwanakijiji

  Nilisimuliwa kisa cha mbayuwayu ambaye alikuwa anaishi katika shamba la Mkulima mmoja huko Ukwereni. Mbayuwayu huyo aliishi na wenzake katika maisha ya kutegemea nafaka na mbegu mbalimbali zinazopatikana katika shamba la mkulima huyo. Pamoja naye walikuwepo ndege wengine wengi ambao nao walipata afueni ya maisha yao katika shamba hilo zuri la Mkwere. Miongoni mwa ndege hao walikuwepo tetere ambao walionekana kama ndio ndege wapendwa wa mwenye shamba.

  Mkulima huyo alikuwa anahakikisha kuwa tetere wanakula na kunenepa pamoja na ndege wengine kama vile kwale na kukumaji. Na walikuwepo pia dudumizi, vigong'ota, zokoyogo na kurumbiza. Ndege wengine wote hawa walifurahia maisha yao katika shamba la Mkwere isipokuwa mbayuwayu.

  Mbayuwayu alikuwa analalamika mara kwa mara kuwa maslahi yake hayaangaliwi na kulindwa kama ya kina tetere. Mara kwa mara mbayuwayu amejikuta akijitafutia riziki yake hata nje ya shamba, amekuwa akikwepa mitego yeye mwenyewe na hata anapowindwa na paka ilimbidi atafute mbenu endelevu za kujilinda. Katika maisha hayo mbayuwayu alijikuta anaishi maisha ya "kiujanja ujanja" ilimradi mdomo uende kinywani.

  Mbayuwayu walikuwa wanalalamika kuwa tetere walikuwa wameachwa kula kwa uhuru wote na wamefikia kula hata vile vidogo vya mbayuwayu. Walilalamika kuwa hata wakionda kuna punje zimedongoka ilikuwa ni vigumu kwani tetere walifika mara moja na kwa kutumia mabavu waliweza hata kuwatimua mbayuwayu hao kwa kuwatishia kuwadonyoa.

  Kwa vile waliona kuwa maslahi yao na maisha yao yanatishiwa na tetere na mwenye shamba inaonekana hajali basi mbayuwayu kwa kutumia umoja wao wa Mbayuwayu (UMBA), waliamua kuitisha mgomo wakidai maslahi zaidi na nafasi zaidi za kutambuliwa na mwenye shamba na kupewa maslahi ambayo yanakaribiana na yale ya tetere. Tetere waliachwa kunawiri, na hata kujengewa matundu ya kisasa ili wao na makinda yao waishi maisha ya raha na amani wakati mbayuwayu wakiachwa kujijengea viota vyao kwenye kona za nyumba na majengo mbalimbali humo shambani. Tetere walikuwa wanaruhusiwa kukaa pamoja na kuimba kwa pamoja huku wakitamba kwa mwenye shamba kuwa;

  Kuku mfupa mtupu
  Mimi nyama tupu!

  Hivyo mbayuwayu wakaamua kutangaza mgomo ili kumshinikiza mwenye shamba kuangalia maslahi yao. Zikiwa zimebakia siku chache za mgomo kufika mbayuwayu walijikuta wameweza kuwashawishi mbayuwayu wa jamii tofauti kuweza kushiriki mgomo huo na kwa pamoja wakaanza kutangaza juu ya ujio wa mgomo wa mbayuwayu wote shambani. Na hata siku ya sherehe ya ndege wote wafanyao kazi zilipofika mbayuwayu waliandamana wakiwa na mabango yaliyosomeka:

  Mwenye shamba tukumbuke
  Mbayuwayu na sisi tuna haki
  Kwanini tetere peke yao?

  Walipita siku hiyo kwa umoja mkubwa japo mwenye shamba na yeye aliamua kufanya sherehe ya ndege wengine ambapo tetere, dudumizi, kurumbiza na wenzake walihudhuria kwa furaha wakiburudishwa na miziki mbalimbali. Katika sherehe ya mbayuwayu msimamo uliendelea kutolewa kuwa ni lazima wagome kwani japo wao ni vindege vidogo na ambavyo vinaonekana havina maana ukilinganisha na Mbayuwayu lakini vina sehemu katika maisha ya shamba, kwani ndio vinatafuna vijidudu vidogovidogo vya hatari, huchangamsha ndege wengine na husaidia sana katika kuhakikisha usalama wa shamba kwani vina uwezo wa kwenda sehemu mbalimbali hata zilizondogo na vina mwendo kasi sana kuweza kuwakwepa adui.

