Kimya hiki kina mshindo wake mkuu

Kimya hiki kina mshindo wake mkuu

Tumaini Makene

JF-Expert Member
Joined
Jan 6, 2012
Posts
2,650
Reaction score
6,085
Kimya Kimya kina mshindo mkuu, ndivyo wambavyo wavyele;
Kimya chataka kumbuu, viunoni mtatile
Kimya msikidharau, nami sikidharawile;

Kimya kina mambo mbele; tahadharini na kimya.
Kimya ni giza kizushi, kuzukia walewale
Kimya kitazua moshi, moto msiyafumbule;
Kimya kina mshawishi, kwa daima na milele

Kimya kina mambo mbele; tahadharini na kimya.
Kimya vuani maonzi, vuani mato muole;
Kimya kitangusha mwanzi mwendako msijikute

Kimya kina mambo mbele; tahadharini na kimya.

Maneno ya Mshairi Bwana Muyanka bin Haji, kama yalivyonukuliwa kwenye Kitabu cha Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania cha Mwl. Julius Kambarage Nyerere yanasadifu kabisa muktadha wa siasa za mabadiliko (Changement? Kama alivyohoji Prof. Issa bin Mariam kwenye Intellectuals at The Hill) ambazo Tanzania inapitia kwa sasa tunavyoelekea Oktoba 25.

Shairi la Bwana Muyanka bin Haji lingeweza kufanyiwa tafsiri inayokidhi muktadha wa namna ambavyo Watawala walioko madarakani wamekuwa wakichukulia ukimya wa Watanzania kuwa ni amani!

Wakati ukweli ni kwamba ukimya huo umekuwa ukiambatana 'volcano' inayochemka vifuani mwa watu kutokana na madhira ambayo wanatendewa na CCM, hadharani mchana kweupe.

Kushindwa kwa sera, mipango na mikakati ya CCM (kushindwa kuongoza) kumezalisha hii social upheaval inayofukuta mioyoni mwa Watanzania. Ndiyo maana moto wa mabadiliko unawaka kila mahali, kiu ya Wananchi kuipumzisha CCM ni kubwa.

Watanzania wa kila mahali, kila rika, makundi mbalimbali wanachemkwa volcano vifuani mwao. Wanatokotwa. Kufanya mabadiliko ya Utawala ambayo yatatoa fursa ya kubadilisha mifumo inayoatamiwa na CCM huku ikiwa ndiyo msingi wa umaskini, ujinga, maradhi na ufisadi unaozidi kuliteka taifa.

Kutoka Kyerwa ambako wananchi wanadhalilishwa na kutezwa utu wao kwa sababu tu wanapenda CHADEMA na wako tayari kufa wakiunga mkono mabadiliko hadi Mtwara ambako akina mama wajawazito wamepigwa risasi kwa sababu tu wanadai haki ya kunufaika na rasilimali gesi ambayo Mwenyezi Mungu ametujalia.

Volcano inachemka kutoka Ulanga, Kilosa, Mvomero-Morogoro ambako damu ya wakulima na wafugaji wasiokuwa na hatia inamwagika kwa sababu viongozi wa serikali ya CCM wameshindwa kupanga matumizi ya ardhi hadi Kiteto ambako wakati watu wakihitaji sehemu ya kulima na wengine mahali pa kufugia, Kiongozi wa Chama hicho badala ya kutafuta ufumbuzi, alithubutu kuwatenga watu kwenye mistari ya kikabila hadharani mithili ya walivyokuwa wakifanya Intarahamwe kule Rwanda 1994.

Volcano inachemka kutoka Zanzibar ambako vitendo wanavyofanyiwa Watanzania mchana na usiku hadi kwenye vyumba vya habari, havijapewa istilahi ya ugaidi na vyombo vyetu vya dola hadi Nzega Tabora ambako wananchi 'wanaonukia' umaskini wa kutupwa jirani na dhahabu, wameambiwa mgodi wa Resolute umefungwa na madini yamekwisha huku wao wakipigwa mabomu na risasi kila wanapojaribu walau kupata mabaki kwenye mashimo yasiyowezwa kufukiwa, waliyoacha wawekezaji watukuzwa. Matokeo ya uwekezwaji.

Si wakulima na wafugaji tu. Volcano iko kila mahali. Walimu wamechefukwa, madaktari wanawaka, walemavu wako wima, Wanafunzi hawako kimya. Almuradi kila kundi limeguswa na ubovu au kushindwa kwa CCM. Hakuna aliyepona.

Lakini kwa muktadha uliokusudiwa hapa, ukimya aliouzungumzia Muyanka bin Haji nataka kuusadifisha na ukimya wa watu makini wanaojiandaa kuiondoa CCM mwaka huu.

