KERO Kivuli cha "Oktoba 29" kilivyoziweka siku 100 za Urais wa Samia kwenye mabano

KERO Kivuli cha "Oktoba 29" kilivyoziweka siku 100 za Urais wa Samia kwenye mabano

Hii ni kero ambayo mwananchi ameiwasilisha JF akitaka wahusika kuchukua hatua
A

Anonymous

Guest
Zikiwa zimepita siku 100 tangu kuapishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuiongoza Tanzania katika muhula wake wa pili, tathmini zimekuwa nyingi na zenye sura tofauti. Wapo wanaotazama kisiasa, wengine kiuchumi, kijamii, kiusalama na hata kidiplomasia. Kila kundi lina taswira yake.

Hata hivyo, katika uchambuzi wa kina, kuna hoja inayojitokeza kwa uzito: Siku 100 za kwanza za muhula wa pili zimekuwa chini ya kivuli cha “Oktoba 29”.

Oktoba 29: Katika muktadha upi?
“Oktoba 29” si tarehe ya kawaida katika muktadha huu. Ni alama ya matukio yaliyojitokeza wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2025, matukio ambayo kwa wengi yameacha alama ya kihistoria, yakisababisha mjadala mpana na maumivu kwa sehemu kubwa ya jamii.

Matukio hayo yalibadili mwelekeo wa mijadala ya kisiasa nchini na kuathiri taswira ya Tanzania ndani na nje ya mipaka yake. Hivyo, siku 100 za Rais Samia haziwezi kutazamwa nje ya muktadha huo; ameanza safari yake ya pili ya uongozi katika mazingira yenye kumbukumbu nzito zenye kivuli cha matukio hayo ya kihistoria.

Haya ni baadhi ya maeneo ambayo kivuli kimejidhihirisha ndani ya siku 100:

Diplomasia na Wadau wa Maendeleo

Diplomasia ni mhimili nyeti kwa taifa linaloendelea. Ni nguzo inayobeba uchumi, misaada, ushirikiano wa kimataifa na taswira ya nchi. Nguzo hiyo ikitikiswa, madhara yake huenea katika sekta nyingi.

Katika siku 100 za mwanzo, Rais Samia na timu yake walikabiliwa na jukumu la kurejesha imani na kuimarisha mawasiliano na washirika wa maendeleo. Umoja wa Ulaya (EU), Umoja wa Mataifa, Marekani na wadau wengine walionesha wasiwasi kuhusu hali ya demokrasia na haki za binadamu kufuatia matukio ya uchaguzi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Mbunge ameonekana akifanya mazungumzo ya kidiplomasia na baadhi ya wadau, jambo linalotafsiriwa na wengi kuwa ni juhudi za kurejesha hali ya kuaminiana. Thabit Kombo ameonekana akitoa ufafanuzi na kushiriki majadiliano mbalimbali. Hata hivyo, ni dhahiri kwamba taswira ya nchi kimataifa imehitaji nguvu ya ziada kuijenga upya—hali inayohusishwa moja kwa moja na kivuli cha Oktoba 29.

Ukosoaji wa Serikali na Changamoto ya Uaminifu wa Umma
Mitandao ya kijamii imekuwa uwanja mkubwa wa mjadala katika siku hizi 100. Kumekuwepo na wimbi la ukosoaji wa maamuzi na kauli za Serikali, huku kumbukumbu za matukio ya uchaguzi zikirejelewa mara kwa mara.

Zaidi ya hapo, changamoto nyingine imejitokeza: baadhi ya kauli za viongozi wa Serikali, hata katika masuala ya kitaifa, zimeonekana kutopokelewa kwa uzito ule ule wa awali. Hali hii inaashiria kupungua kwa kiwango fulani cha imani au kuongezeka kwa mashaka miongoni mwa wananchi.

Kwa taifa lolote, uhalali wa kisiasa na uaminifu wa umma ni mtaji mkubwa. Pale panapokuwa na doa katika mchakato wa kisiasa, athari zake huonekana katika namna wananchi wanavyoipokea Serikali yao.

Mwenendo wa Ziara za Kikazi
Katika kipindi hiki, Rais Samia amefanya ziara chache za kikazi ndani ya nchi, pamoja na ziara moja tu ya nje. Kwa marais wengi, siku 100 za mwanzo huwa kipindi cha kuonesha kasi ya utekelezaji na kuimarisha uhusiano wa moja kwa moja na wananchi kupitia ziara za mara kwa mara.

Uchache huo wa ziara umetafsiriwa kwa namna tofauti. Wapo wanaoamini ni mkakati wa kupunguza taharuki na kujenga utulivu wa ndani kwanza; wengine wanaona ni ishara ya tahadhari kutokana na mazingira ya kisiasa yaliyotangulia. Kwa vyovyote vile, hoja hii pia inarejea katika muktadha wa kivuli cha Oktoba 29.

Upi Mwelekeo?
Siku 100 sio kipindi kirefu katika muhula wa miaka mitano. Hata hivyo, ni kipimo muhimu cha mwelekeo wa uongozi. Kwa Rais Samia, muhula wa pili umeanza katika mazingira yenye kivuli kizito kilichotokana na matukio ya Oktoba 29.

Changamoto kubwa inayoonekana sio tu ya kiuchumi au kiutendaji, bali ni kurejesha imani ndani na nje ya nchi. Ikiwa kivuli cha Oktoba 29 kitaendelea kuathiri taswira ya uongozi, basi juhudi za makusudi zaidi zitahitajika ili kuleta mwelekeo mpya.
 
Back
Top Bottom