komesha ufisadi huu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

komesha ufisadi huu

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by kilimasera, Dec 30, 2010.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  Dec 30, 2010
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  MOJA ya habari kubwa za gazeti hili juzi, ilihusu kuwapo kwa baadhi ya mawaziri wanaotumia nafasi zao kutafuna fedha za serikali vibaya.
  Taarifa hiyo ambayo iliwashtua wengi kutokana na simu nyingi zilizopigwa katika chumba chetu cha habari, inaonyesha fikra za upeo duni wa baadhi ya viongozi wetu.

  Taarifa hiyo ilisema waziri huyo alikodi ndege kwenda Dodoma kwa fedha za serikali kuhudhuria mahafali ya Chuo cha Mipango, lakini aliliagiza pia gari lake la uwaziri aina ya G8 limfuate Dodoma na hivyo kulazimika kuongeza gharama zingine.

  Kwa mujibu wa habari hiyo, wapo watendaji wengi wa serikali wanaofanya hivyo na hivyo kutumia vibaya fedha za serikali ambazo zingeweza kutumika kwa shughuli zingine za maendeleo.

  Tunaandika Tahariri hii tukirejea wito wa mara kwa mara wa Waziri Mkuu Mizego Pinda wa kutaka kupunguza gharama za matumizi ya serikali.

  Pinda amekuwa akijikita zaidi kwenye kupiga marufuku ununuzi wa mashangingi, kuzuia semina, warsha na makongamano yasiyo na tija zaidi ya kulipana posho.

  Lakini kwa bahati mbaya sana, aina hii mbaya ya matumizi ya fedha za serikali, hajawahi kubeza na hilo pengine tunaamini linatokana na kutojua.

  Kwetu sisi hatuoni sababu ya kiongozi kupanda ndege iwe ya kukodi au ya kibiashara halafu aagize shangingi limfuate kutoka Dar es Salaam kwenda kwenye mkoa anaokwenda kufanya ziara. Huu ni ufisadi!

  Karibu katika mikoa yote, hususan Dodoma, kuna ofisi za wizara mbalimbali na wakuu wa mikoa; ofisi zenye magari yenye hadhi ya waziri na madereva waliosomea kazi zao.

  Hivi kuna ubaya gani kwa kiongozi akifika kwenye mkoa husika asitumie magari hayo au hata ya wakuu wa mikoa badala ya kuagiza mashangingi yao kutoka Dar es Salaam?

  Viongozi kumbukeni kuwa serikali ina mambo mengi ya kufanya ambayo kwa sasa yamesimama kutokana na ukosefu wa fedha.

  Mathalani hivi karibuni zaidi ya vijana 16,000 waliohitimu mafunzo yao ya ualimu katika vyuo vya elimu ya juu nchini, tangu Mei mwaka huu hawajapata ajira na kila siku wanaambiwa kwamba serikali haina fedha.

  Katika shule nyingi za sekondari za kata hata zile za mijini, nyingi hazina madawati na walimu; kwa hiyo haingii akilini kuona waziri mmoja akitumia zaidi ya sh milioni 10 kwa siku moja, tena kwa safari ya kwenda kuhudhuria mahafali!

  Tunamtaka Waziri Mkuu Pinda asimamie kukomesha aina hii ya ufisadi ambao unaonekana mdogo, lakini ukifanywa na viongozi wengi na kuwa kama sehemu ya utaratibu; taifa litajikuta linazidi kupoteza fedha nyingi na kuwaacha wananchi wakiendelea kubaki kwenye lindi la umaskini.

  Nchi hii ina mianya mingi mno ya kupoteza mali; huu ukiwa mmojapo. Ni juu ya serikali sasa kuanza kuziba mianya hii ya upotevu wa mapato ya wananchi.
  source mtanzania daima
   
Loading...