Kitabu: Masimulizi juu ya Wazaramo.

Kitabu: Masimulizi juu ya Wazaramo.

Lycaon pictus

JF-Expert Member
Joined
Jan 31, 2021
Posts
10,890
Reaction score
18,836
Na R. Mwaruka. Unaweza kukisoma free ndani ya app ya Maktaba Sauti. Ipo playstore.

SURA YA 1

PAZI KILAMA KATIKA UZARAMO
WAZARAMO ni jumla ya mchanganyiko wa makabila ya Kibantu. Sehemu kubwa ya mchanganyiko huo ni Wakutu na watu wengine wenye asili ya Mwambao. Neno hili 'Uzaramo' linatokana katika 'Kuzalama' na maana yake ni 'Kusehelea'. Kwa hivi, Wazaramo hasa maana yake ni Waseheleaji, yaani watu waliotoka katika nchi mbalimbali na kufanya masikani katika nchi hii. Mabadiliko ya neno hili yalitokea kwa sababu ya matamshi ya watu; neno lenyewe hasa ni Zalamo, yaani nchi iliyosehelewa, lakini baadaye ikabadilika na kuwa Zaramo au pengine hutamkwa Zaramu.

Hatuna hakika ya tarehe maalumu ya kusehelea, ila twafahamu hayo katika masimulizi ya mgawanyiko wa koo mbalimbali za Uzaramo ambazo nyingi zinasimuliwa kwamba zimetoka katika makabila mengine ya Kibantu na kujiunga katika Uzaramo. Lakini wazee wengi wanakubaliana kwamba mkubwa wa Uzaramo alikuwa Pazi Kilama Lukali mwenye asili ya Ukutu.

Pazi huyo aliitwa kwa majina mbalimbali ya ushujaa na kutukuzwa kama hivi ‘Pazi Kibamandu, kihabamanduka na Ulanga wela', maana yake, ‘Pazi Kifuniko, Kikifunuka na mbinguni kweupe!' Na tena aliitwa 'Mwana Mkungwi pala' na 'Mwana Mwizila Kumogo', maana yake 'Mwana wa Utukufu' na 'Mwana ajiwaye kwa heshima'. Na katika kutukuzwa kwake aliitwa 'Gulu Jasi' yaani, 'Mfalme Mkuu'.

Pazi huyo asili yake hasa alitoka Kibwemandu, katika Ukutu, nchi iliyo sasa magharibi ya Uzaramo. Kwa upande mwingine ndio sababu aliitwa Pazi Kibamandu. Ukoo wake ni Mulugoma, na mtala wake ni Kilama na Lukali. Baba yake aliitwa Pazi Mvilama. Huyu Pazi Mvilama alimwoa Mulambena katika kizazi cha Nyambiza, akamzaa Pazi Kilama.

Pazi Kilama aliondokea kuwa shujaa tangu alipokuwa mvulana, maana alikuwa hashindiki katika mapigano na watoto wengine. Alikuwa hodari katika kutupa mishale na mikuki katika uwindaji. Alipokuwa mtu mzima, watu wakamheshimu kwa sababu ya ushujaa wake, maana katika vita vya kabila yeye aliweza kuongoza jeshi na kuwashinda adui. Kwa ajili hiyo, wakamtukuza na kumwita Gulu Jasi. Na kila mtu aliyekwenda mbele yake kumwamkia alijiinamisha na kunyoosha mikono yake mbele na kusema, 'Simbamwenee'! Na Pazi aliitikia, ‘Utwaa!' Kisha mtu huyo humwita kwa jina lake, 'Pazi'! Na Pazi hujibu, ‘Nene Mwana Mkungwi pala, Mwana Mwizila kumogo'. Maamkio hayo ndiyo yaliyotumika katika utawala wa Pazi.

Lakini jambo la kusikitisha ni ya kwamba maamkio hayo ya asili yalianza kupotea baada ya kuingia Waarabu nchi hii. Watu wote waliwatukuza Waarabu na kumheshimu Sultani Said, ndipo maamkio yakawa hivi: aamkiaye husema, 'Mwinyi'! maana yake ‘Bwana' na aitikiaye hujibu, 'Mwinyi Mkuu Saidi', yaani bwana mkubwa ni Saidi tu. Na kwa sababu ya watumwa kuwaheshimu mabwana zao amkio la 'shikamoo' likatukuka zaidi. Shikamoo ni neno lenye maneno mawili pamoja, yaani, 'Nashika miuu'. Miuu maana yake ni miguu, kwa Kimwambao, na umoja wake ni muu. Kwa sababu ya mabadiliko ya matamshi baadaye ikawa ‘shikamuu' na siku hizi ni 'Shikamoo'. Marahaba maana yake ni 'Ahsante'. Kumheshimu mtu kwa kumshika miguu ni adabu nzuri ikiwa mwenye kuamkia anaifahamu maana yake.

Basi tuendelee na habari za Pazi. Pazi alikuwa na miji yake miwili, wa kwanza uliitwa Zongomelo, na wa pili ulikuwa Kinyangulu. Miji hiyo miwili ndiyo iliyokuwa ikivuma kwa fahari ya Pazi Kilama. Pazi alikuwa na dada zake wanne ambao nao walitoa vizazi vya wapwa wa Pazi. Dada zake walikuwa hawa:

(1) Nyamhazi (2) Mulalukali (3) Vinhama, na (4) Matata- hala. Mzao wa wapwa wa Pazi kwa maumbu zake ulikuwa hivi:

Nyamhazi alimzaa Temodimogoke na dada zake wawili, Kidang’hali na Kitumbe. Mulalukali alimzaa Hega. Vinhama aliolewa na Mluguru akamzaa Kingalu. Na Matatahala aliolewa na Mdowe akamzaa Mwene.

Pazi Kilama alikuwa na ndugu zake wawili waliozaliwa kwa baba na mama zao mbalimbali, nao ni Nyamitombo na Dilunga. Huyu Dilunga alikuwa na wapwa zake sita wanaohusika katika urithi wa Uzaramo, nao ni Bofi, Lugeng'he, Malamula, Ditali, Zamvi na Lunyovu; hawa waliishi pamoja na Pazi Gulu Jasi kule Kinyangulu.

Sifa zake Pazi Kilama zinafahamika kwamba alikuwa mkakamavu, nywele zake zilikuwa ndefu hata mara nyingine zilifunika uso wake, nazo hazikunyolewa tangu utoto wake, alikuwa na umbo la kutisha. Mara kwa mara alionekana akitembea na mbwa wake mkubwa aliyefanana na chui, huyu alimtumia zaidi katika mawindo. Watu waliokutana naye hawakuthubutu kumkaribia kwa jinsi alivyojipamba kishujaa. Kinyangulu ni mahali pazuri penye udongo wenye rutuba uwezao kustawisha aina nyingi za mimea.

Mahali alipoishi Pazi palijengwa ngome imara ya kukinga maadui wa kila upande. Ngome hiyo ilizungushiwa miti imara, na mji wa Pazi ulikuwa katikati ya ngome. Ngome ya namna hii iliitwa 'mhongono'. Ngome hiyo ililindwa na askari hodari wenye silaha. Kila siku askari sita walikuwa na zamu ya kuilinda ngome.

Mke wa Pazi Kilama alikuwa Mulamtumbikwa, na kwa sababu alikuwa mke wa Sultani aliitwa 'Sano'. Sano maana yake ni 'Bibi mheshimiwa' au Malkia. Pazi Kilama alijulikana sana tangu Ukutu mpaka Zaramo ya Mwambao. Watu wengi wa nyakati zile walimtegemea kwa sababu ya ushujaa wake. Katika siku alizoishi kule Kinyangulu huko pwani ya Mzizima, Wakamba waliingia na kuanza kuihujumu nchi hii. Vita na unyang'anyi wa Wakamba uliwafanya Wamashomvi walioishi mwambao kutawanyika huko na huko. Wengine walikimbilia visiwani, na wengine walikimbilia bara ya Uzaramo wakajificha misituni. Wakati huo Pazi Kilama hakuwa na habari yo yote juu ya Wakamba walioingia Mzizima. Wakamba walikuwa jeuri na hodari kwa mapigano, nao waliwaogofisha mno watu walioishi Zaramo ya Mwambao siku zile.
 
MATAYARISHO YA KUPIGANA NA WAKAMBA

Katika majira ya kuingia Wakamba Zaramo ya Mwambao siku chache zilizofuata alikuja mtu mmoja mweupe aliyetoka Shirazi, akajinaki kwamba yeye ni mmoja katika ukoo wa Wabarawa; kwa hiyo, watu wakamwita Mbarawa. Mbarawa huyo alipofika pwani ya Mzizima akawakuta watu wote wamekimbia kwa kuwaogopa Wakamba, ila mtu mmoja mmoja alionekana akipitapita kwa hofu. Mbarawa yule aliitamani sana Mzizima, akaazimu kufanya maskani. Akajitahidi kuwatafuta wenyeji hata baadaye akaonana na wale waliojificha visiwani. Mmashomvi mmoja aliyeitwa Makalisani alimpokea yule Mbarawa akamkaribisha kule kisiwani. Baadaye yule Mbarawa akafungua biashara ya nguo, shanga, vikuku na chumvi akisaidiwa kuiendesha biashara hiyo na yule mwenyeji wake Makalisani. Baada ya siku chache Mbarawa alioa mke wa Kimashomvi na akazidi kuhusiana sana na Wamashomvi.

Lakini ule unyang'anyi wa Wakamba ulizidi kuendelea, na mara kwa mara duka la Makalisani liliingiliwa na wanyang'anyi hao. Mbarawa alichukizwa sana na tabia ile ya ukatili wa Wakamba, akatafuta njia ya kuwakomesha lakini haikuwezekana. Baadaye yule Makalisani akatoa shauri akasema, 'Pazi Kilama ni mtu shujaa kabisa. Yeye angeweza kukomesha jeuri hii ya Wakamba, lakini yuko mbali katika bara ya Zaramo.' Kwa maneno hayo, yule Mbarawa akashikwa na hamu ya kumwona Pazi Kilama.

Katika siku zile alikuwako mtu mmoja jina lake Mtandila aliyezaliwa na Wamkwama. Mtandila aliposa bibi mmoja katika ukoo wa Pazi Kilama, hivyo akawa mkwe wa Walugoma. Lakini pia Mtandila alikuwa na bibi mwingine katika pwani ya Mzizima. Yule bibi aliyemposa kwa Walugoma akamweka Kinyangulu. Na yule aliyemposa pwani alimweka Mzizima. Kwa ajili hiyo Mtandila alikuwa akiishi miezi fulani fulani Kinyangulu na miezi fulani fulani Mzizima. Maisha hayo hayakumsumbua maana alikuwa msafiri hodari, akazoea tabia za Wamwambao na za bara ya Zaramo.

