Kilombero bila kivuko toka Uhuru chanzo cha umasikini

engmtolera

JF-Expert Member
Oct 21, 2010
5,150
1,437
mv%20kilombero%20ii.jpg


KIVUKO cha Kilombero licha ya kuwa ni kitovu cha maendeleo ya biashara na uchumi wa wilaya ya Ulanga, lakini bado kimetelekezwa katika kipindi cha miaka 50 tangu kupata Uhuru.Teknolojia ya pantoni inayotumika bado ni ya kizamani kwani hivi sasa pantoni imechakaa kiasi cha kuzibwa na mbao za kawaida.Kwa takribani miaka 30 hadi kufikia miaka ya 1990 pantoni ilikuwa inasukumwa na nguvu za binadamu kwa kuvuta kamba na baadaye ilitumia nguvu za trekta hadi ilipotokea ajali mwaka 2002.

Katika ajali hiyo watu wapatao 34 akiwamo Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Ulanga wa wakati huo walipoteza maisha kufuatia pantoni kuzama kwenye kivuko hicho.Kivuko hicho ambacho kiko umbali wa kilometa tano kutoka mjini Ifakara, makao makuu ya wilaya ya Kilombero, ni tegemeo la wasafiri na wasafirishaji ambao huenda wilayani huko kufuata nafaka hasa mchele.

Hivi sasa bado kilio cha wananchi wa wilaya ya Ulanga ni kuwa na pantoni ya kisasa kwani zaidi ya wakazi 300,000 na wasafiri wanaongia wilayani humo takribani 500 kwa siku bado wanategemea pantoni moja tu ambayo ni mbovu.

Mmoja wa wakazi wa huko, Maria Mpoto anasema kuwa, hivi karibuni walikwama mjini Ifakara kwa siku tatu kufuatia pantoni kuharibika. Safari ya kwenda Ulanga ni ghali na haina uhakika.

“ Kwakweli wananchi wanateseka sana kwani wanaishi katika kisiwa kisichofikika kwa urahisi. Bei za mazao zinaathirika kutokana na matatizo ya kudumu ya kivuko. Wakulima wanateseka sana, ” anasema Mpoto.

Naye Juma Hassani ambaye ni mfanyabiashara anayenunua nafaka huko anasema kutokana na kutokuwa na kivuko cha uhakika wamekuwa wakipata hasara kubwa kutokana na gharama za usafiri kutotabirika.

Anaungwa mkono na Clement Mpunga ambaye anasema ni ajabu sana kuona kuwa wilaya nzima inategemea pantoni moja tu, wakati hapa Kigamboni, Dar es salaam: kuna pantoni imara zaidi ya mbili zinazohudumia wasafiri.

“Wakati tunaaadhimisha miaka 50 ya uhuru wakazi wa Ulanga bado hawajakombolewa kiuchumi kutokana na tatizo sugu la kivuko,” anasema Bw. Mpunga.

Wataalamu wa uchumi wanabainisha athari zake kuwa ni kubwa mno kwani hakuna biashara na shuguhuli imara za uchumi zinazoweza kufanyika katika wilaya hiyo ambayo usafiri wake ni wa mashaka kutokana na kuwapo kwa pantoni kongwe na isiyo na hakika.
Aidha wanasema kuwa ikitokea pantoni hiyo ikasimama kwa siku moja tu zaidi ya tani 300 za bidhaa mbalimbali kutoka na kuingia katika wilaya hiyo hukwama.

Wilaya ya Ulanga ina maelfu ya hekta za ardhi ambazo hazijatumika kabisa kutokana na matatizo ya miundombinu ya barabara, maghala ya kuhifadhi mazao, pantoni, majosho ya mifugo na mashine za kilimo cha umwagiliaji.

Wilaya hii ni miongoni mwa wilaya chache ambapo mkulima anaweza kupata mavuno mengi kwa kila ekari hasa mpunga, mtama, ulezi na mahindi bila kutumia mbolea.

Mazao yanayostawi huko ukiondoa zao maarufu la mpunga ni pamoja na maharage, kunde, mbaazi, njegere, choroko, njugumawe, alizeti, karanga, viazi vitamu, viazi mviringo, na mazao ya bustani kama tangawizi, nyanya, karoti, kabichi, na mchicha.Kuna mazao pia ya miti kwa ajili ya kuvuna mbao kutokana na miti ya kupandwa kama vile mitiki na miti ya mbao ya asili kama mninga na mvule ambayo inastawi kwa kiwango kikubwa katika wilaya hii.

Pia wilaya ina aina nyingi za madini ya vito kama ruby, rhodelite, saphire, green tomarine na mengine mengi. Aidha ina mabonde yenye rutuba na mito mingi.Aidha wilaya inashindwa kutumia fursa ya hifadhi ya taifa ya Udzungwa kukuza biashara ya utalii ukiwemo utalii wa utamaduni, utamaduni wa chakula kama pepeta, bidhaa adhimu miongoni mwa watu wa wilaya hiyo inayotokana na mpunga mchanga.

Jambo baya zaidi kivuko cha cha Kilombero kimekuwa kinatumiwa kama mtaji wa wanasiasa kwa miaka nenda rudi ambapo ahadi kadhaa zimekuwa zinatolewa kuwa kitanunuliwa kipya au kutajengwa daraja ili kuondoa kabisa taabu kwa watu wa huko na kuchangia kasi ya ukuaji wa uchumi katika eneo hilo.

Kama ilivyo katika maeneo mengine ya vijijini, karibu nusu ya wakazi wa Ulanga wanaishi chini ya dola ya marekani moja kwa siku na hivyo kushindwa kugharimia mahitaji muhimu kama vile elimu kwa watoto, chakula bora kwa afya, matibabu ya uhakika na maji salama.

Katika miaka ya 1970, Baba wa taifa, Mwl. Julius Nyerere alisema wakazi wa wilaya za Ulanga na Kilombero wakihamasishwa ipasavyo na kujengewa miundombinu bora na imara wangeweza kuzalisha nusu ya mahitaji ya zao la pamba hapa nchini. Wakati Tanzania ilikuwa na idadi kubwa ya viwanda vya nguo vya umma.

Mwl. Nyerere alisifia ubora wa pamba iliyokuwa inalimwa katika katika wilaya hiyo kwa kuwa ilikuwa ya nyuzi ndefu kuliko yale ya maeneo mengine ya Tanzania, lakini hivi sasa zao hilo limedorora kwa kiwango kikubwa ambapo kiwanda pekee cha kuchambua pamba cha Malinyi wilayani humo kimekufa na hakuna jitihada ya kukifufua.

Hivyo basi ahadi iliyotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa urais na wabunge mwaka 2005 na Rais Jakaya Kikwete kuwa atahakikisha kuwa daraja litajengwa katika mto Kilombero inasubiriwa kutekelezwa kwa hamu kubwa kwa kuwa huo ndiyo ukombozi pekee wa wananchi Ulanga katika kujikwamua kiuchumi.

e-mail: najestz@yahoo.com
Mob. 0754-458911
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom