Kisa cha Craig Robinowitz na penzi la kahaba mcheza uchi..! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kisa cha Craig Robinowitz na penzi la kahaba mcheza uchi..!

Discussion in 'Mahusiano, mapenzi, urafiki' started by Mtambuzi, Jul 13, 2012.

 1. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #1
  Jul 13, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  [​IMG]

  Craig Robinowitz


  [​IMG]

  Stefanie Robinowitz

  [​IMG]

  Shannon Reinhart "Sammer" kahaba mcheza uchi aliyesimama mbele kabisa

  [​IMG]

  Craig Robinowitz na mkewe Stefanie


  Majira ya usiku wa manane siku ya Jumanne ya April 30, 1997 katika wilaya ya Montgomery Pennsylvania nchini Marekani simu ya dharura ya 911 ilipigwa na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Craig Robinowitz. Akiongea kwa sauti ya kutetemeka alisema kwamba amemkuta mkewe akiwa amelala hajitambui kwenye hodhi la kuogea bafuni (Bathtab), na akadai kwamba hahusiki kwa namna yoyote na tukio hilo.

  Baada ya dakika tano ofisa wa Polisi aitwae James Driscoll alifika katika nyumba ya kifahari ya Craig. Akionekana kuchanganyikiwa Craig alimpeleka ofisa huyo wa Polisi hadi ghorofani kilipo chumba chao cha kulala na kuingia naye hadi bafuni ambapo alimkuta mke wa Craig aitwae Stefanie Robinowitz 29, akiwa bado amelala kwenye hodhi la kuogea bafuni akiwa bado hajitambui.Ofisa huyo alisaidiana na Craig kumnyanyua mkewe na kumtoa ndani ya hodhi hilo ambapo alijaribu kumpa huduma ya kwanza kwa kumpulizia hewa mdomoni (Cardiopulmonary resuscitation (CPR)). Muda mfupi baadae gari la kubebea wagonjwa liliwasili na kumchukua Stefanie kumuwahisha hospitali ambapo alipofikishwa ilitangazwa rasmi kwamba amefariki.

  Craig aliwaambia Polisi kwamba siku hiyo alikuwa hapo nyumbani na mkewe pamoja na mtoto wao wa kike mwenye umri wa mwaka mmoja aitwae Ruth. Ilipofika saa 5:30 usiku, mkewe alikwenda bafuni kuoga. Baada ya kuda mfupi alisikia kishindo kikitokea kule ghorofani alipokuwa mkewe, lakini hakutilia maanani. Baada ya dakika ishirini alishangaa kuona mkewe hatoki huko bafuni alikoenda. Aliamua kumfuata ambapo alimkuta mkewe akiwa amelala katika hodhi la kuogea kichwa kikiwa kimezama majini na alikuwa hajitambui.

  Craig alidai kwamba alishikwa na mshtuko kiasi cha mwili wake kufa ganzi. Alimnyanyua mkewe kutoka katika hodhi hilo la kuogea na kumuegemeza. Alidai kwamba alikaa hapo bafuni kwa dakika kadhaa ndipo akapiga simu ya dharura na kisha akashuka sebuleni kufungua mlango wa mbele kwa ajili ya kuwasubiri watu wa huduma ya dharura. Alirudi bafuni ambapo alimshililia mkewe kichwani ili asizame mpaka ofisa wa Polisi alipofika.

  Maelezo ya Craig yalitiliwa mshaka na maofisa wa Polisi lakini ilibidi isubiriwe taarifa ya uchunguzi wa madaktari ili kujua chanzo cha kifo cha mkewe.

  Taarifa ya uchunguzi wa mwili wa Stefanie ilionyesha kwamba hakufa kwa kuzama kwenye maji kama alivyoeleza Craig bali kwa kunyongwa. Kwa kifupi taarifa hiyo ilibainisha kwamba aliuawa. Craig afisa mauzo aliyejiajiri, alikuwa bado ni kijana mbichi aliyekuwa na umri wa miaka 33 wakati huo. Baada ya uchunguzi wa awali, alikamatwa na kufikishwa katika kituo cha Polisi cha Lower Merion kwa mahojiano kuhusiana na kifo cha mkewe. Katika mahojiano hayo Craig alijieleza kwa kirefu kwamba hahusiki kwa namna yoyote na kifo cha mkewe.

