Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 22,455
- 32,981
KITU GANI HIKI WATU KUSHEHEREKEA MAUTI?
Nimeinamisha kichwa changu toka alfajir nawaza hili la watu kusheherekea kifo.
Mtume (SAW) katuasa kasema tuseme mema ya maiti zetu.
Hawa wamepitiliza angalau wangesema.
Hawa wanacheza ngoma kusheherekea kifo.
Nimeinamisha kichwa changu nawafikiria watoto na mke wa marehemu.
Msiba walionao wa mpendwa wao unawatosha hapana haja ya kuwabebesha na hili.
Lilipata kutokea jambo kama hili Dar es Salaam katika miaka ya 1970.
Bwana mkubwa mmoja kapata ajali kafariki dunia.
Mtu mkubwa sana huyu kisha mpigania uhuru na katika wanachama wa mwanzo wa TANU na mtu aliyekuwa karibu sana na Mwalimu Nyerere.
Waliokuwa wanamjua wanasema alikuwa hana miadi ya Mwalimu anawekwenda kwake iwe Ikulu au nyumbani kwa Mwalimu muda wowote na atapokelewa.
Mji wa Dar es Salaam wote una taarifa ya kifo cha bwana huyu.
Jambo la kushangaza.
Kwa kawaida sisi watu wa Pwani msiba ukitokea tu kitu cha kwanza ni kupelea taarifa msikitini kisha nyumbani panafungwa maturubai nje na kutandika majamvi kwa kivuli na watu kukaa.
Na huwa haichukui muda nje barazani watu huanza kujazana.
Wanaume wanakaa barazani wanawake uani na ikiwa ua mdogo hautoshi watatengewa nyumba ya jirani.
Msibani nyumbani kwa marehemu huyu lau taarifa za msiba zimeshafika hapaonekani watu kukusanyika nje nyumbani kwake.
Hili dogo.
Lililofanywa na msikiti wa jirani ndilo kubwa.
Waliufunga msikiti wao ili wasiitwe kushiriki kwa chochote katika msiba wa marehemu huyu.
Waliokwenda msikitini ama kwa kutoa taarifa au kuchukua jeneza hawakukuta mtu.
Lakini wakubwa wa serikali na chama wamefika nyumbani kwa marehemu.
Hali waliyoikuta pale iliwasononesha sana na kupita kiasi.
Iko siku nimekaa nazungumza na Mzee Aboud Jumbe nyumbani kwake Mji Mwema.
Wakati huo wa kifo cha marehemu huyu yeye alikuwa Makamo wa Rais.
Mzee Jumbe anasema yeye ndiye aliyetoa wazo kuwa vijana wa TANU Youth League haraka wakusanywe waletwe nyumbani kwa marehemu kusimamia maziko.
Mtu mmoja kamkuta mwenzie kwenye barza nje ya hoteli anacheza dhumna.
Anamwambia, ‘’Eee bwana we hebu acha huo mchezo twende mazikoni.’’
Mwenzie anamjibu, ‘’Kwani nani kafariki?
Anamtajia jina ingawa anajua kuwa anamcheza shere kwani Dar es Salaam nzima ilikuwa na taarifa.
Hampi jibu anabakia kimya anaendelea na mchezo na waliomzunguka kuangalia mchezo wito ule wa kwenda mazikoni pia unawahusu lakini na wao wamempuuza wako kimya wameshughulishwa na dhumna.
Sasa anawapigia kelele wote wale.
‘’Jamani Eeeh! Twendeni mazikoni.’’
Anajibiwa, ‘’Hii ni fardhi kifaya ukienda wewe kuzika umetuondolea sote dhima mbele ya Allah.’’
Ndugu yao hakutaka kuendelea taratibu alijiondoa mahali pale.
Huyu marehemu aliwafanyia nini nduguze kiasi cha wao kumsusa katika umauti wake?
Ninaitalii upya taazia aliyoandika Mohamed Mlamali Adam katika jarida la Africa Events kuhusu kiongozi mmoja Zanzibar aliyefariki zaidi ya miaka 30 sasa.
Mlamali ni Sheikh.
Sijapatapo kuchoka kuikumbuka taazia hii kwa sababu nashindwa kuiweka mahali pake kuwa ni taazia au kitu kingine cha ‘’satire,’’ yaani kichekesho kumfanya msomaji badala ya kuingiwa na majonzi ya kifo acheke.
Unafanya nini unapomuona mtu anacheza muziki kwa furaha akifurahi msiba mkononi kashika chupa ya bia?
Ikiwa utacheka ni kicheko lakini si kicheko kama kicheko kinavyofahamika.