Afrika, Afrika yangu

Afrika, Afrika yangu

Dotto C. Rangimoto

JF-Expert Member
Joined
Nov 22, 2012
Posts
1,985
Reaction score
1,286
afr.jpg

Katakata walikataa, utumwani kupelekwa,
Tena hawakuzubaa, kizembezembe kushikwa,
Ilizuka hata njaa, kwa kuchelea kudakwa,
Afrika, Afrika yangu, uhuru una ma’na gani?

Mababu watashangaa, kaburini wakitoka,
Watoto walo wazaa, nyumbani wakiondoka,
Yaani kama vichaa, nira wanavyo jivika.
Afrika, Afrika yangu, uhuru una ma’na gani?

Hawaioni thamani, ya mama yetu Afrika,
Walonayo mtimani, Ulaya na Amerika,
Roho waweka rehani, asama ng'ambo kufika,
Afrika, Afrika yangu, uhuru una ma’na gani?

Miji iliyo jengeka, na huduma za jamiii,
Kwayo wanahadaika, vipofu hawasikii,
Bila soni waropoka, Afrika haivutii,
Afrika, Afrika yangu, uhuru una ma’na gani?

Hayo wano yatamani, mbigu gani yalishuka?
Hivi hayawezekani, hapa petu kufanyika?
Jibu sina si utani, mwenzenu nasikitika,
Afrika, Afrika yangu, uhuru una ma’na gani?

Wapo waso fata sifa, zile zinazo vutia
Ni ulevi wa nyadhifa, ndio wana ukimbia
Nani yu tayari kufa, au mwili kuumia?
Afrika, Afrika yangu, uhuru una ma’na gani?

Afrika ina maafa, ikulu hazina haya,
Watu wake ni malofa, ufukara kila kaya,
Watoto wanavyo kufa, nabaki nashika taya.
Afrika, Afrika yangu, uhuru una ma’na gani?

Uhuru wetu Afrika, hivi una ma’na gani?
Kama tunagawanyika, sababu hizi imani,
Si zetu pasina shaka, vipi zivunje Amani?
Afrika, Afrika yangu, uhuru una ma’na gani?

Muislamu asende zika, alo kufa kanisani,
Msikiti kidondoka, mkristo yu furahani,
Na jambia wazishika, mithili ya hayawani,
Afrika, Afrika yangu, uhuru una ma’na gani?

Kwa mambo haya mawili, watu wapanda vihori,
Mosi tamaa ya mwili, pili kuepuka shari,
Wengi hawafiki mbali, wanamezwa na bahari,
Afrika, Afrika yangu, uhuru una ma’na gani?

Hapa ninaweka koma, nashindwa kuendelea,
Mato yanatomatoma, chozi lanielemea,
Nyerere na Nrumah, mzidi kutuombea,
Afrika, Afrika yangu, uhuru una ma’na gani?

Leo tena asubuhi kumepambazuka kwa taarifa ya wahamiaji haramu takribani 42 kufa maji wakijaribu kuingia Ulaya. Wengi wao wanatokea Ethiopi, Sudan, Misri, Libya, Algeria na Morocco.

Mungu azipokee roho za marehemu na wale walio nusurika wapone haraka, chombo kilichozama kilikuwa na wahamiaji haramu 600, hawa ndugu zetu, ni damu zetu, aidha kwa ulimbukeni wao au kwa machafuko katika nchi zao ndio imewafanya wahatarishe maisha yao kwa kuvuka bahari ya mediterania.

Waafrika na viongozi wetu, tukae chini tutafakari, tujiulize wapi tunakosea na vipi tutarekebisha, tufanye hivi, tufanye hivi, tufanye hivi kwa lengo moja, na si lingine bali kusitiri tupu zetu japo kwa viganja vyetu.

Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
Call/Whatspp 0622845394 Morogoro.
 
kweli kabisa. viongozi wetu wangekuwa serious hilo wangelichukulia kama janga la afrika na hatua za haraka zingehitajika. lakini ndo hivyo watu wako kwenye viyoyozi wakilindwa.
 
kweli kabisa. viongozi wetu wangekuwa serious hilo wangelichukulia kama janga la afrika na hatua za haraka zingehitajika. lakini ndo hivyo watu wako kwenye viyoyozi wakilindwa.
hakika tunahitaj kubadilika na kujitafakari.
 
Back
Top Bottom