Kilichojiri Mkutano na waandishi wa Habari CUF-Chama cha Wananchi upande wa Maalim Seif 09.03.2019

knock knock

JF-Expert Member
Mar 8, 2018
326
384
MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI
(PRESS CONFERENCE)

THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF – Chama Cha Wananchi)

MAELEZO YA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-CHAMA CHA WANANCHI) MBELE YA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MUENDELEZO WA HUJUMA ZINAZOFANYWA NA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA NCHINI JAJI FRANCIS KATABAZI MUTUNGI DHIDI YA CUF KWA KUMTUMIA WAKALA WA USAJILI, UFILISI NA UDHAMINI (RITA) PAMOJA NA MSHIRIKA WAO IBRAHIM HARUNA LIPUMBA NA GENGE LAKE

Imetolewa leo Tarehe 09/03/2019 Katika Ukumbi wa Ofisi ya Wabunge wa CUF, Magomeni -Dar Es Salaam.

Ndugu Waandishi wa Habari,
Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia uhai na uzima na kutuwezesha kukutana leo hapa kwa lengo la kuelezea njama na mbinu chafu zinazofanywa na Msajili wa vyama vya Siasa nchini jaji Francis Katabazi Mutungi kwa kutumia Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini(RITA) na kibaraka wake Ibrahim Haruna Lipumba dhidi ya Chama chetu THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-Chama cha Wananchi) ambazo nitazielezea muda mfupi ujao.

Pili, nawashukuru ninyi waandishi wa habari kwa kupokea mwaliko wetu na kuhudhuria mkutano huu. Siku zote mmetupa mashirikiano makubwa katika shughuli zetu na kuufikisha ujumbe wetu kwa umma wa Watanzania na ulimwengu kwa ujumla. Ahsanteni sana.

Ndugu waandishi wa habari,

Mtakumbuka vyema tarehe 28 Juni, 2017 katika ukumbi wa Hotel ya Ramada Encore Dar City Centre jijini Dar es salaam Katibu Mkuu wetu Maalim Seif Sharif Hamad alitoa maelezo ya kina na ya kutosha kwa kile kilichofanywa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa maelekezo ya Msajili wa vyama vya siasa jaji Francis Katabazi Mutungi kwa lengo la kumnusulu kibaraka wake Ibrahim Haruna Lipumba kwa kuhakikisha kwamba Wajumbe wa Bodi feki waliopelekwa na kibaraka Lipumba wanasajiliwa baada ya kuona Bodi halali ya CUF-Chama cha Wananchi ni kikwazo katika kufanikisha mipango yao haramu ya kufungua akaunti mpya ya benki ili kuwezesha wizi wa ruzuku ya Chama.

Lakini pia alieleza masuala kumi (10) yaliyokuwa yanafanywa na serikali ya awamu ya tano kuhujumu Demokrasia na misingi ya Utawala bora ikiwa ni pamoja na;-

1. Kupiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa nchi nzima.

2. Kuzuia matangazo ya moja kwa moja (live broadcasting) ya mikutano ya Bunge ili kuwaziba macho na masikio Watanzania wasisikie mijadala ya Bunge.

3. Kufinya bajeti ya shughuli za Kamati za Bunge ili zisiweze kufanya kazi ya kuisimamia serikali.

4. Kuwakamata, kuwabughudhi, kuwalaza ndani na kuwafungulia mashtaka Wabunge, Madiwani na viongozi wa upinzani.

5. Kuzipa Mahakama maagizo hadharani ya jinsi ya kuamua kesi.

6. Kuwakamata, kuwaweka ndani na kuwafungulia mashtaka watumiaji wa mitandao ya kijamii, wengi wao wakiwa ni vijana, wanaoandika maoni yao kuwakosoa watwala kwa kutumia Sheria ya Makosa ya Mtandao (Cybercrimes Act), sheria ambayo tokea awali ilipingwa kuwa ni sheria kandamizi.

7. Kuwatisha waandishi wa habari na vyombo vya habari hadharani na kufikia hatua ya kuyafungia magazeti yanayoongoza kwa kuandika habari zinazokosoa watawala na kuwakamatana kuwashtaki wahariri na waandishi wa habari.

