- Source #1
- View Source #1
JamiiCheck imefuatilia hotuba iliyotolewa na Stephen Wasira akiwa kwenye mkutano wa kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa mkoani Mwanza tarehe 26-11-2024 ambapo mbali na mambo mengine alisema kuwa Serikali katika awamu hii sita ilinunua magari ya wagonjwa 528, lakini pia CHADEMA ilijipanga kusimamisha wagombea kwa 85% mijini na 60% vijijini.
- Tunachokijua
- Stephen Masato Wasira amekuwa mbunge wa jimbo la Bunda, lakini pia amewahi kuwa waziri wa wizara mbalimbali katika vipindi tofauti tofauti. Akiwa katika mkutano wa kampeni ya wagombea wa serikali za mitaa mwaka 2024 mkoani Mwanza, Wasira alipata nafasi ya kuhutubia wananchi waliokuwepo katika eneo hilo.
Mkutano huo ulikuwa ni wa kufungia kampeni ambao ulifanyika tarehe 26-11-2022 siku moja kabla ya uchaguzi wenyewe uliokuwa umepangwa kufanyika 27-11-2024. Wasira alizungumza na wananchi kwa ajili ya kuwaombea kura wagombea ambapo alizungumza mambo mbalimbali ikiwemo takwimu ya vitu vilivyofanywa na Serikali.
Madai ya magari mapya ya kubebea wagonjwa 528
Wasira alidai kuwa katika uongozi wa Rais Samia magari mapya ya kubebea wagonjwa 528 yalinunuliwa.
Ufuatiliaji umebaini kuwa madai haya ni ya kweli, ambapo Waziri wa nchi ofisi ya Rais TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa aliyakabidhi magari hayo 528 kwa wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mchengerwa alisema kuwa “Leo Mheshimiwa Rais ameridhia kutoa takriban bilioni 52.06, kiwango hiki cha fedha kimenunua takriban magari 528”
Tukio hilo lilitokea kwenye viwanja vya bunge tarehe 10-11-2023, tazama hapa.
Madai ya CHADEMA kuwa na malengo ya kusimamisha wagombea mijini kwa asilimia 85%
Stephen Wasira kwenye hotuba yake alieleza kuwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa ilikuwa na malengo ya kusimamisha wagombea kwa asilimia 80 mjini na asilimia 60 kwa vijijini.
JamiiCheck imefuatilia madai haya na kubaini kuwa ni ya kweli, kwa mujibu wa mkutano alioufanya na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe alieleza kuwa malengo yao kama chama katika uchaguzi wa serikali za mitaa kama wasingeenguliwa kwa upande wa mijini walipanga kuwa na asilimia 85 na kwa upande wa vijijini walipanga kuwa na asilimia 60.
Ushahidi wa alichokisema Mbowe upo hapa kuanzia dakika ya 44.
Madai ya Rais kuwa na mamlaka ya kusamehe wafungwa wliohukumiwa kunyongwa
Stephen Wasira alieleza pia kuwa ukihukumiwa kufungwa ama hata ukihukumiwa kunyongwa Rais ana mamlaka ya kusema nimekusamehe.
Jamiicheck imefuatilia madai hayo na kubaini kuwa ni kweli Rais ana mamlaka ya kusamehe wafungwa wa aina mbalimbali ikiwemo waliohukumiwa kifo kwa mamlaka aliyopewa na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria ya masuala ya Rais (Presidential affairs act).
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, Ibara ya 45(1)(a) inampa Rais mamlaka ya kutoa msamaha (Prerogative of Mercy) kwa mtu yeyote aliyetiwa hatiani na mahakama kwa kosa lolote. Lakini msamaha huo unatakiwa kutolewa kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizowekwa, Sheria ya Presidential Affairs Act (Sheria ya Masuala ya Rais), Kifungu cha 3, kifungu kidogo cha 3 kimetoa mwongozo kwamba;
Iwapo mtu yeyote amehukumiwa kifo, Rais ataitisha ripoti na mwenendo wa kesi ulivyoandikwa na jaji au hakimu wa kesi hiyo, pamoja na taarifa nyingine yoyote iliyopatikana kutoka kwenye kumbukumbu za kesi au sehemu nyingine yoyote anapoweza kuhitaji, ili izingatiwe katika kikao cha Kamati ya Ushauri; na baada ya kupokea ushauri wa Kamati, Rais ataamua kwa uamuzi wake mwenyewe iwapo atumie mamlaka yake chini ya kifungu cha 45 cha Katiba au la.