Sura ya 17
MECCA
Hija ya Mecca ni takwa la kidini ambalo kila Muislamu, iwapo anaweza, anatakiwa alitimize walau mara moja katika maisha yake.
Quran Takatifu inasema kuwa “Hija ya Kaaba ni jukumu ambao binadamu anadaiwa na Mungu; wale wanaoweza wafanye safari.”
Allah anasema: “Natangaza hija kwa watu; watakuja kwako kwa miguu, juu ya ngamia, watakuja kutoka mabonde yote marefu.”
Kwenye vyuo kadhaa, ilitokea baada ya hotuba na tukiwa tumekusanyika kwa maongezi, nilifuatwa na watu kadhaa weupe weupe hivi. Walijitambulisha kuwa wao ni Waarabu na Waislamu kutoka Mashariki ya Kati au Afrika Kaskazini, na wapo Marekani kwa matembezi, kwa masomo au wanaishi hapa. Walisema kuwa, ukiachana na kauli zangu za kuwashutumu wazungu, walihisi kwamba nilikuwa muaminifu katika kujiita kwangu Muislamu, na walihisi kuwa iwapo nitaujua waliouita “Uislamu wa kweli.” “Nitauelewa na kuukubali.” Nikiwa kama mfuasi wa Elijah Muhammad, nilikasirika kila niliposikia hayo.
Lakini nilipokuwa nikitafakari nikiwa mwenyewe baada ya mambo yote yale kutokea, nilianza kujiuliza: kama mtu alikuwa ni mfuasi mzuri wa hiyo dini, kwa nini ajizuie kupata maarifa zaidi kuhusu dini hiyo?
Siku moja katika maongezi niligusia hili kwa Wallace Muhammad, mtoto wa Elijah Muhammad. Alisema ndiyo, hakuna shaka kuwa Muislamu anatakiwa kujifunza Uislamu kadri ya uwezo wake. Siku zote niliyaheshimu sana maoni ya Wallace Muhammad.
Wale Waislamu halisi niliokutana nao, kila mmoja wao alinihimiza kuonana na kuongea na Dr. Mahmoud Youssef Shawarbi. Niliambiwa kuwa ni msomi mkubwa wa dini ya Kiislamu. Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Cairo, akipata shahada yake ya uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha London., mhadhiri wa Kiislamu, mshauri wa Umoja wa Mataifa na muandishi wa vitabu vingi. Alikuwa ni profesa kamili katika Chuo kikuu cha Cairo, na atakuja likizo New York na kuwa kama mkurugenzi wa Shirikisho la Taasisi za Kiislamu katika Marekani na Kanada(F.I.A). mara kadhaa nilipokuwa nikiendesha maeneo ambayo kulikuwa na makao makuu ya F.I.A, nilizuia shauku ya kutaka kuingia kwenye jengo lao, lakini siku moja muuza magazeti Fulani alinitambulisha kwa Dr. Shawarbi.
Alikuwa mwenye urafiki sana. Alisema kuwa huwa ananifuatilia kwenye vyombo vya habari. Nilimjulisha kuwa niliambiwa kumhusu na watu mbalimbali. Basi tukazungumza kwa kama dakika kumi na tano hadi ishirini hivi. Sote tulikuwa na mihadi ya kwenda sehemu Fulani.
Kabla ya kuachana aliniambia jambo fulani ambalo halijawahi kunitoka kichwani. Alisema, “Hakuna mwenye imani kamili mpaka pale atakapotamani yampate ndugu yake yale anayotamani yampate yeye mwenyewe.”
Turudi kwa dada yangu Ella. Sikuweza kutoa akilini mwangu kile alichonifanyia. Nimekwisha sema alikuwa ni mwanamke mweusi shupavu kutoka Georgia. Msimamo wake na ukichwa ngumu wake vilisababisha atengwe kutoka Msikiti Namba Kumi na Moja wa Boston; walimrudisha lakini baadaye akaondoka mwenyewe. Akaanza kujifunza na Waislamu asilia, kisha akaanzisha shule ambayo ilifundisha na Kiarabu! Yeye mwenyewe hakuweza kukiongea, aliajiri waalimu wa kukifundisha. Huyo ndiye Ella! Alikuwa anafanya biashara ya majengo na alikuwa akitunza pesa kwa ajili ya hija. Karibu kila siku usiku tulikaa na kuzungumza; aliniambia kuwa suala hilo halina mjadala. Ni muhimu sana nikienda mimi hija. Wakati wote wa kurudi New York nilikuwa nikimfikiria Ella. Mwanamke shupavu sana. Amevunja ushupavu wa wanaume watatu, akiwa mshupavu kuliko wote watatu wakiwekwa pamoja. Alikuwa na nafasi muhimu sana maishani mwangu. Zaidi yake hakukuwa na mwanamke mwenye nguvu za kutosha kuniongoza; mimi ndiye niliongoza wanawake. Nilimvuta Ella kwenye Uislamu, na sasa alikuwa akigharamia safari yangu ya Mecca.
Sikuzote ukiwa pamoja na Allah, basi naye atakupa ishara kuwa yupo pamoja nawe.
Nilipoenda kuomba visa kwenye ubalozi wa Saudi Arabia, balozi wa Saudi Arabia aliniambia kuwa hakuna Muislamu aliyesilimu akiwa Marekani anayeweza kupata visa ya hija bila ya kupata saini ya kukubaliwa na Dr. Mahmoud Shawarbi. Huo ulikuwa ni mwanzo tu wa ishara kutoka kwa Allah. Nilipompigia simu Dr. Shawarbi, alishangaa sana. “Nilikuwa ndiyo najiandaa kukutafuta,” alisema, “Karibu uje.”
Nilipofika ofisini kwake, Dr. Shawarbi alinipatia barua iliyosainiwa ya kunikubalia kwenda hija, na kisha akanipatia nakala ya kitabu. Kilikuwa ni kitabu kilichoitwa
The Eternal Message of Muhammad kilichoandikwa na Abd-Al-Rahman Azzam.
Dr. Shawarbi alisema kuwa mwandishi alikuwa ametuma nakala hiyo kwa ajili yangu. Aliendelea kunieleza kuwa mwandishi ni raia wa Saudi Arabia aliyezaliwa Misri, mwanadiplomasia mashuhuri na mmoja wa washauri wa karibu wa Mwanamfalme Faisal, mtawala wa Saudi Arabia. “Amekufuatilia sana kupitia vyombo vya habari.” Iliniwia vigumu sana kuamini.
Dr. Shawarbi alinipa namba ya mwanaye aliyeitwa Muhammad Shawarbi, alikuwa ni mwanafunzi huko Cairo, akanipatia na namba ya mwandishi wa kitabu kile, Omar Azzam ambaye aliishi huko Jedda, “Jitahidi uwapigie wote ukifika kituo cha mwisho kabla ya Mecca.”
Niliondoka New York kimyakimya(Sikujua kabisa kuwa kurudi kwangu kutakuwa kwa makelele sana). Ni watu wachache tu waliambiwa kuwa ninasafari. Sikutaka watu wa usalama au wengine wowote waniwekee vizuizi dakika za mwisho. Waliokuja kuniaga uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kennedy walikuwa ni mke wangu Betty, mabinti zangu watatu na watu wangu wa karibu wachache. Ndege ya shirika la Lufthansa ilipoacha ardhi, nilisalimiana na majirani niliokaa nao. Ishara nyingine! Wote walikuwa Waislamu. Mmoja alielekea Cairo kama mimi, na mwingine alielekea Jedda ambako ningefika baada ya siku chache. Tuliongea na majirani zangu wale kwa safari nzima hadi Frankfurt, Ujerumani. Tulipokuwa hatuzungumzi nilisoma kitabu nilichopewa. Tulipofika Frankfurt, ndugu aliyeelekea Jedda alituaga sisi tulioelekea Cairo. Tulikuwa na saa kadhaa kabla ya kuruka kuelekea Cairo hivyo nikaamua kutembeatembea kidogo kuiona Frankfurt.