8. Kuwatishia na kuwakamata wasanii hasa wale wanaotumia vipaji vyao kuwakosoa watawala na kuwazindua Watanzania juu ya mwenendo mbaya wa serikali.

9. Kutishia jumuiya za kiraia zinazojishughulisha na masuala ya Haki za Binadamu, Sheria na Utawala Bora kwa lengo la kuzinyamazisha ili zisitimize wajibu wake kwa jamii.

10. Wakuu wa mikoa na wilaya kujipa mamlaka wasiyokuwa nayo kisheria ya kuitia watu polisi na kutoa amri wakamatwe na kuwekwa ndani, jambo ambalo limelalamikiwa hata na Mkurugenzi mstaafu wa makosa ya jinai, Mhe, Adad Rajab kwamba ni kinyume cha sheria.

Kadhalika alieleza kwa kina hujuma zilizokuwa zinafanywa na dola dhidi ya CUF-Chama cha Wananchi hasa baada ya mafanikio makubwa na ushindi wa kutosha uliopatikana Zanzibar katika uchaguzi wa Oktoba, 2015.
Hujuma hizo dhidi ya CUF-Chama cha Wananchi ndizo zilizaa kesi thelathini na tisa (39) hadi kufikia Tarehe 27 Februari, 2019. Wengi wenu mmekuwa mkifuatilia kesi hizo na kushuhudia ubabaishaji mkubwa wa Msajili wa Vyama vya siasa na vibaraka wake katika kujenga hoja za utetezi. Zaidi ndugu waandishi wa habari ninyi ni mashahidi wa ushindi mkubwa wa Chama Taasisi katika mashauri hayo. Katika keso hizo 39 tayari Chama kimepata ushindi katika kesi/mashauri 18 na nyingine bado zinaendelea Mahakamani hazijafika mwisho.

Leo hatukusudii kurudia kwa urefu mtiririko wa matukio yaliyoanza wakati huo lakini tumewaita kuweka bayana mambo mawili muhimu yafuatayo;

1. USAJILI WA WAJUMBE FEKI WA BODI WA LIPUMBA KWA MAELEKEZO YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA JAJI WA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA FRANCIS KATABAZI MUTUNGI

Ndugu waandishi wa habari;

Mtakumbuka kuwa mnamo tarehe 12 Juni, 2017 Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa maelekezo ya jaji Francis Katabazi Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa alisajili kinyume kabisa cha sheria, watu walioitwa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini (purported trustees) wa CUF-Chama cha Wananchi kwa lengo la kufuta kesi zote zilizokuwa zimefunguliwa dhidi ya Msajili wa vyama vya siasa, Lipumba na genge lake na kuweza kufungua akaunti ya Bank kwa minajili ya kuwezesha wizi wa ruzuku ya serikali iliyostahiki CUF-Chama cha Wanachi.

Jaribio la kufuta kesi kupitia barua iliyowasilishwa kwa Msajili wa Mahakama Kuu tarehe 19/6/2017 lilishindikana baada ya kuthibitika na mahakama kuwa wajumbe feki waliosajiliwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini(RITA), hawakuwa wahusika wa kesi hizo kwa sababu kesi zilifunguliwa na Bodi kama taasisi (Corporate entity) na sio wajumbe wa Bodi (trustees). Muhimu kufafanua hapa kuwa kisheria, Bodi kama taasisi haifi au kupoteza nguvu yake kwa kupungukiwa au kufa wajumbe wake. Bodi huendelea kuwa hai na uwezo wake wa kushitaki na kushitakiwa hubaki mpaka inapokuwa imefutwa kisheria. Hiyo inatokana na dhana ya uendelevu (perpetual succession). Baada ya jaribio hilo kushindikana, kutokana na upotoshwaji uliokuwa ukifanywa na wakili wa Lipumba Mashaka Ngole na maelekezo ya Msajili Mutungi, Lipumba na genge lake walifungua mashauri manne (4) wakiomba kuingia katika kesi zilizofunguliwa na Bodi kama wadaawa (to join as interested parties) wakitafuta fursa ya kuzihujumu. Jaribio hilo la pili nalo pia lilishindindikana baada ya kushindwa kujenga hoja kinzani zenye mashiko katika mashauri yote na hivyo kufutiliwa mbali. Hata walipojaribu kukata Rufaa katika shauri la ruzuku Mahakama ya Rufaa pia walishindwa na kesi yao kutupwa kwa gharama.