  Ofisa wa Polisi aliyehusika na mahojiano hayo aliwaambia wandishi wa habari kwamba waliongea na Craig kama marafiki. "Tuliongea naye kama tunavyoongea na marafiki zetu na majirani zetu, kwa kifupi yalikuwa ni mazungumzo ya kawaida sana." Alisema makamu mwanasheria wa wilaya aitwae Bruce Castor. Polisi pia walifanya uchunguzi katika nyumba ya Craig mara kadhaa.

  Siku tatu baadaye Craig alikamatwa na kushitakiwa kwa kosa la kumuua mkewe na kuwahadaa Polisi. Akizungumza na wandishi wa habari mwanasheria wa wilaya Mishael D Morino alisema, hakuna shaka yoyote kwamba, Stefanie Robinowitz ameuawa. Kisha akaendelea……..

  "Kulikuwa na watu watatu tu katika nyumba ile, Bwana Craig, Bi, Stefanie na binti yao wa mwaka mmoja. Milango yote ilikuwa imefungwa na hakuna mtu aliyeingia katika nyumba hiyo. Kwangu mimi ninavyoliangalia tukio hili, ushahidi wote unamuelemea yeye (Craig Robinowitz). Alimnyonga na kumuweka kwenye hodhi la kuogea ili kuishawishi dunia iamini kwamba mkewe alikufa kwa ajali ya kuzama katika Hodhi hilo la kuogea."

  Mwanasheria huyo alibainisha kwamba, Stefanie alikuwa na michubuko katika mwili wake inayoonyesha kwamba aliburuzwa baada ya kuuawa na kutumbukizwa kwenye hodhi la kuogea. Pia alibainisha kwamba mwili wa Stefanie ulikutwa kwenye hodhi hilo ukiwa na saa ya dhahabu mkononi na vidani vya dhahabu shingoni……

  "Tunaamini kwamba hakuna mtu anayeweza kuoga kwa mtindo huo" Alisema mwanasheria huyo…..

  Morino alisema kwamba, sababu (Motive) ya mauaji hayo ni kutaka kujinufaisha kifedha na alibainisha kwamba Stefanie Robinowitz alikuwa amekata bima ya maisha thamani ya dola 1.5 Milioni wiki nne kabla ya kifo chake na aliyetajwa kunufaika na bima hiyo pindi akifa ni mumewe Craig Robinowitz. Morino aliendelea kusema kwamba kuna maoni kwamba Craig alikuwa amekumbwa na mgogoro wa kifedha, lakini bado hawajathibitisha tuhuma hizo.

  Taarifa hiyo ya Craig kutajwa kuhusika na mauaji ya mkewe kwa kumnyonga zilipokelewa kwa mshtuko na marafiki zao pamoja na wafanyakazi wenzao. Wanandoa hao vijana walikuwa wanapendana kiasi cha kuchukuliwa mfano bora wa ndoa imara ya vijana. Walikuwa wanamiliki nyumba nzuri ya kifahari na ndio walikuwa wamejaaliwa kupata mtoto wao wa kwanza katika ndoa yao.

  "Walikuwa ni wandoa waliopendana na wengi tuliwachukulia kama mfano, na walikuwa wanapenda sana." Alisema Rocky Heller, muuzaji wa nyumba ambaye ndiye aliyewauzia nyumba wanayoishi mwaka 1995 kwa dola 250,000.

  Pia mwanasheria wa familia hiyo Jeffrey Miller alikubaliana na maoni ya Rocky Heller na aliongeza kwamba wanandoa hao walikuwa wanapendana sana kiasi cha kumvutia kila aliyewafahamu. "walikuwa kama wanaishi kwenye dunia yao peke yao kwa jinsi walivyopendana." Alisema Jeffrey.

