Dotto C. Rangimoto
JF-Expert Member
- Nov 22, 2012
- 1,985
- 1,286
Koma mwana nakuasa, dunia hino yatisha,
Koma tena koma hasa, siyapupie maisha,
Koma sicheke garasa, turufu huja na kwisha,
Koma mwanangu koma, koma uishi salama.
Koma kumcheka mamba, mtoni wenda kupita,
Koma kwako kujigamba, kuteta ulo wakuta,,
Koma kujitia mwamba, kwa wembe utakukata,
Koma mwanangu koma, koma uishi salama.
Koma kutia mchele, bila tui kupunguza,
Koma usisonge mbele, anza njia kuchunguza,
Koma wangu chaudele, nisije kukuchalaza,
Koma mwanangu koma, koma uishi salama.
Koma kupiga wakati, ukumbuke ni ukuta,
Koma kuzidi kuchati, fesibuku mara twita,
Koma leo sikuwati, yasije yakakukuta,
Koma mwanangu koma, koma uishi salama.
Koma nami nimekoma, kiti chako nilikaa,
Koma usije pogoma, yaani kama kichaa,
Koma ninaweka koma, yatosha niloandaa,
Koma mwanangu koma, koma uishi salama.
Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
Call/whatspp 0622845394 Morogoro.