Lengo la kufungua akaunti kuwezesha wizi wa fedha za ruzuku ya Chama lilifanikiwa baada ya kula njama na tawi la Bank ya NMB Temeke ambalo liliruhusu ufunguaji wa akaunti Na. 2072300456 na kuwezesha uporaji wa jumla ya Tshs. 1,076,982,032.12 hadi kufikia tarehe 20 Januari, 2018. Aidha NMB tawi la Malindi Zanzibar liliruhusu kufunguliwa kwa akunti nyingine Na. 22910021328 ikimilikiwa na Haroub Shamis, Khalifa Suleiman Khalifa na Mohamed Habib Mnyaa lakini akaunti hii haikufanikisha utoroshaji wa fedha kutokana na msajili kujifunga kwa kutaka akaunti ya ruzuku kuwa moja tu kwa kila Chama.

Chama kilifungua shauri Na. 68/2017 kuomba kibali (leave) kuwasilisha MAOMBI RASMI YA UCHUNGUZI JUU YA WIZI WA RUZUKU na baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu ya Dar es salaam, kutoa kibali tayari Bodi ya Wadhamini imefungua kwa hati ya dharura (Certificate of Urgency) shauri la msingi Na. 2/2019 (Miscellaneous Cause No. 2/2019) sanjali na shauri dogo Na. 7/2019 (Miscellaneous Civil Application No. 7/2019) ambayo yamepangwa kutajwa tarehe 14 Machi, 2019 mbele ya jaji Mpogolo.

Ndugu waandishi wa habari;

Mtakumbuka kuwa wajumbe feki wa Lipumba waliosajiliwa tarehe 12 Juni, 2017 na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa maelekezo ya Msajili wa vyama vya siasa jaji Francis Katabazi Mutungi, walipingwa Makakamani na Mhe. Ally Saleh Mbunge wa CUF jimbo la Malindi kupitia shauri Na. 13/2017 na kushinda kesi hiyo ambapo Mahakama ilifutilia mbali usajili wao tarehe 18 Februari, 2019.
Katika hukumu yake jaji Benhajj Masoud alitoa mapungufu kadhaa yafuatayo;

Mapungufu yaliyobainiwa na Mahakama katika mawasilisho ya Lipumba na Sakaya;

1) Hakukuwa na kikao halali kwa mujibu wa Katiba ya CUF

2) Kaimu Katibu Mkuu Magdalena Sakaya si cheo kinachotambuliwa na Katiba ya CUF

3) Usajili ulizingatia maelekezo ya Msajili wa vyama vya siasa na si matakwa ya sheria

4) Lipumba na Sakaya ni viongozi wa CUF wenye mashaka tangu 21/8/2016 na 28/8/2016 kila mmoja kwa upande wake

5) Kikao cha uteuzi hakikusimamiwa na mamlaka ya serikali

6) Fomu TI4 na TI5 zilikuwa na makosa

7) Hakukuwa na muhtasari wa kikao cha uteuzi

8) Mihutawsari yote iliyowasilishwa ilikuwa haina akidi (quorum)

9) Lipumba na Sakaya hawakuitwa kutoa ushahidi na hazikuelezwa sababu za kutoitwa kwao

10) Masharti ya kifungu cha 17(1) cha sheria ya Muunganiko wa Wadhamini (The Trustees Incorporation Act Cap 318 RE 2002) hayakuzingatiwa

Mahakama imebaini mapungufu yafuatayo kwa upande wa mawasilisho ya Katibu Mkuu Seif Sharif Hamad;

1) Kikao cha uteuzi hakikusimamiwa na mamlaka ya serikali

2) Hakukuelezwa sababu kwa nini kilisimamiwa na Katani Ahmed Katani badala ya Mwenyekiti wa Taifa kama yalivyo matakwa ya Katiba ya CUF.

3) Katibu Mkuu hakuja kutoa ushahidi na hazikuelezwa sababu na kutoitwa.

