Kubeba asobebeka, akibebwa habebeki! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kubeba asobebeka, akibebwa habebeki!

Discussion in 'Jukwaa la Lugha' started by Mzee Mwanakijiji, Jun 22, 2010.

 1. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #1
  Jun 22, 2010
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,364
  Likes Received: 6,396
  Trophy Points: 280
  Ya'rabi miye nalia
  Haya n'nashuhudia
  Ya shari twajitakia
  Ya mambo ya kuchukia
  Kubeba asobebeka, akibebwa habebeki!

  Twaona yanatukia
  Kama giza latujia
  Wenyewe twashingilia
  Totoro twaliingia
  Kubeba asobebeka, akibebwa habebeki!

  Kwa mbwembwe wametujia
  Ahadi watumwagia
  Tabasamu za udhia
  Nazo wanatupatia
  Kubeba asobebeka, akibebwa habebeki!

  Ati kura watakia
  Zamu tena walilia
  "Zaidi" waaahidia
  Wabongo twashingilia!
  Kubeba asobebeka, akibebwa habebeki!

  Kasi zaidi zajia
  Nguvu zaidi walia
  Ari zaidi mamia
  Na uzembe zidia!
  Kubeba asobebeka, akibebwa habebeki!

  Nikisema wachukia
  Eti ninapandizia
  Chuki isiyoishia
  Kwa wale wenye nia
  Kubeba asobebeka, akibebwa habebeki!

  Sasa nawaulizia
  Ni vipi tutafikia
  Yale tunayotakia
  Kwa mwendo wa kurudia
  Kubeba asobebeka, akibebwa habebeki!

  Ubovu ukirudia
  Kwa kasi ya kuzidia
  Fisadi ukimpatia
  Nguvu ya kumzidia
  Kubeba asobebeka, akibebwa habebeki!

  Vipi mtaifikia
  Njozi mnayotakia
  Mazuri mnayolilia
  Si kwamba mmefulia
  Kubeba asobebeka, akibebwa habebeki!

  Zaidi mwaitakia
  Hiyo mtajipatia
  Na zaidi mtalia
  Huku mnashangilia
  Kubeba asobebeka, akibebwa habebeki!

  Mwenye akili sikia
  Ubongo wako tumia
  Usifuatie hisia
  "zaidi" kukumbatia
  Kubeba asobebeka, akibebwa habebeki!

  Lazima kuulizia
  Ni vipi walishindwia
  Zaidi kutupatia
  Miaka iloishia?
  Kubeba asobebeka, akibebwa habebeki!

  Mbona waliwaachia
  Mafisadi kutambia
  Kamati kuwaundia
  Na kesi kuwatungia?
  Kubeba asobebeka, akibebwa habebeki!

  Mbona hawakutupatia
  Ubora wa kuzidia
  Elimu ikazidia
  Maisha kushangazia?
  Kubeba asobebeka, akibebwa habebeki!

  Majambazi wazidia
  "zaidi" wamejazia
  Ni vipi watazidia
  Ya zaidi kuzidia?
  Kubeba asobebeka, akibebwa habebeki!

  Barabara twapitia
  Mahandaki yazidia
  Na magonjwa pindukia
  "zaidi" twajitakia?
  Kubeba asobebeka, akibebwa habebeki!

  Zaidi mwajizidia
  Mmezidi twachukia
  Mmbwembwe mmetuzidia
  Twazidi kuwakimbia!
  Kubeba asobebeka, akibebwa habebeki!

  Natamati natamia
  Beti ninazifungia
  Wazo nimewapatia
  Ya nini cha kuchukia
  Kubeba asobebeka, akibebwa habebeki!

  ZAIDI NTAZIDIA
  WAKIZIDIA NAZIDIA
  NIKIZIDI NAZIDIA
  ZAIDI YA KUZIDIA!
  Kubeba asobebeka, akibebwa habebeki!

  Na. M. M. Mwanakijiji (Ngurumo ya Ushindi a.k.a Sauti ya Kijiji)
   
 2. D

  Divele Dikalame Member

  #2
  Jun 22, 2010
  Joined: May 4, 2010
  Messages: 77
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0


  shairi lako zuri sana ndugu mwanakijiji lakini ukumbuke kasema mzee Sadan Abdul Kandoro ya kuwa
  Mtu chake apendacho,hakina hila machoni
  huridhika kuwa nacho, japo hakina thamani
  mapenzi hayana kicho, yaamkapo moyoni
  mwenye mapenzi, haoni ingawa macho anayo

  kwa maana hiyo hata iweje atabebwa hivyo hivyo kwa kuwa tumempenda
   
 3. Fisherscom

  Fisherscom JF-Expert Member

  #3
  Jun 22, 2010
  Joined: Mar 13, 2008
  Messages: 1,441
  Likes Received: 255
  Trophy Points: 180
  Ahsante mkuu kwa utenzi murua,hakika tunajivuna kuwa na mtu kama wewe katika jamvi hili lisoisha ukoko. Tunaburudika,tunaelimika,tunakosoana inapobidi.
   