  Naye bosi wa Stefanie Robinowitz aitwae David Fineman ambaye alikuwa ni meneja na mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo ya Fineman and Bach, inayojihusisha na mambo ya Kisheria ambapo ndipo Stefanie alipokuwa akifanya kazi kama mwanasheria akiongea na waandishi wa habari, alisema, "Stefanie alikuwa ni mmoja wa watu waliokuwa na furaha sijapata kuona. Alikuwa na mwansheria mahiri, mwenye kutumia akili na mchangamfu kwa kila mtu. Alikuwa na mapenzi kwa kazi yake, waumini wenzake anaosali nao na familia yake."

  Maisha ya Stefanie yalionyesha kwamba, alikuwa ni msomi wa sheria akiwa amesoma katika chuo cha Bryn Mawr na baada ya kuhitimu hapo mnamo mwaka 1992 alipata kazi katika kampuni hiyo maarufu ya Fineman and Bach. Maisha ya Craig Robinowitz hayakuonekana kuwa ya wazi sana, na ilionyesha kwamba baadhi ya marafiki zake walikuwa wanajua mengi kuhusu tabia na mwenendo wake. Walikuwa wanajua kwamba alikuwa anaendesha biashara ya jumla nyumbani kwake lakini walikuwa hawajui ni biashara ya aina gani na pia walikuwa wanajua kwamba anajiendeleza kielimu katika chuo kikuu.

  Alikuwa ni mchezaji wa softball katika timu ya Merion Jewish Community na alionekana kupendwa na wachezaji wenzake pamoja na wapenzi wa timu hiyo, kutokana na umbo lake lililojazia kimichezo. Kulikuwa na maoni kwamba hakuwa mkorofi wala mtu wa shari awapo uwanjani, pamoja na kuwa na mwili mkubwa uliojazia kimichezo. Pamoja na maoni hayo yaliyojaa sifa nzuri zinazomhusu Craig, lakini bado Mwanasheria wa wilaya na maofisa wa Polisi wa kituo cha Lower Merion bado waliamini kwamba Craig ndiye mtuhumiwa namba moja wa mauaji ya mkewe. Walianza kuchimba zaidi kuhusu maisha halisi ya Craig, na hatimaye ukweli ulijulikana na nia (Motive) ya mauaji hayo, nayo ilijulikana.

  Picha tofauti kuhusu maisha ya Craig Robinowitz yawekwa wazi.

  Wapelelezi waligundua kwamba, Craig alikuwa katika mgogoro halisi wa kifedha. Alikuwa na mkopo wa nyumba (Mortgage) ambao ulifikia dola 300,000 ukiwepo mkopo wa dola 100,000 ambao aliuchukua wiki mbili kabla ya kifo cha mkewe. Pia kulikuwa na deni dhidi ya biashara yake ambalo lilikuwa halijulikani matumizi yake na zaidi ya hapo pia alikuwa anamiliki zaidi ya dola 30,000 katika kadi yake ya malipo ya American Express na dola 60,000 katika kadi zake za malipo za Visa na Master. Pia kulikuwa na minong'ono kuwa anayo madeni kutoka kwa baadhi ya marafiki zake na ndugu zake. Kwa ujumla Craig alikuwa anadaiwa kiasi cha dola 750,000.

  Wapelelezi wa kesi hiyo walichotaka kujua, inakuwaje Craig awe anadaiwa madeni ya kiasi hicho cha fedha kwa mtu kama yeye asiye na kazi? Pamoja na kwamba mkewe alikuwa anafanya kazi lakini ilikuwa ni kazi ya mkataba na kipato cha mshahara wa mkewe kilikuwa ni dola 30,000 kwa mwaka.

  Haraka sana wapelelezi wa kesi hiyo walipata jibu la swali hilo. Craig Robinowitz alikuwa na matumizi makubwa yaliyotokana na uraibu (addiction). Haikuwa ni madawa ya kulevya, haikuwa ni pombe, na wala haikuwa ni kamari, bali alikuwa ni mpenzi wa vilabu vya wanawake wanaosasambua na kucheza uchi (Strip Clubs), na alikuwa ni mpenzi wa klabu moja maarufu katika mji huo wa Philadephia. Alikuwa ametokea kumpenda mwanamke mmoja katika klabu ambaye alikuwa akipenda sana kumuona jukwaani akisasambua na kucheza uchi.