Basi Mtandila alipokwisha kuhesabu siku zake za kukaa Kinyangulu akafanya safari ya kwenda pwani kama ilivyokuwa desturi yake. Lakini alipofika karibu ya Mzizima, sehemu za Pugu, akawakuta watu wamefanya maskani na kujenga vijumba vidogo vidogo. Watu hao walikuwa wenyeji wa Mzizima waliokimbia vitisho vya Wakamba, na hata bibi yake Mtandila alikuwa katika kundi hilo hilo la wahamiaji. Mtandila alipohoji habari ile, akajulishwa kuwa nchi ya Mzizima imeingiliwa na vita, na ya kwamba watu wengine wamehamia visiwani. Kwa maelezo hayo, Mtandila hakutosheka, ila aliazimu kwenda mpaka Mzizima ili akashuhudie mwenyewe. Mawazo ya kushuhudia yalimjia Mtandila kwa sababu alitaka apate ushahidi safi wa mambo yalivyotokea ili arudipo Kinyangulu apate kumweleza Pazi Kilama.

Alipofika Mzizima akaona kweli yale aliyoambiwa yalikuwa sawasawa. Alitembea huko na huko katika Mzizima asimwone mtu ye yote ila mahame tu. Baadaye Mtandila alikutana na Makalisani pamoja na yule Mbarawa ambao walikuwa na wasiwasi na shauku ya kumpata Pazi Kilama. Baada ya kuulizana habari, Mtandila akawafahamisha kuwa yeye anatoka Kinyangulu, na ya kwamba ni mkwe wa Pazi Kilama. Baada ya majulishano yao, yule Mbarawa alimtaka radhi Mtandila wafuatane kwenda Kisiwani. Mtandila akaridhika, akafuatana nao mpaka Kisiwani.

Kule Kisiwani Makalisani na Mbarawa wakafanya mipango ya kumtuma Mtandila aende Kinyangulu kumwomba Pazi Kilama aje awafukuze Wakamba. Mbarawa alitoa ahadi ya kumpa Pazi Gulu Jasi zawadi kubwa ikiwa atawapiga Wakamba na kuwafukuza. Kisha akasema, 'Sisi wageni twapenda kukaa nchi hii na kufanya biashara kwa amani, lakini udhalimu wa hawa Wakamba unatuvunja uwezo wetu.' Kisha akatoa zawadi ya kikanda cha chumvi akampa Mtandila na huku akisema, 'Mpelekee Sultani zawadi hii, kisha umtake aje huku pwani aone matatizo tuliyonayo juu ya Wakamba.' Wakati ule chumvi ilikuwa kitu cha tunu sana katika Zaramo ya bara.

Basi Mtandila akatwaa ule mzigo wa chumvi, akafanya safari hadi Kinyangulu. Alipofika kule, akamkabidhi Sultani zawadi ile, kisha akamweleza mkasa na masumbufu yaliyoko pwani. Akamweleza hahari za jeuri ya Wakamba na ushujaa wao, akamweleza jinsi Mbarawa na jamaa wengine wa pwani wanavyohitaji msaada wa kuwafukuza Wakamba.

Pazi alisikiliza kwa makini maneno yote ya Mtandila, kisha akafungua mzigo wake alioletewa akatwaa sehemu akawagawia nduguze na baba yake. Nao walipoionja wakapendezewa sana, wakasema, ‘Hakika huko pwani kuna mtu mwema ametuletea kitu cha tunu, anastahili kusifiwa kwa ajili ya zawadi hii.'

Lakini Pazi alipoambiwa habari ile ya kuwafukuza Wakamba alikataa, akasema, 'Ah! huyo Mkamba ni mgeni tu, atakaa kwa muda kisha ataondoka, wala hakuna maana ya kupeleka majeshi ya vita kwa ajili ya wapita njia.' Baba yake alipoyasikia maneno hayo akamwambia, 'Tazama, mwanangu, mtu akikuingilia katika nchi yako nawe ukitulia tu, basi fahamu kuwa mwishoni mtu huyo atakutawala, nawe hutokuwa na uwezo wo wote juu yake. Wakamba hao wameingia pwani iliyo nchi yako, wanafanya masumbufu makubwa kwa watu, bila shaka hao ni maadui, wanastahili kupigwa na kufukuzwa. Angalia.' Mzee aliendelea, ‘Kama hakuna kizuizi cho chote cha kuwazuia, basi watafika mpaka huku tuliko na kuleta balaa kubwa la vita.' Je! Unapenda vita vikujie mpaka miguuni ndipo ujue kama kuna hatari? Fahamu kuwa watu hao ni mashujaa na ikiwa utawaacha mpaka wafike huku, bila ya shaka tutapoteza mali zetu, watoto na wanawake watakuwa katika shida pevu.'

Nao dada zake Pazi waliyaingilia mashauri hayo na kumshawishi Pazi akusanye majeshi ya kuwapiga Wakamba. Maneno ya baba na ya wale maumbu yaliingiza tashititi moyoni mwa Pazi Kilama na watu wengine waliokuwapo. Pazi Kilama alifikiri mengi juu ya ushujaa wake, akawaza kuwa kama akiyadharau maneno ya baba yake na maumbu zake, bila shaka heshima yake ya ushujaa itapungua au kupotea kabisa. Na hasa kwa maneno mengine waliyotamka wale maumbu waliposema, 'Tungekwenda kupigana nao hao Wakamba tujue kama watatushinda ndipo tuwaachie nchi hii waitawale, na kama tutawashinda waondoke kabisa katika nchi yetu, lakini ah, wanawake hawawezi kutenda hivyo !' Na hapo baada ya matokeo mengi ya maneno, mama wa Pazi pia alisema, 'Mwanangu ukidharau yasemwayo hapa yatakukuta makubwa, ni bora ufanye shauri la kuwafukuza Wakamba kabla hawajafika huku tuliko.'

Basi baada ya hapo Pazi alikubali kufanya matayarisho ya kupigana na Wakamba, akaondoka kwenda kutazamia katika mzimu. Alitaka kujua kama akienda vitani atashinda au atashindwa. Mzimu ulimfahamisha kuwa hawezi kushinda ila kwa kufanya uganga na kutoa kafara. Akamwajiri mganga mmoja aliyeitwa Kuyawa. Mganga huyo alikusanya vipande vya miti na wadudu wa aina mbalimbali, akatengeneza uganga wa kumpa nguvu Pazi ashinde katika mapigano. Kafara lilitolewa kwa kumwua chatu na kupata damu yake ambayo ilichanganywa na masizi yaliyopatikana kwa kuwachoma moto wadudu wenye sumu kali, pamoja na mafuta ya mbarika. Mchanganyo huo ulitiwa katika kibuyu, kisha akapewa Pazi ili ajipake mwili mzima kabla ya kufunga safari ya vitani. Mchanganyo huo uliitwa 'vumba'. Vumba hilo lilitumiwa pia kwa kuwapaka askari waliokwenda vitani katika jeshi la Pazi.

Mwanamke mmoja aliyeitwa Mulanjechele Nyakitimba alikuwa msaidizi wa Kuyawa. Mwanamke huyo, kwa asili hasa, alikuwa Mndengereko. Mulanjechele alionekana kila mara akifuatana na Kuyawa; alikuwa akipeleka mkoba wa uganga na usinga mkononi.

Pazi alikuwa na ngoma zake mbili, ngoma moja kubwa na nyingine ndogo, na zote zilikuwa zikipigwa kwa kujulisha ishara maalumu. Ile ngoma kubwa iliitwa Kuwahukuwe, nayo ilipopigwa iliwajulisha watu wakusanyike kwa Sultani kuna mkutano. Wamashomvi wa mwambao nao walikuwa na ngoma yao kubwa iliyoitwa 'Goma la Enzi' nayo ilitumika pia kwa kuitisha mkutano.

Ile ngoma ya pili ya Pazi iliyokuwa ndogo iliitwa 'Msingili'. Ngoma hiyo iliwambwa kwa ngozi ya mtu, nayo ilipopigwa tu iliwajulisha watu kuwa vita i tayari. Kila mwanamume asikiapo mlio wa ngoma hiyo, hukusanya silaha zake na kuwa tayari kwenda vitani.

Basi kwa siku zile Pazi alipokwisha tengenezewa vumba, akaipiga ile ngoma kubwa ili raia wakutanike kwake. Watu waliposikia mlio wa ngoma walikusanyika upesi, baada ya hapo Pazi akawahutubia na kuwaeleza habari za Wakamba. Akawaambia kuwa wawe tayari kwenda vitani kupigana na Wakamba walioingia katika nchi yao. Watu wote waliokusanyika siku ile waliitikia kwa umoja wakasema, "Tutapigana nao mpaka tuwashinde.' Wakaweka siku maalumu ya kwenda kupigana nao. Lakini siku zile zile Pazi alipokuwa akifanya matayarisho ya vita, Wakamba walikuwa wanasogea kuelekea upande wa Kinyangulu. Kama Pazi angeajizika na kukaa kwake muda wa mwezi mmoja tu, Wakamba wangeingia Kinyangulu na kuiteka nchi ghafla.

Hata siku ya mkusanyiko wa kwendea vitani ilipowadia, Pazi hakukawia kuonyesha miujiza yake. Pale uwanjani palikuwa na mti mkubwa wa mpingo. Pazi aliukazia macho sana ule mpingo, kwa ghafla mpingo ule ukapasuka katikati, ukafanya nafasi kubwa ya kuweza kupita mtu. Kweli ilikuwa ajabu, mpingo ule ulikuwa mbichi, lakini kwa ajili ya miujiza ya Pazi ulipasuka mara moja na kuacha nafasi ya njia katikati yake. Pazi akatwaa ngozi ya pofu akaitandika chini pale karibu ya mlango wa ule mpingo, kisha akawaambia watu wote wakanyage ile ngozi na kupita katikati ya ile nafasi. Pazi alitaka wapite mmoja mmoja ili apate kujua wingi wa askari zake wote.

Watu wakaanza kukanyaga ile ngozi na kupita mmoja mmoja. Yasemekana kwamba tokea majira ya asubuhi watu waliendelea kupita mpaka jioni. Walipokwisha kupita wote, Pazi akaona kwamba ile ngozi aliyotandika imesagikasagika kabisa, akatambua kuwa askari alio nao ni wengi, wanatosha kupigana vita na kuwashinda Wakamba.