Nilipokuwa maliwatoni pale uwanja wa ndege, nilikutana na Mmarekani wa kwanza aliyenitambua, alikuwa ni mwanafunzi wa kizungu kutoka Rhode Island. Aliniangalia kwa muda kisha akanifuata, “Wewe ni X?” Nilicheka na kumwambia ndiyo, sijawahi kusikia nikiitwa hivyo. “Haiwezekani!” alisema kwa mshangao. Hakuna mtu atakayeniamini nikimwambia hili!” Alisema kuwa alikuwa anasoma huko Ufaransa.
Mimi na yule ndugu yangu Muislamu tulishangazwa sana na urafiki wa watu wa Frankfurt. Tulitembelea maduka mengi, tuliingia kwenye duka na kupokelewa kwa bashasha sana. Ndani ya Marekani unaweza ingia dukani na kutumia dola mia moja na kuondoka na bado ukawa mpita njia tu.
Wote, wewe na muuzaji mnakuwa kama kila mmoja anamfanyia mwenzake hisani. Watu wa Ulaya wanaubinadamu zaidi. Ndugu yangu Muislamu ambaye aliweza kuzungumza Kijerumani kwa kiasi, aliwaeleza kuwa tulikuwa Waislamu, hapo niliona kitu kile kile pale watu waliponichukulia kama Muislamu na si mtu mweusi. Watu wakikuchukulia kama Muislamu wanakuchukulia kama binadamu, na wanakutendea kwa njia tofauti sana.
Tulirudi uwanja wa ndege na kuchukua ndege ya shirika la ndege la United Arab kuelekea Cairo. Watu wengi—bila shaka Waislamu waliokuwa wanaelekea hija, walikuwa wakikumbatiana na kusalimiana kwa bashasha. Walikuwa watu wa rangi na jamii mbalimbali, yalikuwa mazingira ya kirafiki sana. Niliingiwa na hisia kuwa hakukuwa na tatizo la rangi mahali hapa. Nilihisi kama vile mtu aliyetoka tu kutoka gerezani.
Nilimwambia ndugu yangu yule kuwa nilitaka kutalii jiji la Cairo kwa siku kadhaa kabla ya kuelekea Jedda. Alinipa namba yake na kuniambia nimpigie sababu alitaka kuniunganisha na rafiki zake ambao waliweza kuongea Kiingereza na walikuwa wakielekea hija, na kuwa watafurahi kuniongoza.
Basi nilitumia siku mbili za furaha kutalii jiji la Cairo. Nilipendezwa sana na shule za kisasa, nyumba za makazi za umma, barabara kubwa na maendeleo ya viwanda niliyoyaona. Nilikuwa nimesoma na kusikia kuwa Rais Nasser alikuwa amejenga moja ya nchi iliyoendelea zaidi kiviwanda katika Afrika. Jambo lililonishangaza zaidi nikuwa magari na mabasi yalikuwa yakitengenezwa pale pale Cairo.
Nilikuwa na wakati mzuri nilipokutana na mtoto wa Dr. Shawarbi, Muhammad Shawarbi, alikuwa ni kijana wa miaka kumi na tisa, alikuwa akisomea uchumi na sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Cairo. Aliniambia kuwa ndoto ya baba yake ni kujenga Chuo Kikuu cha Kiislamu ndani ya Marekani.
Watu wengi wenye urafiki niliokutana nao walishangaa sana kusikia kuwa nilikuwa Muislamu kutoka Marekani! Moja ya watu hao alikuwa mwanasayansi mmoja wa Misri pamoja na mkewe—nao wakiwa safarini kwenda hija Mecca. Bwana huyo alinisisitiza kwenda pamoja nao kwenye mgahawa uliokuwa eneo moja la Cairo lililoitwa Heliopolis. Walikuwa wenzi wenye akili na maarifa sana. Ukuaji wa kiviwanda wa Misri ilikuwa ndiyo moja ya sababu iliyofanya mataifa ya magharibi yaichukie sana. Mwanasayansi yule aliniambia kwa sababu ilikuwa ikizionyesha nchi zingine za kiafrika yale zinayozipasa kufanya. Mke wake aliniuliza, “Kwa nini watu duniani wanakabiliwa na njaa wakati Marekani inachakula kingi sana cha ziada? Wanakifanyia nini, wanakitupa baharini?” Nilimjibu “Ndiyo, lakini vingine wanaweka kwenye maghala na vyumba vya kutunza baridi na kuviacha huko, kukiwa na watu wa kuvitunza mpaka pale vitakapokuwa havifai tena kuliwa. Kisha watu wengine watakuja na kuvitoa ili kupata nafasi kwa ajili ya vipya.” Aliniangalia akiwa haamini kabisa. Pengine alihisi natania. Lakini walipa kodi wa Marekani wanafahamu kuwa ni kweli.
Lakini sikumwambia kuwa hata Marekani kwenyewe kuna watu wanateseka na njaa.
Nilimpigia simu yule rafiki yangu Muislamu kama alivyoniagiza, kisha nikaonana na rafiki zake waliokuwa wanakwenda hija. Jumla na mimi tulikuwa watu nane, kati yetu walikuwemo jaji na afisa kutoka wizara ya elimu. Waliongea Kiingereza kizuri na walinikubali kama ndugu yao. Niliichukulia hiyo kama ishara nyingine kutoka kwa Allah, kila nilikoenda kulikuwa na mtu aliye tayari kunisaidia na kuniongoza.
***
Maana halisi ya
Hajj katika Kiarabu ni kuchukua hatua katika kufanya jambo fulani. Kwenye sheria za Kiislamu, inamaanisha kwenda Kaaba, Nyumba Takatifu, na kutimiza takwa la hija. Uwanja wa ndege wa Cairo ndipo palikuwa mahali ambapo vikundi kadhaa vya Mahujaji vinakuwa
Muhrim yaani kuingia katika hali ya
Ihram(Kunuia na kujiweka tayari kwa hija na kujitenga na mambo ya dunia). Baada ya kupokea ushauri, niliamua kuacha mizigo yangu yote pale Cairo, ikiwa pamoja na kamera zangu nne, moja ikiwa ya video. Pale Cairo nilinunua mkoba mdogo wa kutosha suti moja, shati, nguo za ndani na jozi za viatu. Kwenye safari ya kwenda airport nilikuwa na wasiwasi sana, nilifahamu kuwa kuanzia hapo itanipaswa kuwaangalia watu wanaofahamu wanachokifanya na kujaribu kuwaiga.
Katika kuingia hali ya
Ihram, tulivua nguo zetu na kujifunga mataulo mawili meupe. Moja linaloitwa
Izar, lilikuwa la kujifunga kiunoni. Jingine,
Rida lilizungushwa shingoni na mabegani na kuacha bega na mkono wa kushoto wazi. Pia kulikuwa
na’l , makubadhi ambayo yaliacha kifundo cha mguu wazi. Juu ya fundo la kiunoni la
Izar kulikuwa na mkanda wenye mfuko wa pesa, na kwa ajili ya kubebea passport na nyaraka zingine muhimu, kama ile barua niliyopata kutoka kwa Dr. Shawarbi.
Kila mmoja kati ya maelfu ya watu waliokuwepo uwanjani pale wakijianda kwenda Jedda, alivalia namna hii. Unaweza kuwa mfalme au mkulima masikini na mtu yeyote asijue. Baadhi ya watu wakubwa ambao nilionyeshwa kwa siri walikuwa wamevalia kama mimi tu. Mara tu baada ya kuvalia hivi, wote tulianza kuita kwa kupokezana “
Labbayka! Labbayka!” (Nakuja kwako Ee Mungu!) Uwanja wa ndege ulijaa sauti kubwa za
Muhrim wakitaja nia yao ya kufanya Hija.
