Kilio cha wanamuziki: Vanessa is a wake up call. Chanzo na suluhisho

Idimi

JF-Expert Member
Mar 18, 2007
14,970
10,462
Nimeandika thread ndefu kiasi chake, unahitaji muda kuisoma. Samahani kwa hilo ndugu msomaji...

Tuanze hapa hapa:-

Utangulizi
Wanajamvi, hapa majuzi mwanamuziki Vanessa Mdee aliamua kufunguka na kuongea ukweli wake kwamba muziki unampa msongo wa mawazo “stress” kwa sababu analazimika ku fake maisha ili kuridhisha hadhira inayomzunguka, ambayo ndio wanaomuweka mjini. Alisema kwamba kiuhalisia maisha anayoishi sio maisha yake halisi, anaishi maisha ya juu kuliko kipato chake ili kuwaridhisha mashabiki.

Hali hii ndio iliyokuwa inamtesa, mpaka akatangaza kuachana na uimbaji wa muziki na kufanya mambo mengine. Ni wanamuziki wengi ama ma star wengi sana wanaishi maisha haya mpaka leo. Wanaishi na madeni makubwa sana, kwa sababu wanaishi maisha yasiyo ya kwao. Nitatoa mtazamo wangu hapa chini wa namna maisha haya FAKE yanavyowatesa watu maarufu wengi na namna wanavyoweza kujua shida ilipo na kuiepuka. Naandika haya kama mshabiki na mpenzi wa muziki huu na wala sina maslahi mengine yoyote Zaidi ya upenzi wa muziki tu.

Kilio cha Vanessa Mdee (Vee Money) hakijaanza leo wala jana, kuna walioanza kulia kwamba muziki hauwalipi ama wanabaniwa na makundi kadhaa ya watu ama vyombo vya habari. Kwa sababu hiyo, wanaamua kuishi maisha feki kwa sababu muziki wao ni mkubwa kuliko kipato chao. Baadhi ya wanamuziki waliolalamikia hali hiyo ni hawa hapa:-

1. Mhe. Joseph Mbilinyi, Mr II aka Sugu aka Jongwe. Ukisikiliza wimbo wake wa “Moto chini” alioimba na mwanamuziki Waweru wa Kenya (upo hapo chini),, kwenye verse ya kwanza anasema “
...na machizi wangu wote sasa zidisheni hasira, ni wakati wa kumaliza ule utumwa wa kibiashara, sasa ni muda mrefu wanatufanya mafala, tunaingiza mamilioni, wanahonga mademu Vitara. Hamuwezi kunitisha katika kuthibitisha, nawawasha na tafadhali sahauini kuhusu Sugu. Kuna wimbo mwingine anasema, “Tunatangaza rasmi sasa kwamba adui zetu ni Wadosi”. Suala na hakimiliki, kama wote tunaibiwa, mbona wao hawalalamiki? Katika wimbo wake wa “Sugu” anasema akiamua kukomaa mapromota wenyewe wanakaa!

2. Mike Tee (Mnyalu) – Huyu katika wimbo wa Kimya Changu aliomshirikisha AY (upo hapo chini) analalamika (verse ya kwanza) .....kwamba wanamuziki akiwamo yeye wanadhulumiwa sana kwenye muziki, huku wao waking’ang’ana na bling bling kwenye TV huku mfukoni wakiwa hawana kitu, huku uzee ukiwakaribia. Anawalalamikia wanouza muziki wao (wahindi kwa wakatim huo) wa kipindi hicho. Anasema kaamua kuachana na kuendelea na kuzalisha muziki (production) akiwa na studio yake ya My Key records. Hilo la bling bling kwenye redio na TV ndilo linalomtesa Mdee pia, huku akiishi maisha feki.

3. Mwanamuziki Selemani Msindi aka Afande Sele katika wimbo wa “Watu na pesa” (upo hapo chini) anasema…tatizo mapromota na ma-redio presenter, wachache sasa wanafuata, fani wanaiboronga, top ten za kupanga, yaani hawajali ubora, watakazo ndizo wanapiga, nyimbo za ujinga ujinga ndio kila muda wanatwanga, bila kujali ujumbe, ilimradi umekata panga, na kama hauna kitu basi utakoma kuringa, hili mie nalipinga, japo kwangu afadhali, vipi wasanii wachanga? Mbele wataweza songa? Thubutu! Kama mwendo ndio huu, milele hawatasimama, kama hawatasimama basi na rap itazama, yote sababu ya pesa, wazimu, pesa haina nidhamu, loh wala pesa sio haramu hata ipakazwe damu.