Pazi alipokwisha kufanya miujiza yake, mpwawe aliyeitwa Kingalu akasimama mbele za watu wote waliokuwapo akasema, 'Mjomba Pazi amefanya jambo zuri la kumbukumbu la kuwajulisha watakaozaliwa baadaye. Sisi tuliopo tumepata onyesho kubwa la matayarisho ya vita, tutawasimulia watoto wetu, na wao watawasimulia watoto wao. Na wengine wowote watakaotaka kujua habari za vita hivi wataambiwa kwamba hii ndio alama ya mpingo walipopita askari wa Pazi.'

Kingalu alipomaliza kusema, Pazi akamjibu akasema. 'Wewe unataka mpingo huu uwe ndio alama ya kuwajulisha watoto wetu wajao, lakini huu ni mti tu, hauna maisha ya kuendelea.' Akawageukia wote waliokuwapo akawaambia, 'Ngojeni niweke alama ya kudumu miaka yote waione watu wa ulimwengu huu na wa ulimwengu ujao, alama ya kudumu mpaka mwisho wa dunia,' Ndipo akawaambia wote waliokuwapo wafuatane naye mpaka mlima wa Kinyangulu. Pale pana jiwe kubwa sana lililo mfano wa mwamba mgumu, akatoa dawa kutoka katika kibuyu kidogo akalipaka lile jiwe akasema, kwa kupaza sauti ‘Kibwe banduka ulanga wela.' Maana yake 'Jiwe megeka mbinguni kweupe!' Lile jiwe likawa laini kama tope, Pazi akainua mguu wake wa kuume akalikanyaga, na mbwa wake akakanyaga karibu naye. Kisha akatwaa mkuki wake mkubwa ulioitwa Palala akausimika juu ya jiwe lile lile, mara akarukia upande wa pili pamoia na mbwa wake na Palala yake mkononi. Baada ya vile alama ya unyayo wake, alama ya fumba la mbwa pamoja na alama ya msimiko wa mkuki zikabaki juu ya lile jiwe. Alama hizo zipo kule Kinyangulu mpaka leo.

Ndipo Pazi alipomwambia Kingalu na wote waliokuwapo akasema, 'Hii ndio alama yetu sisi, pamoja na watoto wetu, na watu wote wa siku zijazo wataambiwa kuwa alama hii ni ya Pazi Gulu Jasi wakati alipopita kwenda vitani kupigana na Wakamba.
 
VITA VYA PAZI NA WAKAMBA

Alipokwisha kufanya miujiza ile, Pazi akaondoka na jeshi la wote waliokuwapo, wakafanya safari kwenda kupigana na Wakamba. Wakapakaa ile dawa na ngoma ndogo ya kujulisha safari ya vitani ikapigwa. Wakasafiri kwa muda wa siku tatu, hata siku ya nne wakakutana na jeshi la Wakamba. Mahali walipokutana paliitwa Kisilimisi. Kwa vile Wakamba walijiweka tayari kwa mapigano basi vita vilianza pale pale Kisilimisi. Mapigano yalikuwa makali sana, walipigana kwa muda wa siku nne, na Wakamba kabisa hawakuweza kukimbia.

Pazi alipoona kuwa Wakamba hawashindiki akawaza kuwa huenda pengine jeshi lake likashindwa kwa kuzidiwa nguvu. Basi usiku ulipoingia akamwita mtumwa wake mmoja aliyekuwa mwerevu sana, jina lake Baraka. Huyu Baraka alipendwa sana na Pazi Kilama kwa sababu ya uhodari na werevu wake. Pazi akampa dawa Baraka akamwambia, 'Chukua dawa hii, fanya hila ufike kwenye kambi ya Wakamba, kisha itie dawa hii katika moto wanaoutumia, ukifaulu kufanya hivyo basi rejea upesi.' Akampa na dawa ya kuwapumbazisha Wakamba wasimwone. Baraka akapokea ile dawa akafanya hila usiku ule hata akafika kwenye kambi ya Wakamba, akaenda mpaka kwenye moto waliouwasha, akatwaa ile dawa akaitia motoni. Kisha akaondoka kierevu na kurudi kambini kwake salama, akawasilisha majibu ya utumishi wake kwa Pazi kwamba kazi aliyotumwa amekwisha itimiza.

Katika vita hivi vya Pazi na Wakamba wapwa zake Pazi wote walikuwamo, nao pia walikuwa mashujaa katika vita. Basi asubuhi na mapema Pazi na watu wake wakaamkia vita. Vita vikawa vikali kuliko siku za mwanzo. Wakamba wakaelemewa vibaya, wakafukuzwa kwa nguvu. Walifukuzwa toka pale Kisilimisi mpaka Minamina kando ya mtu Ruvu. Mahali hapo palikuwa na kina kirefu cha maji. Hapo Wakamba walikuwa wanatawanyika ovyo, hawakuweza kuyavuka maji yale yenye kilindi kirefu, na huku nyuma mishale ya jeshi la Pazi iliwaelemea vibaya. Sehemu nyingine ya mto ilikuwa na mawe mengi makubwa, basi wengine walikuwa wakitumbukiza mawe mtoni ili kupunguza urefu wa kilindi cha maji, lakini hayakufaa kitu. Vita vilizidi kuwa vikali, Wakamba wengi mno walitumbukia mtoni wakafa maji. Ile dawa iliyotiwa motoni usiku iliwafanya Wakamba asubuhi waone giza katika mapigano ya mwisho, na nguvu zao zikalegea.

Basi katika pambano lile pale mtoni, Wakamba wengine walijitahidi kupanda juu ya mawe wakavuka wakawa ng'ambo ya pili ya mto upande wa magharibi, na wengine walitawanyika upande wa mashariki. Wale waliotawanyika waliufuata mto Ruvu wakaelekea upande wa Bagamoyo. Pazi na jeshi lake waliwafuata maadui hawa na kuwashambulia. Lakini baadaye waliona ni bora kuvuka mto tena ili wawafuate wale waliokimbilia upande wa magharibi ya mto maana ndio waliokuwa wengi.

Walipokuwa wakitafuta njia ya kuvukia mto, mara Baraka akazaa hila ya kuvuka mto, akatafuta kamba akaifunga hodari katika shina la mti upande huu, kisha akatwaa ile ncha nyingine akaogelea nayo mpaka upande wa pili, na kule akafunga pia katika shina la mti. Sasa ikawa njia ya kuvuka mto kwa kamba imepatikana. Wakaanza kuvuka askari kadha wa kadha, kisha akavuka Mwene, lakini alipotaka kuvuka Pazi mwenyewe ili askari waliobaki nao wavuke, Mwene akaikata ile kamba ya kuvukia. Pazi na jeshi la askari waliobaki wakashindwa kuvuka wakabaki ng'ambo hii. Tendo hili lilimchukiza sana Pazi Kilama, na pale pale akatoa maneno ya uchungu sana juu ya mpwawe akasema, ‘Mwene, unaniacha mimi nipite upande huu wa pwani bila ya sababu yoyote, kweli umefanya jambo baya sana, lakini basi haidhuru, ila nakuagiza neno moja, huko uendako mchukue mama yako Matatahala umtie ndani ya mtungi kisha umfunike kwa chungu.' Pazi alipokwisha kusema vile akaongoza upande wa pwani pamoja na jeshi lililobaki.

Kule ng'ambo Mwene alishangazwa sana na maneno ya mjomba wake, lilikuwa fumbo lililomtatiza hata hakujua maana ya kumtia mama yake katika mtungi. Na kwa siku zile Matatahala alikuwa hawezi. Mwene aliposhindwa kutambua maana ya maneno ya mjomba wake akaingiwa na wasiwasi sana juu ya ugonjwa wa mama yake. Basi katika kundi akawaambia ndugu zake Wadowe wamchukue mama yake aliye mgonjwa wamwue. Nao Wadowe wakamchukua Matatahala wakamwua wakamla. Mwene alifikiri kwamba huo ndio ufumbuzi wa maneno ya mjomba wake Pazi. Lakini maneno yale ya Pazi hakuna aliyeweza kuyatambua. Na tangu siku zile ndipo walipojulikana kuwa Wadowe ni wala watu.

Basi Mwene aliongoza jeshi lililomfuata, akaendelea kuwafuatia Wakamba upande wa magharibi ya mto, na huko alipambana nao akafanya vita vikali sana. Jeshi lile aliloliongoza Mwene lilikuwa na nguvu, maana yule mtumishi Baraka alikuwa upande ule pamoja na ile dawa ya kushinda katika mapigano. Wakamba wakapigwa na kuuawa, na waliosalimika wakakimbia moja kwa moja.

Lakini kule alikopitia Pazi mapigano hayakuwa na nguvu, askari wa Pazi walilegea kabisa, wala hapakuwa na dalili ya kuwashinda tena Wakamba, na Pazi mwenyewe alikuwa na mashaka kwa kuona mapigano yake hayaendelei vizuri. Mapigano yalipozidi kumwendea vibaya, Pazi akapoza hasira yake juu ya mpwawe Mwene, akaona ni vema amwite mpwawe ili aje kumsaidia mapigano. Akamtuma Mtandila (wengine husema aliyetumwa kumwita Mwene ni Kirumbi), ili akamwite Mwene arejee upande wa mashariki pamoja na jeshi lake. Mtandila alikwenda mpaka kwa Mwene akamweleza unyonge wa askari wa Pazi na jinsi vita vinavyowaendea kombo, na ya kuwa mjomba wake anamwita ili kupata msaada wake.

Mwene hakukawia kuitikia wito wa mjomba wake, na kwa vile upande wake ulikuwa shwari, akakusanya jeshi lake akaondoka kumfuata mjomba wake. Akavuka kijito kilichoitwa Bahamani baada ya kuuvuka mto Ruvu katika nchi ya Bagamoyo, akasafiri mpaka Masaki, pale akakutana na mjomba wake. Siku zile Wakamba wengi walikuwa wakielemea mahali panapoitwa sasa Mkamba, na sababu au asili ya jina hili Mkamba maana yake ni mahali alipokimbilia Mkamba wakati wa vita, basi kwa ajili ya mahali pale kuwa kambi ya Wakamba pakaitwa Mkamba mpaka leo.

Pazi alipoonana na mpwawe Mwene hasira yake yote ikatoweka, akamsimulia shida zote zilizomkabili katika mapigano na Wakamba. Mwene naye akamwambia mjomba wake hila za Wadowe na jinsi ya kuwashinda Wakamba waliobaki, akasema, 'Wakati wa mapigano makali ukiwaona Wakamba wanakimbia na hali maiti za wenzao wameziacha nyuma, basi waambie watu wawachukue wafu hao na kuwakata vipande vipande, kisha nyɛma zao zipikwe katika vyungu. Sehemu nyingine za mifupa zitupwe ovyo ili ye yote apitaye aweze kuona, na vile vyungu vya nyama viachwe motoni vikichemka kwenye kambi yenu. Nanyi mwondoke kambi hiyo na kutafuta kambi nyingine. Wakamba watakapofika hapo kambini na kuona nyama za watu zinapikwa na mifupa imetawanywa huko na huko, basi wataingiwa na hofu na kukimbia, wataogopa kuliwa nyama zao.'

