Kikwete ni mdhaifu, muungwana au mateka? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kikwete ni mdhaifu, muungwana au mateka?

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by Halisi, Sep 23, 2010.

 1. Halisi

  Halisi JF-Expert Member

  #1
  Sep 23, 2010
  Joined: Jan 16, 2007
  Messages: 2,810
  Likes Received: 83
  Trophy Points: 145
  Kikwete ni mdhaifu, muungwana au mateka?

  [​IMG]
  Msomaji Raia​
  Septemba 22, 2010 [​IMG]
  WIKI iliyopita nilihoji ikiwa Rais Jakaya Kikwete ni msahaulifu au ni mzembe? Nikaeleza kuwa ana uwezo mkubwa wa kukumbuka marafiki zake wa sasa na wa zamani, lakini ni mwepesi wa kusahau ahadi anazotoa katika mikutano yake ya kampeni.
  Matokeo ya tabia yake hii, siku hizi anapotoa ahadi katika mikutano ya wazi au vikao vya ndani hakuna anayejali, kwa sababu yeye “anajifanya” kuahidi na wananchi sasa “wanajifanya” kuamini. Huu mchezo wa “kujifanya” si mzuri hata kidogo, na hatima yake si nzuri huko tuendako.
  Baada ya makala hiyo, nilipokea barua pepe nyingi kutoka kwa watu mbalimbali, lakini katika makala hii nitajadili kwa kifupi moja iliyotoka kwa mtu anayeitwa Joseph. Katika hali ya dharau na kutojali, Joseph aliamua kumtetea Rais Kikwete pale alipoamua kuwatumia watu wa familia yake katika majukumu mbalimbali ya utawala wa nchi.
  Alitetea masuala mengi lakini katika makala hii napenda nijadili hoja ya Joseph kwa kubainisha kuwa si sahihi kwa Rais kuajiri au kutumia ndugu zake katika utawala wa nchi.
  Bwana Joseph alisema hivi: “Mwisho si dhambi kumteua rafiki yako, msingi awe na sifa, kwani awe rafiki, mwanao, tajiri, masikini wana haki ya kuwa viongozi. Huwezi kumbagua mtu kutokana na hali, uhusiano au chochote kile haimuondolei haki yake ya kuwa katika Ofisi ya Umma. Anabaki na haki zake kama binadamu jambo la muhimu atekeleze majukumu yake vizuri na awe na sifa, basi.”
  Tangu aingie madarakani mwaka 2005, watu wengi wamekuwa wanajadili iwapo Rais Kikwete ni kiongozi dhaifu au ametekwa na kundi fulani la watu wenye uadilifu unaotia shaka. Lipo kundi jingine ambalo hata Kikwete analiunga mkono kwa ujanja, nalo ni lile linalosema Kikwete ni kiongozi safi na muungwana lakini anaangushwa na watendaji wake. Yote haya yamejadiliwa kwa muda mrefu na sidhani kama naweza kuleta jipya katika makala hii.
  Kwangu, yote matatu yana ukweli usiopingika unapoiangalia historia ya utawala wa Rais Kikwete. Ni kweli, Kikwete ni kiongozi dhaifu, tena mwenye ujasiri mkubwa wa kunadi udhaifu wake! Ni kweli, Kikwete ni mateka wa kundi la mafisadi waliosaidia kumwingiza madarakani. Walimpa kila kitu alipoingia madarakani, lakini wakamnyima uhuru wa kufanya maamuzi yanayoweza kugusa maslahi yao.
  Miaka mitano inaisha, Kikwete amebaki ni mateka wa kundi hilo, akitii bila kuhoji maelekezo yote anayopata kutoka kundi hilo. Kundi hili lina nguvu, fedha na ushawishi mkubwa na kwa hiyo, limemuweka Rais Kikwete katika hali ngumu sana.