[Mawasilisho ya Katibu Mkuu yalipitiwa kwa faida tu (interest of justice) kwa sababu chini ya kifungu cha 26 cha sheria ya Muunganiko wa Wadhamini (The Trustees Incorporation Act Cap 318 RE 2002) hakukuwa na sababu kwa wajumbe ambao hawakusajiliwa kujadili suala lao]

Kutokana na mapungufu hayo Mheshimiwa Jaji Benhajj Masoud alifutilia mbali wajumbe FEKI wa bodi ya Wadhamini wa Lipumba waliosajiliwa na RITA.

MUENDELEZO WA MIKAKATI YA HUJUMA DHIDI YA CUF

Ndugu waandishi wa habari,

Katika hali isiyo ya kawaida Msajili wa vyama vya siasa alifanya kikao na genge la Lipumba tarehe 19/2/2019 na kuwasilisha majina upya RITA wakiomba usajili. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Lipumba kwa vyomo vya habari, kikao hicho cha uteuzi kilihudhuriwa na wajumbe 40 wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kati ya Wajumbe wote aliodai ni 49. Unaweza kujiuliza swali la udadisi, kuwa kutoka wajumbe 15 waliohudhuria vikao vya uteuzi uliopita, wakiwemo marehemu wawili, sasa wajumbe 40 wamepatikanaje? Ni lini uliitishwa Mkutano Mkuu wa Taifa kufanya uchaguzi wa wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa? Ajabu katika mazingira yale yale ya kughushi na ubabaishaji, tarehe 6/3/2019 Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) amesajili majina yaliyowasilishwa na Lipumba kwa maelekezo ya Msajili wa vyama vya siasa kuwa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya CUF-Chama cha Wananchi. Kwa mara nyingine tena; licha ya barua ya Katibu Mkuu kumtanabaisha, wajumbe wa kikao halali cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa kilichohudhuriwa na jumla ya wajumme 37 na kwasilishwa na Katibu Mkuu RITA hawakusajiliwa.

Ni dhahiri njama na hujuma za Msajili wa vyama vya siasa jaji Mutungi zinaendelea. Na kikubwa hapa kinachotafutwa ni mambo mawili. Moja ni kutaka kulinda wizi wa ruzuku na pili kufuta kesi zote ikiwemo ile maarufu Na. 23/2016 inayotegemewa kutolewa hukumu tarehe 18 Machi, 2019; baada ya kuhairishwa mara nne, ambayo Msajili wa vyama vya siasa jaji Mutungi ni mtuhumiwa mkuu.

Ni imani yetu kama walivyoshindwa katika jaribio la kwanza mwaka 2017, watashindwa katika hatua hii ya sasa. Hata hivyo, kutokana na haja ya kupata haki ya kisheria mahakamani, wasomi mawakili wa Chama wako katika hatua za mwisho za kuwasilisha kesi mahakamani kupinga usajili huo wa kihuni na usiozingatia sheria na katiba ya CUF-Chama cha Wananchi (Toleo la 2014).

2. KUHUSU KUFANYIKA KWA MKUTANO MKUU FEKI WA LIPUMBA NA GENGE LAKE:

Baada ya kuona CUF-Chama cha Wananchi kimeendelea kusimama imara kujilinda kupitia hatua za kisheria na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa, sasa dola imeamua kukamilisha mpango wake mchafu na haramu kwa kumtumia kibaraka na malaya wa kisiasa Ibrahim Haruna Lipumba kuitisha mkutano mkuu feki kumfukuza uanachama Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad na viongozi wenzake halali.

Ndugu waandishi wa habari;

Njama za kutaka kumuengua Katibu Mkuu kinyume na Katiba kama zilivyobainishwa katika mawasiliano ya siri kati ya jaji Francis Mutungi na kibaraka Lipumba sasa ndio zinashika kasi. Njama hizo zinaendeshwa kwa mashinikizo makubwa ya dola kupitia taasisi ya Msajili wa vyama vya siasa, kwa ufadhili mkubwa wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kwa lengo la kuisambaratisha kabisa CUF. Ndugu waandishi wa habari jambo hilo sio siri, kwani wakati wa usikilizwaji wa shauri Na. 13/2017 la Mheshimiwa Ally Saleh dhidi ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) na wenzake, wakili mkuu wa serikali Gabriel Malata alitamka bayana mahakamani kuwa kesi za CUF zinaendeshwa kwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hujuma dhidi ya CUF ni kwa kiwango hicho.