Pazi alipokwisha ambiwa hila ile asubuhi na mapema akaandalia vita, na kwa msaada wa askari aliokuja nao Mwene pamoja na ule uganga wa mapigano, vita viliandaliwa bila ya mashaka. Baada ya kujiweka tayari, vita vilianza tena, yakawa mapigano makali mno. Kambi ya Wakamba, kule Mkamba, ilishambuliwa vibaya. Wakamba walitatizwa kila upande, na hasa walipogundua kuwa nyama za maiti za ndugu zao zinapikwa na kuliwa. Wakaingiwa na hofu kubwa sana. Wakawaza kuwa adui zao hawapigani kwa kuwania ushindi tu, ila pia wanapigana kwa kujipatia mahitaji yao ya kula nyama za watu. Wakamba walishindwa kabisa kuendelea na mapigano, wakakimbia kurejea tena Masaki, baadaye wakakimbia tena kuelekea kusini mpaka kuvuka mipaka ya nchi ya Rufiji na Zaramo.

Nchi yote ya Masaki pale zamani iliitwa Kibwegere, na ile sehemu iliyo Masaki hasa iliitwa Nghumbuluni, lakini siku zile za mapigano watu waliojeruhiwa katika jeshi la Pazi na Mwene waliuguzwa pale Nghumbuluni. Neno hili SAKI kwa Kizaramo ni mahali pa kuuguzia wagonjwa, na ikiwa sehemu za kuuguzia ni nyingi basi huitwa MASAKI. Na hii ndio sababu sehemu ile ikaitwa MASAKI mpaka leo.

Wakamba waliobaki katika mapigano wakazunguuka kurejea upande wa kaskazini wakafika katika nchi ya Bagomoyo mahali panapoitwa sasa Kondo, maana ya jina hili hasa ni Mkondo, maana jeshi la Wakamba waliokimbia walipita mahali hapo wakafanya mkondo mkubwa, ndio sababu pakaitwa 'KONDO DA WAKAMBA', na kwa siku hizi panaitwa Kondo tu.

Baada ya kuhakikisha kuwa vita vimekwisha, Pazi na majeshi yake wakarudi vitani kwa furaha, wakaenda hata Mzizima kuonana na yule Mbarawa ili kupata ujira wa kuwapa watu waliopigana, kwa maana yule Mbarawa wakati alipomtuma Mtandila aliahidi kutoa zawadi kubwa ikiwa Wakamba watafukuzwa katika nchi hii. Walipofika Mbweni wakakutana na yule Mbarawa ndipo wakafuatana naye mpaka Mzizima, pale Mzizima wakakusanyika mahali penye mivinje miwili, hapo ndipo walipojadiliana mambo ya mwisho wa vita na ujira wa askari. Wakachukua shuka moja kubwa wakaitundika katikati ya mivinje ili kufanya pazia. Kisha wakatwaa shuka nyingine nayo wakaitundika kufanya pazia. Sasa pazia hizi mbili zilitenga sehemu tatu, sehemu ya kwanza alikaa Pazi, sehemu ya pili alikaa Mwene, na ile sehemu ya tatu waliketi Wamashomvi na yule Mbarawa. Walifanya hivi kusudi wasionane wakati wa kutolewa ujira wa mapigano ya vita. Ndipo yule Mbarawa akaondoka pamoja na watumishi waliomsaidia, akatwaa nguo nyingi akazipanga katika ile mivinje miwili. Lakini mvinje uliokuwa upande wa Pazi ulijaa nguo nyingi zaidi kuliko ule uliokuwa upande wa Mwene, kwa sababu yule Mbarawa aliishiwa katika ghala yake.

Kabla ya mgawanyo Mwene aliondoka upesi pale alipoketi akarukia upande wa Pazi wenye fungu kubwa, akadai kuwa fungu lile kubwa ni lake. Naye Pazi alipoona vile akadai kwamba ule mvinje uliopungua ujazwe nguo mpaka uwe sawa na ule anaodai Mwene, madai yalikuwa hivyo lakini yule Mbarawa hakuweza. Baada ya hapo wakajadiliana juu ya kodi itakayotolewa kila mwaka kumpa Pazi kwa sababu ya kulinda amani katika nchi. Kodi hii iliwahusu wageni waliopenda kuishi humu nchini wamlipe Sultani Pazi, nayo iliitwa Kanda la Pazi au mrabaha. Walipokwisha kukubaliana juu ya Kanda la Pazi, Gulu Jasi akakubali kumwachia mpwawe Mwene lile fungu kubwa alilodai, naye akatwaa lile fungu dogo. Kisha Pazi akagawanya fungu lake katika sehemu mbili, sehemu moja akachukua yeye pamoja na dada zake na wapwa zake wengine (isipokuwa Mwene); na sehemu ya pili akawagawia baadhi ya askari zake, hasa wale walioitwa Wampeta. Jina hili la Wampeta amelitoa Pazi kwa sababu askari wa ukoo huu ndio waliokuwa wakihesabu watu na kuwapanga katika mapigano, na huyo mkubwa wa Wampeta ndiye aliyekuwa askari mkubwa, jina lake aliitwa Lugeng’he Kitindi. Askari na wapagazi katika vita walikuwa chini ya Kitindi. Huyu Lugeng'he Kitindi kwa ajili ya uhodari wake alitukuzwa kwa maneno haya 'Kitindi mwagila mhwani zuwa jagila maswelo' maana yake, 'Kitindi apoteleaye pwani na jua lachwa machweo'. Na lile jina la Wampeta maana yake 'Wanaohesabu au Wahesabuji'.

Mambo yote ya kugawanya nguo na majadiliano ya kanda la Pazi yalipokwisha, Pazi Kilama akaazimu kurudi kwao Kinyangulu, lakini watu wengi aliokuja nao walibaki nchini humu wakasehelea na kufanya maskani. Mwene na watu wake wakarudi kwao Udowe, lakini pia Wadowe wengine walibaki Uzaramo wakasehelea na kufanya maskani.

Katika siku zile za vita kule Masaki Pazi Kilama alimposa bibi mmoja katika ukoo wa Wavinyogoli, naye aliishi naye mpaka siku zile za kujiwa na mpwawe Mwene ndipo akamwacha bibi yule na kuendelea na mapigano ya vita. Mwanamke yule baadaye alionekana na himila, na siku zake za kujifungua zilipowadia akazaa mtoto mwanamume. Pazi hakuwa na habari yo yote juu ya mimba wala kuzaliwa kwa mtoto, mradi alipokwisha kumaliza matengenezo yote ya kanda lake akawa anarudi kuelekea Kinyangulu. Wavinyogoli walipopata habari wakafanya wasiwasi, wakamchukua mama na mtoto wake wakamfuata Pazi ili wamkabidhi. Kwa bahati wakamkuta njiani, basi wakampa mtoto wake, wakamkabidhi na bibi yake. Pazi akamshika mtoto wake, akautikisa mguu wa mtoto, kisha akautikisa na mkono, halafu akasema 'Mtoto huyu ni wangu, jina lake Pazi Mnyalangulu.'

Jina lile la Mnyalangulu alilitoa Pazi kwa sababu mama wa mtoto alipata taabu ya kukauka miguu kwa sababu ya kumfuata yeye. Hivyo Mnyalangulu maana yake 'Mkauka miguu', na hilo ndilo jina lililovuma kwa mwana wa Pazi aliyezaliwa kwa Wavinyogoli.

Baada ya hayo Pazi aliendelea na msafara wake hadi Kinyangulu.

Tukirejea habari za Pazi na Wamashomvi twafahamishwa kwamba Wamashomvi ni Wazaramo halisi wa mwambao, lakini Wabarawa ni wageni waliokuja nchi hii kufanya biashara. Siku ile ya kugawiwa nguo chini ya mvinje tumeona kuwa Wamashomvi waliketi pamoja na Mbarawa, hivyo ilikuwa kwamba Wabarawa walio wageni wakae pamoja na wenyeji wao Wamashomvi.

Baada ya vita vya Pazi na Wakamba kumalizika, nchi ilionekana kwamba imetulia, ndipo Pazi akapata nafasi ya kuwagawia wapwa zake sehemu za nchi. Pazi aliwatukuza sana wapwa zake kuliko wanawe, na kwa sababu hii ndio maana baadaye Wazaramo katika mila waliwarithisha mali wapwa zao. Kila mwana aliachwa akarithi kwa mjomba wake. Mabadiliko ya urithi, yaani, mwana kumrithi baba yake yaliletwa baadaye na wageni kwa ajili ya sheria za dini.

Basi Pazi akampa Mwene nchi yote ya Udowe aitawale. Kule Kisaki na Mvuha akamgawia mpwawe wa pili aliyeitwa Hega. Uluguru na Ukutu akapewa Kingalu. Sehemu ya Uzaramo tangu mto Ruvu mpaka Mzizima akapewa Temodimogoke. Zamani zile Temodimogoke alikuwa akipita nchi hii toka Kinyangulu akienda pwani kuchukua kanda la Pazi, watu wengi wa siku zile waliifahamu njia maalumu aliyopita Temo, (maana ndivyo walivyomwita kwa mkato, Temo).

Miaka miwili baada ya vita vya Wakamba, watu walikaa kwa amani, lakini mwaka wa tatu mapigano yalitokea tena. Sultani mmoja aliyetokea upande wa magharibi ya Kinyangulu aliongoza jeshi la askari kadha ili kuja kupigana na Pazi Kilama, Sultani huyu alikuwa Hambalule. Huyu Hambalule alisikia sifa za ushujaa wa Pazi Kilama na jinsi nchi yake ilivyostawi, basi akafanya mpango wa kukusanya majeshi ili amwendee Pazi na kumpokonya utawala wake. Lakini Pazi aliposikia maingilio ya maadui zake akamfuata Hambalule ili amlaki njiani, basi naam, walikutana na mapigano yakaanza. Lakini vita hivi havikuendelea siku nyingi maana Pazi alifanya mwujiza mpya ambao ndio uliomaliza vita kwa haraka. Yasimuliwa kwamba katika vita hivi Pazi hakupigana kwa mishale wala mikuki, ila aliwaambia askari wakusanye kokoto kwa wingi, kisha akatwaa ngozi ya tembo, akatengeneza kumbewe kubwa aliyoiita 'Yamila'. Kumbewe hiyo aliijaza kokoto kwa wingi, wakati alipoizunguusha na kuzitupa kokoto zilitawanyika kwa nguvu zikavuma kama risasi, maadui zilipowapata zikawavunja macho na kuwatoboa vichwa zikawaua. Wachukuzi wote walilazimika kubeba mizigo ya kokoto, na Pazi mwenyewe pamoja na askari fulani fulani walishika kumbewe mikononi. Kila walipowakaribia maadui walijaza kokoto katika kumbewe na kuzitawanya hewani kwa nguvu zikavuma na kuwashambulia.