  Ni kweli pia, watendaji wake aliowateua kumsaidia wanapungukiwa na mambo mengi ya msingi yanayowafanya wasiweze kutenda kazi zao kwa misingi na weledi unaohitajika.
  Sifa moja ya kiongozi mdhaifu ni kupenda kufanya kazi na watu wasio makini ili wanapofanya makosa iwe rahisi kwake kujitetea kuwa anaangushwa na watendaji. Sifa nyingine ya kiongozi mdhaifu ni hulka ya kuajiri watu kwa misingi ya urafiki, undugu na ushabiki.
  Kiongozi mdhaifu hupenda kundi hili kwa sababu huwa hajiamini, na hivyo kuishi kwa hofu ya mambo yasiyoonekana. Ili kujilinda na hofu hii, kiongozi mdhaifu huona ni vema akawa na ndugu na marafiki katika nafasi mbalimbali ili awe “salama”. Utetezi wa Joseph hapo juu unathibitisha dalili hii.
  Katika asasi zilizo na maadili ya utendaji, ni marukufu kwa ndugu wawili kufanya kazi katika asasi hiyo au asasi tanzu yake. Hata ikitokea mtu anaingia kwa kuchaguliwa na si kuajiriwa katika taasisi hiyo, wale walio ndugu zake, hulazimika kuondoka.
  Wakati mwingine fursa ya mtu huyo kuchaguliwa inaweza kuzuiwa na uwepo wa ndugu zake kadhaa katika ajira za asasi hiyo. Hii hufanyika ili kuepusha uwezekano wa migongano ya kimaslahi.
  Kwa mantiki hii, utetezi wa Joseph kuwa Kikwete anao uhuru wa kuajiri ndugu, marafiki na watoto wake kwa sababu tu wanazo sifa, hauna nguvu hata kidogo kwa sababu, mara nyingi hata kuwa ndugu au mtoto wa anayeajiri ni sifa inayomwondolea mtu uwezekano wa kuajiriwa.
  Tumewahi kusikia Rais wa Benki ya Dunia, Paul Wolfowitz alivyoachishwa wadhifa wake huo baada ya kugundulika kuwa rafiki yake wa kike alikuwa amepandishiwa mshahara na marupurupu.
  Hapa Tanzania, wakati nchi ikiwa bado katika misingi ya uadilifu, kwa kiongozi kuonekana anaongozwa na mashinikizo ya familia, ilitosha mtu huyo kuondolewa katika wadhifa huo. Mama mmoja maarufu aliwahi kuwekwa kwenye “kizuizi” cha nyumbani kwa kujaribu kuingilia majukumu ya idara nyeti ya Serikali wakati wa utawala wa Awamu ya Kwanza.
  Watoto wa viongozi wakati wa Awamu ya Kwanza, baadhi yao waliwekwa ndani na polisi pale walipokamatwa wakitenda makosa ya jinai kwa kutumia majina ya wazazi wao. Nchini Marekani wakati wa utawala wa George Bush, binti yake pacha, Jenna alikamatwa na polisi pale alipojaribu kutumia kitambulisho bandia ili kununua pombe kabla ya umri unaoruhusiwa.
  Ni marais wadhaifu au mafisadi tu, walio na ujasiri wa kuajiri wake zao, au watoto wao, na ndugu zao kwa kisingizio cha kuwa wana sifa na wana haki sawa na raia wengine. Kuajiri ndugu, watoto na marafiki humpunguzia rais uwezo wa kufanya maamuzi kwa uhuru na kudumaza hali ya utendaji kwa ujumla.
  Wote tumeshuhudia jinsi Rais Kikwete anavyopata taabu kufanya maamuzi magumu hasa wakati wa migogoro. Leo atatoa ruhusa kwa rafiki yake amilikishwe ardhi kwa ajili ya uwekezaji, kesho wananchi wakipiga kelele, atawaahidi kuwa watarudi katika ardhi yao. Mwekezaji akija kulalamika kwake, atamwambia aende mahakamani apate amri ya kuzuia mtu yeyote asiingie. Baada ya hapo Rais atawaambia wananchi wavumilie kwa sababu suala sasa liko mahakamani!