Hapa ukimsikiliza analaumu mapromota wa shoo zao na watangazaji wa redio. Kwenye wimbo wake wa Mtazamo, (upo hapo chini) aliowashirikisha Profesa Jay na Solo Thang, Solo Thang kwenye verse ya kwanza kabisa anaimba…wapi ulipo uajabu, unakuwa mtumwa ili upate promo kuuza, ama kama ni binti ukalale kwa prodyuza, mapromota wanauma tu, hawajui na kupuliza, na siku wakipuliza jua kidonda kishaoza. Natamani kuwa huru mnyonyaji asinidhuru….


Adui yao ni nani hasa?

Kwa mujibu wa wanamuziki wenyewe kupitia tungo zao, maadui wao wakubwa ni hawa hawa:-

  • Watayarishaji wa muziki (Producers)
Kwenye wimbo za Mtazamo wa Afande Sele, Solo Thang anaimba kwamba wapi ulipo uajabu, unakuwa mtumwa ili upate promo kuuza, ama kama ni binti ukalale kwa prodyuza.......Baadhi ya wazalishaji wa kazi za wasanii wamekuwa wakiwataka wasanii wa kike kimapenzi, ili kuwategenezea kazi zao.

Kuna wakati mtayarishaji maarufu wa muziki Master Jay aliapa kwamba asingeruhusu wanae kuimba kutokana na “takataka” anazoziona kwenye muziki huo. Huenda aliyaona yale ambayo wengine hawayaoni, wanayopitia wasanii wa kike. Wasanii wa kiume pia hawajasalimika kwenye hili. Wagosi wa Kaya walirekodi albamu moja pale Bongo records, ndimo zilimo single za Taxi Driver na Kibaka Kaokoka. Haijulikani waliingia ugomvi gani na P Funk, mpaka kesho ile album haijawahi kutoka. Ikabidi wakamalizie kurekodi baadhi ya nyimbo kwa marehemu Saimoni Sayi (Complex) na kwa Master Jay chini ya Marko Challi. Ndipo ikatoka album yenye wimbo wa nyeti na ule wa Hotuba. Yako mengi ya producers. Yanahitaji therad yake.

  • Madalali wa muziki (Promoters & managers)
Hawa mie nawaita madalali wa muziki. Mameneja na ma promota ni chupa na kizibo, tofauti yao ni ndogo sana. Ni watu muhimu sana kwenye kukuza ama kudidimiza muziki, kwa kuwa ni kiungo kati ya mashabiki ama wateja wa muziki na wanamuziki. Mwanamuziki Suma G wa kundi la Hotpot Family, kwenye wimbo wake wa “Muulize meneja aliomshirikisha Profesa Jay (upo hapo chini) , analalamika kwamba inakuwaje kwenye mapato ya milioni yeye mwanamuziki anapewa laki? Pesa zote za shoo kachukua meneja na anasema anajenga jina la msanii.

Anasema mtaani haeleweki na wadau kwa sababu jina ni kubwa na hana pesa. Ukisikiliza wimbo wa “Hawa Watu”, (upo hapo chini) mwanamuziki Dataz (Florence Kassela) akimshirikisha kaka yake aitwaye George Kassela (Squeezer) kwenye verse ya kwanza kabisa anaimba….kuna promota, huyu hutizama maslahi yake Zaidi, akikuachia msanii anaona utafaidi, si kama nawasakama, NO, ila kwa mapromota feki nitazidi kuwa kaidi, akikukuta msanii wa kike ndio Zaidi, ataku-promoti kimuziki na mwili wako a-promoti ikibidi.

Kwenye wimbo wa Mtazamo, wa Afande Sele akishirikiana na Msafiri Kondo (Solo Thang) na Joseph Haule (Jay), Solo Thang anaimba…wapi ulipo uajabu, unakuwa mtumwa ili upate promo kuuza, ama kama ni binti ukalale kwa prodyuza, mapromota wanauma tu, hawajui na kupuliza, na siku wakipuliza jua kidonda kishaoza. Natamani kuwa huru mnyonyaji asinidhuru. Profesa Jay akishirikiana na Wagosi wa Kaya pia kwenye wimbo wa Promota anabeep, amelalamikia unyonyaji wa mapromota.