Hambalule na watu wake walilemewa vibaya sana, wakaanza kurudi nyuma, na hapo ndipo Pazi akapata nafasi ya kuwafukuza. Hambalule alifukuzwa na Pazi mpaka mto Ruaha, akatokomea moja kwa moja wala hakurudi tena. Ikawa ndio mwisho wa vita vya Pazi na Hambalule.

Itaendelea. . .
 
Mnaona mambo hayoo kumbe wazaramu nao walikua na mashujaa wao ,ningeyajua wapi haya alafu mkuu usisahau kuhadithia na vingoma ngoma stori za wazaramo bila ngoma hainogi ,
 
Nao Wadowe wakamchukua Matatahala wakamwua wakamla. Mwene alifikiri kwamba huo ndio ufumbuzi wa maneno ya mjomba wake Pazi. Lakini maneno yale ya Pazi hakuna aliyeweza kuyatambua. Na tangu siku zile ndipo walipojulikana kuwa Wadowe ni wala watu.
🫢🫢😶🫣
 
Mnaona mambo hayoo kumbe wazaramu nao walikua na mashujaa wao ,ningeyajua wapi haya alafu mkuu usisahau kuhadithia na vingoma ngoma stori za wazaramo bila ngoma hainogi ,
Pazi Kilama ni kama Mwanamalundi wa Kizaramo.
 
SURA YA 2

HABARI ZA WATAWALA WENGINE
BAADA ya mapambano ya vita na Sultani Hambalule, Pazi Kilama akahama Kinyangulu na kukaa Madege nchi iliyo kandokando ya mto Ruvu. Pazi hakuishi miaka mingi kule Madege, mara akapatwa na maradhi akaifariki dunia. Maiti yake ilizikwa pale pale Madege, na kila mwaka ndugu zake walifika mahali hapo na kulizuru kaburi lake. Lakini yule mzee Pazi Mvilama, baba wa Gulu Jasi, hakuhama Kinyangulu ila alipokufa alizikwa kule kule Kinyangulu juu ya Kilima. Watu wa baadaye walioliona kaburi la baba wa Gulu Jasi walithibitisha kwamba mzee huyo alikuwa mrefu sana.

Kifo cha Pazi Kilama kiliwafadhaisha watu wengi waliompenda kwa sababu ya ushujaa wake. Baada ya hivyo yule mpwawe Temo hakuwa na uwezo wo wote wa kudai kanda la Pazi katika Uzaramo, na kwa vile hakuwa shujaa kama mjomba wake basi watu walimdharau, na daraja yake katika nchi hii ikafa.

Baadaye Pazi Mazongela akapata nguvu ya kusimamisha utawala. Huyu Pazi Mazongela alikuwa mtu wa Mulegele katika nchi ya Masaki, naye alizaliwa na Wamkali kiumeni kwake, mama yake alizaliwa na Nyapazi dada wa Pazi Kilama, kwa hiyo Pazi Mazongela alikuwa mjukuu wa Nyapazi. Kwa sababu hiyo yeye aliupata Upazi kutoka kukeni kwake. Mazongela alikuwa na kaka yake aliyeitwa Pazi Kivulenze, lakini Kivulenze hakuwa shujaa kwa hiyo hakuweza kudai utawala. Mazongela aliondokea kuwa shujaa kweli, hata aliweza kukusanya jeshi na kufanya mapigano na Waarabu waliokuja nchi hii, ingawa baadaye alifanya urafiki nao. Alipokuwa kijana kabla hajatawala alipatwa na ugonjwa wa majipu 20 ambayo yalimvimba mwili mzima. Baba yake alikwenda kutazamia kwa mganga wa ramli, mganga akasema, 'Ugonjwa huu hautapona ila mpaka kwanza mgonjwa apelekwe kwa babu yake Pazi Gulu Jasi ili akatambikiwe kwenye mzimu ndipo tiba zitafanikiwa na mgonjwa atapona.' Siku zile Pazi Kilama alikuwa hawezi kule Madege. Basi Mazongela akapelekwa Madege kuonana na babu yake. Ingawa Pazi Kilama alikuwa mgonjwa, akajitahidi kama alivyoweza akamtambikia mjukuu wake, kisha akampatia waganga wakamponya maradhi yake. Mazongela alipokuwa akimwaga babu yake ili arudi kwao Mulegele baada ya kupona majipu, babu yake akamkabidhi vazi la utawala akamwambia, ‘Nenda salama, siku zijazo utakuwa mtawala shujaa kama mimi.'

Mazongela alipofika kwao Mulegele akatawalishwa jina la Upazi hasa na kupewa heshima ya usultani. Baadaye alipokuwa na makamo ya kutawala akawa anapokea kanda la Pazi mahali pa babu yake, wakati ule Waarabu walioingia nchi hii walikataa kumheshimu Mazongela na kumpa kanda la Pazi, ndipo Mazongela akakata shauri la kupigana nao. Lakini kwa kuwa Waarabu walikuwa werevu kwa sababu ya biashara ya utumwa wakapatana naye Mazongela na kufanya urafiki. Kwa hiyo vita yao haikuendelea. Waarabu walikubali kulipa kanda la Pazi kwa muda, baadaye uwezo wao ulipozidi sheria ya kanda la Pazi ikafutika.

Mazongela alipozidiwa uwezo, utawala katika Uzaramo ukazidi kufifia, na nguvu ya utawala wa Waarabu ikazidi kustawi. Lakini kule Zaramo ya Ruvu mtu mmoja aliyeitwa Dipangalala alidai kuurithi utawala wa Pazi. Huyu kwa asili alikuwa binamu yake Pazi Kilama, lakini kwa kweli hakuwa shujaa kama Pazi mwenyewe. Dipangalala aliishi Kipepelo kando ya mto wa Ruvu, mahali alipoishi palikuwa na mibuyu mingi. Mbuyu mmoja uliokuwa mkubwa ndio ulioitwa hasa Kipepelo, na mahali hapo kwa ajili hiyo pakaitwa Kipepelo kwa Dipangalala. Lakini baadaye hatujui kwa sababu gani mahali hapo pakaitwa Mkangazi.

Kukeni kwake Dipangalala alizaliwa na Mulakiluwa binti Vundege katika ukoo wa Walugoma. Alikuwa na ndugu zake wanne wa kiume, nao ni Ngubi, Msumi, Minyoli Mkungwipala na Pazi Mbwezeleni. Dipangalala hakupata furaha ya kuendelea kuishi pamoja na ndugu zake, maana wakati fulani ndugu zake wote walifariki dunia mfululizo hata hatimaye akabaki yeye na mama yake tu. Na kwa vile Dipangalala hakuwa shujaa nchi yake ilikuwa katika hofu ya kushambuliwa na maadui. Na wala haikupita miaka mingi katika hofu hiyo Wamafite waliingia katika nchi yake. Mulakiluwa alifahamu kuwa mwanawe hawezi kupigana na Wamafite, akamwonya mwanawe kuwa asithubutu kufanya vita nao, akamshauri awabembeleze Wamafite kwa kuwapa zawadi ili nchi yake isalimike.

Mmafite wa kwanza aliyeingia nchi ile aliitwa Mmahuhu; huyu pamoja na kundi lake walipofika kwa Dipangalala hapakutokea vita, maana Dipangalala mwenyewe alimkaribisha Mmahuhu na kumpa zawadi ya mtumwa aliyeitwa Magesa, kisha akampa doti thenashara za nguo na kanda la chumvi. Mmahuhu na watu wake walifurahi sana kwa zawadi zile wakapita salama katika nchi ya Dipangalala bila ya kufanya vita. Lakini walipofika nchi ya Mvungwi walifanya matata na kunyang'a'nya mali za watu.

Mara ya pili walikuja Wamafite chini ya kiongozi wao aliyeitwa Mpepo. Wamafite hawa walipofika nchi ya Dipangalala walipata zawadi ya mjakazi aliyeitwa Mulang'honde, wakapata pia doti thenashara za nguo na kanda la chumvi pamoja na majogoo fulani ya kuku. Nao walifurahi hawakufanya matata ya vita.

Mara ya tatu walikuja tena Wamafite walioongozwa na mkubwa wao aliyeitwa Ngahokola. Hawa nao walipata zawadi ya mjakazi aliyeitwa Mulamtonga, wakapata pia kanda la chumvi na doti zipatazo kumi za nguo.

Baadaye walikuja Wahehe katika nchi ya Dipangalala, naye Dipangalala alishindwa kutoa zawadi kuwapa Wahehe maana aliishiwa. Basi naam, Wahehe waliushambulia mji wa Dipangalala wakazichoma moto nyumba zote, wakateka mali zote zilizokuwako, wanaume na wanawake walikimbia wakauacha mji katika hali ya ukiwa. Naye Dipangalala baada ya kusalimika akabaki hohe hahe, na kwa taabu na shida zake akamtwaa binamu yake wa kike aliyeitwa Mulamng'hango akamweka rehani katika utumwa kwa mzee mmoja jina lake Moto. Mulamng’hango aliishi kwenye utumwa kwa miaka mingi, hata Wadachi walipoingia nchi hii walimkuta utumwani, nao ndio waliomtoa katika utumwa.

Katika Zaramo ya Mwambao alikuwako Kawambwa Mshale ambaye kwa ushujaa wake aliweza kusimamisha utawala katika Mwambao, naye ndiye aliyefanya mapigano ya nguvu na Wamafite. Hapo mwanzo Kawambwa Mshale alifanya urafiki na Waarabu, akapata kwao bunduki na baruti kwa wingi. Bunduki zilizotumiwa siku zile zilikuwa namna ya gobori zilizoitwa 'butu' na 'sindikali' zilizoletwa na Waarabu. Siku zile, jeshi moja la Wamafite lilikuwa Kisaki. Basi Kawambwa Mshale alipopata habari zao, akakusanya jeshi lake akasafiri hadi Kisaki. Kule akawakuta Wamafite waliokuwa tayari kwa vita. Hapa Kisaki mapigano makali yalifanyika, na Wamafite walizidiwa nguvu; wengi waliuawa na waliobaki wakakimbia. Kawambwa Mshale aliwafuata Wamafite hadi nchi ya Mahenge, na huko jeshi la Wamafite likaongezeka. Matokeo ya vita yalikuwa mabaya sana upande wa Kawambwa Mshale, maana jeshi lake likashambuliwa kwa nguvu; Wazaramo wengi waliuawa. Mwishoni Kawambwa Mshale alitoroka na watu wake waliobaki, akafanya safari kurudi kwao Uzaramo.
Itaendelea. . . .
 