Ndege zilizojaa mahujaji zilikuwa zikipaa kila dakika, lakini bado uwanja ukawa umejaa wengine wengi pamoja na ndugu na rafiki zao waliokuja kuwaaga. Wale ambao walikuwa hawaendi walikuwa wakiwaomba wengine wasali wa niaba yao huko Mecca. Tulikuwa tayari ndani ya ndege ndipo nilipotambua kwa mara ya kwanza kuwa hakukuwa na nafasi yangu lakini walikuwa wamefanya mipango na mtu fulani alishushwa sababu hawakutaka
kumuangusha Muislamu kutoka Marekani. Nilipatwa na hisia mchanganyiko, dhamira ikinisuta kuwa nilisababisha mtu mwingine ashushwe kwa ajili yangu, na pia nilijihisi mnyenyekevu na mwenye shukrani sana kwamba niliheshimiwa kiasi kile.
Ndani ya ndege kulijaa watu weupe, wa kahawia, wekundu na wamanjano, wenye macho ya bluu, nywele za rangi ya dhahabu na mimi mwenye nywele nyekundu zilizojikunjakunja, wote kama ndugu! Wote tukimtukuza Mungu mmoja, Allah, wote tukiheshimiana.
Kutoka kwa mtu fulani wa kwenye kundi letu, habari zilianza kusambaa kiti hadi kiti kuwa nilikuwa Muislamu kutoka Marekani. Watu walinigeukia na kunisalimu kwa tabasamu. Chakula cha mchana kilipitishwa, tulipokuwa tunakula, habari zilifika chumba cha marubani kuwa ndani ya ndege kulikuwa na Muislamu kutoka Marekani.
Rubani wa ndege alikuja kunisalimu. Alikuwa ni Mmisri, alikuwa na weusi wa ngozi kuliko hata mimi; angeweza kutembea katika mitaa ya Harlem bila mtu hata mmoja kumshangaa. Alifurahi sana kukutana na Muislamu kutoka Marekani. Aliponialika kutembelea chumba cha rubani nilikubali mara moja.
Rubani msaidizi alikuwa ni mweusi kuliko hata yeye. Siwezi kukuelezea jinsi nilivyohisi. Sijawahi kuona mtu mweusi akirusha jeti. Ile paneli iliyojaa vitufe: hakuna mtu anayeweza kuelewa vilimaanisha nini. Marubani wote walijawa na tabasamu, wakinitendea kwa heshima kama nilivyotendewa tokea nitoke Marekani. Nilisimama ndani mle nikiangalia anga juu yetu. Katika Marekani nilipanda ndege mara nyingi pengine kuliko mtu mweusi mwingine yeyote
yule, lakini sijawahi karibishwa kwenye chumba cha marubani. Lakini tazama hapa nimekaa na Waislamu wenzangu wawili, mmoja kutoka Misri na mwingine kutoka Arabia, sote tukielekea Mecca, na mimi nikiwa kule kwenye chumba cha marubani. Ndugu! Nilijua kuwa Allah yuko pamoja nami.
Nilirudi kitini kwangu. Kwa safari nzima ya kama saa moja, mahujaji tulikuwa tukipiga kelele, “
Labbayka! Labbayka!” Ndege ikatua uwanja wa ndege wa Jedda, ni mji wa bandari katika bahari ya Shamu. Ni sehemu ambayo mahujaji wote wanaoenda na kurudi kutoka Mecca hupita. Mji wa Mecca upo umbali wa maili arobaini mashariki ya Jedda.
Uwanja wa ndege wa Jedda ulionekana kujaa watu kuliko hata ule wa Cairo. Kikundi chetu kikawa moja tu ya vikundi vingi vya watu kutoka mataifa mbalimbali vilivyokuwa vikipishana pale uwanjani. Kila kikundi kilikuwa kinaelekea kupanga mstari mrefu kwenye ofisi za uhamiaji. Kabla ya kufika ofisi za uhamiaji, kila kikundi cha mahujaji kilipewa mtu aliyeitwa
Mutawaf, huyu jukumu lake lilikuwa ni kusafirisha kikundi hicho kwenda Mecca. Baadhi ya mahujaji walikuwa wakipaza sauti wakisema
“Labbayka!” wengine, baadhi yao wakiwa vikundi vikubwa, walikuwa wakisema sala kwa pamoja, nitaitafsiri sala hiyo, “Sijisalimishi kwa mwingine yoyote ila wewe. Ee Allah, sijisalimishi kwa mwingine ila wewe. Najisalimisha kwako kwa sababu huna mshirika. Sifa na Baraka zote zinatoka kwako. Nawe upo peke yako katika ufalme wako.” Dhumuni kubwa la sala hiyo ni kukiri Mungu mmoja.
Ni maafisa tu ndiyo hawakuvaa mavazi ya
ki-Ihram au kofia nyeupe, kanzu nyeupe na makubadhi waliyovaa
Mutawaf, yaani wale waliowaongoza mahujaji. Katika kiarabu neno
Mutawaf linamaanisha “Yule anayeongoza” mahujaji kwenda
“Tawaf” ambacho ni kitendo cha kuizunguka Kaaba.
Nikiwa katikati ya kikundi chetu, niilisonga kwenye mstari wa kusubiria passport zetu zikaguliwe, nilijawa na wasiwasi. Siamini kuwa nipo kwenye chimbuko la Uislamu, nawapatia passport ya Marekani ambayo inawakilisha kitu tofauti kabisa na kile ambacho Uislamu unakisimamia.
Jaji aliyekuwa kwenye kundi letu alihisi wasiwasi wangu, alinishika begani kunituliza. Upendo, unyenyekevu na undugu wa kweli ulionekana kila nilikogeuka. Mwishowe kundi letu likamfikia karani aliyechunguza passport na mikoba ya mahujaji kwa makini kabla ya kuwaruhusu kusonga mbele.
Nilikuwa na wasiwasi sana kiasi kwamba nilipofungua mkoba wangu kwa ufungua na ukagoma kufunguka, niliufungua kwa nguvu, nikiogopa kuwa wasije hisi kwenye mkoba wangu nina vitu nisivyotakiwa kuwa navyo. Karani akaona kuwa nina passport ya Marekani, aliishika huku akiniangalia, kisha akasema jambo fulani kwa kiarabu. Rafiki zangu niliokuwa nao wakaanza kuongea kwa ajili yangu haraka haraka kwa kiarabu. Jaji, kwa Kiingereza akaniuliza kuhusu barua kutoka kwa Dr. Shawarbi, aliichukua na
kuiweka mezani pa karani. Karani aliisoma na kuirudisha huku akisema kuwa nilitakiwa kusema mapema. Ubishi kunihusu ukaendelea, nilijihisi kama mpumbavu, sikuweza kusema chochote wala kuelewa kilichokuwa kikisemwa.Mwishowe, kwa unyonge, jaji alinigeukia na kusema kuwa nilitakiwa kupitia
Mahgama Sharia. Ilikuwa ni mahakama kuu ya Kiislamu. Ilichunguza Waislamu wasio wa kweli waliojaribu kuingia Mecca. Ilikuwa wazi kuwa ni marufuku kabisa kwa asiye Muislamu kuingia Mecca.
Iliwabidi rafiki zangu wandelee kwenda Mecca bila ya mimi. Walionekana kujaa wasiwasi juu yangu. Nami nilijawa na wasiwasi lakini nilipata maneno ya kuwafariji, niliwaambia, “Nitakuwa sawa. Allah ananiongoza.” Walisema kuwa watasali kila saa kwa ajili yangu.
Mutawaf woa aliwahimiza kuendelea mbele ili kuondoa msongamano pale uwanja wa ndege. Tulipungiana mkono, nikiwaangalia wakienda zao.
