Kilimo cha Maharage: Mbinu za kulima, Ushauri na Masoko yake

Informer

JF-Expert Member
Jul 29, 2006
1,445
2,000
Maharage ni zao jamii ya mikunde ambalo hulimwa kwa ajili ya kuliwa kama mboga au futari linaweza kama maharage mabichi au maharage makavu. Pia majani yake mni chakula cha mifugo na yanatumika pia kama mboga kwa binadamu. Katika ekari moja unaweza kupata Kg 600 hadi 1200 za maharage.

Maharage ni moja kati ya mazao ambayo yanalimwa sana na ni moja kati ya mazao yanayo waongezea kipato wakulima wengi sana nchini Tanzania lakini kwa kufuata kanuni za kilimo bora

Maharage n zao muhimu kwa chakula, lishe na kipato kwa familia na Taifa. Kwa mavuno mengi ni vizuri kuzingatia kanuni bora muhimu za kilimo bora cha Maharage. Mavuno mengi na yenye ubora huchangiwa na matumizi ya mbegu bora. Mbegu bora ni mojawapo ya pembejeo muhimu katika Kilimo. Ubora wa mbegu unatakiwa kufuata hatua zote za uzalishaji mbegu shambani, uvunaji, usafirishaji, kupakia kwenye vifaa, kufunga, usambazaji, kuhifadhi na uuzaji.

Mbegu ya kuazimiwa ubora (quality declared seed) huzalishwa na wakulima wadogo wadogo na vikundi vya wakulima wadogo vijijini, chini ya usimamizi wa washauri wa Kilimo wa Wilaya.

Maharage ni lishe ya pili kwa umuhimu nchini Tanzania baada ya mahindi. Maharage yanaweza kuliwa yakiwa machanga/mateke (green/French beans) na yakiwa mabichi au yamekauka baada ya kukomaa.

Maharage ni chanzo muhimu cha protini kwa binadamu na husaidia udongo katika utengenezaji wa madini ya nitrogen kutoka kwenye hewa kwa kupitia mizizi ya maharage ambayo husaidiana pamoja na rhizobium/ryzobium bacteria kwenye udongo. Nitrogen ni muhimu kwa ukuaji na uzalishaji wa mahindi.

Kwa miaka mingi maharage yamekuwa yakilimwa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani lakini hali inabadilika kwasababu soko la maharage limekua, bei yake kuongezeka na mahitaji ya maharage yameongezeka. Hii imesababisha kuongezeka kwa uzalishaji na biashara ya maharage nchini na nje ya nchi.

Maharage hutumika kama chakula cha binadamu na pia majani yake huweza kutumika kama chakula cha mifugo. Katika chakula cha binadamu maharage hutumika kama kiambatanishi (mboga) cha vyakula vingine kama vile wali au ugali.

Maharage ni chanzo kizuri cha kupunguza cholesterol mwilini, cholesterol nyingi mwilini ni chanzo cha magonjwa mengi. Pia maharage husaidia kukinga viwango vya sukari kwenye damu kuongezeka ghafla baada ya mlo, hivyo ni muhimu sana kwa watu wenye kisukari.

Zaidi ya yote vyakula vya jamii ya maharage vimeonekana kupunguza uwezekano wa kupata mshituko wa moyo. Tafiti za hivi karibuni zimegundua kuwa ulaji wa maharage hupunguza uwezekano wa kupata saratani (cancer) tofauti na nyama ambayo huongeza uwezekano wa kapata saratani.


HALI YA HEWA IFAAYO

Hustawi vizuri maeneo yenye mwinuko wa mita 1000 hadi 2000 kutoka katika usawa wa bahari .Pia yanaweza kulimwa pungufu ya mita 1000 au zaidi ya mita 2000 kutoka usawa wa bahari. Maharage huitaji mvua ya kutosha kipindi cha kabla ya uwekaji maua na kipindi cha ukuaji wa vitumba vya maharage.

Huitaji unyevu kidogo kipindi cha kuweka maua na ukavu kipindi cha kukomaa na kukauka vitumba. Maharage hulimwa Kwa Wingi MBEYA, IRINGA, KAGERA, KIGOMA, ARUSHA, KILIMANJARO, Morogoro N.K

UDONGO

Hustawi vizuri katika udongo usiotuamisha maji na ambao ni mfinyanzi kichanga ambao una mboji ya kutosha wenye pH 5.5 – 7.Pia unaweza kulima katika udongo wa aina tofauti tofauti.