  Leo atakubaliana na Ripoti ya Mwakyembe (Dk. Harrison) kuhusu Richmond na kesho atakwenda Monduli kumpigia kampeni Edward Lowassa akisema alionewa! Leo atahutubia Baraza la UVCCM na kusema Masauni (Hamad) aligushi umri, lakini hapo hapo atamtuliza kuwa atapangiwa kazi nyingine, na kabla hajatekeleza ahadi hiyo, Rais ataongoza Halmashauri Kuu (NEC) kupitisha jina la Masauni kuwa mgombea ubunge!
  Ataiambia NEC kuwa Bashe (Hussein) si raia wa Tanzania, na wiki inayofuata ataagiza Bashe aende kusaidia kampeni na baada ya uchaguzi atapangiwa kazi nzuri.
  Nape Nnauye akivutana na Benno Malisa, Kikwete ataamua wote waachie nafasi hiyo ili mtu mwingine atafutwe.
  Atakubaliana na Baraza la UWT kuwa Husna Mwilima ni mzembe, na kesho yake atamteua kuwa Mkuu wa Wilaya (DC).
  Orodha inayoonyesha udhaifu wa kiuongozi na kigugumizi wa Rais Kikwete katika kufanya maamuzi magumu, ni ndefu. Kwa wale wanaonufaika na udhaifu huu, hawaiiti tabia hii kuwa ni udhaifu, bali eti ni uungwana na upendo kwa watu!
  Mapema kabla ya kampeni za uchaguzi unaokuja hazijaanza, “alionywa” na wanaomtakia mema kuwa asiwe mwepesi wa kutoa ahadi nyingine wakati bado kuna maswali mengi juu ya utekelezaji wa ahadi za uchaguzi uliopita.
  Kama kawaida yake alikubali, lakini wote tumeona kuwa hata mahali pasipo na kituo cha mkutano wa kampeni, anasimama kumwaga ahadi zisizo na maandalizi.
  Rais amefikia hatua ya kuahidi mashine za kusaga kwa kikundi, sare za kikundi cha kwaya, bajaji za wajasiriamali, n.k. Hivi ni vitu vidogo ambavyo viko ndani ya uwezo wa wanasiasa wa kada nyingine.
  Si siri kuwa ameshusha mno hadhi na majukumu ya rais. Si ajali kusema; Ikulu imegeuka mgodi wa familia na marafiki wa rais. Kila mmoja wao anakazana kuchimba na kuvuna wakati huu na miaka mitano ijayo.
  Utetezi wa Joseph kuhusu uamuzi wa Kikwete kutumia marafiki na ndugu, umethibitisha pasipo shaka hoja niliyoitoa wiki iliyopita kuwa hivi sasa Ikulu kuna maofisa wasio na maadili na kwa hiyo wanamuweka Kikwete katika shaka kubwa.
  Watu wa namna hii, hawana maadili ya kutunza siri za Ikulu yetu, na zaidi ya yote hawana uwezo wa kutetea kwa weledi maamuzi yanayofanywa na Rais. Hawa ni wachumia tumbo, hawana uchungu na Taifa. Ni bahati mbaya kuwa tumejikuta tuna watu na namna hii katika Ikulu yetu.
  [​IMG]


  SOURCE: Raia Mwema
   
 2. Kiwi

  Kiwi JF-Expert Member

  #2
  Sep 23, 2010
  Joined: Sep 30, 2009
  Messages: 1,009
  Likes Received: 197
  Trophy Points: 160
  Asante sana kwa posts nzuri. Nimezisambaza kwa watu wangu, na ni vizuri zisomwe na watu wengi ili waelewe ukweli kuhusu serikali hii ya sasa. Ndugu zetu mlioko nyumbani tusaidieni kwa kuleta mabadiliko ya kweli kweny uchaguzi wa 31 Oktoba. Vizazi vijavyo vitatuhukumu tusipofanya uamuzi sahihi.
  Mungu Ibariki Tanzania!
   
 3. Msanii

  Msanii JF-Expert Member

  #3
  Sep 23, 2010
  Joined: Jul 4, 2007
  Messages: 6,427
  Likes Received: 370
  Trophy Points: 180
  Reeeeady to RUMBLE!!!!!!
  tunasubiri oktoba 31 tukamkamue mtu
   
Loading...