  Wakati mkewe akifanya kazi kwa nguvu zake zote katika kampuni ya kisheria ili kuboresha maisha ya familia yao, kumbe masikini hakujua kwamba mumewe kipenzi alikuwa anatumia muda wake wa mchana kwenye klabu hiyo ghali ya wanawake wasasambuaji na wacheza uchi inayojulikana kwa jina la Delilah Dean ambayo ipo katika mji wa Philadephia akitumia mamilioni ya fedha kwa kumhonga mwanamke msasambuaji na mcheza uchi aitwae Shannon Reinhart maarufu kwa jina la "Summer."

  Chanzo kimoja kilibanisha kwamba, kwa takriban miezi sita kabla ya mkewe hajafariki Craig Robinowitz alikuwa anatumia muda wake mwingi wa mchana katika klabu hiyo na alikuwa akisisitiza mwanamke huyo (Summer) ndiye amburudishe kwa kusasambua na kucheza uchi mbele yake.

  Kwa mujibu wa chanzo hicho, Craig alikuwa na kawaida ya kuweka fedha kiasi cha dola 1,000 mpaka 3,000 kwa wiki katika maduka mbalimbali kwa ajili ya manunuzi ya chupi aina ya G-String kwa ajili ya mwanamkie huyo.

  Wapelelez wa Polisi kupitia taarifa za kibenki na kadi zake za malipo walibaini kwamba Craig alikuwa na kawaida ya kuchukua chumba katika Hoteli kubwa zenye hadhi ya nyota tano kwa gharama inayofikia dola 500 lakini alikuwa akitumia chumba hicho kwa masaa kadhaa kisha kurudisha chumba hicho ambacho alikilipia kwa usiku mzima. Walipozungumza na baadhi ya wafanyakazi wa hoteli hizo alizokuwa akizitembelea, wapelelezi hao walibaini kwamba chumba alichokuwa akikilipia Craig kilikuwa kinaonyesha kwamba walikuwa wako wawili, lakini huyo mtu wa pili hakuweza kutambuliwa, ingawa hata hivyo ilibanika kwamba huenda akawa ni Shannon Reinhart (Summer) lakini alipoulizwa alikanusha kuwahi kufanya mapenzi na Craig.

  Je fedha hizi ambazo Craig alikuwa akizitapanya alikuwa anazipata wapi?

  Wakati Polisi wa upelelezi walipokuwa wakifanya uchunguzi nyumbani kwa Craig waligundua kitabu cha kutunzia kumbukumbu za hesabu maarufu kama Ledger Book. Awali hawakuelewa zile hesabu zilizoandikwa zilizokuwa na maana gani, lakini baadae walikuja kugundua kwamba Craig alikuwa anajishughulisha na mchezo wa upatu maarufu kama Ponzi Scheme.

  Kwa mujibu wa askari hao upelelezi, walibaini kwamba, Craig alikuwa anakopa pesa kutoka kwa marafiki zake na baadhi ya ndugu zake kwa maelezo kwamba anataka kuwekeza katika biashara na alikuwa akihidi kulipa kwa riba.

  Alikuwa akilipa deni la awali ikiwemo na riba kwa kutumia mkopo kutoka kwa mtu mwingine. Na ili kulipa deni lingine alilokopa alikuwa anakopa tena kwa mtu mwingine na kulipa deni hilo na hivyo kujenga uaminifu, na mduara huo wa kukopa kiasi kikubwa cha fedha kutoka sehemu moja ili kulipa deni analodaiwa na kubaki na kiasi fulani cha fedha kwa matumizi yake ya anasa kilikuwa kinaendelea na kuendelea na kuendelea………

  Hata hivyo Craig aliwaonya hao rafiki zake na ndugu zake aliokuwa akiwakopa wasimweleze mkewe kwa sababu alitaka mkewe amuone kuwa ni mhangaikaji na mchapa kazi wa kutafuta pesa kwa ajili ya familia.
  kutokana na kazi aliyokuwa akifanya mke wa Craig, Stefanie Robinowitz kuwa ya heshina na yenye kulinda maadili katika jamii, lakini pia alikuwa na uelewa wa kutunza hesabu na kusimamia matumizi sahihi ya mapato ya familia, Askari hao wa upelelezi walijenga nadharia kwamba, huenda Stefanie angemuacha na kuondoka na mwanae kama angegundua juu nya utapeli aliokuwa akifanya mumewe, wa kuchukua fedha kutoka kwa ndugu na marafiki zake.