VITA VYA HEMBE NA VUMBI

Hembe alikuwa mwana wa Pazi Mazongela, naye aliondokea kuwa shujaa wa vita, lakini aliuawa vitani wakati angali kijana, kwa hiyo hakuwahi kurithi utawala wa baba yake. Hembe alikuwa na rafiki yake aliyeitwa Vumbi, mtu wa Maruwi aliyekuwa akiishi karibu ya kijito cha Mfunyezi. Siku moja, Vumbi alikwenda Mulegele kumtembelea rafiki yake, kule akapokewa na kukaribishwa vizuri, akakaa siku nyingi akiongea na kufurahi pamoja na rafiki yake Hembe. Hata siku zilipozidi, Vumbi akatamani kurudi kwake Maruwi, akamwaga rafiki yake na kumwambia kuwa anataka kurudi nyumbani. Hembe akampa zawadi ya kikanda cha mtama na kumwambia kuwa awapelekee watoto nyumbani. Na kwa vile Vumbi hakuwa na mtoto wala mtumishi aliyekuja naye, basi Hembe akamtoa mtumwa wake mmoja ili amchukulie mzigo rafikiye. Ndipo Vumbi akafanya safari ya kurudi nyumbani kwake akifuatana na mtumwa wake Hembe, wakafika nyumbani salama.

Walipolala na kuamka asubuhi Vumbi akamwambia yule mtumwa, 'Twende porini tukawinde ili upate nyama ya kumpelekea rafiki yangu.' Yule mtumwa akakubali, lakini alitaka na yeye pia apate bunduki ya kuwindia. Basi Vumbi akatoa bunduki mbili, moja akaishika yeye mwenyewe na nyingine akampa yule mtumwa akampa pia baruti na risasi tayari kwa uwindaji. Wakaondoka wote wawili pamoja na wafuasi wachache wakaenda porini kuwinda.

Walipofika mwituni yule mtumwa alimwona pofu, na kwa shabaha yake akamwua pofu kwa mshindo mmoja tu. Na mara ile Vumbi naye akamwona pofu mwingine akikimbia, akamfuata na kumpiga, lakini kwa bahati mbaya alimvunja mguu, na pofu akawa anaendelea kukimbia kwa miguu iliyosalia. Hapo yule mtumwa akapiga mbio kumfuata akawahi kumpiga risasi ya shingo akamwua. Hivyo mawindo yao yalifanikiwa kwa kupata pofu wawili. Basi wakawachuna pofu wale wakazikausha nyama kwa moto, na zile ngozi wakazianika juani kwa kuziwamba kwa vijiti. Ngozi zilipokauka, wakafunga mizigo yao ya nyama pamoja na zile ngozi wakajitwika na kurejea nyumbani kwa Vumbi. Kazi hizo zilipokwisha zimekwisha pita siku sita tangu siku waliyofika kutoka Mulegele, na ambapo yule mtumwa wa Hembe alipewa siku nne tu za kusafiri na kurudi Mulegele. Kwa ajili hiyo mtumwa yule aliomba aruhusiwe kurudi nyumbani kwa bwana wake. Vumbi akamruhusu yule mtumwa, akampa zawadi ya mzigo wa nyama ili aipeleke kwa Hembe. Lakini zile ngozi zikawa mali ya Vumbi ingawa mafanikio ya uwindaji yalitokana na kazi iliyotendwa na yule mtumwa. Basi mtumwa yule akajitwika mzigo aliopewa akaaga na kurudi kwa bwana wake Mulegele.

Alipofika Mulegele akamsimulia bwana wake mambo yote ya safari yake, na hasa yale yaliyotendeka kule porini katika uwindaji. Hembe aliposikia habari zile akaingiwa na chuki moyoni mwake, akawaza kuwa kwa nini hakupewa ngozi ya pofu aliyeuawa kwa mkono wa mtumwa wake. Kwa ajili ya chuki hiyo, Hembe hakuweza kuvumilia, akafanya safari kwenda Maruwi kuonana na rafiki yake Vumbi. Alipofika kule akasimuliwa habari zote zilizotokea katika uwindaji. Lakini Hembe kabisa hakuridhika, akataka apewe ngozi ya pofu aliyeuawa kwa mkono wa mtumwa wake. Vumbi naye akakataa kutoa ngozi, akasema, 'Siwezi kukupa ngozi, nimekuletea mzigo wa nyama ndilo fungu la zawadi yako, lakini ngozi zote ni mali yangu, maana bunduki na vifaa vya uwindaji vyote ni vyangu, na ile safari ya porini nimeiazimu mimi wala si wewe. Na kama mtumwa wako alikwenda kuwinda, basi alikwenda kwa sababu yangu na akatumia bunduki yangu.' Madai na mabishano yao yaliendelea kwa kitambo, lakini hata hivyo Hembe hakufaulu kuipata ngozi. Baadaye Hembe akaingiwa na hasira sana, akasema, ‘Ukisikia Hembe Mwana wa Mazongela ndiye mimi, nakujulisha kuwa ngozi hizo hutozitumia kwa mwaka wote mzima, nitakuletea vita hivi karibuni nione uhodari wako.'

Lakini Vumbi hakutishika na vitisho vya Hembe, mradi naye akasema, 'Nawe kama humjui Vumbi basi mwaka huu utamtambua; ukileta vita, mimi ni tayari kabisa.'

Basi baada ya mabishano yenye hasira kali kali, Hembe akarudi kwao Mulegele; kule akakusanya watu na kuwaweka tayari kwa vita. Kisha, akampanga yule mtumwa wake awe kiongozi wa kupeleka jeshi la askari mpaka Maruwi kwa Vumbi. Lakini yule mtumwa hakupendelea wazo lile la bwana wake, mradi katika siku zile za matayarisho ya vita akatoroka akaenda hadi Maruwi kwa Vumbi. Alipofika kule akaonyesha upenzi mkubwa mbele ya Vumbi, akamjulisha mambo yote yanayotayarishwa Mulegele kwa ajili ya vita, akasema, ‘Rafiki yako anatayarisha mapigano kwa sababu ya kunyimwa ile ngozi, eti amenitaka mimi niwe kiongozi wa vita hiyo, lakini mimi sikupendelea shauri lake ndio sababu nimetoroka kuja kwako ili nijiunge nawe. Na kama utanikubali nitakujulisha mambo yote ya uganga wake anaotumai anapokwenda vitani kuwashinda maadui.'

Shauri la mtumwa lilimfurahisha sana Vumbi, na mara ile akawa tayari kusikia yote kutoka kwa yule mtumwa. Naye mtumwa alipokubaliwa kuwa shirika na Vumbi katika vita akaanza kueleza siri za uganga wa Bwana wake Hembe, akasema, 'Mambo ya Hembe ni makubwa katika hila za kushinda vita, lakini tukitaka kumshinda upesi tumtoe makomwe yake ya nduga yaliyo mwilini, maana kwa kufanya hivyo tutamwua mara moja.' (Makomwe ya nduga ni uganga wa kukinga mwili usidhurike kwa siliha yoyote). Basi yule mtumwa aliendelea kusema, 'Jambo jepesi la kumshinda ni silaha ya maboga, mara utakapomwona Hembe anakuja na majeshi yake waamuru watu wako watwae maboga wayapasue kisha wamwonyeshe seheme za ndani za maboga yaliyopasuliwa. Hembe atakapoyaona maboga hayo ataogopa sana maana maboga yaliyopasuliwa ndio mwiko mkubwa kwa makomwe yake ya nduga. Baada ya hivyo silaha yoyote atakayopigwa nayo itamdhuru na kumwua mara moja.'

Vumbi aliyasikiliza kwa makini maneno ya mtumwa, baada ya hapo akatayarisha jeshi la vita, akaweka tayari zana zile za kumshinda Hembe. Hazikupita siku nyingi, mara Hembe aliingia nchi ya Maruwi pamoja na jeshi lake; Lakini kabla hajafika Maruwi humo njiani alifanya miujiza akawaonyesha watu wake; alishika tawi la mgude mrefu akaliinamisha chini, kisha akashika ncha zake akazifunga fundo, lakini fundo lile mara likalegea; na alipoliachilia lile tawi likarudi kama vile lilivyokuwa mwanzo. Ishara ile ikaanza kumtia wasiwasi, maana ilibashiri kutoshinda vitani, lakini hata hivyo Hembe alijipa moyo akaongoza jeshi lake mpaka Maruwi. Maruwi ni nchi yenye vilima na mabonde. Alipokuwa akitelemka na jeshi lake alionekana waziwazi na Vumbi, na kwa kuwa maarifa yake yote yamekwisha tolewa nje na yule mtumwa, basi watu wa Vumbi hawakukawia kumlaki Hembe. Walipomwona tu wakatwaa maboga yaliyopasuliwa wakamwendea na huku wakiimba wimbo wa ushindi:

Bundi lelo! Bundi lelo!

Hooyee! Hooyee!

Bundi mwee, donung'ha lukugu!​

Hembe alipoyaona maboga na kusikia ule wimbo akataharuki sana, akaanza kukata tamaa, akastaajabu kuona kuwa maarifa yake ya makomwe yamegunduliwa. Mikono na miguu yake ikaanza kutetemeka, akaingiwa na fadhaa kubwa ya hofu. Mara ile mtu mmoja katika kundi la Vumbi akatupa mshale mmoja akamchoma Hembe mguuni, akaanguka pale pale akafa, na askari wake walipojaribu kujitetea katika mapigano wakashambuliwa vibaya; wengi wao wakauawa, na wengine wakajeruhiwa, waliosalimika wakakimbia na kurudi kwao Mulegele.

Huo ulikuwa mwisho wa majisifu na uhai wa Hembe, ameuawa angali kijana akaacha msiba mkubwa kwa baba yake Mazongela aliyekuwa hai siku hizo. Hayo yote yalitokea kwa sababu ya uhaini wa mtumwa wake. Waungwana wa mwambao siku zile za utumwa walitunga nyimbo nyingi za chuki wakieleza tabia za watumwa, ingawa wao wenyewe walipendelea sana kufuga watumwa na kuwauza watu kama kuku. Huu ni wimbo mmojawapo katika nyimbo zilizoimbwa kwa ushairi juu ya mtumwa : . . . .

