SoC03 Kilio cha Mwalimu Mlevi

Stories of Change - 2023 Competition

MombaDier

Senior Member
Jul 24, 2022
102
205
Tanzania Tanzania, nakupenda Tanzania. Nchi yangu nzuri, nakupenda Tanzania. Kimbilio la wanyonge, nakupenda Tanzania. Uliyezengukwa na misitu tele, nakupenda Tanzania. Mito shazi na bahari, nakupenda Tanzania. Mbuga za wanyama na vivutio vya watalii, nakupenda Tanzania. Ardhi ya rutuba na madini, nakupenda Tanzania. Watu wako mashuhuri, nakupenda Tanzania. Wakarimu na wapole, nakupenda Tanzania. Ukatawaliwa na Amani isiyo na mfano, nakupenda Tanzania.

Huu ni wimbo ambao pengine huufahamu kwasababu haukuimbwa na Les wanyika ama fahari ya Morogoro Mbaraka Mwishehe. Huufahamu kwakuwa haukuimbwa naye Ali Kiba ama Nasibu wa Abduli. Huenda labda ungeufahamu angeuimba Nandi ama Ray C wa kiuno bila mfupa. Vipi ungeimbwa na Jide usingeujua? ama angeuimba Isha Mashauzi ungeachaje kujua? Au ulitaka uimbwe na watu wa singeli ndiyo uujue? Ila isivyo bahati kuna mlevi mmoja alikuwa akiuimba sijui aliusikia wapi binafsi sikuweza kujua.

Nilimsogelea kwa lengo la kuongea naye, lakini niligundua alikunywa pombe kali za kienyeji yaani nkangala na boha. Ilihitaji uvumilivu mkubwa kumsikiliza mtu wa aina hii ambao hata hivyo nilibahatika kuwa nao, uvumilivu huo ulinifanya nijifunze vingi kutoka kwake.

Mlevi yule alinieleza kuwa anaipenda sana nchi yake kama wimbo unavyojieleza, ila kuna kitu kimoja pekee ambacho kwake hakimvutii kutoka kwa watu wake hasa viongozi. Alisema kuwa viongozi wengi wamekuwa siyo waadilifu kwa taifa lao lililojaaliwa utajiri wa maliasili badala yake wamekuwa wabadhilifu, mafisadi na wasio ridhika kwa kile wanachokipata na mbaya zaidi wamekuwa wapenda anasa na wala rushwa kupitiliza.

Alisema mpaka wakati ule anaishukuru sana nchi yake kwa kumpatia sehemu ya ardhi ambayo anastawisha mazao yanayomfanya aweze kupata chakula cha kila siku, pamoja na ardhi aliyojengea nyumba inayomhakikishia hifadhi kwa familia yake. Aliendelea kuishukuru nchi yake kwa kumpatia fursa ya kutumia misitu inayomnufaisha katika uvunaji wa kuni ila anasikitishwa kwa kuona kuwa hana fursa ya kufaidi matunda ya nchi zaidi ukiachana na neema hizo.

Mlevi yule alisema kuwa madini ni miongoni mwa rasilimali tulizojaaliwa nchini lakini wanufaika wamekuwa siyo wananchi wake, viongozi wameiuza tunu hii kwa mabeberu kwa kivuli cha uwekezaji. Wamewapatia nguvu zote za uendeshaji migodi huku wao wakisubiri wapate asilimia kumi maofisini. Kwani hukuwahi kusikia mchanga wa madini unakwenda kusafishwa nje ya nchi? ina maana wanashindwa kuusafishia hapahapa nchini kweli?

Alitoa mfano kuwa hakuna mkulima atakayeng’oa hindi na mti wake (mabua) shambani eti akavitenganishe nyumbani, hapana hindi utalitenganisha na bua hukohuko shamba ikitokea bua limeenda nyumbani ujue lina manufaa aidha amepelekewa ng’ombe akale ama yanaenda kuezekea banda la kuku na hapo mabua yatafuatwa wiki mbili baada ya hindi lenyewe kufika nyumbani. Vinginevyo ng’ombe wenyewe kesho yake wataingizwa shambani ili kuepusha gharama za kusafirisha, bua haliwezi kwenda nyumbani pamoja na hindi kamwe.

Tuachane na hilo je, unayafahamu madini ya Tanzanite? Nambie ni nchi zipi zinaongoza kuwa na madini hayo, nafahamu hujui ila Tanzania si nchi ya kwanza wala ya pili kwenye soko la kimataifa kunufaika na mauzo ya madini hayo. Ukilitafakari hili kwa undani utagundua kuwa kuna uozo mwingi katika usimamizi wa maliasili zetu viongozi hawako tayari kujitoa kwa ajili ya taifa na wananchi wake, wanatuangusha. Hayo madini yanapatikana kwenye ardhi ya Tanzania pekee lakini cha ajabu ni kuwa wanufaika wa mauzo yake kwa kiwango kikubwa si watanzania wala Tanzania yenyewe hii si sawa mwanangu.

Hivi hukuwahi kusikia habari juu ya utajiri wa gesi na makaa ya mawe yaliyopo kwenye ardhi yetu? ila mpaka leo bado tunategemea umeme wa maji, maji ambayo binadamu tunayahitaji kwa shughuli za nyumbani na viwandani, maji ambayo tumeshaivuruga misitu na mazingira yake na sasa hatuna uhakika wa kuzipata mvua za kutosheleza na bado hatuna miundombinu sahihi na endelevu ya kuyatunza maji hayo japo kwa uchache wake.

Ni ajabu mpaka leo hii hatuna umeme wa uhakika kiasi kwamba waajiriwa kwenye taasisi ya umeme ajira yao kuu ni kukata umeme kama yule kiungo wa Yanga. Hii yote ni kwa sababu viongozi wetu wameshindwa kuzisimamia tunu alizotupendelea Mwenyezi Mungu.

Mimi hapa unayeniona siyo tu kuwa ni mlevi, ni mwalimu mstaafu nimelitumikia taifa kwa zaidi ya miaka thelathini lakini cha ajabu hakuna linalobadilika upande wa maslahi, walimu tumedharaulika wastaafu ndiyo kabisa. Hatuna wakutufuta machozi maana hata tuliowafundisha tukidhani watakua watetezi wetu wameishia kujijali wao tu, yaani haina tofauti na kumtuma mtu umeme wa luku akarudi na mshumaa.

Usicheke mwanangu walimu maslahi yetu ni duni mno tukiwa tunafundisha na mara hata baada ya kustaafu, mbaya zaidi tukistaafu wanatufanyia tafrija kwa hela tulizochanga kwenye mifuko ambayo binafsi naitambua kama mifuko nyonyezi tunalipa hivyohivyo tu hakuna jinsi. Kwakuwa wanajua tutapata kiinua mgongo basi palepale kwenye tafrija wanatuletea vijana matapeli wakidai ni wanatushauri namna ya kuwekeza hela zetu, yaani eti kijana wa mjini anielekeze mstaafu namna ya kuwekeza kiinua mgongo changu! Sawa ukiwasikiliza hawana jipya wanatusimulia miradi ya matikiti, sarafu mtandaoni na ununuzi wa matrekta ambayo kwa tunatakiwa kuungana wengi ili tulipate moja matokeo yake wiki mbili tu mstaafu huna kitu mwisho wa siku unaangukia kwenye ulevi kama mimi wakati tuliowafundisha tuliwaasa wasiisogelee pombe hata kidogo.

Tulizungumza mengi na nilipomuuliza ni kipi kifanyike juu ya yote hakuwa mchoyo wa maneno alisema kuwa viongozi ni lazima wawe waungwana, wenye hofu ya Mungu na kusimamia maadili ya uongozi ambayo ni uwajibikaji kwa raia wake. Aliongeza kuwa viongozi ni lazima wakumbuke walikotoka na kuacha ubinafsi kwani wengi wao wamekumbwa na kashfa za kusafirisha maliasili na kupeleka fedha nchi za ng’ambo, wakati fedha hizohizo zinaweza kutumika katika kuboresha miundombinu nchini itakayosaidia kusafisha madini na mchanga wake badala ya kuwanufaisha mabeberu kwa kuvisafirisha nchini kwao ambako mrejesho wake wamekuwa wakidai kuwa hawapati faida na kutuacha patupu.

Alisema kuwa wakuu wa nchi waache kujitizama peke yao kwani kiinua mgongo anachopewa mstaafu aliyelitumikia taifa kwa miaka zaidi ya thelathini na kile anachopewa mbunge aliyehudhuria vikao vya bunge kwa miaka chini ya mitano na kushindwa kutetea kiti chake jimboni kinaonesha wazi ni kwa namna ipi wamekua wabinafsi.

Hayati baba wa taifa alisema kuwa “Utumishi wa umma ni kazi ya kujitolea sio pa kujilipa mamilioni” akimaanisha kuwa ukiwa kiongozi unatakiwa kuwa muwajibikaji kwa unaowaongoza na siyo kujilimbikizia mali za umma kwasababu tu hakuna wa kukupinga si sawa na havikubaliki.

Mlevi yule alimaza kwa kusema Nakupenda Tanzania, ni mimi fahari ya Tanga Tembeleeni Handeni
 
Back
Top Bottom