  Hata hivyo, mwenye shamba alikasirika alipoona kuwa mbayuwayu kweli wamedhamiria kuitisha mgomo. Yakiwa yamebakia masaa machache kabla ya mgomo huo mkubwa kuanza mwenye shamba akaitisha mkutano wa ndege wazee na kuanza kuwahutubia kwa ukali akielezea ni kwanini mbayuwayu hawastahili maisha ya tetere!

  Akizungumza kwa ukali na akifoka hadi mapovu yakimtoka mdomoni mwenye shamba aliwaambia mbayuwayu kuwa yeyote atakayegoma atakiona cha moto kwani wawindaji wote wameruhusiwa kutumia bunduki, manati na hata mizingi ili kuhakikisha kuwa mbayuwayu hawaleti madhara katika shamba kwa kugoma kwao. Aliwahakikishia kuwa shamba lake haliwezi kuwapa maslahi kama ya tetere! Aliwahakikishia kuwa serikali yake ya shamba lake haina uwezo wa kutoa maslahi kwa mbayuwayu kwani uwezo uliopo hadi hivi sasa ni kuweza kuhakikisha tetere, dudumizi na kwale wanaendelea kuishi maisha ambayo wanastahili.

  Aliwaambia wazi kuwa hata wakigoma hatokuwa na uwezo wa kuwapa maisha ya kitetere kwani wao ni mbayuwayu! Na akawaambia kuwa endapo watagoma basi paka wote wa shamba watapewa leseni ya "kuwaleta wakibisha walipuliwe". Huku akishangiliwa na ndege wazee ambao wengine hata manyoya walikuwa hawana tena na macho yao yakisinzia kwa uchovu, mwenye shamba aliapa kuwa kama anahitaji kura basi hizo za mbayuwayu siyo za lazima kwani tetere na wengine wako tayari kumpatia kura zao!

  Ndege wote shambani walishangaza na ukali wa mwenye shamba. Walishangaa kwanini hajawahi kuwa mkali hivyo kwa dudumizi na mwewe ambao wamekuwa wakila hadi vifaranga vya mbayuwayu? Walishangaa ilikuwaje mwenye shamba awe mkali kwa mbayuwayu ambao walitaka tu wakumbukwe kama tetere na wapewe maisha yanayokaribiana na kitetere wakati ndege wakubwa na wenye nguvu wakiwa wanatambaa shambani na kula mbegu na matunda yote mtini huku wakiwafukizia mbali mbayuwayu?

  UMBA ilishangazwa na ukali wa mwenye shamba kwa mbayuwayu; ukali ambao hawajawahi kuuonesha dhidi ya ndege waharibifu wa mazao ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakienda na kuchimbua hata mbegu zilizopandwa na kula na kugawana? Ilikuwaje mwenye shamba awe mkali hivyo kwa mbayuwayu?

  Hata hivyo, baada ya tafakari mbayuwayu wakaamua kusitisha mgomo wao; walijua kuwa kwa kadiri ya kwamba ndege wamegawanyika kwenye shamba la mkulima, ndege hawawezi kupata haki zao. Mbayuwayu walijua kuwa kwa kadiri ya kwamba bado hawajaweza kuungana na kuonesha umoja wa kudai maisha kama ya tetere na kurumbiza basi hawawezi kufurahia maisha ya shamba hilo. Kutokana na uelewa huo mbayuwayu walidhamiria kuona kuwa shamba hilo linaenda kwa mtu mwingine au apewe mkulima mwingine mwenye kujali maslahi ya ndege wote siyo wale tu wenye sauti nzuri na rangi za kuvutia kama tetere!

  Mbayuwayu waliamua kurudisha majeshi yao nyuma huku wakiruka ruka kivyao wakiimbiana na kupeana pole kwa sauti za chini ambazo mwenye shamba hakuweza kuzisikia;

  Pole mbayuwayu
  Maskini mbayuwayu
  Laiti ungelikuwa tetere!
  Labda angekujali Mkwere!
   
 2. tzjamani

  tzjamani JF-Expert Member

  #2
  Oct 30, 2010
  Joined: Oct 9, 2010
  Messages: 997
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0
Loading...