Wakati huo ilikuwa ni kama saa tatu asubuhi, siku ya Ijumaa. Sijawahi kuwa kwenye msongamano wa watu mkubwa kama ule, lakini sijawahi kujihisi mpweke na mnyonge tokea nilipokuwa mtoto. Mbaya zaidi ni kuwa, siku ya Ijumaa kwenye ulimwengu wa Kiislamu ni kama Jumapili kwenye ulimwengu wa Kikristo. Siku ya Ijumaa Waislamu wote hukusanyika kwa ajili ya kusali pamoja. Tukio hilo huitwa
yawn al-Jumu’a “siku ya kukusanyika.” Ilimaanisha kuwa hakuna mahakama iliyofanya kazi siku ya Ijumaa. Itanibidi kusubiri hadi Jumamosi.
Afisa mmoja alimwita msaidizi wa
Mutawaf. Kwa kiingereza kibovu afisa yule alinielekeza kuwa nitapelekwa eneo ambalo lilikuwepo palepale uwanja wa ndege. Passport yangu ilibaki ofisi za uhamiaji, nilitaka kupinga kwa sababu sheria ya kwanza ya msafiri ni kutoachana na passport yake, lakini sikufanya hivyo. Nikiwa kwenye mataulo na makubadhi, nilimfuata muongozaji yule aliyekuwa amevaa kofia nyeupe, kanzu nyeupe na makubadhi. Nafikiri ilivutia kututazama. Watu tuliopishana nao waliongea kila aina ya lugha. Sikuweza kuongea lugha yoyote nyingine. Nilikuwa kwenye hali mbaya sana.
Nje tu ya uwanja wa ndege kulikuwa na msikiti, na sehemu ya juu ya uwanja wa ndege kulikuwa na jengo kubwa lililokuwa kama bweni. Wakati huo ilikuwa karibu na mapambazuko, ndege zilikuwa bado zinaruka na kutua—taa zao za mkiani zikimulika-mulika anga. Mahujaji kutoka Ghana, Japan, Indonesia, Urusi na kwingineko, walikuwa wakiingia na kutoka kwenye jengo lile la bweni nilikokuwa napelekwa. Sidhani kama kuna kamera ya video imewahi chukua picha ya binadamu wenye pilika pilika kama niliyochukua kwa macho yangu. Tulifika kwenye jengo na kuanza kupanda hadi ghorofa ya nne, ghorofa ya juu kabisa. Njiani tulikutana na watu wa kila aina duniani. Wachina, Waindonesia, waafghanistani. Wengi wao wakiwa bado hawajavaa nguo za
ki-Ihram, bado wamevalia mavazi ya kitamaduni ya nchi zao. Ilikuwa kama kuangalia kurasa za jarida la
National Geographic.
Tulipofika ghorofa ya nne, muongozaji wangu alinielekeza kwenye chumba changu ambacho kilikuwa na watu wengine kama kumi na tano. Wengi wao wakiwa wamelala kwenye mazulia yao. Niliweza kuona kuwa wengine walikuwa ni wanawake, wakiwa wamejifunika kutoka usoni hadi miguuni. Kulikuwa na Muislamu mmoja mzee na mke wake ambao walikuwa macho. Walinishangaa
kistaarabu. Waislamu wawili kutoka Misri na mwingine wa kutoka Iran waliamka wakati wakati muongozaji wangu aliponiingiza ndani. Kwa ishara, alisema kuwa atanionyesha njia sahihi ya kukaa wakati wa kusali. Fikiria kuwa Imam wa Kiislamu, kiongozi katika Taifa la Kiislamu la Elijah Muhammad lakini ukawa hujui taratibu za sala!
Nilijaribu kufanya alivyofanya, nilijua kuwa sikuwa nafanya sahihi. Niliweza kuona macho ya Waislamu wengine yakinitazama. Vifundo vya miguu vya mtu wa Magharibi haviwezi kufanya kile ambacho vifundo vya Muislamu vimekuwa vinafanya maisha yake yote. Watu wa Asia huchuchumaa wanapoketi, watu wa magharibi huketi wima vitini. Muongozaji wangu alipokuwa ameinama, nilijitahidi kila niwezavyo kufanya kama alivyofanya lakini sikuweza. Baada ya kama saa moja muongozaji wangu aliondoka na kuashiria kuwa atarudi baada ya saa moja.
Hata sikuweza kulala. Niliendelea kufanyia mazoezi mkao wa kusali. Nilijizuia kufikiria jinsi nilivyoonekana kituko mbele yao. Baada ya muda kidogo nikawa nimejifunza mbinu ya kuniwezesha kuinama hadi sakafuni, lakini baada ya siku mbili au tatu kifundo changu cha mguu kilikuja kuvimba.
Kulipokucha Waislamu waliamka na walitambua uwepo wangu mara moja, tuliendelea kushangaana huku wakiendelea na shughuli zao. Nilianza kuona jinsi ambavyo zulia ni muhimu sana katika maisha ya Waislamu. Kila mtu alikuwa na zulia dogo, na kila mtu na mkewe au na kundi kubwa, walikuwa na zulia kubwa. Waislamu hawa walisali kwenye mazulia yao mulemule chumbani. Baada ya hapo waliweka kitambaa cha mezani juu ya zulia na kuanza kula, hivyo zulia likawa chumba cha chakula. Baada ya kutoa vyombo na kitambaa cha mezani, waliketi zuliani, likawa sebule. Wanapolilalia linakuwa chumba cha kulala. Kabla ya kuondoka, ikanijia akilini na kuelewa kwa nini mtu yule aliyenunua vitu vya wizi nilipokuwa jambazi kule Boston alilipia pesa nyingi sana kwa ajili ya mazulia ya mashariki. Ni kwa sababu mazulia kutoka nchi ambazo mazulia ni muhimu sana yalishonwa kwa ustadi sana. Baadaye nilipokuwa Mecca, nilijionea umuhimu mwingine wa mazulia. Iwapo mzozo wowote ulitokea, mtu aliyeheshimiwa sana na ambaye hakuhusika na mzozo aliketi kwenye zulia huku wale wanaozozana wakimzunguka, na hilo lilifanya zulia kuwa mahakama. Nyakati nyingine lilikuwa darasa.
Mmoja wa Waislamu kutoka Misri alikuwa akiniangalia sana kwa jicho la wizi. Nilimuangalia na kutabasamu. Aliinuka na kunifuata. “Hel-lo-” alisema, alisikika kama wakati Lincoln anatoa hotuba kwenye makaburi ya Gettysburg. Nilimjibu, “Hello!” Nilimuuliza jina lake, lakini hakuelewa vizuri kiingereza. Nafikiri alikuwa na maneno ishirini tu ya kiingereza. Nilikuwa nasema chochote kilichonijia kichwani. Mwishowe nilisema, “Muhammad Ali Clay-”Waislamu wote waliokuwa wakisikiliza walinga’aa kwa shangwe kama mti wa Krismasi. “Ni wewe? Ni wewe?” alisema rafiki yangu akinionyeshea kidole. Nilitingisha kichwa na kusema, “Hapana, hapana, Muhammad Ali ni rafiki yangu!” Baadhi walielewa kiasi, wengine hawakuelewa kabisa na hivyo ndivyo ilivyoanza kusambaa kuwa nilikuwa Cassius Clay, bingwa wa ndondi wa uzito wa juu duniani. Baadaye nilikuja kufahamu kuwa karibu kila mwanaume, mwanamke na mtoto wa Kiislamu alikuwa amesikia jinsi ambavyo Sonny Liston(Mtu ambaye kwa Waislamu alikuwa kama zimwi mla watu) alipigwa na Cassius Clay kama vile Daudi alivyompiga Goliati, Cassius ambaye baadaye aliutangazia ulimwengu kuwa jina lake ni Muhammad Ali na dini yake ni Uislamu na Allah ndiye aliyempa ushindi.