MBEGU BORA ZA MAHARAGE

Kuna aina mbalimbali za mbegu bora za maharage kama vile canadian wonder, Tengeru, Uyole, SUA, Ilonga na Lyamungo.

Aina mbili ya mbegu bora za maharage zimeendelezwa/zimezalishwa katika kituo cha utafiti wa kilimo kilichopo Uyole mkoani mbeya. Mbegu hizo ni BILFA 16 na UYOLE 04.

Kuzalishwa kwa mbegu hizi bora ni juhudi za muda mrefu za mpango wa kuzalisha mbegu bora za maharage lengo likiwa ni kuongeza uzalishaji na maharage yakiwa katika sifa na ubora unapendekezwa na wakulima pamoja na walaji, wakulima hupendelea mbegu zinazohimili magonjwa, zinazohimili ukame na zenye mazao mengi wakati walaji hupendelea maharage yenye ladha nzuri na yanayoiva kwa urahisi yakiwa katika bei yenye unafuu.

MBEGU YA UYOLE 04
hutambaa, huzaa maharage yenye ukubwa wa wastani mpaka kubwa kabisa zikiwa na rangi ya maziwa, zinahimili magonjwa sugu kama kutu ya maharage na anthracnose, huiva haraka yakipikwa na huwa na ladha nzuri sana

Wakati wa kupanda mbegu hii hutegemea msimu wa kuanza na kuisha kwa mvua, kwa mfano sehemu ambazo mvua huisha mwisho wa mwezi wa 4 au mwanzo wa mwezi wa 5 basi upandaji uanze mwezi wa 3 kwa sababu ukuaji wa mbegu hizi mpaka kukomaa huchukua wastani wa siku 105.

Kiasi cha mbegu zinazohitajika kupanda ni kilo 70 – 80 kwa hekta ambapo miche 200,000 huota na huweza kuzalisha kiasi cha tani 1.5 – 1.8 kwa kila hecta, mbegu hii hufaa sana kupandwa nyanda za juu kaskazini (mikoa ya Mbeya, Iringa, Songea na Rukwa) ambako ardhi imeinuka wastani wa mita 800 – 2000 kutoka usawa wa bahari na kuna baridi.

MBEGU YA BILFA 16 huwa na rangi nyekundu mchanganyiko na maziwa kama nguo ya jeshi, mbegu ni za ukubwa wa wastani, huweza kuhimili sana magonjwa, mimea ni ya kijani kibichi yenye majani madogo madogo huwa na matawi 4 – 5 maua huwa na rangi ya pinki na vishubaka vya maharage huwa vyeupe na vikikomaa huwa rangi ya maziwa.

Kiasi cha mbegu zinazohitajika kupanda ni kilo 70 – 80 kwa hekta ambapo miche 200,000 huota na huweza kuzalisha kiasi cha tani 1.2 – 1.5 kwa kila hecta, ambacho ni kidogo ukilinganisha na UYOLE 04, mbegu hii hufaa sana kupandwa nyanda za juu kaskazini (mikoa ya Mbeya, Iringa, Songea na Rukwa) ambako ardhi imeinuka wastani wa mita 800 – 2000 kutoka usawa wa bahari na kuna baridi. Na mbegu hii hukoma baada ya siku 80 – 84 tangu kupandwa kwa hiyo hufaa kwenye maeneo yenye mvua za muda mfupi.

SIFA ZA MBEGU BORA/VIPIMO VYA UBORA WA MBEGU:

- Mbegu za aina moja (uhalisia wa kizazi) – Ili kuwa na sifa hii ukaguzi lazima uanzie kwenye shamba la kuzalisha mbegu.

- Mbegu safi – Zisizochanganyika na aina zingine au mazao mengine, mbegu za magugu, zisizoliwa na wadudu na uchafu kama udongo na takataka zingine.

- Mbegu zilizokomaa na kukauka vizuri – Kama zimekauka vizuri haziwezi kuoza na kuvunda, na huota vizuri pia haziwezi kushambuliwa na wadudu kwa urahisi. Hii huiwezesha mbegu ibaki na ubora wake kwa muda mrefu.