Basi wimbo huu uliowaonya waungwana kujihadhari juu ya watumwa unafanana sana na maelezo ya kifo cha Hembe kilichotokea kwa sababu ya uhasidi wa mtumwa wake.

Kwa habari za kujikinga katika vita, wazee wasimulia kwamba zamani kulikuwa na dawa za kuzuia mwili usidhurike kwa mkuki, mshale, risasi na kadhalika, na nyingine zilikuwa za kuzuia mwili usidhurike kwa moto. Dawa hizo ziliitwa 'Makomwe'. Zile za kukinga risasi au mkuki usipenye mwilini ziliitwa 'Makomwe ya Nduga' na zile za kujikinga kwa moto ziliitwa 'Makomwe ya Moto'. Lakini ilisadikiwa kwamba kila dawa ya makomwe ilikuwa na mwiko wake. Wengine walikuwa na miiko ya kula pombo na kunywa maji ya mto, na wengine walizuiwa kula maboga au namna fulani ya ndege na kadhalika. Mtu mwenye makomwe akitumia kitu alichoambiwa na waganga kwamba ni mwiko, basi makomwe yote humtoka mwilini akawa kama mtu wa kawaida.
Itaendelea. . .
 
MGAWANYIKO WA MAPAZI

Kwa ajili ya Pazi Kilama, jina hili la Pazi lilikuwa tukufu sana katika Uzaramo, hata mara nyingine jina lenyewe lilikuwa linaleta maana ya 'Mheshimiwa' kama vile lilivyokuwa jina la Mwene katika Udowe, maana yule Mwene aliyemsaidia Pazi katika vita vya Wakamba alikuwa Mwene Kajeing'anga, lakini baada ya kufariki Kajeing'anga walitokea Mamwene wengi, kwa mfano, Mwene Mhila, Mwene Milao nk.

Katika Uzaramo watu waliohusika na mzao wa Pazi Kilama waliitwa 'Mapazi'. Kuna Mapazi wengi katika nchi hii, lakini hawa wote wanafahamika katika makundi mawili, kundi la kwanza ni wale walioupata Upazi kutokana na nasaba ya Pazi Gulu Jasi mwenyewe, hawa kwa jumla ni wajukuu na virembwe wa Pazi Kilama, kwa mfano: Mzao wa Pazi Mazongela wa Mulegele; vizazi vya Pazi Kibasila wa Kisangire; vizazi vya Pazi Dipangalala wa Ruvu na wengine katika nasaba ya Pazi Kilama. Kundi pili ni wale waliopata majina ya Pazi kwa namna ya kupewa. Katika hao wengine walipewa jina hilo na Pazi mwenyewe, na wengine walipewa jina hilo kwa sababu ya ushujaa wao au heshima zao katika ukoo, na pia wengine walijipa jina hilo wao wenyewe. Mpaka sasa mila zote za Uzaramo zinaitwa Upazi.

Kwa wale waliopata jina la Pazi kwa kupewa na Pazi Kilama ilikuwa hivi; Pazi Kilama alipokuwa anakwenda vitani akimkuta mwanamke katika kijiji anajishuku na mara akizaa mtoto mwanamume, basi hapo Pazi Gulu Jasi alitoa jina la mtoto akamwita, 'Huyu ni Pazi fulani'! Kwa njia hii, watu wengi walipata jina la Pazi hata wakawarithisha watoto na wajukuu.

Katika Zaramo ya Bagamoyo, tumesikia habari za Pazi Mazongela wa Yombo lakini huyo wa Yombo ni tofauti na yule Pazi Mazongela wa Mulegele, maana Mazongela wa Yombo alipata upazi wa kupewa kwa sababu ya heshima tu. Kutoka Yombo, tukiendelea hadi Mbwawa, twafika kwa Pazi Madenge. Tukifika kijiji cha Kitemvu, twamkuta Pazi Uziwila. Tukitembea tena katika nchi mpaka kufika Nyani, twakuta vizazi vya Pazi Ugong'ho. Katika sehemu ya Dunda alikuwako Pazi Changuku. Mapazi wengine waliokuwa maarafu ni Pazi Haumotile, Pazi Mabuge, Pazi Mbwezeleni, na Pazi Kawambwa.

Basi hao tuliowataja wanatosha kuonyesha mfano wa Mapazi. Lakini siku hizi jina hilo la Pazi halina heshima kama zamani, maana sasa mtu ye yote wa kawaida aweza kujiita Pazi. Mila za Kizaramo zinazoitwa Upazi sasa zinazidi kufifia, tena kuna hatari kwamba baada ya miaka mingi mila hizo zitatoweka kabisa.

Kabla hatujafunga masimulizi yetu juu ya Mapazi ingefaa tueleze habari za mtu mmoja ambaye hakuwa mmoja katika hao Mapazi lakini jina lake linakumbukwa kila siku, huyu alikuwa Lumango katika ukoo wa Walupungwi. Lumango alikuwa na dada yake aliyeitua Nyamtegami, ndugu hawa wawili walizaliwa na Mtegani Mulupungwi. Lumango na dada yake walifanya maskani mahali wakajenga nyumba. Nyamtegami alipanda mwembe ambao mpaka leo hivi upo katika mji we Maneromango, mahali ulipo mwembe huo ndipo hasa penye asili ya jina la Maneromango. Mwembe upo kati ya Walugoma na Wahemezi. Jina lile la Lumango lilikuwa la urithi, yaani Lumango bin Lumango bin Mtegami Mulupungwi.

Zamani zile watu walikuwa na heshima katika kuitana majina, hasa wanawake walipowaita wanaume waliwaita kwa majina ya baba zao wakitanguliza neno ‘Mwana'. Kwa hiyo Lumango alipokuwa kijana aliheshimiwa kwa sababu ya tabia zake aliitwa Mwana, na kwa vile yeye alizaliwa na Lumango akaitwa 'Mwana Lumango’. Basi baadaye watu walizoea kusema kila waendapo pale, ‘Nakwenda kwa Mwana Lumango', na vivi hivi mpaka mahali pale pakaitwa Mwanalumango. Baadaye mabadiliko ya matamshi yakatokea kama ilivyo desturi ya wanadamu pakaitwa Maneromango mpaka leo.

Basi kila tunapotaja Maneromango tukumbuke jina la mtu yule Lumango aliyezaliwa na Lumango Mtegami Mulupungwi. Mzee mmoja alisimulia kwamba mahali pale kabla ya Lumango paliitwa Chanika.
Itaendelea. . . .
 
SURA YA 3

MAINGILIO YA WADOWE



KATIKA sura ya kwanza tumesimulia kwamba baada ya vita vya Pazi na Wakamba kumalizika Mwene na majeshi yake walirudi Udowe, na kwamba Wadowe wengine walibaki Uzaramo wakasehelea. Lakini hatufahamu sawasawa habari za hawa waliosehelea wakati huo, ila tutaeleza habari za Wadowe waliokuja kusehelea Uzaramo siku za nyuma baada ya vita vya Wakamba.

Katika majeshi ya Mwene Kajeing'anga alikuwako mtu mmoja katika ukoo wa Wanyange ambaye kwa ushujaa wake akawa kama jemadari wa vita, huyu aliitwa Maluka, na maana yake jina hilo ni 'Msusi' au Msukaji wa majina. Yeye ndiye aliyekuwa akitunga majina ya vyeo na kuwapa waliohusika, na kwa sababu hiyo ndipo akaitwa 'Maluka wa mazina' yaani 'Msusi wa majina ya vyeo', na kwa kifupi akaitwa 'Maluka'. Mwene na watu wake waliporudi Udowe wakafanya mipango mipya ya kugawanya nchi katika kutawala na kufanya maskani. Mwene mwenyewe akaishi Kiwangwa, na yule jemadari Maluka Mnyange alipendelea kupata maskani pale Kiwangwa au mahali pengine katika Udowe kwa kustahili cheo chake, walakini sehemu aliyopata haikumtosha kufanya maskani. Wakati ule Mwene alimpa heshima Maluka, akamwahidi kwamba atakapokufa atazikwa juu ya kichuguu kama wazikwavyo masultani wa Udowe.

Basi, Maluka Mnyange alipokufa akazikwa kwa heshima ya Kisultani kama alivyoahidiwa. Lakini ndugu zake na wanawe baada ya hapo hawakupata starehe ya kutosha katika Udowe. Baadaye mwanawe mkubwa aliyerithi jina la Maluka akaazimu kuihama nchi ya Udowe na kufanya maskani katika nchi nyingine. Akataka shauri kwa Mwene, naye Mwene akamkubalia, akamwambia, 'Ikiwa unataka kuhama Udowe nakushauri uende katika nchi ya mjomba wetu Pazi Kilama, huko utapata maskani ya kutosha, kwa maana mjomba anayo nchi kubwa.'

Huyo Maluka mrithi wa jina aliondokea kuwa shujaa kama baba yake, katika ujana wake aliweza kupambana na mtu yeyote katika mapigano. Basi Maluka akawakusanya nduguze na jamaa waliopenda kumfuata akasafiri nao kutoka Udowe kuja Uzaramo. Alipofika Zaramo ya Ruvu akataka kufanya maskani, lakini Pazi Mazongela alipopata habari za Wadowe kuingia Uzaramo akadhania kuwa wamekuja kutawala. Basi katika shaka ile akawapelekea mshenga Wazaramo wa Ruvu kuwaambia kuwa wawapige Wadowe na kuwafukuza warudi kwao. Mkuu wa sehemu ile ya Ruvu wakati ule alikuwa Kolongo Mhangala, naye alipopata taarifa ya Mazongela akakusanya jeshi akafanya vita na Wadowe. Vita ilitokea kuwa motomoto, lakini baadaye Kolongo na watu wake wakashindwa kabisa, wakapata hasara kubwa katika vijiji vyao.

Baada ya kwisha vita Maluka alihutubia kwamba yeye hakuja nchi hii kwa mapigano, ila aliruhusiwa na Mwene kuja kufanya maskani na kuishi pamoja na wajomba zake Wazaramo. Kolongo alipopata habari zile akafanya urafiki mkubwa na Maluka. Baada ya vile Maluka na watu wake hawakuweza tena kufanya maskani katika nchi ya Kolongo, ila waliendelea kufuata mto Ruvu wakielekea kusini. Walipovuka nchi ya Dundangulu mtu mmoja aliyeitwa Dilunga akazuia msafara wao kwa jeuri. Hapo vita ikatokea tena kati ya watu wa Dilunga na watu wa Maluka, lakini Dilunga na watu wake wakashambuliwa vikali, nyumba zao zikachomwa moto, wengi wao wakajeruhiwa vibaya. Baadaye Dilunga aliangukia na kupatana na Wadowe. Pazi Mazongela alipopata hakika kwamba Wadowe hawakuja kutawala akapeleka salam za urafiki kwa Maluka.

