Kingine cha zaidi kuhusu hayati Edward Ngoyai Lowassa

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,118
Ningependa kuzungumzia Edward Ngoyai Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu aliefariki dunia leo Februari 10, 2024.

Nimekaa nikawaza naandika nini kuhusu Edward Lowassa ambacho umma wa Watanzania hawaujui? Naelezea nini kipya kuhusu kada mkubwa wa CCM ambae akageuka na kuwa tishio kubwa la kumaliza utawala wa chama alicho saidia kukijenga?

Nasema nini kipya kuhusu Waziri Mkuu aliekua na ushawishi mkubwa kuliko Waziri Mkuu mwingine yoyote ukimuacha Nyerere? Sijui kama nitaandika kitu kipya ila natumai nitaandika kitu kitakacho tufanya tujadili legacy ya mwamba huyu wa siasa kwa upana wake.

Maisha ya kiutumishi ya Edward Lowassa yanaweza kugawanyika katika sehemu kuu tatu, utumishi wake jeshini, utumishi wake ndani ya CCM na utumishi wake ndani ya serikali.

Na mwisho kabisa tunaweza zungumzia kipekee 2015, mwaka ambao Edward Lowassa alitikisa siasa za Tanzania na kupelekea kampeni za chaguzi zilizokua na msisimko kuliko zote zilizo wahi kutokea.

Edward Lowassa alipata kuwa Afisa Mwanafunzi Kundi la Nane (Intake 08) mwaka 1978 katika kilichokuwa kinaitwa Chuo cha Taifa cha Uongozi (CTU), Wilaya ya Monduli. Alipata Kamisheni ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania mwaka huo huo 1978.

Akiwa jeshini alitumikia akiwa na wanasiasa wengine wakogwe Jakaya Kikwete na Abdulrahman Kinana (kumbukeni kauli ya "hatukukutana njiani").

Akiwa Luteni, Edward Lowassa alishiriki kikamilifu Vita vya Kagera akiwa 206 KV (Kundi la Vikosi) chini ya Brigedia Jenerali Silas Mayunga. Baadaye Kundi la Vikosi 206, liliongezewa nguvu maradufu na kupewa jina la Task Force, likiongozwa na Meja Jenerali Silas Mayunga.

Ni Task Force hii iliofanikiwa kukomboa maeneo yote Magharibi ya Uganda hadi kuukamata mji wa Koboko uliopo mpakani mwa Uganda na Sudani Kusini, alikozaliwa Iddi Amin.

Mara Baada ya Kumaliza Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam aliajiriwa na CCM kama Katibu Msaidizi na baadaye Katibu wa Wilaya. Alipata kuwa msaidizi wa Mzee Rashidi Mfaume Kawawa, Daudi Mwakawago na Horace Kolimba.

Edward Lowassa aliingia katika siasa za serikali mwaka 1985 alipoteuliwa kuwa Mbunge kupitia Umoja Wa vijan UVCCM sambamba na Anne Makinda na Jenerali Ulimwengu akiwa na umri wa miaka 32 tu.

Akiwa bado mbunge, mwaka 1989 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Cha Arusha (AICC) ambako alihudumu hadi mwaka 1990 alipochaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Monduli hadi alipo staafu 2015.

Baada ya kushinda kura za ubunge, aliteuliwa kuwa Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, akishughulikia Mahakama na Bunge kuanzia mwaka 1990 hadi 1993. Baadaye, aliteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Mijini kuanzia mwaka 1993 hadi 1995.

Mwaka 1995, Edward Lowassa aliamua kujihusisha katika mchakato wa kutafuta mgombea urais kupitia chama cha CCM.

Wakati huo, aliombwa na Umoja wa Vijana kupitia kikao cha Baraza Kuu la Taifa achukue fomu, akiwa miongoni mwa wanachama wanne wa CCM ambao vijana waliamini wangesaidia taifa kufanya maendeleo ya haraka kuelekea ustawi endelevu.

Wengine walio ombwa ni Salim Ahmed Salim, Laurance Gama, na Jaji Mstaafu Mark Bomani.

Edward Lowassa alikua kati ya wagombea 11 wa kito cha uraisi kupitia CCM. Aliposhindwa kufika hatua ya tatu bora akaamua kumuunga mkono kijana mwenzie Jakaya Mrisho Kikwete (nakumbusha tena kauli ya "hatukukutana njiani").

Na ni katika kipindi hichi jina la Boys To Men lilipo anza kutumika. Edward Lowassa alirudi kwa makundi mbalimbali wakiwemo vijana wa CCM ambao walihoji kwa nini ameenguliwa, na yeye kwa unyenyekevu kwa CCM aliwataka vijana na viongozi wengine waheshimu maamuzi ya chama na kumuunga mkono Kikwete.

Tetesi zinasema kwenye uchaguzi wa uraisi CCM, uongozi uliamua kuwa katika majina matatu yatapelekwa majina ya mzee mmoja (Cleopa Msuya), mtu mzima mmoja (Benjamin Mkapa) na kijana mmoja (Jakaya Kikwete).

Moja ya tetesi za kukatwa kwa jina la Edward Lowassa ilikua minong'ono ya wanachama waliokua wanahoji yeye kupata fedha nyingi katika kipindi kidogo cha utumishi wa umma. Benjamin Mkapa alishinda kinyangayiro na hatimae kuwa rais wa nne wa Tanzania.

Edward Lowassa alihudumu kwenye baraza la mawaziri la Benjamin Mkapa kuanzia mwaka 1997 mpaka 2005.

Mwaka 2005, Edward Lowassa aliamua tena kumuunga mkono Jakaya Kikwete. Edward Lowassa na Jakaya Kikwete pamoja na wakina Samuel Sitta na Bernard Membe waliunda kikundi kilicho kuja kujulikana kama wanamtandao.

Hapa tena kuna tetesi za kisiasa zinao dai kuwa alieahidiwa mwanzo kupewa Uwaziri Mkuu ni Samuel Sitta. Ila matokeo yake Samuel Sitta akawa Spika wa Bunge na Edward Lowassa akateuliwa kuwa Waziri Mkuu, mengine kama wanavyo sema ni historia.

Edward Lowassa alihudumu kama Waziri Mkuu kuanzia 2005 hadi 2008 alipojiuzulu kutokana na skendo ya Richmond. Tarehe 7 Februari 2008, Lowassa alijiuzulu baada ya kushtakiwa kwa kuhusika katika kashfa ya Richmond.

Kamati ya Bunge ilichunguza mkataba kati ya kampuni ya TANESCO na kampuni ya Richmond Development Company LLC kutoka Houston, Texas. Kamati hiyo, iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Harrison Mwakyembe, ilibaini kuwa mkataba huo ulikuwa wa udanganyifu.

Hapa kuna tetesi tena kuwa Edward Lowassa alipo tangaza kuwa kamuandikia barua Rais Jakaya Kikwete kujiuzulu ni kwamba hakuwa ameandika barua hiyo na matarajio yalikua kwamba baada ya kutangaza kujiuzulu rais angetangaza kuto kukubali kujiuzulu kwake.

Wafuatiliaji wengi wa siasa wanaamini siasa za kutafuta uraisi 2015 ndizo zilizo pelekewa Edward Lowassa kuangushiwa jumba bovu la Richmond.

Kama ilivyo tarajiwa na wengi, mwaka 2015 Edward Lowassa akatupa karata zake kuwania uraisi kupitia CCM. Katika hali ilioshangaza wengi, mwanasiasa huyo maarufu na mwenye nguvu ndani ya CCM hakufika hata tano bora.

Hatua hii ikapelekea Sophia Simba, Adam Kimbisa, na Karibu Mkuu wa sasa wa CCM Emmanuel Nchimbi kutoka hadharani na kulalamikia mchakato uliotumika kuengua jina la Edward Lowassa.

Hatimaye ni katika hali ya kushangaza, hayati John Pombe Magufuli akateuliwa kuwa mgombea wa CCM.

Katika tukio lililo tikisa siasa za Tanzania ni kitendo cha Edward Lowassa kuhamia Chadema Julai 2015. Ikumbukwe kwa miaka saba kabla ya hapo, Chadema walikua vinara wa kumuita Edward Lowassa fisadi hali iliopelekea watu wengi kushangazaa na kitendo cha kumpokea na kumteua kuwa mgombea wa urais wao kupitia muungano wa UKAWA.

Sio siri kwamba mchuano kati ya Edward Lowassa na John Magufuli ilikua ndio uchaguzi wa kusisimua kuliko zote kuwahi kutokea. Kwa mara ya kwanza kulikua na hisia kwamba CCM inaweza ikaangushwa.

Wafuasi wa UKAWa waliita kadi za kupigia kura "vichinjio" wakiamini wanaenda kuichinja CCM na kuitoa madarakani. Naamini siongezi chumvi nikisema hakuna mtu mmoja ambae alitishia madaraka ya CCM kama Edward Ngoyai Lowassa na katika mazingira tofauti yawezekana ndie angekua rais wa awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Japo hakushinda uchaguzi huo ila matukio ya mwaka 2015 yalihakikisha kwamba jina la mwanamonduli huyo halitakuja kusahaulika katika historia ya Tanzania.

Pumzika mahali pema peponi, ndugu Edward Ngoyai Lowassa. Sisi wapenzi wa siasa tutaendelea kukuenzi na kujadili mchango wako katika historia yetu.

Ufa ulioweka mwaka 2015 bado unaonekana wazi. Tunasubiri kuona iwapo CCM itajitahidi kuziba ufa huo au upinzani utazidi kuchimba katika ukuta wa madaraka ya CCM. Ingawa tunakuzika ukiwa na bendera ya kijani, wapinzani nao wana sababu ya kukuenzi.
 
Mungu ampumzishe Mzee (Komred) wetu mahala pema anapo stahili (aamina).

Ni Nuru/ tunu ya kiongozi mpambanaji imezima.

R. I. P Lowassa.
 
Back
Top Bottom