Kuanza kuwasiliana kulisaidia sana. Kuwa kwangu Muislamu kutoka Marekani, kulibadili mtazamo wao, kutoka kuniangalia tu hadi kutaka kunisaidia. Sasa wengi wakaanza kutabasamu. Walikuja karibu na, walinitazama juu hadi chini-
kistaarabu. Nilikuwa kama mtu kutoka sayari ya Mirihi.
Yule msaidizi wa
Mutawaf alirudi na kuonyesha ishara kuwa nimfuate. Alionyeshea Msikiti ulikokuwa na nikafahamu kuwa alikuja kunichukua kwa ajili ya sala ya alfajiri, El Sobh iliyofanyika kabla ya jua kuchomoza.
Nilimfuata na njiani tulikutana na maelfu ya mahujaji, wakiongea lugha mbalimbali isipokuwa Kiingereza. Nilijichukia kwa kutojifunza taratibu halisi za sala kabla ya kuondoka Marekani. Kwenye Taifa la Kiislamu la Elijah Muhammad hatukuwahi kusali kwa Kiarabu. Miaka kadhaa nyuma, nilipokuwa gerezani, Muislamu mmoja asilia kutoka Boston aliyeitwa Abdul Hameed, alinitembelea na baadaye akanitumia sala zikiwa katika kiarabu. Wakati huo nilijifunza sala zile. Lakini sikuwahi kuzitumia tena.
Niliamua akilini kuwa nitamuacha muongozaji wangu afanye kila kitu kwanza nami nitamuangalia. Haikuwa kazi ngumu kumfanya aanze kufanya kwanza, alikuwa na shauku ya kunionyesha. Nje ya msikiti kulikuwa na mabomba yamejipanga. Udhu ulifanyika kabla ya sala. Hilo nililifahamu. Lakini hata baada ya kumuangalia sikuweza kufanya kwa usahihi. Kulikuwa na njia sahihi ya kujiosha, na kufanya kwa njia sahihi ilikuwa muhimu sana.
Nilimfuata kuelekea msikitini, nyuma yake nikimuangalia kwa makini. Aliinama, kichwa chake kikagusa chini. Nami nikafanya hivyo.
“Bi-smi-llahi-r-Rahmain-r-Rahim-” (“Kwa jina la Allah, mwenye kuruzuku na mwenye rehema”) sala zote za Waislamu huanza hivyo. Baada ya hapo nadhani nilikuwa nasema vitu visivyo sahihi, lakini niliendelea kusema.
Si nia yangu jambo hili lionekane kama mzaha. Kwangu haukuwa mzaha hata kidogo. Hakuna ambaye alikuwa karibu ambaye angeweza kusema kuwa nilikuwa sisemi yale waliyokuwa wanasema wengine.
***
Baada ya sala hiyo, muongozaji wangu alinipeleka hadi kwenye makazi yangu. Kwa ishara, aliniambia kuwa atarudi baada ya saa tatu, kisha akaondoka.
Sehemu tuliyokuwa ilituwezesha kuona eneo la uwanja wa ndege vizuri sana. Nilisimama kwenye kibaraza nikiangalia. Ndege zilikuwa zinaruka na kutua bila kupumzika. Maelfu elfu ya watu kutoka kote duniani walipita huku na kule. Niliona vikundi vilivyokuwa vinaelekea Mecca kwa mabasi na magari madogo. Niliona wengine walioamua kutembea maili zile arobaini. Nilitamani name ningeanza kutembea. Walau hilo nilijua jinsi ya kulifanya.
Nilikuwa naogopa hata kufikiri yatakayotokea. Je nitakataliwa kuingia Mecca kuhiji? Niliwaza maswali ya kunipima yatakuwaje na muda gani nitafika mbele ya Mahakama Kuu ya Kiislamu.
Yule Muislamu kutoka Iran alinifuata. Alinisalimu kwa kusita kidogo, “Mmare . . . Mmarekani?” alionyesha ishara kuwa anataka niende kujumuika naye na mkewe kwenye kupata kifungua kinywa, kwenye zulia lao. Nilifahamu kuwa ni ukarimu mkubwa sana alikuwa akinifanyia. Haunywi chai na Muislamu pamoja na mkewe kirahisirahisi. Sidhani kama Muiran yule alinielewa nilipotingisha kichwa na kutabasamu, nikimaanisha “Hapana, ahsante.” Hata hivyo aliniletea chai na biskuti. Mpaka wakati ule nilikuwa sina kabisa wazo la kula.
Wengine walifika na kunisalimu kwa ishara ya kichwa huku wakitabasamu. Rafiki yangu wa kwanza, yule aliyeongea kiingereza kidogo alikuwa amekwishaondoka. Nilikuwa sifahamu kinachoendelea, lakini alikuwa amesambaza taarifa kuwa kwenye ghorofa ya nne kulikuwa na Muislamu kutoka Marekani. Msongamano wa watu ukaanza kupita kuelekea kwenye makazi yetu. Waislamu wakiwa wamevalia mavazi ya
ki-Ihram, na wengine wakiwa bado wamevaa mavazi yao ya kitamaduni, walinipita polepole huku wakitabasamu. Jambo hilo liliendelea kwa muda mrefu niliokuwepo eneo lile. Lakini sikufahamu kuwa mimi ndiye nilikuwa kivutio.
Siku zote nimekuwa mtu asiye na utulivu na mwenye wasiwasi. Maidizi wa
Mutawaf hakurudi baada ya saa tatu kama alivyokuwa amesema na hilo lilinifanya niingiwe na wasiwasi. Niliogopa kuwa atakuwa ameamua kuachana na mimi kwa kuona kuwa siwezi kusaidika. Na wakati huo njaa nayo ilianza kunibana. Waislamu wote katika chumba chetu walikuwa wamenikaribisha chakula nami nilikataa. Naomba nikiri kuwa tatizo ni sikudhani kama nitaendana na namna yao ya ulaji. Kila kitu kiliwekwa kwenye poti moja juu ya zulia lililokuwa chumba cha chakula, na niliona wote wakila humo kwa kutumia mikono yao.
Niliendelea kusimama kibarazani pale nikiangalia uwanja wa ndege kule chini, mwishowe nikaamua nitembee-tembee kidogo. Nilishuka chini mpaka kwenye ua, nilionelea kuwa nisiende mbali, mtu anaweza kuja kunitafuta. Basi nikarudi chumbani kwetu. Baada ya kama dakika arobaini na tano nikashuka tena chini, safari hii nilienda, mbali kidogo. Niliona mgahawa mdogo uliokuwa karibu na ua. Niliingia ndani moja kwa moja. Ulikuwa umejaa huku lugha mbalimbali zikisikika. Kwa kutumia ishara, nilinunua kuku mzima wa kukaanga na chips nene za viazi. Nilirudi uani na kumchanchana kuku yule, nikitumia mikono yangu. Waislamu wote walionizunguka walikuwa wanafanya hivyo hivyo. Niliona wanaume wa walau miaka sabini wakikaa kwa kukunja miguu mpaka wakawa wanaonekana kama wamejifunga hivi. Wakila kwa furaha na kuridhika kama vile wapo ndani ya mgahawa mzuri, wakiwa wamezungukwa na wahudumu. Wote walikula pamoja na kulala pamoja. Kila kitu kuhusu mazingira ya hija, kilionyesha umoja wa binadamu chini ya Mungu mmoja.