Tunaelezwa kuwa katika lengo kuu hilo kuna lengo mahsusi ambalo ni kummaliza kabisa kisiasa Maalim Seif Sharif Hamad ambaye anaonekana mwiba mkali kwa CCM. DHAMBI KUU YA MAALIM SEIF NI KUSHINDA KWA ASILIMIA KUBWA UCHAGUZI MKUU WA URAIS WA ZANZIBAR MWAKA 2015 NA KULE KUBAKIA KUWA NGUZO KUU YA CUF KATIKA KUENDELEZA UMOJA WA WAPINZANI (UKAWA NA VYAMA VINGINE) AMBAO UNAHATARISHA NAFASI YA CCM KATIKA SIASA ZA TANZANIA. Haya ni miongoni mwa sababu za kuandaliwa na kupitishwa haraka Muswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa (The Political Parties Ammended Act 2018) kuhakikisha kuwa Msajili wa vyama vya siasa anakuwa na mamlaka makubwa kudhibiti kisheria vyama vya siasa, kuweka katazo la kumshitaki mahakamni na hivyo kukandamiza demokrasia ya vyama vingi nchini.

Chama kilikwisha pata taarifa za njama hiyo ya uitishwaji wa Mkutano Mkuu wa Taifa feki wa Lipumba na Msajili Mutungi na kupitia Manibu Katibu Mkuu Mhe. Joran Lwehabura Bashange na Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, mapema tarehe 9 Mei, 2018 walifungua shauri mama Na. 84/2018 (Civil Case No. 84/2018) na shauri dogo Na. 248/2018 (Miscellaneous Civil Application No. 248/2018) kupinga kuitishwa kwa Mkutano huo feki. Mashauri hayo yalimuhusisha wakili wa Lipumba Mashaka Ngole ambaye amekuwa akijihusisha na mambo ya utawala na uongozi wa Chama wakati hana wadhifa wowote kikatiba.

Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala ya Dar es salaam mbele ya Mheshimiwa Jaji Magoiga, Tarehe 28 Februari, 2019 ilitoa hukumu baada ya kuhitimisha kusikilza shauri dogo Na. 248/2018 na KUTOA AMRI YA ZUIO (COURT INJUNCTION ORDER) IKIMZUIA LIPUMBA NA GENGE LAKE, WAKALA WAO AU YEYOTE ANAYEFANYA KAZI CHINI YAO; KUITISHA MKUTANO MKUU WA TAIFA KWA JINA LA CUF-CHAMA CHA WANANCHI MPAKA HAPO SHAURI LA MSINGI NA. 84/2018 LITAKAPOSIKILIZWA NA KUTOLEWA UAMUZI. Amri hiyo inapatikana katika ukurasa wa 8 na 9 wa hukumu ya Mheshimiwa Jaji Stephen Magoiga ambayo tutawapatia nakala yake ili muweze kuipitia kwa ushuhuda na hatua zenu.

Kwa jeuri na majivuno, Lipumba na genge lake baada ya kikao mkakati na msajili wa vyama vya siasa (ambaye kwa sasa kutokana na uhovyo wake anaoufanya katika kadhia hii ndani ya CUF ameharibu kwa kiwango kikubwa hadhi na kuivunjia heshima taaluma na cheo cha UJAJI), wameazimia kupuuza amri hiyo ya mahakama na kuamua kendelea na Mkutano Mkuu wao huo FEKI kama walivyotangaza kuwa utafanyika tarehe 12–15 Machi, 2019 katika ukumbi wa LEKAM uliopo Buguruni Malapa wilaya ya Ilala Dar es salaam. Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa ya Jaffari Mneke kupitia vyombo vya habari Tarehe 6/3/2019. Tayari Msajili wa vyama vya siasa alikwisha wapatia fedha takribani shilingi bilioni moja (1 billion). Taarifa kutoka vyanzo sahihi zinaonyesha kuwa wameshafanya maandalizi yote ikiwemo uchapishaji wa fulana (Sampuli hii hapa), kuchoresha mabegi ya Mkutano huo na kuhakikishiwa ulinzi wa polisi.

CUF – Chama cha Wananchi kwa kuheshimu utii wa sheria kimemwandikia barua Inspekta Generali wa Polisi (IGP Simon Sirro) kumtanabaisha juu ya hatua hiyo na kunakili barua hiyo kwa Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali, Mkuu wa Polisi (RPC) mkoa wa Ilala, OCD kituo cha Polisi Buguruni na jumuiya ya Kimataifa kuwataarifu juu ya kusudio la uvunjaji wa AMRI HALALI YA MAHAKAMA (DISOBEDIENCE OF COURT ORDER AND RULE OF LAW BY THE REGISTRAR OF POLITICAL PARTIES, JUDGE FRANCIS SALES KATABAZI MUTUNGI, LIPUMBA AND THEIR ALLIES). Katika hatua nyingine, Meneja wa ukumbi wa LEKAM amepewa taarifa kumtaadharisha juu ya kujiingiza katika jinai ya kuingilia uhuru wa mahakama (Contempt of Court) endapo ataendelea kukubali ukumbi wake kutumika kuvunja amri ya Mahakama. Barua hiyo kwa Meneja wa ukumbi wa LEKAM imenakiliwa kwa mkuu wa kituo cha polisi cha Buguruni.

Ni imani yetu kuwa kwa hatua hizo zilizochukuliwa na Chama, Msajili Mutungi, Lipumba na genge lake watatafakari upya kusuka au kunyoa. Wasomi mawakili wa Chama wako katika hali ya tahadhari kuchukuwa hatua endapo itabidi kufanya hivyo.

Aidha, Chama kinatoa wito na tahadhari kwa wale wote wanaojiita wajumbe wa Mkutano Mkuu huo FEKI wa Lipumba, kutokuja Dar es Salaam kwa makusudio hayo. Wanachama wa CUF Jijini Dar es salaam na walinzi wote wa Chama watafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa wanakilinda Chama kwa gharama yoyote. CUF na Viongozi wake haitawazuia wanachama wake kuchukua hatua zozote kwa kadri watakavyoona inafaa ili kuzuia upuuzi huu wa Lipumba, genge lake na wote walionyuma yao kuwasaidia kupanga, kuratibu na kutekeleza hujuma na upuuzi wao dhidi ya CUF. Kwa hakika dunia imeshuhudilia ustaarabu na uvumilivu wetu kwa kiasi cha kutosha, tunasema Inatosha, tunasema Inatosha, tunasema Inatosha, sasa basi.


HAKI SAWA KWA WOTE

____________________________________
JORAN LWEHABURA BASHANGE
NAIBU KATIBU MKUU(B)

Contact Persons:
Director: Salim Bimani +255777 414112, +255655 314112
Deputy Director: Mbarala Maharagande +255767 062577, +255715 062577

email: cufhabari2008@yahoo.com
email: maharagande@gmail.com
 
Baada ya ile rushwa ya mil 300 kuwadhalilisha makamu wawili wa Rais baada ya wasamalia wema kuvujisha siri , jambo lililosababisha jaji kukimbia siku ya hukumu wameamua sasa kutumia njia ya kimafia bila aibu yoyote ile
 
Ukiona mtu kaandika mada ndefu hata kusoma unaona unachoka Sana ujue aliyeandika mwongo
 
Halafu anatokea mtu anatamba kabisa eti upinzani umekufa, au eti CCM wanashinda/watashinda chaguzi kwa kishindo.

Ukweli uliodhahiri CCM bila Dora hawawezi shinda uchaguzi wowote ule.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Nasikia Lissu anatarajia kuungana na Lipumba kupeperusha bendera 2020 kupitia CUF. Tz raha sana kura zangu 6M mumpatie nanihii mmesikia...
 
Nasikia Lissu anatarajia kuungana na Lipumba kupeperusha bendera 2020 kupitia CUF. Tz raha sana kura zangu 6M mumpatie nanihii mmesikia...
...hahaaaaa uyo manywele anazani izo kura alitunziwa stoo! lipumba haeleweki kama ilivyo seifu na mbowe hapo ndo huwa naamini siasa ni biashara nchi hii
 
Back
Top Bottom