Mkaruka
JF-Expert Member
- Feb 5, 2013
- 19,932
- 34,919
KUABUDU MTU NA MATOKEO YAKE!
FEBRUARI 25, 1956, Katibu Mkuu wa Chama cha Komunisti, Nikita Krushchev, alitoa hotuba maarufu iliyoitwa “The Personality Cult and Its Consequences” – “Kuabudu Mtu na Matokeo Yake". Pia huitwa “Hotuba ya Siri.”
Ukumbi wa Great Kremlin, Moscow, Urusi, ukiwa na jopo la wajumbe 1,500 kutoka nchi za Umoja wa Sovieti, pamoja na mamia ya wageni waalikwa, walinyamaza kimya kwa saa 4 (dakika 240), wakimsikiliza Krushchev akitema nyongo.
Sio tu kwamba wajumbe na wageni waalikwa walinyamaza, bali pia walishindwa hata kugeuza shingo kutazamana wao kwa wao. Wote macho yao yalikuwa pima kumtazama Krushchev, kwa hofu kubwa. Krushchev aliamua kuvaa mabomu kuusema ukweli ulioogopwa na wengi.
Krushchev alitoa hotuba hiyo ikiwa ni miaka mitatu kasoro siku tisa tangu kifo cha aliyekuwa Mtawala wa Sovieti, Joseph Stalin kilichotokea Machi 5, 1953. Tangu kufa kwa Stalin, hakuna lolote baya lililotamkwa kuhusu kiongozi huyo ndani ya Sovieti.
Viongozi waliofuata baada ya Stalin, walipitia kipindi kigumu kwa kila walichofanya. Maana walipimwa kwa utendaji wa Stalin. Ndani ya Urusi na Sovieti yote, Stalin alitukuzwa mithili ya Mungu mtu.
Tangu kufa kwa Stalin, Komunisti hawakuwa wamefanya Mkutano Mkuu mpaka Februari 14, 1956. Mkutano huo ulichukua siku 11. Ndipo wakati wa hotuba yake ya kufunga mkutano, Krushchev akaamua kuwaambia watendaji wakuu wa chama na Serikali za Sovieti unyama wote uliofanywa na Stalin.
Krushchev alisema, Stalin aliua watu wengi, wapinzani wake, watiifu wa chama pamoja na kutekeleza unyama mwingine wa kila aina, na hayo ni matokeo ya kumtukuza mno na kumwabudu kama Mungu.
Baada ya hapo, Krushchev alimtangaza Stalin kama mtu mwovu. Kumbukumbu mbalimbali za Stalin zilianza kuondolewa. Stalin alipokufa mwili wake haukuzikwa, ulihifadhiwa jirani na Kiongozi wa zamani Sovieti na Chama cha Komunisti, Vladimir Lenin, ndani ya jumba la Makumbusho la Lenin.
Mwaka 1961, katika kuhakikisha kumbukumbu za Stalin zinafutwa na haadhimishwi, mwili wake uliondolewa kwenye Jumba la Makumbusho la Lenin, ukazikwa makaburi ya Kremlin Wall kama mtu wa kawaida. Lenin ndiye pekee mwili wake umetunzwa mpaka leo.
SOMO: Madikteta huwa na sumu ya ajabu sana kwa umma. Hutokea kupendwa na kuabudiwa licha ya kufanya unyama mwingi. Kuna wanaomuenzi Mobutu Sese Seko, wapo wanaosema Idi Amin alikuwa kiongozi mzuri. Hata Adolf Hitler anaenziwa. Katika utawala wake, Stalin anahusishwa moja kwa moja na vifo vya watu wanaofikia 20 milioni.
Ndimi Luqman MALOTO