Siku ile nilifanya safari kadhaa kati ya chumbani kwetu na kwenye ua wa jengo, kila wakati nikienda kutembea mbali kidogo. Nilikutana na wanaume wawili weusi na nikawasalimia kwa kichwa. Ilikuwa karibu nipige kelele kwa shangwe baada ya mmoja wao kunisalimu kwa Kiingereza chenye lafudhi ya Uingereza. Hatimaye nilikutana na Waislamu wawili waliozungumza kiingereza, bahati mbaya ndiyo walikuwa wanaondoka. Kabla ya kikundi chao kuondoka kuelekea Mecca, tulizungumza kidogo. Nikajitambulisha kuwa ni Mmarekani na wao wakaniambia ni Waethiopia. Waethiopia wale walikuwa wamepata elimu yao katika jiji la Cairo na sasa walikuwa wakiishi na kufanya kazi katika jiji la Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia. Baadaye nilishangaa sana baada ya kufahamu kuwa kati ya raia milioni kumi na nane wa Ethiopia, milioni kumi walikuwa ni Waislamu. Watu wengi hudhani kuwa Ethiopia ina Wakristo wengi. Lakini ni serikali yake tu ndiyo ina Wakristo wengi. Siku zote nchi za magharibi zimeisaidia serikali ya Kikristo kubaki madarakani.
Nilikuwa nimeishasali sala yangu ya jioni, El Maghrib; nikawa nimelala kitandani kwangu kwenye chumba chetu. Nikijihisi mpweke na mnyonge ndipo ghafla ukaja mwanga!
Lilikuwa ni wazo la ghafla. Katika safari zangu za kwenda kwenye ua wa jengo lile, mahali palipokuwa pamejaa watu, nilikuwa nimewaona maafisa wanne waliokuwa wamekaa karibu na simu. Nikakumbuka namba alizonipatia Dr. Shawarbi kule New York, namba ya mtoto wa mwandishi wa kile kitabu alichonipatia, ambacho tayari nilikuwa nimekimaliza kukisoma. “Baba yangu atafurahi sana kuonana nawe,” alisema Dr. Azzam.
Nilimuuliza maswali kuhusu baba yake. Abd-Al-Rahman Azzam alijulikana zaidi kama Azzam Pasha, au Bwana Azzam mpaka wakati wa mapinduzi ya Misri pale Rais Nasser alipofuta vyeo vyote vya “kibwana.” “Nadhani atakuwepo nyumbani kwangu tukifika huko,” alisema Dr. Azzam. “Anatumia muda mwingi New York kwenye kazi yake ya Umoja wa Mataifa, amekufuatilia kwa ukaribu sana.”
Nilibaki mdomo wazi.
Ilikuwa ni alfajiri tulipofika kwenye nyumba ya Dr. Azzam. Baba yake alikuwepo pale. Pia walikuwepo kaka wa baba yake, ambaye alikuwa ni mkemia na rafiki yao mwingine, wote wakiwa macho mapema ile wakitusubiri. Kila mmoja alinikaribisha kwa bashasha kama vile nilikuwa mwana wao niliyepotea kwa muda mrefu. Sikuwahi kuwaona watu hao maishani lakini walinitendea kwa ukarimu sana! Nikuambie tu kuwa sijawahi heshimishwa namna ile maishani mwangu wala kuona ukarimu wa kweli kiasi kile.
Mhudumu alituletea chai na kahawa, kisha akaondoka. Niliambiwa nijisikie nipo nyumbani. Hakuna mwanamke aliyeonekana. Ukiwa Arabia unaweza dhani nchi haina wanawake.
Dr. Abd-Al-Rahman azzam ndiye aliyeongoza mazungumzo. Kwa nini sikupiga simu mapema? Hawakuelewa kwa nini sikufanya hivyo. Walionekana kufedheheka kuwa nilikaa uwanja wa ndege; na kwamba nilicheleweshwa kuingia Mecca. Nilijitahidi kuwaaminisha kuwa nilikuwa sawa na hakuna shida yoyote hawakukubali. “Unatakiwa kupumzika,” alisema Dr. Azzam, kisha akaenda kupiga simu.
Sikujua mtu huyu muungwana alikuwa anafanya nini. Nilipoambiwa nitarudishwa baadaye kwa ajili ya chakula cha jioni, na kuwa wakati huo nirudi garini, sikujua kabisa kuwa nilikuwa naenda kupokea ukarimu mkubwa kabisa wa Kiislamu.
Abd-Al-Rahman Azzam anapokuwa nyumbani Saudi Arabia huwa anaishi kwenye hoteli ya Jedda Palace. Kwa sababu niliwatembelea nikiwa na barua kutoka kwa rafiki yao, yeye aliamua kuishi nyumbani kwa mwanawe na kuniacha mimi nitumie makazi yake ya hotelini mpaka nitakapokwenda Mecca.
Nilipokuja kufahamu jambo hilo nilikuwa nimeishachelewa na sikuweza tena kupinga; tayari nilikuwa ndani ya makazi yale na Dr Azzam mdogo akawa ameishaondoka. Hakukuwa na wakumbishia. Makazi yake ya hotelini yalikuwa na vyumba vitatu vikubwa vya kulala. Kulikuwa na bafu kubwa kama mara mbili ya yale ya hoteli ya Hilton ya New York. Yalikuwa makazi namba 214. Na hata kulikuwa na kibaraza nje yake na hivyo kukuwezesha kuona vizuri mji ule wa pwani ya bahari ya Shamu.
Hapo kabla hisia zangu hazijawahi guswa kusali kama siku ile-na nikafanya hivyo. Nikasali kwenye zulia lililokuwako sebuleni.
Katika maisha yangu ya aina mbili niliyoishi kama mtu mweusi wa Marekani, hakuna hata moja iliyonipa mtazamo wa kiitikadi. Siku zote akili yangu ilichunguza sababu la lengo la mtu yeyote liyenitendea jambo ambalo sikustahili. Na siku zote, kama mtu huyo ni mzungu niliweza kuona lengo lake la kibinafsi.
Lakini siku ile hotelini pale ilikuwa ni moja ya mara chache sana ambazo nilipigwa na butwaa kiasi cha kushindwa kupinga. Mzungu yule—walau kwa Marekani angechukuliwa kuwa ni mzungu, alikuwa na undugu na mtawala wa Saudi Arabia ambaye alikuwa ni mshauri wake, mtu mkubwa kimataifa ambaye hana lolote la kupata kwa kunikarimu aliniachia makazi yake ya hotelini! Hakuwa na uhitaji wowote na mimi. Alikuwa na kila kitu. Ukweli ni kuwa alikuwa na vingi vya kupoteza kuliko kupata. Alikuwa amenifuatilia kwenye vyombo vya habari vya Marekani. Na kama alifanya hivyo, alifahamu vyema kuwa sikuwa na chochote zaidi ya kupewa sifa mbaya na kunyanyapaliwa. Nilikuwa dubwana lenye mapembe. Nilikuwa “mbaguzi wa rangi.” Nilikuwa “Mchukia wazungu” na yeye kwa muonekano alikuwa mzungu. Nilitwa mhalifu; na si hilo tu, bali kila mtu alikuwa akinishutumu kutumia dini yake ya Uislamu kama kichaka cha falsafa zangu na matendo yangu ya kihalifu. Na hata kama alikuwa na lengo la kunitumia, alifahamu vyema kuwa nilitengana na Elijah Muhammad na Taifa la Kiislamu, “nguzo zilizonipa nguvu,” kama vilivyodai vyombo vya habari vya Marekani. Taasisi pekee niliyokuwa nayo ilikuwa na majuma machache tu tokea ianzishwe. Sikuwa na kazi. Sikuwa na pesa. Na hata kufika pale nilikuwa nimekopa pesa kutoka kwa dada yangu.
Asubuhi ile ndipo nilipoanza kumtafakari “mzungu” tena. Ndipo nilipoanza kuchukulia kuwa neno “mzungu”, kama ambavyo limezoeleka kutumika, halimaanishi kutokana na rangi yake hasa, bali hasa linamaanisha tabia na matendo yake. Ndani ya marekani “mzungu” linamaanisha tabia na matendo fulani kuelekea mtu mweusi na watu wengine wote wasio weupe. Lakini kwenye ulimwengu wa Kiislamu, niliona watu wenye rangi nyeupe wakiwa na upendo wa kweli kuliko niliowahi kuuona kutoka kwa yeyote yule.
