Wa kijiji una mambo,kwa mzee wa makamo
Au niseme mtambo,wangu huu msimamo
Bwana Joni wa kitambo,si enzi tu za kilimo
Ukijua jina lake,waijua siri yake
Huna haja kuwazua,ukafanya mashindano
Huitaji pekechua,sikiza yake soprano
Wadada waigundua,hata katika maono
Mkasi wake mdomo,na kichwa chenye ujazo
Jibu nimelisikia, rafiki mpendwa Suki,
Bw. Joni atishia, utadhania fataki,
Wengine atutambia, ayeya kama hataki,
Kama jinale ni siri, si kinyozi, kinyonyozi!
Atufunze na wengine, hicho anachonyonyoa,
Kweupe tena saa nane, Joni ati ananyoa,
Fundi mwingine nene, mbona sina cha kunyoa!
kama jinale ni siri, si kinyozi, kinyonyozi!
Tuwashauri wa dada, wamejaa kijijini,
Vinyozi wasio ada, na mikasi mikononi,
Wananyoa na ziada, akili himo kichwani,
Kama jinale ni siri, si kinyozi, kinyonyozi!