  Askari hao pia waligundua kwamba Craig alikuwa amefikia katika kiwango cha juu cha madeni na uwezo wa kuendelea na mchezo ule ulionekana kufika ukingoni, na hapo kulikuwa na dalili zote za mkewe kuujua ukweli kuhusu mchezo huo mchafu aliokuwa akiucheza mumewe aliyempenda sana……………

  Muda ulikuwa ukienda na Craig alikuwa anahitaji fedha kwa ajili ya kulipa madeni hayo na kuondokana na fedheha. Kulikuwa na eneo moja tu ambalo ndilo lingeweza kumpatia fedha za kutosha na kuondokana na mzigo huo wa madeni na kubakiwa na ziada ambayo ingemuwezesha kuishi maisha ya kifahari, nayo haikuwa nyingine isipokuwa ni malipo ya bima ya maisha.

  Akiandika hati ya kukataa dhamana ya Craig kwenda katika mahakama, mwanasheria wa wilaya alidai kwamba, wamekuta ujumbe wa simu ya mkononi ya Craig kutoka kwa mwanamke huyo mcheza uchi muda mfupi tu baada ya Stefanie Robinowitz kufariki. Katika hati hiyo mwanasheria huyo wa wilaya alibainisha pia kwamba, Craig alitembelea klabu hiyo ya Delilah Dean siku moja baada ya kifo cha mkewe na alimwambia "Summer" kwamba mkewe amefariki baada ya kulala kwenye hodhi la kuogea (Bathtub).

  Hati hiyo pia ilibainisha kwamba, Shannon Reinhart (Summer) alikiri kupokea zawadi nyingi kutoka kwa Craig zikiwemo vito na samani za ndani zenye thamani ya zaidi ya dola 3,000 kutoka duka moja maarufu linalojulikana kwa jina la Seaman Department Store.

  "Craig Robinowitz alikuwa amechanganyikiwa kutokana na madeni hayo," aliandika mwanasheria huyo wa wilaya.

  "Deni lake lilimfikisha mahali ambapo alikuwa na uchaguzi wa mambo mawili……. aidha aieleze familia yake na marafiki zake kwamba maisha yake yalitawaliwa na udanganyifu na ulaghai, au kumuua mkewe na kujipatia mamilioni ya dola kutokana na bima ya maisha aliyomkatia mkewe. …….Chaguo la pili lilikuwa ndio muafaka kwake kwa sababu baada ya malipo ya bima ambayo ngeyapata baada ya kifo cha mkewe angeweza kuishi maisha ya anasa na mwanamke msasambuaji na mcheza uchi (Summer) aliyempenda sana. Ilikuwa ni katika jitihada zake za kutaka kuweka mazingira mazuri kwa maisha yake ya baadae na kusahau maisha yake ya nyuma yaliyotawaliwa na madeni…………. Kifo cha mkewe hakikusababishwa na ajali……… yalikuwa ni mauajia ya kupangwa, na aliyapanga mauaji hayo siku chache zilizopita au wiki kadhaa zilizopita."

  Ilisema sehemu ya hati hiyo aliyoiandika mwanasheria huyo wa wilaya.

  Pamoja na hati hiyo ya kupinga Craig kupewa dhamani, hata hivyo Mheshimiwa Jaji wa mahakama ya Montgomery Samuel Salus alikubali Craig aweke dhamana ya dola milioni tano kiasi ambacho Craig hakukimudu na hivyo dhamana yake kufutwa.

  Askari wa upelelezi waligundua kwamba, Craig na mkewe Stefanie siku za karibuni kabla ya kifo cha mkewe walipata tatizo la kukosa usingizi (Imsomnia) tataizo ambalo liliwalazimu waende hospitalini ambapo walipewa dozi ya dawa ambayo ingewasaidia kupata usingizi iitayo Ambien.

  Jioni ya April 28, 1997 baada ya kupata chakula cha usiku wakiwa pamoja na wazazi wa Stefanie ambao waliwaalika hapo nyumbani kwao, Craig alimuwekea mkewe vidonge vitatu vya dawa hiyo ya usingizi katika kinywaji chake, na baada ya mkewe kupitiwa na usingizi mzito alitumia muda huo kumnyonga.

  Askari hao wa upelelezi walijenga nadharia kwamba, Craig alikuwa ana uhakika wa kujinasua katika tuhuma za kuhusishwa na mauaji ya mkewe kutokana na mambo ya fuatayo:

  1. Taarifa kwamba mkewe amekufa kwa ajali ya kuzama kwenye Hodhi la kuogea haitatiliwa mashaka

  2. Umaarufu wake na muonekano aliojijengea kwa marafiki zake na familia kwamba, ni baba mzuri mwenye kujali familia ungeweza kuondoa kabisa hisia katika jamii iliyomzunguka kuhusishwa na mauaji ya mkewe

  3. Mila na desturi zao za Ki-Jewish zinazotaka mwili wa mtu aliyekufa kuzikwa haraka pasipo kucheleweshwa, ingeweza kumnusuru na uchunguzi wowote wa maiti kwa sababu kifo cha mkewe kingeonekana ni cha ajali tu ya kuzama kwenye hodhi la kuogea…………….

  Pamoja na Craig kupiga mahesabu yake kwa umahiri mkubwa, lakini alisahau kuhusu uchunguzi wa kitabibu ambao kwa mujibu wa sheria ni lazima ufanywe pale inapotokea kifo cha kijana wa umri wa kati ambaye kifo chake kinaonekana kutokuwa ni cha kawaida, bila kujali matakwa ya dini au mila na desturi za mtu huyo.
  Kutokana na ushahidi kuwa wazi, kesi yake haikuonekana kuwa ngumu kusikilizwa na kufikia uamuzi. Kwa kulijua hilo Craig Robinowitz hakukana mashitaka. Alikiri wazi mbele ya jaji na jopo lake la washauri kwamba ni kweli alimuua mkewe. "Nilikuwa nimepoteza mawasiliano kiakili na kukosa uwezo wa kutotambua lipi baya na lipi zuri…." Alitumia muda wa dakika 15 kuelezea ni kwa kiasi gani alikumbwa na jinamizi la kifo cha mkewe tangu alipotekeleza mauaji hayo.

  Kesi hiyo haikuchukua muda mrefu kusikilizwa kwake. Mnamo Octoba 30, 1997 Craig Robinowitz alihukumiwa kifungo cha maisha jela bila uwezekano wa kufungwa kifungo cha nje (Parole).

  Craig Robiniwitz anatumikia kifungo chake katika gereza la SCI lililopo katika mji wa Houtzdale katika jimbo la Pennsylvania akiwa ni mfungwa mwenye namba DL 1960.
   
 2. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #2
  Jul 13, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Leo tena.......... Ni ijumaa nyingine kama kawaida nimekuja na kesi hii iliyowahi kutokea nchini Marekani. Ni kesi ambayo inasisimua na inafundisha, lakini pia inasikitisha kwa kifo cha mama huyu aliyeuawa na mumewe aliyempenda na kumuamini.
  Fedha.... hapa inaonekana fedha ndio iliyosababisha umauti wa mama huyu, lakini kibaya zaidi fedha hizo zinatafutwa kwa ajili ya mwanaume kutimiza haja yake ya uraibu aliyo nao wa vilabu vya wanawake wacheza uchi........
  Unaweza kujiuliza inakuwaja mambo haya, lakini naomba ufahamu kwamba wengi tunaumwa, tena sana na tuna maudhaifu ambayo kwa kweli mwisho wake hutuletea maumivu makubwa sana............

  Tutafute tiba..............................!
   
 3. fazaa

  fazaa JF-Expert Member

  #3
  Jul 13, 2012
  Joined: May 20, 2009
  Messages: 2,986
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 0
  Afadhali ulipo toa comment hii ndo nimeweza kuelewa mana usinge kuja na point hii nisinge soma.