Baada ya hapo Maluka na jamaa zake wakaendelea kusafiri mpaka Zaramo ya Konde, kule wakafanya maskani katika sehemu inayoitwa Mangungu. Baadaye Mangungu ilikuwa mji mkubwa wa Wadowe, wakafuga ng'ombe kwa wingi na kulima mashamba, mji wao wakaujengea ngome imara inayoitwa 'Mhongono'. Hata wakati mmoja Pazi Mazongela alikwenda Mangungu kuonana na Maluka na kudai kwamba Wadowe walipe mrabaha au kanda la Pazi. Lakini Maluka na watu wake walikataa, wakasema kwamba Pazi ni mjomba wao, kwa ajili hiyo hawawezi kutozwa mrabaha. Wakajadiliana kwa kirefu, hata mwishoni wakakubaliana kwamba Wadowe wasitozwe kanda la Pazi. Basi Mazongela akarudi Mulegele bila ya mapigano.

Baadaye, Wamafite walifika Mangungu, wakaivunja ngome ya Wadowe na kufanya mashambulio ya kikatili, wakawajeruhi watu na wengine wakawaua. Wakateka ng'ombe na mbuzi na baadhi ya nyumba zao wakaziteketeza kwa moto. Ingawa Wadowe walijitahidi kupigana nao lakini hawakuweza kuwashinda. Wamafite hao walipoondoka mji wa Wadowe ukanyongea sana, ikawapasa kujenga tena nyumba zao na kutengeneza upya ngome yao. Baada ya vita ile Maluka akafanya urafiki mkubwa na Kirumbi, ili kusaidiana kama vita ikitokea upande wa Maluka au wa Kirumbi.

Maluka alikuwa na wana watatu, nao ni Fundi, Mzigila na Muhando. Fundi alizaliwa Udowe, akaja Uzaramo wakati angali kijana mdogo akifuatana na baba yake. Mzigila na Muhando walizaliwa Uzaramo. Huyu Mzigila akikuwa kama mwana wa Mizimu, maana kabla hajazaliwa, baba yake alikwenda katika mzimu wa Kolelo kutambika, na huko mzimuni akaambiwa kuwa atapata mtoto mwanamume na jina lake aitwe Mzigila. Lakini baadaye Mzigila alipopata makamu ya uvulana aliondokea kuwa shujaa, mwenye akili nzuri na mwelekevu wa mambo, ndipo baba yake akambadili jina na kumwita Kapita. Jina hili la Kapita ndilo lililotumika sana katika ujana wake. Kapita alipatana sana na ndugu yake Fundi, na kwa ajili ya ushujaa wao wakawa kama majemadari katika mji wa Wadowe.

Baadaye, Maluka pamoja na wanawe wakahama kule Mangungu wakaenda Kuruwi kufanya maskani. Pale wakajenga mji na ngome, wakakusanya watumwa na mifugo yao na kulima mashamba. Wadowe waliobaki Mangungu waliendelea kuishi kule chini ya wakubwa wao akina Mkawa, Mtengwa, Madeni na wengine.

Kule Kuruwi yule mzee Maluka akapatwa na ugonjwa wa macho, na kwa ajili ya uzee au ubovu wa macho, akaishiwa nguvu ya kuona akawa kama kipofu. Fundi na Kapita wakaushika mji wao wa Kuruwi katika hali ya imara, wakafanya urafiki na Wazaramo na kuzoeana nao, wakati ule ndugu yao Muhando alikuwa mvulana. Hata wakati mmoja Mzaramo mmoja wa Msanga aliingia katika mji wa Kuruwi, akamwiba mjakazi wa Maluka na kwenda naye kwao kwa jeuri. Basi Fundi na Kapita walipeleka jeshi lao kule Msanga, wakafanya vita katika mji wa yule mwizi, wakampata mjakazi wao, wakawajeruhi watu na kumwua yule mwizi. Na mwana wa yule mwizi wakamteka na kumtia utumwani kwa Wadowe. Nao Wadowe katika vita ile walipata hasara, mtu wao mmoja aliuawa, na Fundi akajeruhiwa mkono kwa upanga. Kijana yule aliyetekwa aliishi utumwani katika mji wa Kuruwi mpaka Wadachi walipoingia nchi hii wakamtoa katika utumwa.

Basi naam, vita hiyo ya Msanga ilizaa fitina na chuki nyingi kati ya Wazaramo na Wadowe wa Kuruwi. Ndipo Ulembo wa Maneromango, Kawambwa Mshale wa Vikindu na Kibasila wa Kisangire wakapeleka maneno ya chuki juu ya Wadowe, wakamwambia mkuu wa Mission ya Kisarawe aliyeitwa Greiner, wakamwomba apeleke vita kwa Wadowe awapige ili kulipiza kisasi cha jamaa walioshambuliwa kule Msanga. Bwana Greiner akayakubali maombi yao, akakusanya watu wachache akawafanya askari, akawapa bunduki, wengine wakabeba madebe ya mafuta ya taa, akasafiri nao hadi Kuruwi kwa Wadowe. Akafika kule siku ya pili asubuhi wakati watu wote wako makondeni. Lakini yule mzee Maluka, ambaye kwa siku zile alikuwa mbovu wa macho, alibaki nyumbani pamoja na mkewe aliyeitwa Mzungu. (Bibi huyo alikuwa mweupe sana, sijui ndio sababu akaitwa Mzungu). Pamoja nao alikuwako mjakazi wao ambaye mara kwa mara alikuwa akimtumikia mzee huyo wakati watu waendapo kondeni.

Mtumwa mmoja aliyekuwa akilinda ngome ya mji alimwona bwana Greiner pamoja na askari wakiukaribia mji. Akaenda haraka kumjulisha mzee Maluka na mkewe, kiisha tena akatoka haraka akakimbia kuwajulisha walio makondeni. Yule bibi Mzungu alipoitoka ngome na kujaribu kumkimbia Greiner aliuawa, na Fundi akajeruhiwa mkono kwa upanga. Kijana Greiner na kikosi chake wakaendelea kupiga bunduki na kuivunja ngome wakaingia mjini. Maluka na mjakazi wake walisimama mahali wakajibanza wasionekane. Askari waliochukua madebe ya mafuta wakayamwaga juu ya manyasi yaliyoezekwa wakazichoma moto nyumba kadha, kisha wakateka ng'ombe waliokuwamo zizini wakaenda nao. Ng'ombe wengine waliokuwako malishoni ndio waliosalimika.

Imesimuliwa kwamba Maluka pale aliposimama pamoja na mjakazi wake hawakumwona kwa sababu ya uganga, na hata kama wangemwona na kumpiga risasi hangekufa kwa sababu yeye alikuwa na makomwe ya nduga hata akawarithisha wanawe Fundi na Kapita na kama Fundi na Kapita wangekuwapo asubuhi ile, Greiner angeuawa kwa mkuki tu. Basi Greiner na watu wake walipopata mateka yao, wakaondoka na kurudi Kisarawe. Watu waliporudi kutoka makondeni na kuona hasara iliyopita, wakaomboleza kwa vilio na masikitiko, wakaingiwa na hofu kuwafuata maadui zao.

Baada ya hapo mji wa Kuruwi ukajengwa tena. Fundi na Kapita wakazidi kueneza urafiki wa damu kwa jirani zao Wazaramo, wakaungana na Ulembo, Kibasila, Haumotile na Kawambwa Mshale.

Walipoingia Wadachi, Fundi akachaguliwa kuwa jumbe wa kwanza pale Kuruwi. Lakini hakuendelea sana katika kazi hii, akapatwa na maradhi ya ndui akaifariki dunia. Maradhi hayo yalipoingia yaliwateketeza wengi katika mji wa Wadowe, hata Muhando ambaye alikuwa kijana sana alifariki dunia kwa maradhi hayo. Muhando na Fundi walizikwa pale Kuruwi.

Ndugu yao Kapita ndiye aliyesalimika na kifo ingawa naye pia wakati ule aliugua. Baada ya hapo Kapita akashika ujumbe wa Kuruwi, lakini hazikupita siku nyingi mara yule mzee Maluka naye akaifariki dunia. Maiti yake ikapelekwa Mangungu ikazikwa. Ndipo baadaye Kapita akarithishwa jina la baba yake akaitwa Maluka. Lakini kwa sababu ya mabadiliko ya matamshi baadaye jina hili likawa Mwaruka. Na wana wote waliozaliwa na mzee huyo walitumia jina hilo katika matamshi na maandishi pia ‘MWARUKA'.
Itaendelea. . .
 
Kinyangulu ipo wapi? Mkoa/wilaya gani
Kinyangulu kwa Jiografia ya leo ipo Kata ya Selembala, Wilaya ya Morogoro Vijijini, mkoa wa Morogoro, nje kidogo mwa Nyerere National Park ( Jukumu Society, Selous Open Area) Ipo magharibi mwa kijiji cha Kidunda, mashariki mwa kijiji cha Kisaki na kusini mwa kijiji cha Kiburumo.
Kinyangulu ya sasa ni pori la wanyama ingawa kuna stesheni ya TAZARA baada ya Kidunda na kabla ya stesheni ndogo ya Matambwe.
 
Kinyangulu kwa Jiografia ya leo ipo kando kidogo mwa Nyerere National Park kwenye hifadhi ya Selous Game Reserve ( Jukumu Open Area) Ipo magharibi mwa kijiji cha Kidunda, mashariki mwa kijiji cha Kisaki na kusini magharibi mwa kata ya Selembala kijiji cha Kiburumo.
Kinyangulu kuna stesheni ya TAZARA baada ya Kidunda na kabla ya stesheni ndogo ya Matambwe.
Kwa sasa Kinyangulu ni pori la wanyama, hakuna makazi ya binadamu
Umeelezea vizuri sanaa, Morogoro
 
Na kila mtu aliyekwenda mbele yake kumwamkia alijiinamisha na kunyoosha mikono yake mbele na kusema, 'Simbamwenee'! Na Pazi aliitikia, ‘Utwaa!' Kisha mtu huyo humwita kwa jina lake, 'Pazi'! Na Pazi hujibu, ‘Nene Mwana Mkungwi pala, Mwana Mwizila kumogo'. Maamkio hayo ndiyo yaliyotumika katika utawala wa Pazi.
Salaam ya kibantu ilikuwa nzuri.
Tunaweza kuirudisha baada ya kuirekebisha kidogo
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom