singidadodoma
JF-Expert Member
- Nov 11, 2013
- 4,394
- 1,536
BALOZI wa Uingereza nchini Tanzania, Diana Melrose amekubali kutoa msaada wa magari 34 ya kubeba wagonjwa kwa hospitali na zahanati zilizopo wilaya ya Kinondoni, kwa lengo la kusaidia utoaji wa huduma za afya.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda kuomba ubalozi huo kuwapatia magari ya kubeba wagonjwa kwa kila kata. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Balozi Melrose alisema wataisaidia wilaya hiyo kutoa vifaa vya kuhudumia wagonjwa ikiwemo magari hayo kwa ajili ya kufanikisha malengo yao ya kutoa huduma bora za afya.
Aliahidi pia kutoa kompyuta zaidi ya 16,000 kwa lengo la kusaidia shule za sekondari za wilaya hiyo ili kila mwanafunzi kuweza kusoma vitabu kupitia mitandao. ‘’Ni mara yangu ya kwanza kutembelea wilaya ya Kinondoni na nimeahidi kutoa magari kwa ajili ya kusaidia kuwabeba wagonjwa,’’ alisema Melrose.
Aidha alisema kuwa kutokana na bomoa bomoa inayoendelea Dar es Salaam, watasaidiana na mkuu wa wilaya hiyo kuhakikisha wanaweka alama katika maeneo hatarishi. Alisema lengo la kuweka alama hizo ni kusaidia wananchi waweze kuepuka kujenga nyumba katika maeneo ambayo ni hatari kwa maisha yao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Makonda alisema kuwa moja ya mikakati yake ni kuhakikisha kwamba anakutana na mabalozi wote ili kutathimini namna ya kuwasaidia wakazi wa Kinondoni.