Asubuhi ile ndipo ndipo mtazamo wangu mzima juu ya “mzungu” ulipobadilika.
Ngoja ninukuu kutoka kwenye kijitabu changu. Niliandika haya mchana ule nilipokuwepo hotelini: “Siwezi kuelezea shangwe niliyonayo nikiwa nimekaa hapa nikisubiri kwenda mbele ya Kamati ya Hajj. Dirisha langu linaangalia upande wa Magharibi, iliko bahari. Mitaa imejaa mahujaji kutoka kote duniani. Sala zinatolewa kwa Allah na aya za Quran zipo kwenye midomo ya kila mmoja. Sijawahi ona jambo zuri kama hili, wala kushuhudia, wala kulihisi.
Ninajihisi salama, maelfu ya maili kutoka kwenye maisha tofauti kabisa niliyoishi. Piga picha kuwa saa ishirini na nne zilizopita nilikuwa kwenye chumba kilichokuwa katika ghorofa ya nne pale uwanja wa ndege, nikiwa nimezungukwa na watu ambao siwezi kuwasiliana nao, nikiwa sijui kabisa mustakabali wangu utakuwaje na kujihisi mpweke sana, lakini simu moja tu kama Dr. Shawarbi alivyonielekeza, imefanya nikutane na mmoja ya watu wenye nguvu sana katika Ulimwengu wa Kiislamu. Muda si mrefu nitalala kitandani pake ndani ya hoteli ya Jedda Palace. Natambua vyema kuwa nimezungukwa na rafiki ambao hawana unafiki na ni watu ninaoweza kuhisi nguvu ya imani yao. Inanipasa kusali tena kumshukuru Allah kwa Baraka hii, inanipasa kusali kwa ajili ya mke wangu na watoto wangu waliopo Marekani ili nao wapokee Baraka siku zote kutokana na kujitoa kwao.”
Nilisali sala mbili zaidi kama nilivyoandika kwenye kijitabu changu. Baada ya hapo nikalala kwa saa nne mpaka pale simu ilipoita. Alikuw ani Dr. Azzam mdogo. Alisema kuwa baada ya saa moja atakuja kunichukua kwa ajili ya kwenda kupata chakula cha jioni. Nilijiumauma wakati wa kujaribu kutafuta maneno ya shukrani. Alinikatisha kwa kusema, “Ma sha’a-llah” neno linalomaanisha, “Mungu ndiye aliyepanga.”
Wakati wa kumsubiri Dr. Azzam, nilikimbia mara moja kwenda ukumbi wa mapokezi ya hoteli. Nilipokuwa natoka nilionana koridoni na mtu mmoja aliyevalia kiramsi huku akiwa amezungukwa na wahudumu. Ilionekana wazi kuwa anaishi pale. Naye alikuwa anashuka chini. Nilifuatana nao walipokuwa wanashuka hadi kupita ukumbi wa mapokezi. Nje kulikuwa na msafara mdogo wa magari ukiwasubiri. Jirani yangu yule alipotokea mlango wa mbele wa hoteli, watu walimkimbilia na kumbusu mkono. Nilikuja kutambua kuwa alikuwa ni Mufti Mkuu wa Jerusalem. Baadaye hotelini pale nilipata wasaa wa kuongea naye kwa kama nusu saa. Alikuwa mtu mwenye urafiki na mwenye kujiendesha kwa heshima sana. Alifahamu vyema mambo ya dunia, na hata matukio yaliyokuwa yanaendelea Marekani.
Sitakuja kusahau ule mlo wa jioni nyumbani kwa Azzam. Nitanukuu daftari langu tena: ‘Akilini mwangu sikuweza kujiambia kuwa watu hawa ni ‘wazungu.’ Kwa nini, kwa sababu walinitendea kama vile ni ndugu yao, Dr. Azzam mkubwa kama baba yangu. Maneno yake ya kibaba na kiuanazuoni yalinifanya nimhisi kama baba yangu. Haikuwa kazi ngumu kugundua kuwa alikuwa mwanadiplomasia mbobezi, mtu mwenye maarifa mengi. Alifahamu mambo yanayoendelea duniani kama mtu anavyofahamu yanayoendelea sebuleni kwake.
‘Kadri tulivyozungumza, ndivyo maarifa yake juu ya mambo mbalimbali yalivyoonekana hayana kikomo. Aliongelea jamii ya vizazi vya Mtume Muhammad, na alionyesha jinsi ambavyo walikuwepo weupe na weusi. Alionyesha pia jinsi ambavyo tatizo la ubaguzi wa rangi kwenye ulimwengu wa Kiislamu lipo kwenye maeneo yale tu yaliyoathiriwa na nchi za magharibi. Alisema kuwa kiasi cha ubaguzi wa rangi anachokutana nacho mtu sehemu fulani kinaashiria kiasi cha ushawishi wa magharibi katika eneo hilo.’
Wakati wa chakula nilifahamishwa kuwa nilipokuwa hotelini, Kamati ya Hajj ilijulishwa kuhusu suala langu, na kwamba asubuhi natakiwa kufika huko. Nilifanya hivyo.
Jaji alikuwa ni Sheikh Muhammad Harkon. Mahakamani hakukuwa na watu isipokuwa mimi na dada mmoja kutoka India ambaye zamani alikuwa ni mprotestanti na sasa amesilimu, na kama mimi tu, naye alikuwa anajaribu kufanya hija. Alikuwa na rangi ya kahawia na sura ndogo ambayo ilikuwa imezibwa kwa sehemu kubwa. Jaji Harkon alikuwa mtu mpole na thabiti, tuliongea na aliniuliza maswali kadhaa, akijaribu kuona kama nimeamini kweli. Nilimjibu kwa ukweli wangu wote. Si tu kuwa alinitambua kama Muislamu wa kweli, bali pia alinipatia vitabu viwili. Kimoja kimeandikwa kwa Kiingereza na kingine kwa Kiarabu. Aliandika jina langu kwenye orodha takatifu ya Waislamu wa kweli na tukawa tumemaliza. Aliniambia, “Natumaini utakuwa mhubiri mkubwa wa Uislamu katika Marekani.” Nilimwambia kuwa nami nina matumaini hayo na nitajaribu kuyatimiza.
Familia ya Azzam ilifurahi sana kusikia kuwa nimekubaliwa kwenda Mecca. Nilipata chakula cha mchana kwenye hoteli ya Jedda Palace kisha nikalala tena kwa saa saba, simu ndiyo iliyoniamsha.
Alikuwa ni Muhammad Abdul Azziz Maged, makamu mkuu wa protokali wa Mwanamfalme Faisal. “Gari maalumu itakusubiri kwenda Mecca mara tu baada ya chakula cha jioni,” aliniambia. Aliniambia nile vya kutosha sababu taratibu za Hajj zinahitaji nguvu nyingi. Mpaka wakati huo sikuwa nashangaa tena.
Waarabu wawili vijana waliambatana nami kwenda Mecca. Barabara kubwa ya kulipia iliyokuwa na mwanga wa kutosha ilifanya safari iwe rahisi sana. Walinzi wa njiani walitizama ndani ya gari mara moja na dereva aliwaonyeshea ishara na tukaruhusiwa kupita, bila hata ya kupunguza mwendo. Kwa wakati huohuo mmoja, nilikuwa mtu niliye muhimu na mnyenyekevu na mwenye shukrani.
Mji wa Mecca ulionekana kama mji wa kale sana. Gari letu lilipita kwenye barabara za mitaa zilizojipindapinda, zikiwa
zimejaa maduka pembeni yake. Mabasi, magari na makumi elfu ya mahujaji kutoka duniani kote walifurika mitaani.