Ni kilio cha muda mrefu sana cha wasanii kuhusu unyonyaji wao. Kwenye wimbo wa “Ndege Tunduni” wa Wanaume Halisi, Juma Nature na wenzake wamemlalamikia waziwazi meneja Said Fella kwamba anawanyonya kwenye kazi zao, hivyo waliobakia akina Chegge na Mheshimiwa Temba wataendelea kunyonywa. Kwa sasa Saidi Fella kaachana na akina Temba na Yamoto Band mpaka ikavunjika, yuko kwa Diamond. Nadhani unaelewa nini naongelea hapa, kama ulikuwa unadhani meneja yupo kumuendeleza msanii. Hali kadhalika Babu Tale kawakimbia akina Madee (Tip Top Conenction) kaungana na Fella kuwa meneja wa Diamond. Hihitaji kuwa na shahada kuelewa connection iliyopo hapa!
Mifano ipo mingi sana, lakini nahofia kuwachosha wasomaji.

  • Radio/TV presenters
Kiufupi hawa ni miungu watu kwa wanamuziki. Ni wapokea rushwa wakubwa sana. Mwanamuziki asipowapa chochote basi asahau nyimbo zake kupigwa redioni ama kwenye TV. Wanataka mwanamuziki akubaliane na masharti wanayotaka wao, ili wimbo upigwe. Sometimes watangazaji wanakuwa mameneja wa wanamuziki, mfano, kuna wakati mtangazji Hellen Kazimoto alikuwa meneja wa mwanamuziki Innocent Sahani (D Knob).

Unadhani meneja wa aina hii angetenda haki kwa wanamuziki wengine kwenye kupiga nyimbo redioni? Hili limelalamikiwa na wanamuziki wengi sana. Afande Sele kwenye wimbo wa “watu na Pesa” amelalamikia kitendo cha watangazaji kupiga nyimbo zisizo na ubora, ilimradi mwenye wimbo ametoa chochote kwa mtangazaji husika. Kuna baadhi ya radio mpaka sasa hazipigi nyimbo za baadhi ya wanamuziki, kwa sababu hizi hizi, hata kama wimbo ni maarufu kwenye jamii.

Haya yamewakuta Lady JD, Mr II, Diamond na Dudubaya dhidi ya radio moja iliyoko Mikocheni Dar Es Salaam. Hali hii pia alikutana nayo Dully Sykes dhidi ya mtangazai mmoja wa redio ambaye sasa ni mkuu wa wilaya mojawapo mkoani Tanga, akiwa mtangazaji wa redio moja (ni Times kama sijakosea). Wimbo wa Dully wa Historia ya kweli ulikuwa namba moja kwenye top ten iliyokuwa inaandaliwa na mtangazaji huyo, kila wiki ulikuwa haupigwi kwa sababu alizokuwa anasema ziko nje ya uwezo wa mtangazaji huyo.

Leo kuna wimbo wa Ben Pol unaitwa Jikubali, humo ndani kamtaja Diamond, ilipofika sehemu anayotajwa Diamond, DJ amescratch ili neno hilo lisisikike, kisa tu mwanamuziki Diamond ana ugomvi na redio hio. Wanapitia magumu mengi wanamuziki hawa.

  • Wauzaji wa kazi za wasanii (Marketing agencies)
Ingawa kwa sasa inaonesha wanamuziki wengi wameaha kutoa albamu, lakini malalamiko mengi sana ya wanamuziki yalielekezwa kwa wafanyabiashara wa kihindi. Hizi zilikuwa ni syndicates za wauzaji wa kazi za wasanii, kwa maana ya muzuki na filamu. Hawa walilalamikiwa sana kwa kuuza nakala nyingi za kazi za wasanii huku wakionesha kwamba wameuza nakala chache. Hii nadhani inatokana na ubovu wa sharia zetu kwenye suala la haki miliki za wasanii. Kulikuwa na kampuni za FK Mitha, Wananchi na King’s music (FKW), na GMC za Kariakoo. Hawa walikuwa ni wauzaji wakubwa wa kanda na CD na wanamuziki walilalamikia sana kusaini nakala chache wakati wao wao wanauza nakala nyingi zaidi ya wanazoweka wazi!

  • Wanamuziki wenyewe
Wanamuziki wao wenyewe ni shida kubwa. Ni wanafiki kupita kiasi na wala hawapendani kabisa. Wakiwa kwenye mahojiano na vyombo vya habari wengi wao hawasemi matatizo yao, kwa kuwa vyombo vya habari ni sehemu ya tatizo kwenye muziki wao. Kila mtu anakufa na tai shingoni. Wanaoyasema matatizo yao hadharani ndio wanaishia kununiwa na kubaniwa nyimbo zao kupigwa kwenye redio ama kuandikwa magazetini.

Nimewataja hapo juu baadhi yao, waliofungua midomo kulalamikia madhira ya vyombo vya habari na mawakala wa muziki. Ndio sababu kama hizi za unafiki zinazosbabisha wanashindwa kuomba marekebisho ya sheria mbalimbali za hakimiliki za kazi zao kwa serikali, kwa sababu wakiitwa, ni wachache sana wanahudhuria wito. Hilo kalisemea sana Mhe. Temba kwenye wimbo wake wa “Enzi zetu”, verse ya kwanza kabisa Temba anasema mashetani ni wao wenyewe wasanii.

Suluhisho
Nimeweka ushahidi hapo juu kwamba wanamuziki na wasanii wetu kwa ujumla wao wanajua kabisa shida yao ilipo, isipokuwa wanakosa umoja na uthubutu wa kumfunga paka kengele kwa kuogopa kutupwa kapuni. Lakini wangeamua kusimamia maslahi yao kwa mapana yake, hakuna mwamba ambao ungewasumbua.

Nyimbo za wanamuziki niliowataja hapo juu naziweka hapa chini ili nanyi mzisikilize, lakini pia nawasihi msikilize mahojiano ya Dudubaya na online tv ya Carry Mastory kuhusu yaliyomkuta Vanessa Mdee na namna wanamuziki wanavyoteseka. Naamini kitachangia sana kuongeza uelewa wa wanamuziki kuhusu haki zao, Dudubaya ametiririka sana ingawa wengi wanamuona kama mropokaji. Lakini ameongea facts nyingi sana ambazo si wanamuziki wengi wanathubutu kuongea hadharani.

Nakomea hapa. Nawasilisha

Asanteni
 

Attachments

  • Mr II - Moto chini-Sugu_.mp3
    4.2 MB · Views: 4
  • Mike Tee - Kimya changu ft. AY.mp3
    4.1 MB · Views: 3
  • Afande Sele - Watu na Pesa.MP3
    2 MB · Views: 4
  • Afande Sele ft Solo Thang & Prof Jay - Mtazamo.mp3
    6.2 MB · Views: 3
  • Suma G ft Professor Jay - Muulize Meneja.mp3
    4 MB · Views: 3
  • Dataz ft Squeezer - Hawa watu.mp3
    3.4 MB · Views: 4
  • TMK - Ndege Tunduni.mp3
    5.5 MB · Views: 3
  • Prof Jay - Promota ana beep.mp3
    3.6 MB · Views: 4
  • Mh Temba - Enzi Zetu.mp3
    6.3 MB · Views: 6
Hoja nzito na yenye mashiko hii, naamini wanamuziki watajirekebisha kwanza waishi maisha yao halisi, lakini pia watafute namna ya kufanya kazi ili wanufaike wao kwanza then hao wengine wapate.
 
JayDee anayajua haya
IMG_20200624_205917.jpg
IMG_20200624_205840.jpg
 
Bongo music sawa,ila bongo muvi hawastahili huruma wala kuamshwa!! Waache waendelee na maujinga yao,ukiniambia mtu kama JB eti naye analia kuibiwa au ana hali ngumu ntakuambia tu mwache akafie mbele.
 
Bongo music sawa,ila bongo muvi hawastahili huruma wala kuamshwa!! Waache waendelee na maujinga yao,ukiniambia mtu kama JB eti naye analia kuibiwa au ana hali ngumu ntakuambia tu mwache akafie mbele.
Kwanini mkuu? Kwani kulalamika ni jambo baya?
 
Back
Top Bottom