Watanzania, wapenda mabadiliko, wanaowaka tamaa ya ustawi wa nchi hii na watu wake, wanaosumbuliwa na kiu ya kuukomesha huu utawala wa miaka zaidi ya 50 wanahoji mgombea wao atajulikana lini?

Wakati anajiandaa kujiuza kwa sababu atakuwa nazo sifa za uzuri, wapiganaji wana hamu kubwa ya kumsaidia katika hilo. Wana shauku ya kuingia kazini. Wanajisikia wajibu wa kubeba majukumu makubwa ya kuwa sehemu ya historia itakayoandikwa mwaka huu. Wako tayari kuutafuta ushindi. Imani iko juu. Moyo kabla ya silaha.

Walioko jikoni hawaachi kuwasihi wapiganaji kuwa wasichoke kupandisha mori wa kusubiri chakula kinachopikwa kwa ustadi. Waendelee kujiandaa kumuuza mgombea atakayekuwa kiongozi wa kila mtu, Watanzania katika mamilioni. Kimya hiki kama alivyosema Bin Haji, ni kingi na kitakuwa na mshindo mkuu, wambavyo wavyele.

Huyu atakuwa Kiongozi wa nchi si mtu wa kuzunguka zunguka na vitu vidogo kama kutaja idadi ya miradi. Tunao tayari maofisa miradi kuanzia ngazi ya taifa hadi kijiji na Kwenye miradi mahsusi mbalimbali. Hatutafuti hao. Watanzania wanajiandaa kumchangua mtu mwadilifu, anayechukizwa kwa dhati kabisa na maadui wa Taifa hili. Anayetambua kuwa tumekwama. Tunatakiwa kujikwamua na kwamba atakuwa mstari wa mbele kutoa mwongozo.

Wanamsubiri mtu ambaye atakuwa akitoa mwelekeo wa taifa linakopaswa kwenda. Rais wa namna hiyo atatokea UKAWA!

Lakini ukimya huu pia ni tishio kubwa kwa wale waliotuonesha majuzi kuwa kweli wameshindwa. Wakafanya hata yale ambayo kwa akili ya kawaida mtu makini hathubutu kufanya. Kuosha nguo chafu za ndani hadharani! Ndiyo. Walimzomea Kiongozi wao. Wakauweka wazi mporomoko unaokikabili chama chao kutokana na nguvu kubwa ya Wananchi wanaotaka mabadiliko.

Bin Haji hajakosa neno linalosadifu kuwaambia CCM kutokana na ukimya (wa mipango na mikakati) wa UKAWA kuwa;

"Kimya ni giza kizushi, kuzukia walewale
Kimya kitazua moshi, moto msiyafumbule;
Kimya kina mshawishi, kwa daima na milele"

Huu utakuwa Uchaguzi wa kihistoria na inshallah Watanzania wanajiandaa kuzungumza na mabadiliko hayaepukiki. Wakati wao wametanguliza kufuli, wananchi wanakuja na funguo!


Makene
 
Nimesoma heading tu na short paraphrase, Kila la heri
 
Mkitoka kwenye huo ukimya wenu mkaja na fisadi kuwa ndo mgombea urais wa ukawa mtakuwa mmejiloga wenyewe. Endeleeni kukaa kimya lakini waleteeni watanzani mtu anayekubalika na kuaminika.
 
"wametanguliza kufuli sis tutakuja na funguo" Funguo ndiyo kila kitu kufuli kazi yake kuakaa mlangoni au getini tu.
 
Huwajui vizuri Mbowe na Mtei wakiona pesa
The Boss

Sikuwahi kufikiria unaweza kuwa Kwenye level ya hicho ulichoandika. Nilipoona ile comment yako iliyotangulia hii nikadhani umetoa maoni genuinely...

Kuhusu comment yako ya awali. Nimeshatoa ufafanuzi kuhusu Edward Lowassa na hicho mnachokitangaza mkiita ni move. Sina haja tena ya kuendelea kulijadili hapa maana itageuka kuwa publicity...jambo ambalo team yake wanaweza kukodi kampuni ya kufanya au kutumia watu wanaoweza kuwa wanamwandika hata mahali pasipo mwafaka.

Cheers mkuu.
 
Last edited by a moderator:
Siasa za Tanzania niza ajabu kweli.

Ni nani huyu atailipua hii volcano unayodai iko kila sehemu nchini wakati hata kupata mgombea Urais mmeshindwa kuafikiana achilia mbali kupamabana na mgombea wa CCM.

Kauli zako za jana kuhusu mgombea Urais wa tiketi ya UKAWA zilinikumbusha zile za Mohammed Saeed al-Sahhaf!

Yetu macho na masikio!
 
Back
Top Bottom