Gari ilisimama mahali ambapo
Mutawaf alikuwa akinisubiria. Alivalia kofia nyeupe na kanzu nyeupe, kama wale wa uwanja wa ndege. Alikuwa mwarabu mmoja mfupi na mweusimweusi hivi, jina lake aliitwa Muhammad. Hakuongea kiingereza hata kidogo.
Tulipaki karibu na Msikiti Mkuu wa Mecca. Tulifanya udhu na kuingia. Ndani kulijaa mahujaji waliosongamana. Wengine wakiwa wamelala, wengine wamekaa, wanaotembea na wengine wakisali.
Sina maneno ya kuuelezea msikiti mpya uliokuwa unajengwa kuzunguka Kaaba. Nilifurahi kufahamu kuwa ulikuwa ni moja ya miradi mikubwa ya ujenzi kati ya ile iliyosimamiwa na Dr. Azzam mdogo, mtu aliyekuwa mwenyeji wangu. Msikiti Mkuu wa Mecca utakapokamilika, utalipita jengo la Taj Mahal la India kwa uzuri.
Nilimfuata
Mutawaf nikiwa nimebeba makubadhi yangu. Kisha nikaiona Kaaba. Jengo kubwa katikati ya Msikiti Mkuu. Lilikuwa linazungukwa na maelfu-elfu ya mahujaji wanaosali, watu wa jinsia zote, rangi, maumbo na kila aina kutoka pande zote duniani. Niliifahamu sala iliyopaswa kutolewa mara tu mahujaji anapoiona Kaaba. Tafsiri yake inasema, “Ee Mungu, wewe ni amani na amani inatoka kwako. Tunaomba Ee Mungu utukaribishe kwa amani.” Baada ya kuingia ndani ya Msikiti Mkuu, mahujaji anatakiwa kuibusu Kaaba iwapo anaweza, lakini kama umati unamzuia kuifikia, anapaswa kuishika. Na kama umati unamzuia kufanya hivyo, anatakiwa kuinua mkono juu na kupaza sauti, “Takbir!” (“Mungu ni Mkubwa”). Sikuweza kufika karibu. “Takbir!”
Hisia zangu mahali pale katika Nyumba ya Mungu zilikuwa kama nimepigwa ganzi.
Mutawaf wangu aliniongoza hadi kwenye umati wa mahujaji waliokuwa wakitoa sala huku wakiizunguka Kaaba mara saba. Wengine walikuwa wamepinda na ngozi zao kujikunja sababu ya uzee; ilikuwa taswira ambayo si rahisi kukutoka kichwani. Niliona mahujaji walemavu wakiwa wamebebwa. Sura zao ziking’aa kwa furaha. Kwenye mzunguko wa saba, nilisali Rak’a mbili, nikiinama hadi kichwa kugusa chini. Nilianza kwa kusali aya ya Quran “Sema yeye ni Mungu, Mungu pekee”, sala ya pili: “Sema ee nyinyi msioamini, siabudu kile mnachoabudu ”
Nilipokuwa nikisali,
Mutawaf wangu aliwazuia mahujaji wengine wasije kunikanyaga-kanyaga.
Kisha mimi na
Mutawaf wangu tukanywa maji kutoka kisima cha Zamzam. Baada ya hapo tukakimbia kati ya vilima viwili, Safa na Marwa, mahali ambapo Hagari alitangatanga akitafuta maji kwa ajili ya mwanawe Ishmaeli.
Baada ya hayo, nilitembelea Msikiti Mkuu mara tatu na kuizunguka Kaaba. Asubuhi iliyofuata tulienda kwenye mlima Arafat, tulikuwa maelfu ya watu, tukipaza sauti kwa pamoja, “Labbayka! Labbayka!” na “Allah Akbar!” Mecca imezungukwa na milima ya kutisha ambayo sijawahi kuona mahali pengine; ni kama vile ilitengenezwa kwa uji wa chuma kutoka kwenye tanuri. Hakuna kitu chochote kilichoota juu yake. Tulipofika ilikuwa tayari mchana, tulisali mpaka jua lilipozama, tulifanya huko sala maalumu za mchana na jioni.
Mwishowe tuliinua mikono yetu na kutoa sala na shukrani, tukirudia maneno ya Allah: “Hakuna Mungu isipokuwa Allah. Hana mshiriki. Yeye ni mwenye mamlaka na sifa. Mema yanatoka kwake naye ni mwenye nguvu juu ya vitu vyote.”
Kusimama juu ya mlima Arafat ndiyo jambo la mwisho kwa mahujaji wa Mecca kutimiza. Hakuna mtu anayeweza kujiita mahujaji iwapo hajatimiza hilo.
Ihram ikawa imeisha. Tulimtupia shetani mawe saba. Wengine walikata nywele na ndevu zao. Niliamua kuwa nitaziacha ndevu zangu. Nilijiuliza mke wangu Betty na binti zangu wadogo watasema nini baada ya kuniona na ndevu nitakaporudi New York. New York ilionekana kama ipo umbali wa maili milioni moja. Sikuona gazeti lolote ninaloweza kusoma toka nitoke New York. Sikujua chochote juu ya yanayoendelea huko. Chama cha watu weusi waliomiliki bunduki ambacho kilikuwepo Harlem kwa miaka mingi kilikuwa “Kimegunduliwa” na polisi; ilikuwa inatangazwa kuwa nilikuwa nyuma ya suala hilo. Taifa la Kiislamu la Elijah Muhammad lilikuwa limenifungulia kesi, wakitaka kunitoa mimi na familia yangu kwenye nyumba tuliyoishi huko Long Island.
Magazeti makubwa, vituo vya redio na televisheni vya marekani vilikuwa na wawakilishi jijini Cairo waliokuwa wakijaribu kuniwinda kila sehemu, kujua niko wapi ili wanihoji juu ya mambo yanayoendelea huko New York, mambo niliyoshutumiwa kusababisha wakati sikujua chochote kuyahusu.
Kitu pekee nilichofahamu ni yale niliyoyaacha nilipoondoka Marekani, mambo ambayo ni kinyume kabisa na niliyoyakuta kwenye ulimwengu wa Kiislamu. Waislamu kama ishirini hivi tuliokuwa tumemaliza Hajj tulikuwa tumekaa kwenye hema kubwa lililokuwepo kwenye mlima Arafat. Nikiwa kama Muislamu kutoka Marekani, macho mengi yalinielekea. Waliniuliza ni kitu gani katika Hajj kilichonipendeza sana. Mmoja ya walioweza kuzungumza Kiingereza aliuliza na kisha kuwatafsiria wengine majibu yangu. Jibu langu kwa swali hilo halikuwa lile walilotegemea, lakini walielewa vyema nilichomaanisha.
Nilisema “
Undugu! Kitendo cha watu wa kila aina na rangi, kutoka kote duniani kuja pamoja kama kitu kimoja! Kimenithibitishia nguvu za Mungu Mmoja.”
Pengine hapakuwa mahala pake, lakini hilo lilinipa nafasi ya kuwahubiria kidogo kuhusu ubaguzi wa rangi uliopo Marekani na madhira yake.
Niliweza kuona jinsi hilo lilivyowagusa. Walikuwa wanafahamu madhira waliyokutana nayo watu weusi wa Marekani, lakini hawakujua kama walitendewa kama wanyama, kwamba kilichofanyika kilikuwa sawa na kuhasiwa kisaikolojia. Watu hawa kutoka maeneo mbalimbali ya dunia walishangazwa sana. Wakiwa kama Waislamu, walikuwa na mioyo ya huruma sana kwa wale waliokuwa wanapitia taabu, na watu waliguswa sana haki na kweli. Walielewa vyema mtazamo wangu wa mambo—kwamba kwangu mimi uovu mkubwa sana duniani ni ubaguzi wa rangi, na viumbe wa Mungu kushindwa kuishi kama kitu kimoja katika ulimwengu wa Magharibi.
***