Kikwete, usiwasikilize CHADEMA; msikilize Lowassa

JOHN MADIBA

JF-Expert Member
Jan 30, 2011
251
155
Tangu Serikali ya awamu ya nne ichukue madaraka mwaka 2005, kumekuwa na malalamiko yasiyoisha kwenye fasheni, kuwa Serikali hii inaogopa kuchukua maamuzi magumu.

Waandishi na wachambuzi wameibatiza hali hii na tabia hii majina mengi. Wapo walioiita kuwa ni ombwe la uongozi. Wapo waliosema nchi iko kwenye "auto-pilot" yaani inajiendesha kama ndege kubwa ikishafika kwenye anga za juu.

Wengine wamesema Serikali iko likizo, huku wengine wakisema Serikali hii imeugua kigugumizi kikali. Yote haya yanalenga kueleza ukweli kuwa Serikali yetu hii inashindwa kufanya maamuzi magumu.

Matokeo ya kusita sita huku, ama hali ya nchi inaelekea kwenye giza na ombwe la utawala, au panajitokeza dalili za kuibuka kwa mtawala mwingine anayeweza kutupeleka mahali tusipotaka maadam anaonekana kuchukua hatua za kutuongoza. Ikumbukwe kuwa hata wanaoelekea kuangamia huwa wana kiongozi anayewapeleka huko.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekuwa kikiipigia kelele hali hii ya kukosa mwelekeo na uongozi thabiti. Kwa muda mrefu, kimebezwa na watawala wanaodai CHADEMA ni chama cha Upinzani ambacho kazi yake ni kupinga tu na kujifanya vipofu wa kutokuona mazuri yanayofanywa na Serikali.

Rais Kikwete amekibatiza CHADEMA majina mbalimbali, mabaya na yenye kejeli nyingi chama hiki na kuwakebehi viongozi wake hadharani. Mara awaite ni wana harakati, mara aseme wanapayuka mpaka povu linawatoka mdomoni, mara akiite CHADEMA kuwa ni chama cha msimu na wakati mwingine aseme hakijajipanga kushika dola.

Matokeo ya kebehi hizi ni Rais mwenyewe na wasaidizi wake kutokuchukua muda kushughulikia kero za wananchi kwa kudhani kuwa wakifanya hivyo CHADEMA kitaonekana kimesema ukweli.

Wakati fulani, Rais na wakuu wa vyombo vya dola walikutana kujadili namna ya kushughulikia malalamiko ya wananchi na wahisani kuhusu rushwa na ufisadi. Katika mkutano huo, waliishia kusema kuwa wakishughulikia masuala hayo wataonekana wanawaunga mkono CHADEMA na agenda yao ya ufisadi.

Mkutano uliisha bila hitimisho linaloeleweka kwa hofu kuwa kuchukua hatua thabiti juu ya malalamiko ya wananchi na wahisani wanaokwamishwa na urasimu wa kifisadi, itaonekana Serikali imejisalimisha kwa CHADEMA. Serikali nzima inaona bora ijisalimishe kwa mafisadi kuliko kuonekana inakubaliana na CHADEMA.

Katika vikao vya baraza la mawaziri na hata katika vikao vya pamoja vya makatibu wakuu wa wizara mama, kila wakati mjadala wa kumaliza kero kuu zinazowasumbua wananchi haumaliziki kwa sababu ya kusita kuchukua hatua ambazo zitatafsiriwa kuwa zinakiunga mkono CHADEMA.

Kila mtendaji anayejitokeza katika vikao hivyo kupendekeza njia mbadala ya kumaliza tatizo la kero za wananchi, anaanza kuchunguzwa kama ana uhusiano na CHADEMA. Matokeo ya kusita huku, ni Serikali kuonekana iko likizo au haina ubavu wa kushughulikia masuala magumu na kukimbilia kushughulikia mambo mepesi mepesi.

Kimsingi, CHADEMA kimeifikisha Serikali mahali ambapo hata yenyewe haikutarajia kuwa ingefika kirahisi katika eneo hilo la kupooza kivitendo.

Wiki iliyopita, Waziri Mkuu aliyejiuzuru kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa aliamua kuzungumza bungeni. Mambo kadhaa kabla ya kuchambua alisema nini, yafaa yatajwe. Kwanza, kuzungumza kwake kuliwashtua wengi kwa sababu kulionekana kuwa kulikuwa kunasubiriwa sana.

Pili, wabunge wengi waliunga mkono maneno yake na kuonekana kuvutiwa na hotuba yake. Tatu, tofauti na wengi tulivyotarajia, alizungumza kwa kujiamini sana. Haya matatu, yanahitaji mada pekee siku zijazo kwa sababu yalituma ujumbe mzito kwa wale waliokuwa wanaimba wimbo wa kujivua gamba. Hili tuliache kwa sasa.

Lowassa bila kumung'unya maneno alisema Serikali inaogopa kuchukua hatua kwa kufanya maamuzi magumu. Pili, alisema Serikali hii imefanya mengi katika miaka 50 lakini inapata kigugumizi kuelezea mafanikio hayo.

Tatu, alisema Taifa lina utajiri mkubwa sana wa rasilimali za asili ambazo hazijatumiwa na kama zikitumiwa vizuri shida ya umasikini itaisha. Yote matatu, Serikali imeshindwa kuyashughulikia kwa hofu ya kuogopa kulaumiwa. Lowassa akaipa ushauri nasaha kuwa, ni heri kulaumiwa kwa kufanya maamuzi mabaya au kuyafanya vibaya kuliko kulaumiwa kwa kutokufanya chochote.

Ujumbe wa Lowassa ni mzito kwa Serikali na chama chake. Itake isitake, yeye amesema hata kama ujumbe wake unafanana sana na ujumbe wa CHADEMA ambao umekuwa unapuuzwa kwa muda mrefu. Serikali isiyoamua na kutenda haina tofauti na kutokuwa na Serikali. Watendaji wa Serikali wanakwepa sana kufanya maamuzi na ‘kuwasakizia' wengine.

Rais wetu amediriki kufungia majalada mengine kabatini baada ya kujaa mezani na kumnyima nafasi ya kufanya kazi nyingine. Kuna watendaji wanafuatilia maamuzi ya madokezo ikulu kwa miezi mingi na wasiweze kupata majibu ya madokezo yao.

Kwanza kwa nini madokezo mengi yaende Ikulu? Kwa nini madokezo yatoke Ikulu kwenda Lumumba? Kwa nini yarudi kutoka Lumumba yakiwa hayana majibu? Kwa nini yanapandishwa kwenye ndege ya Serikali kwenda Chamwino, Dodoma halafu yanarudi Dar es Salaam bila kuamuliwa?

Kwa nini madokezo ya uteuzi yanachukua muda mfupi kuliko madokezo yanayohitaji maamuzi mengine ya utendaji? Kwa nini Rais afikie kuwalaumu baadhi ya watendaji kuwa wanashindwa kufanya maamuzi wakati ni yeye au wasaidizi wake walioagiza kuwa madokezo yaletwe kwake kwa uamuzi wa mwisho?

Pamoja na kuwa na vyama vingi vya siasa katika Taifa, maslahi ya Taifa hayana budi kutangulizwa mbele. Ustaarabu wa kisiasa huonekana pale wana siasa wanapoamua kuacha tofauti za kiitikadi na kutanguliza maslahi ya Taifa mbele.

Mathalani, kitendo cha Lowassa kuishauri Serikali ichukue hatua za kushughulikia matatizo ya wananchi kinapongezwa hata kama inafanana sana na ushauri wa CHADEMA ambao umepuuzwa kwa muda mrefu. Ukomavu wa kisiasa huonekana pale mwanasiasa mmoja au kundi wanapoamua kukatiza msitari wa kati na kwenda kwa wapinzani ili kushughulikia masuala ya msingi katika mustakabali wa Taifa.

Bila kufanya hivyo, chama tawala kinakuwa kinakaribisha hatua kali kutoka kwa wapiga kura. Kusitasita kuchukua maamuzi magumu ni dalili ya kushindwa kuwajibishana katika Serikali. Hali hii ikizoeleka hukaribisha uwezekano wa Serikali yenyewe kuwajibishwa na wananchi.

Ifike mahali CCM ikubali kuwa CHADEMA wanasema mambo ya msingi kwa Taifa, na CHADEMA pia kifike mahali kikubali kuwa kuna mambo mazuri Serikali ya CCM imefanya hata kama kwa sasa imeugua midomo na inashindwa kuyatetea na kuyaeleza vizuri kwa wananchi.

Kama CCM bado inaona shida kuwakubali CHADEMA na hoja zao, basi sasa imepata sababu nzuri ya kuendelea kuwakataa CHADEMA lakini ikafanya yale yanayosemwa na CHADEMA kwa mdomo wa Edward Lowassa.
 
basi bora wafuate ya chadema na wabadilike ili mambo yawe mazuri na kama wanataka mabadiliko hawana budi kufuatana na cdm kuliko kujipalia makaa..
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom