SoC03 Kizuri chajiuza kibaya chajitembeza

Stories of Change - 2023 Competition
May 9, 2023
18
13
KIZURI CHAJIUZA KIBAYA CHAJITEMBEZA

UTANGULIZI

Dhana ya utawala bora na uwajibikaji ni kama pande mbili za sarafu moja, ili kuwepo na utawala bora uwajibikaji ni nguzo muhimu ambayo ni ya msingi. Utawala bora huusisha usimamizi katika msingi mkuu wa ujumuishaji na ushirikishwaji wa wahusika wote walio ndani ya jamii katika maamuzi yanayohusu ustawi wa maendeleo yao. Dhana ya uwajibikaji huusisha utayari wa kujibu,kubeba dhamana na kutoa maelezo kwa wananchi juu ya maamuzi katika kutekeleza dhamana aliyopewa kiongozi huyo. Mfano katika Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 kupitia ibara ya 8 (1)(c) imeeleza kwamba serikali inapaswa kuwajibika kwa raia wake.

Dhana ya utawala bora na uwajibikaji ni mhimili kwa maendeleo ya nchi yetu kisiasa, kiuchumi na kijamii. Utawala bora huundwa na msingi ifuatavyo; demokrasia, utawala wa sheria, haki na usawa, ushirikishwaji wa wananchi, pamoja na uwajibikaji na uwazi.

Zifuatazo ni hoja zinazochochea mabadiliko kuhusu uwajibikaji na utawala bora katika nyanja mbalimbali kama ifuatavyo;

Nyanja ya kiuchumi; utawala bora na uwajibikaji husaidia kutokomeza ubadhilifu wa mali za umma pamoja na vitendo vya rushwa katika jamii. Mfano mzuri kufuatia Taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali ya mwaka 2023 imeonyesha kwamba kuna changamoto ya ubadhirifu wa fedha za umma pamoja na vitendo vilivyokithiri vya rushwa ambayo vinafanywa na viongozi kupitia taasisi mbalimbali za umma hivyo kupelekea utoaji wa huduma kupitia taasisi hizo uwe wa kudorora na usioridhisha. Katika kuhakikisha utawala bora na uwajibikaji Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aliagiza viongozi kuwajibika kwa ubadhirifu huo.
inbound8461091210983083139.jpg

(Chanzo; jamii forums. Com.)

Nyanja ya kisiasa; Utawala bora na uwajibikaji husaidia kuimarisha utawala wa kidemokrasia pamoja na kudumisha utawala wa sheria. Mfano katika maamuzi ya kesi ya madai kati ya Mariam Mashaka Faustine na wenzake dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wenzake. Kesi Namba 88/2010 katika mahakama kuu ya Tanzania iliyopo dar es salaam. Mahakama ilisema kwamba ili kuhakikisha kwamba kuna utawala bora na uwajibikaji serikalini haina budi kuimarisha utawala wa kidemokrasia pamoja na kudumisha utawala wa sheria ambapo kila mtu anapaswa kuzingatia na kuongozwa na katiba ya nchi, sheria, na kanuni zilizopo ndani ya nchi, na kuhakikisha hakuna kiongozi kujiweka juu ya sheria au kufanya kitendo chochote kinyume na sheria.
(Chanzo: Kesi ya madai kati ya Mariam Mashaka Faustine na wenzake dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wenzake.kesi namba 88 / 2023 . Mahakama kuu ya Tanzania iliyopo dar es salaam.)

Nyanja ya Afya; Afya bora ni haki na msingi ya binadamu na kiungo muhimu cha kufanikisha ajenda ya maendeleo katika jamii. Serikali kupitia dhana ya uwajibikaji na uongozi bora ina wajibu wa kuhakikisha huduma za afya zinakuwepo kwa kila mtu na popote pale kwa kuboresha huduma za afya kupitia kuwekeza katika nguvu kazi ambapo serikali ina wajibu wa kuajiri watoa huduma za afya pamoja na kuhakikisha kwamba kuna vitendea kazi vya kutosha kama vile madawa, hospitali na zahanati za kutosha. ambavyo kwa pamoja husaidia kukuza uchumi na hivyo kupunguza umaskini.( Chanzo UN News https//www. News. Com)

Nyanja ya Elimu; uwajibikaji na utawala bora ni nguzo muhimu katika ukuaji wa sekta ya elimu nchini Tanzania. Ambapo elimu inatolewa pasipo kuangalia hali ya kifedha, dini, jinsia wala kabila. Ili kuthibitisha hili serikali chini ya Uongozi wa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inahakikisha kwamba Elimu inatolewa bila malipo kuanzia elimu ya awali mpaka kidato cha sita. Pia katika elimu ya juu. Serikali imetoa hela ya kujikimu kwa wanafunzi wa elimu ya Juu kama moja wapo ya njia za kusapoti sekta ya elimu nchini Tanzania..
inbound6407032141425612650.png

(Chanzo; Gazeti la mwananchi la tarehe 12 mwezi februari 2023.)

Nyanja ya ajira; katika nchi zinazoendelea tatizo la ajira kwa wananchi wake limekuwa ni tatizo ambalo limeshindwa kutatuliwa kwa muda muafaka. Hali hii imekuwa ni mbaya zaidi hususani nchini Tanzania ambapo vijana wenye elimu na wasio na elimu wako mtaani bila kazi. Ukweli ni kwamba uwajibikaji ndiyo suluhisho la tatizo hili la ajira kwa kuanzia kwa mtu mmoja mmoja , ngazi ya familia, asasi na taasisi mbalimbali pamoja na serikali kwa ujumla.
inbound3821857303296433838.png

Chanzo( kijani jitathmini. Blogspot. Com.)

HITIMISHO
Utawala bora pamoja na uwajibikaji ni nyenzo za kusukuma maendeleo ya nchi mbele kupitia kupunguza umaskini na ili tuwe na jamii bora inayowajibika yenye misingi ya utawala bora hatuna budi kupiga vita vitendo vyote ambavyo vinachochea, uovu, ubadhirifu, rushwa, kwa kufanya hivyo tutakuwa na jamii bora yenye kufuata misingi ya haki na usawa baina ya wananchi ndani ya nchi..

IMEANDALIWA NA
MWESIGA FROLIAN - Mwanasheria.
 
Back
Top Bottom