Dotto C. Rangimoto
JF-Expert Member
- Nov 22, 2012
- 1,985
- 1,284
Salama ninaumia, mizigo kukubebea,
Ndani unapo ingia, na nje kujitokea,
Michubuko wanitia, mwenyewe wachekelea,
Mengi umenitendea, ukome kunitumia.
Hamu yako ulegee, na pumzi zikuishie,
Hapa pale uchezee, lengo hilo ufikie,
Natangulizwa kulee, kunako nikaingie,
Kama chuki uchukie, nataka nipotezee.
Huoni na husikii, chozi langu hulijui,
Wallahi hufikirii, kwa fujozo sipumui,
Ujuacho usanii, kulia na wako bui,
Mi' ndururu siijui, kazi kubeba madhii.
Ujue nina kilio, cha miaka si cha leo,
Wanitesa mtwangio, mawio hadi machweo,
Naomba tega sikio, waumiza mchezeo,
Kwako sina tegemeo, jalala langu fikio.
Tisa kumi sisahau, ufikapo kule juu,
Tanishika kidharau, na mate tatema, puu!
Sina thamani mdau, pamoja na kazi kuu,
Nabaki kutota tuu, nawe wakauka kau.
Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
call/whatspp 0622845394 Morogoro.