- Mbegu zilizovunwa kutoka mimea yenye afya kutoka shamba lenye mazao mazuri – Mbegu zilizovunwa kutoka kwenye mimea dhaifu haziwezi kuota vizuri na kwa wakati mmoja na mimea yake huwa dhaifu.

- Mbegu yenye afya nzuri – Mbegu ambayo haiwezi kuwa chanzo cha magonjwa. Fungu la mbegu isiyo salama kiafya isitumike kama mbegu. Vime vya magonjwa huweza kusambazwa kwa njia ya mbegu kama mbegu hii itatumika.

- Mbegu zenye uwezo wa kuota kwa zaidi ya asilimia tisini (90%).

- Mbegu za aina bora zinazokibalika (chagua aina ya mbegu kulingana na mahitaji).

- Mbegu mpya (pre-basic/foundation), isirudiwe kupandwa zaidi ya misimu miwili.


UPANDAJI WA MAHARAGE

Panda sehemu zenye udongo usiotuamisha maji na wenye rutuba. Panda mbegu katika maeneo yenye mwinuko wa mita 400m-1800m kutoka usawa wa bahari kwa nyanda za juu kusini. Sehemu kavu zenye mvua ya muda mfupi kama, panda mwezi Disemba hadi Februari. Sehemu zenye maji ya umwagiliaji panda wakati wa kiangazi.

Tenga aina mbalimbali za mbegu kwa nafasi ya mita zisizopungua mita 3.Usipande mbegu katika mchanganyiko wa mazao mengine.


Maharage hupandwa mwishoni mwa msimu wa mvua kuepusha kunyeshewa kipindi cha uekaji maua. Yanawezwa kupandwa mwezi Februari, Machi, Aprili inategemea mvua katika eneo lako zinaisha mwezi gani, hivyo hakikisha angalau yanapata mwezi mmoja wa mvua ya kutosha.

Fukia mbegu zako katika kona cha sm2.5 hadi 4 katika ardhi kutegemea na aina ya udongo shambani kwako.

Maharage hupandwa kwa kutumia mbegu ambazo ni safi na hazijaharibika kwa kuvunjika au kuliwa na wadudu.Kabla ya kupanda maharage yako unaweza kuyatibu kwa kutumia Rhizobia Bacteria ambapo itakupunguzia matumizi makubwa ya mbolea za nitrojeni. Maharage yapandwe kwa nafasi ya sentimeta 40-60 mstari hadi mstari na sentimeta 15-20 shina hadi shina.


MBOLEA

Unaweza kupanda katika shamba lililotawanywa mbolea ya samadi. Pia uanweza kwa uzuri zaidi kupandia mbolea za viwandani kama vile TSP au Minjingu kwa kiasi cha kg 50-100 kwa ekari. Wakati wa mmea kuanza kuweka maua unaweza kutumia mbolea ya N.P.K au SA au Kwa Kiasi Kidogo CAN au UREA Angalizo Mbolea hizi zikizidi maharage huwa na majani mengi kuliko maua na kusababisha mavuno kuwa machache.

UPALILIAJI

Inashauriwa kupalilia mimea kabla haijatoa maua. Shughuli hii inatakiwa ifanywe kwa uangalifu ili kukinga mimea isiharibike kwenye mizizi kwani uharibifu wa aina yoyote huweza kusababisha magonjwa kwa mmea. Inashauriwa kupanda mimea kwa kuzunguka (crop rotation) ili kupunguza uwezekano wa magugu na mardhi kuweza kushambulia mimea.

Upaliliaji inabidi ufanyike mapema mara tuu maharage yanapoota na shamba kuwa na magugu. Palizi ya kwanza inaweza kufanyika Kati ya siku 8-12 baada ya mmea kuota na yapili ifanyike siku ya 20 na 30 baada ya palizi ya kwanza. Ili kuyalinda maua ya maharage yako yasipukutike wakati wa palizi hakikisha unaepuka palizi kipindi cha uwekaji maua. Unaweza kutumia madawa ya kuuwa magugu kama Galex, Stomp, Dual Gold, Sateca n.k

WADUDU

Funza wa maharage ni wadudu wanaoshambulia mimea michanga ya maharage. Funza wa maharage hawa huweza kusababisha uharibifu hadi kufikia asilimia 100 kufuatana na hali ya hewa-unyevu kidogo, rutuba kidogo, kuwepo kwa maotea ya aina ya maharage na magonjwa kwenye udongo, kurudia kupanda zao la maharage kila msimu na aina ya naharage.

NJIA NZURI YA KUDHIBITI FUNZA WA MAHARAGE NI HIZI:

1. Kupanda mapema

2. Kupakaza mbegu dawa kama endosufan, Acephate, Murtano (mchanganyiko wa dawa ya fungas na wadudu) nasaidia kuzuia funza wa maharage na visababishi vya kuozesha mizizi

TAHADHARI: Dawa ya Murtano ni sumu kali hivyo mbegu zenye dawa hii zisitumike kwa chakula.

3. Kunyunyizia dawa mfano DUDUBA au DUDUALL Karate 5EC au Actellic 50EC ndani ya siku 4 hadi 5 baada ya maharage kuota

4. Kupanda mbegu zenye afya kwenye udongo wenye rutuba

5. Kupanda mbegu zenye ukinzani wa funza wa maharage

6. Kuweka matandazo kama pumba ya mpunga husaidia kuotesha mizizi mipya n kurudisha afya ya mmea wa maharage.

Pia maharage yanaweza kushambuliwa na wadudu mbalimbali kama vile nzi weupe wa maharage na wengineo ambao wanaweza kuzuiwa kwa kutumia dawa mbalimbali za wadudu.

MAGONJWA

Maharage hushambuliwa na wadudu na magonjwa. Miongoni mwa njia za kuzuia, kukinga na kufukuza wadudu ni kuhakikisha kuwa mimea ipo katika hali nzuri (imepaliliwa, nafasi ya kutosha na haijaharibika).

Pia kubadilisha aina ya mimea inayopandwa kwenye shamba moja mara kwa mara husaidia kupunguza uwezekano wa wadudu kuongezeka. Kwa baadhi ya wadudu kama vile viwavi (African Ballworm) huweza kufukuzwa kwa kutumia muarobaini au vitunguu saumu. Maji ya muarobaini ni dawa nzuri sana kwaajili ya kufukuzia wadudu na haina madhara yoyote kwa binadamu.


Magonjwa maarufu ni ndui ya maharage, madoa pembe, kutu, magonjwa yanayosababishwa na bacteria na virusi. Mbegu iliyoambukizwa, udongo na takataka za maharage ni vyanzo vikubwa vya uambukizaji kwa magonjwa yote isipokuwa ugonjwa wa kutu ya majani.

1. Punguza athari kwa kupanda mbegu safi, zenye afya zisizo na vidonda/ magonjwa, aina zinazovumilia na kutunza shamba

2. Panda kwa mzunguko wa mazao ya jamii nyingine

3. Ondoa na kuchoma yaliyougua

4. Tumia dawa zilizopendekezwa kama Kocide, Funguran, Bayleton n.k kwa kuzuia magonjwa yanayosababishwa na ukungu na bacteria.


KILIMO MCHANGANYIKO

Ni vizuri sana na inashauriwa kupanda maharage pamoja na mimea ya jamii nyingine kama vile mahindi kwani husaidia katika kusambaza madini ya nitrogen na kwa maharage yenye kutambaa, hupata sehemu ya kujishikilia au kutambalia. Maharage yanaweza yakapandwa katikati ya mistari ya mahindi. Pia viazi huweza kupandwa pamoja na maharage.

UVUNAJI

Wakati wa mavuno kunatakiwa kuwe na ukavu ili maharage yasiharibikie shambani. Maji mengi yaliyotuama na ukame siyo nzuri kwa maharage na husababishia mmea magonjwa na kuoza au kukauka. Maharage huvunwa mara tuu yanaponza kukauka na kabla vitumba havijapasuka. Ng’oa mashina ya maharage na na upigepige kuyaondoa katika vitumba vyake.

Baada ya kuyapiga na kupeta kuondoa uchafu yaanike juani kwa siku kazaa kuhakikisha yamekauka na hayana unyevu unaoweza kusababisha yapate fangasi.yahifadhi katika magunia, kama yatakaa muda mrefu bila kuliwa basi hakikisha unayahifadhi kwa kutumia dawa za kuulia wadudu kama vile Shumba, Kama vile ACTELLIC DUST au MALATHION. au Tumia mifuko maalum ya kuhifadhia nafaka.