  Ijumaa kareem time ya kwenda msikitini kusali.
   
 4. Neiwa

  Neiwa JF-Expert Member

  #4
  Jul 13, 2012
  Joined: Feb 17, 2012
  Messages: 730
  Likes Received: 44
  Trophy Points: 45
  Dunia inatisha sana sasa hivi, unaishi na mwenza wako ukidhani wamjua kumbe hata chembe hujui. Wana bahati wa zamani walikuwa wakioana kwa ukoo na kujua huyo mtu roots na tabia za majumbani. Sie tunaokutana mijini, club, vyuoni na makazini Mungu tu atulinde. Ni mtihani kwa kweli. Na hizi bima za vifo hizi za kungalia sana, ni hatari aisee...
   
 5. Mama Stan

  Mama Stan Member

  #5
  Jul 13, 2012
  Joined: Apr 17, 2010
  Messages: 87
  Likes Received: 43
  Trophy Points: 25
  Mmh hiki kisa kinasikitisha..! Kweli moyo wa mtu ni kiza kinene...hausomeki.
   
 6. Gamaha

  Gamaha JF-Expert Member

  #6
  Jul 13, 2012
  Joined: Jul 17, 2008
  Messages: 2,695
  Likes Received: 753
  Trophy Points: 280
  Mkuu Mtambuzi ilibaki kidogo nikuulizie kuhusu kisa cha ijumaa ya leo, naona umeisha weka ahsante ngoja sasa nikisome kwa utulivu
   
 7. Blaine

  Blaine JF-Expert Member

  #7
  Jul 13, 2012
  Joined: Jan 11, 2012
  Messages: 2,285
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 0
  habari nzuri yenye somo. big up Mtambuzi
  Neiwa hii ilitokea 1997, so ni zamani kidogo
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 8. Paloma

  Paloma JF-Expert Member

  #8
  Jul 13, 2012
  Joined: Jan 22, 2008
  Messages: 5,341
  Likes Received: 16
  Trophy Points: 135
  Kisa kinasikitisha sana kwa kweli.
  Najiuliza ni wangapi waliopo katika ndoa wanaoutumika mradi kunufaisha wenza wao...pasipo kujua pesa hizo zinatumikaje.....ni wengi aisee!!!

  Mtambuzi, heko na shukrani kwako, nimeongeza msamiati....uraibu = addiction!!!
   
 9. Blaki Womani

  Blaki Womani JF-Expert Member

  #9
  Jul 13, 2012
  Joined: Feb 28, 2011
  Messages: 8,460
  Likes Received: 3,715
  Trophy Points: 280
  kisa kinasikitisha......unamwamini mtu lakini yeye yupo kinyume nawe yaliyopo moyoni mwa mtu ayajua mwenyewe...... usiuseme moyo wa mtu
   
 10. NATA

  NATA JF-Expert Member

  #10
  Jul 13, 2012
  Joined: May 10, 2007
  Messages: 4,516
  Likes Received: 16
  Trophy Points: 135
  Thanks Mtambuzi Kwakweli hivi visa vinasikitisha sana

  Huu ni ubinafsi wa hari ya juu.
  Huyu baba alikuwa mbinafsi mkubwa.

  Na hivi ndivyo wanaume wengi walivyo, kupenda chupi wako radhi kudhuru wale watu wanaowa thamini na kuwapenda hasa wake zao.
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 11. NATA

  NATA JF-Expert Member

  #11
  Jul 13, 2012
  Joined: May 10, 2007
  Messages: 4,516
  Likes Received: 16
  Trophy Points: 135
  Mtambuzi huyu ni ndugu ya RA mbona wanafanana sana?
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 12. Katavi

  Katavi Platinum Member

  #12
  Jul 13, 2012
  Joined: Aug 31, 2009
  Messages: 39,474
  Likes Received: 4,134
  Trophy Points: 280
  Inasikitisha sana, kweli moyo wa mtu haueleweki.
   
 13. Katavi

  Katavi Platinum Member

  #13
  Jul 13, 2012
  Joined: Aug 31, 2009
  Messages: 39,474
  Likes Received: 4,134
  Trophy Points: 280
  Ha ha ha haaah!! NATA bwana, kwanza huyo mtu siku hizi yupo wapi??
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 14. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #14
  Jul 13, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Wanasema duniani wawili wawili, mbona wewe unafanana sana na naniliu........................! LOL
   
 15. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #15
  Jul 13, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Kuna kitu wenzetu wazungu wanaita obsession......nimejaribu kutafuta neno hilo kwa kiswahili lakini nimelikosa
  Hali hiyo ya obsession ndiyo iliyomkuta huyo bwana, yaani alimpenda mwanamke mcheza uchi kupita kiasi mpaka akajikuta anapoteza uwezo wa kiakili unaomuwezesha mtu kutenganisha baya na zuri..........
  Huu ni ugonjwa wa kisaikolojia na wataalamu wanakiri kwamba una tiba. Kama mtu akijijua ana hali hiyo kisha akahitaji msaada wa kisaikolojia, basi anaweza kutibiwa na kupona kabisa.
  Kwa hapa kwetu tatizo hilo lipo sana sema tu halizungumziwi na kama watu watalizungumzia basi itahusishwa na ushirikina. haiyumkini kile tunachoita LIMBWATA huenda ikawa ni tatizo hilo.......................
  Unakuta mwanaume anampenda mwanamke na kuitelekeza familia yake kwa sababu tu ya hawara, na anaweza kufikia kuuza vitu vyake vya thamani na hata nyumba ili kumridhisha hawara yake, lakini watu watadai kwamba kapewa limbwata, kumbe sio kweli ni kupagawishwa na mihemko ya kimapenzi tu.
  Wanawake nao pia wanaweza kutokewa na hali hiyo.............
  Unaweza kukuta mwanamke anaye mpenzi wake lakini akageuka kuwa mtumwa hasa wa mapenzi, yuko tayari kufanya lolote ilimradi amridhishe mpenzi wake huyo na mwisho wa siku yeye ndiye huumia.
   
 16. vanmedy

  vanmedy JF-Expert Member

  #16
  Jul 13, 2012
  Joined: Oct 12, 2011
  Messages: 2,245
  Likes Received: 176
  Trophy Points: 160
  so saaaad....
   
 17. NATA

  NATA JF-Expert Member

  #17
  Jul 13, 2012
  Joined: May 10, 2007
  Messages: 4,516
  Likes Received: 16
  Trophy Points: 135
  Mtambuzi na hapa kwetu ogonjwa huu uwapata sana wanaume wastaafu na vijicent vyao kwanini?
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 18. Ruttashobolwa

  Ruttashobolwa JF-Expert Member

  #18
  Jul 13, 2012
  Joined: Feb 22, 2012
  Messages: 43,747
  Likes Received: 12,839
  Trophy Points: 280
  Mapenzi na pesa ni mambo hatari sana. Yana fanya mtu ana kosa hutu na kumu ua mke wako! Ina sikitisha sana,binadamu tuna kuwa wadhaifu linapo kuja swala la pesa.
   
 19. kamwendo

  kamwendo JF-Expert Member

  #19
  Jul 13, 2012
  Joined: Apr 19, 2012
  Messages: 404
  Likes Received: 268
  Trophy Points: 80
  Nakubaliana nawe Mtambuzi hiyo inawezekana ni Obsession aka limbwata...ila kisa kinasikitisha kwa kweli sijui nani alibuni pesa,imeniuma kwa kweli mwenzako anajitahidi kufanya kazi kwa bidii ili mpate fedha ya kuitunza familia wewe unafanya upumbavvu kwa kutawanya pesa hovyo...sijui inakuwaje mpaka mtu unakuwa na usaibu wa kupenda wanawake kiasi hiki mpaka unashindwa kutambua unachokifanya.....kwel binadamu si wa kuaminiwa.
   
 20. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #20
  Jul 13, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Kuna kisa nitakiweka hapa siku zijazo cha mwanaume mmoja aliitelekeza familia yake ikiwa ni miaka mitatu tu tangu afunge ndoa kwa sababu ya hawara, tena na mateso juu mpaka mkewe akajinyonga kutokana na sononi......... hiyo ni obssesion tu
   
Loading...