 4. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #4
  Jun 23, 2010
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,364
  Likes Received: 6,396
  Trophy Points: 280
  umenikumbusha mbali sana!! thanks!
   
 5. Shalom

  Shalom JF-Expert Member

  #5
  Jun 23, 2010
  Joined: Jun 17, 2007
  Messages: 1,315
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Tutapingana, tutatofautiana lakini wote tukiipenda nchi tunaweza kuikomboa!
   
 6. Askofu

  Askofu JF-Expert Member

  #6
  Jun 23, 2010
  Joined: Feb 14, 2009
  Messages: 1,668
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 133
  Umekuja ki-vingine...

  Atabebwa tu mwisho tutaingia naye shimoni.... kisa, mapenzi upofu
   
 7. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #7
  Jun 23, 2010
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,364
  Likes Received: 6,396
  Trophy Points: 280
  utakapojua tunapatana zaidi kuliko kupingana na kutofautiana tutabakia tunashangaana.. LOL
   
 8. Mentor

  Mentor JF-Expert Member

  #8
  Jun 23, 2010
  Joined: Oct 14, 2008
  Messages: 18,740
  Likes Received: 8,329
  Trophy Points: 280
  nami naunga mkono
  tuendako mimi simo
  tutaja pigana vigongo
  tutapomrudisha humo
  Kibeba visobebeka, silie vikilemea!

  Akili zetu zi wapi
  tumeshalewa makapi
  sasa tukipewa pipi
  hatujali letu lipi
  Kibeba visobebeka, silie vikilemea!

  Kura zetu tulikupa
  imani nayo kakupa
  mwenzetu ukatutupa
  ukaiba hata EPA
  Kibeba visobebeka, silie vikilemea!

  Machozi najililia
  mejiwa maharamia
  nchi yangu Tanzania
  amka taja jutia
  Kibeba visobebeka, silie vikilemea!

  Kasi gani waongeza
  nguvu ipi watubeza
  ya mwanzo we hukuweza
  ya zaidi utaweza
  Kibeba visobebeka, silie vikilemea!

  na bado twashangilia
  ajapo kutunadia
  sera mpya watumia
  ya kale umeitua
  Kibeba visobebeka, silie vikilemea!

  naomba mheshimiwa
  tumechoka kuvamiwa
  tweleze lifanikiwa
  kuuondoa ukiwa
  Kibeba visobebeka, silie vikilemea!

  ama ndo yaleyale
  watupigia kelele
  na kutupeleka kule
  likotutoa Nyelele
  Kibeba visobebeka, silie vikilemea!

  nabaki naililia
  nchi yangu Tanzania
  e Mola ninakujia
  watoe watatuua
  Kibeba visobebeka, silie vikilemea!

  wametunyonya kutosha
  nini wametubakisha
  milango tu wanabisha
  kututawala maisha
  Kibeba visobebeka, silie vikilemea!

  ila kwako ninakuja
  najua wewe si Yahya
  tuepushie hili ja
  mpaka waone haya
  Kibeba visobebeka, silie vikilemea!

  walitutukana sana
  raisi bila hiyana
  kura zetu siyo zana
  kumnyima rudi tena
  Kibeba visobebeka, silie vikilemea!
   
 9. Mentor

  Mentor JF-Expert Member

  #9
  Jun 23, 2010
  Joined: Oct 14, 2008
  Messages: 18,740
  Likes Received: 8,329
  Trophy Points: 280
  What are you insinuating wakijiji!??? na wewe mmoja wao nn???!
   
 10. Ngambo Ngali

  Ngambo Ngali JF-Expert Member

  #10
  Jun 23, 2010
  Joined: Apr 17, 2009
  Messages: 3,197
  Likes Received: 135
  Trophy Points: 160
  Aliyasema Sadani, Abdul bin Kandoro,
  Alilighani zamani, Wakati giza totoro
  Zile Zama ujanani, elimu yetu totoro,
  Kwa nini bado tubebe, kitu kiso na thamani?

  Mapenzi hayana kificho, hiyo kweli nakubali,
  Chochote nilichonacho, thamaniye ni halali,
  watu kutolea macho, thamani yake dalili,
  Katu tusiridhike, na kitu kiso thamani.

  Mtu chake apendacho, budi kupendwa na wengi,
  kuonwa na kila jicho, kusemwa na walio wengi
  Umma ukisema hicho, pasipo kujali rangi
  Kitu chenye thamani, ni kinachopendwa na wengi
   
 11. Safari_ni_Safari

  Safari_ni_Safari JF-Expert Member

  #11
  Jun 23, 2010
  Joined: Oct 5, 2007
  Messages: 22,481
  Likes Received: 5,862
  Trophy Points: 280
  Marehemu Joseph Mulenga alitungia wimbo akiwa na Sikinde
   
Loading...