KUVUNA NA KUTAYARISHA MBEGU

Vuna maharage mar yatakapokauka. Kausha kwa kuanika juani, piga, peta na kausha tena juani. Unaweza kuvuna kilo 600 hadi 800 kwa ekari kabla ya kuchambua endapo utafuata kanuni za kilimo bora.

Chambua mbegu vizuri kwa kuondoa uchafu, udongo, mbegu za aina nyingine, punje zilizopasuka na zilizohafifu. Pia ondoa punje zenye vidonda/mabaka na zilizotobolewa na wadudu. Hakikisha mbegu zimekauka vizuri kabla ya kuhifadhi.

KUHIFADHI MBEGU

Safisha vyombo au ghala na ondoa wadudu. Zuia wadudu kwa kutumia dawa za asili au za viwandani. Tumia dawa za kuhifadhia mbegu kama Actellic (gramu 100 za Actellic super Dust kwa kilo za mbegu za maharage), Murtano (gramu 300 za Murtano kwa kilo 100 za mbegu za maharage) na dawa zinginezo kwa kiwango kinachoshauriwa na wataalamu.

Weka mbegu mbali na maharage ya chakula pamoja na vyakula vingine. Epuka sehemu zenye unyevu na paa zinazovuja na zuia panya. Usihifadhi mbegu kwa zaidi ya misimu miwili maana baada ya hapo uwezo wa kuota hupungua.

KUPIMA UWEZO WA KUOTA

Pima uwezo wa uotaji kabla ya kupanda. Uotaji mzuri ni wa zaidi ya asilimia tisini (90%). Panda mbegu 100 katika kila sehemu tatu zinazofanana na zenye unyevu. Baada ya siku kumi chunguza miche iliyoota vizuri na kuihesabu.

Tumia kanuni ifuatayo: Asilimia ya uotaji = miche iliyoota vizuri × 100 gawanya kwa 300.
 

ANKOJEI

JF-Expert Member
Nov 11, 2010
701
250
Kuna aina ya maharage yanaitwa ngwala, waungwana najaribu kutafuta kwenye neti siyapati.
Sifa,
yanastail ukame hasa umasaini
pili yana soko kubwa apo ulaya, marekani na asia,
yeyote mwenye habari ya jina yake ya kiingereza please help!
 

snochet

JF-Expert Member
Mar 31, 2011
1,286
2,000
nilishaanzishaga topic siku nyingi kuhusu hili zao,ila sikupewa majibu ya kuridhisha,yana bei kubwa sana,ila ukuaji wake ni taratibu.....naungana na Ankojei kuomba wanaojua....asanteni
 

Bushloiaz

JF-Expert Member
Nov 2, 2010
606
500
Mwaka huu nimepata gunia 6 ya zao hili na wakati navuna toka shambani nimepewa kila gunia 140,000/

Yaelekea ina bei sana kule Nchi Kenya na hata kwingineko!
Ngoja wadau waje!
Mkuu natumaini hujayauza kwa bei hiyo kwa sababu bei ya gunia moja ni zaidi ya hicho kiwango.Nina fikiria kulima hayo maharage Ruvuma,huku hakuna shida ya mvua.Ningependa kujua mbegu zake vipi na kila heka ina toa kiasi gani in terms ya gunia.
 

Kivumah

JF-Expert Member
Jan 7, 2008
2,430
2,000
Mwaka huu nimepata gunia 6 ya zao hili na wakati navuna toka shambani nimepewa kila gunia 140,000/

Yaelekea ina bei sana kule Nchi Kenya na hata kwingineko!
Ngoja wadau waje!
@ Red, Mkuu funguka basi, mbegu zake zinapatikana wapi, ulimaji wake ukoje, hali ya hewa n.k
 

gmosha48

JF-Expert Member
Oct 19, 2010
2,391
2,000
Hiyo kitu wataalam wanaita Fiwi. Tumewahi kufanya market research ya hii kitu miaka ya 2003/ au nne kwa maeneo ya Same na Babati. Sehemu kubwa ya zao hili kutoka Tanzania inauzwa Kenya an India.
 

Kig

JF-Expert Member
Aug 13, 2012
1,069
1,250
Yaani gunia zima linauzwa tsh 140,000 tu halafu tunasema haya maharage yana bei sana. Hilo gunia lina kilogram ngapi? Kwa nini tuendelee kuuza vitu kwenye kipimo cha gunia badala ya kupima uzito kwa kgs. Gharama za kuzalisha gunia moja la hayo maharagwe ni sh ngap? Maana tusiangalie tu pato la jumla tuangalie tofauti ya gharama ya uzalishaji na bei ya bidhaa ndio tujue kuna faida au hasa. Bei kuwa na figure kubwa haimanishi kuna faida kwa mkulima.
 

LiverpoolFC

JF-Expert Member
Apr 12, 2011
11,019
2,000
@ Red, Mkuu funguka basi, mbegu zake zinapatikana wapi, ulimaji wake ukoje, hali ya hewa n.k

Kivumah! Haya maharage yanapatikana ktk mbegu ya aina zaidi ya tatu na inastahili ukame na hata mvua nyingi! Na hayana gharama ktk kusema unatumia dawa kwani si rahisi kushambuliwa na wadudu waharibifu kwa mazao!
Na ktk ekari moja waweza hata ukapata zaidi ya gunia kumi na mbili.

Kwa kweli ni zao moja ambalo ni zuri sana ktk hali ya biashara kwani hapa A town ina wateja sana!
Ila sasa Mi hizo chache nilizouza kwa bei hiyo ni kwmb wamenikuta nilikuwa ktk wakati mgumu sana shambani na nikaamua kuuza kusudi nijikombowe kwa muda ule!
Ila kuna kipindi hata gunia moja yenye debe 6 huuzwa mpaka laki mbili bila ya kukosea.

Kwa ujumla ni zao safi sana kwa biashara jamani na mbegu zake utazipata ktk maduka ya TFA hapa Ar
 

Kivumah

JF-Expert Member
Jan 7, 2008
2,430
2,000
Kivumah! Haya maharage yanapatikana ktk mbegu ya aina zaidi ya tatu na inastahili ukame na hata mvua nyingi! Na hayana gharama ktk kusema unatumia dawa kwani si rahisi kushambuliwa na wadudu waharibifu kwa mazao!
Na ktk ekari moja waweza hata ukapata zaidi ya gunia kumi na mbili.

Kwa kweli ni zao moja ambalo ni zuri sana ktk hali ya biashara kwani hapa A town ina wateja sana!
Ila sasa Mi hizo chache nilizouza kwa bei hiyo ni kwmb wamenikuta nilikuwa ktk wakati mgumu sana shambani na nikaamua kuuza kusudi nijikombowe kwa muda ule!
Ila kuna kipindi hata gunia moja yenye debe 6 huuzwa mpaka laki mbili bila ya kukosea.

Kwa ujumla ni zao safi sana kwa biashara jamani na mbegu zake utazipata ktk maduka ya TFA hapa Ar
..Asante Mkuu. Nitapita TFA
 

ANKOJEI

JF-Expert Member
Nov 11, 2010
701
250
Bosi tutafutane nko Arusha kwa sasa,
Kivumah! Haya maharage yanapatikana ktk mbegu ya aina zaidi ya tatu na inastahili ukame na hata mvua nyingi! Na hayana gharama ktk kusema unatumia dawa kwani si rahisi kushambuliwa na wadudu waharibifu kwa mazao!
Na ktk ekari moja waweza hata ukapata zaidi ya gunia kumi na mbili.

Kwa kweli ni zao moja ambalo ni zuri sana ktk hali ya biashara kwani hapa A town ina wateja sana!
Ila sasa Mi hizo chache nilizouza kwa bei hiyo ni kwmb wamenikuta nilikuwa ktk wakati mgumu sana shambani na nikaamua kuuza kusudi nijikombowe kwa muda ule!
Ila kuna kipindi hata gunia moja yenye debe 6 huuzwa mpaka laki mbili bila ya kukosea.

Kwa ujumla ni zao safi sana kwa biashara jamani na mbegu zake utazipata ktk maduka ya TFA hapa Ar
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom