Kikwete ndani ya ccj

baraka boki

Senior Member
Sep 20, 2010
181
80
11



NYOTA ya spika wa zamani wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta imezimwa, MwanaHALISI limeelezwa.

Sitta, ambaye Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilitegemea akibebe katika kugombea urais mwaka 2015, amehusishwa na uasisi wa "chama ndani ya chama."

Hiki ni Chama cha Jamii (CCJ) kilichoanzishwa kwa makeke karibu na uchaguzi mkuu wa mwaka jana, kikihofiwa kubeba viongozi ndani ya CCM ambao walionekana kupinga ufisadi.

Aliyemwaga hadharani siri za Sitta kuwa nyuma ya ujio wa CCJ, ni Fred Mpendazoe, kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Wengine aliowataja kuwa ama washiriki au waanzilishi wa CCJ, ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, mbunge wa Lupa Victor Mwambalaswa (CCM), katibu msaidizi wa CCM wilayani Moshi Mjini, Daniel ole Porokwa na kada wa chama hicho, Paul Makonda.

Akiongea kwa kujiamini, Mpendazoe alisema, "Wote hao, ni wasaliti. Wasiwadanganye kuwa wanapambana na ufisadi wakati ni wanafiki wakubwa."

Kwa mpangilio huo, Rais Jakaya Kikwete yumo katikati ya wapinzani wake au waliokuwa wamejiandaa kuwa wapinzani wake wakuu kisiasa.

Pamoja nao, taarifa zinasema kulikuwa na wabunge wapatao 20 ambao wangechomoka CCM pindi chama hicho kingesajiliwa. Gazeti halikuweza kupata orodha yao.

Akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara katika mji wa Njombe, juzi Jumatatu, Mpendazoe alisema, "Sitta ndiye aliyekuwa mwanzilishi wa CCJ. Mkakati ulikuwa ni kuondoka ndani ya CCM kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010."

Mpendazoe ambaye huongea kwa vituo ili kusisitiza hoja yake, aliuambia umati wa wasikilizaji "…ilikuwa baadaye tuungane na CHADEMA ili kuongeza nguvu ya kupambana na ufisadi na kuuondoa uongozi mbovu wa CCM."

Hata hivyo, Mpendazoe alisema, "Nasikitika sana, mwenzangu huyu (Sitta), alinisaliti dakika za mwisho baada ya kuahidiwa cheo na Kikwete. Ni kwa sababu hawakuwa na dhamira ya dhati. Waliongozwa na uchu wa madaraka."

Kuvuja kwa taarifa za kuwamo kwa Sitta, Dk. Mwakyembe na vigogo wengine waandamizi wa CCM katika mkakati wa kuanzisha CCJ, kulianza kwa Mpendazoe kusema, wiki iliyopita, kuwa Nape alikuwa mwanzilishi wa CCJ.

Kesho yake, Nape alinukuliwa akikubaliana na kauli za Mpendazoe kwa kutokanusha, bali kusema tu kuwa kinachohitajika ni kujadili ya leo na siyo yaliyopita.

Ni mwaka mmoja sasa tangu zipatikane taarifa kwamba baadhi ya vigogo wa CCM wanataka kuunda chama cha siasa.

Kwa mujibu wa taarifa za kishushushu, siri za vigogo kuanzisha chama zilivujishwa na mmoja wa viongozi hao sita.

Hilo lilifuatiwa na mizengwe ya usajili ikiwa ni pamoja na msajili wa vyama vya siasa, John Tendwa kudai wakati mmoja kuwa hana fedha za kuzunguka nchi kuthibitisha wanachama wa CCJ.

"Hapa, kama Kikwete hakujua hili mapema, lazima atakuwa ameachwa mdomo wazi. Sasa abaki na Sitta ambaye amehusishwa na ujio wa CCJ au abaki na maswahiba zake wa siku nyingi – Edward Lowassa na Rostam Aziz," ameeleza mjumbe mmoja wa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho kwa sauti ya uchungu.

Sitta alikuwa ameanza kutajwa katika duru za siasa kuwa pekee ndani ya CCM anayetoka eneo lenye wapigakura wengi na anayeweza kuokoa chama hicho kwa msimamo wake.

Spika huyo wa zamani anatoka mkoani Tabora ambako wafuasi wake kwa misingi ya ukaribu, lugha na kuelewana, wanaunda idadi kubwa ya wapigakura kikanda.

Katika mahojiano yake na gazeti hili kwa njia ya simu mara baada ya kumaliza kuhutubia maelfu ya wananchi, Mpendazoe alitaja ushiriki wa kila mmoja kwenye CCJ.

Alisema, "Sitta ndiye alikuwa akilipia pango la ofisi. Alitoa fenicha za ofisi na ndiye alikuwa analipa mishahara ya katibu mkuu wa CCJ, Renatus Muabhi na mwenyekiti wake, Richard Kiyabo."

Alisema naye Dk. Mwakyembe, ndiye aliandaa katiba ya CCJ. Alikuwa akitoa ushauri wa kisheria kwa wabunge waliokuwa wanataka kuondoka CCM na ndiye alikuwa anashughulikia masuala yote ya fedha kwa maelekezo ya Sitta."

"Hata yule Makonda aliletwa CCJ na Mwakyembe. Walimuachisha shule kule Chuo cha Ushirika Moshi ili kuja kusimamia usajili wa CCJ kabla sisi wengine hatujajitokeza," alisema Mpendazoe kwa sauti ya kusisitiza.

MwanaHALISI halikuweza kumpata Sitta kujibu tuhuma hizo. Simu yake ya mkononi ilitoa jibu, "Simu unayopiga, haipatikani kwa sasa."

Kwa upande wake, Dk. Mwakyembe alisema, "Ninakushauri kwenda kwa msajili wa vyama, kule kuna orodha ya viongozi waasisi, wadhamini na wanachama waanzilishi. Kueni waangalifu, msiwalishe watu porojo za kina Mpendazoe."

Alisema, "…uandishi wa Kitanzania umekuwa wakipuuzi tu. Wewe si unajua kuna msajili wa vyama? Nendeni huko mtaona."

Majibu ya Mwambalaswa hayakutofautiana na yale ya Dk. Mwakyembe, labda pale aliposema, "Wanaoropoka barabarani wanataka kudhoofisha vita dhidi ya ufisadi, ambayo inakaribia kushinda."

Naye Nape ameelezwa kuwa ndiye alipewa jukumu la kusaidia upatikanaji wa taarifa juu ya mipango ya siri ya CCM dhidi ya Sitta na wenzake. Alipewa pia jukumu la kwenda kwa wafadhiri kuwashawishi ili wasaidie chama hicho.

Mtoa taarifa wa gazeti hili amesema, kabla ya Mpendazoe kujiondoa CCM, kulifanyika majadiliano ya kina na wenzake hao, huku Sitta akimhakikishia kulipwa mafao yake ya ubunge.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari, 30 Machi 2010, katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dar es Salaam, Mpendazoe alisema, ameamua kuondoka CCM kwa kuwa ndani ya chama hicho "kuna kansa ya uongozi."

Alisema, "Sijutii uamuzi wangu huu…kuna wenzangu, muda si mrefu watanifuata."

Alisema, "Chama legelege kinazaa serikali legelege. CCM kimekuwa ngome ya mafisadi na kimebeba watu waliopoteza maadili ya uongozi."

Alimtuhumu mwenyekiti wa chama hicho, Rais Kikwete, kwa kukosa uwezo wa kusimamia maadili ndani ya chama chake kwa madai kuwa "ameingizwa madarakani na watu wachafu."

MwanaHALISI limetajiwa sababu kuu tatu za kuanzishwa CCJ. Kwanza , ni CCM kuendelea kukosa hadhi mbele ya jamii kwa kukumbatia ufisadi.

Pili, woga kwamba wabunge wapambanaji dhidi ya ufisadi "watafyekwa" wakati wa kura za maoni, hivyo wawe na pa kukimbilia.

Tatu, kusambaa kwa uvumi kwamba Rais Kikwete anataka kumsafisha Edward Lowassa (aliyekuwa waziri mkuu) na kumrejesha madarakani.

Gazeti lilipowasiliana na Paul Makonda juu ya ushiriki wake katika CCJ, haraka alianza kumtuhumu Mpendazoe kuwa amelenga kuwagombanisha na viongozi wakuu wa CCM.

"Anachokifanya sasa Mpendazoe ni kutaka kutugombanisha na viongozi wakuu wa chama chetu. Hebu tujiulize, madhara ya CCJ ni yapi? Hapa tuna vita moja tu: Kumwondoa Lowassa katika chama chetu," alisisitiza.

Kwa kauli hii ya Makonda, waanzilishi wa CCJ walitaka kuondoka CCM ili kujitenga na Lowassa.

Alipoulizwa kama haoni kuwa vita ya kuondoa Lowassa na wenzake ndani ya chama hicho inaweza kuwa ngumu kutokana na kuibuka kwa tuhuma hizi, Makonda alisema, "Ni kweli. Bali lazima tutashinda."

Renatus Muabhi ambaye alikuwa katibu mkuu wa CCJ, alipoulizwa kuhusu madai ya Mpendazoe, kwanza alisita, kisha akasema, "Hayo mambo sijui..."

Alipobanwa juu ya ununuzi wa samani za ofisi na pango la ofisi ya chama hicho, Mwananyamala jijini Dar es Salaam, ambavyo Mpendazoe amedai kuwa vilitolewa na Sitta, Muabhi alikiri kuwa ni kweli.

Hata hivyo, Muabhi alisema suala la Sitta kusaidia chama chake halina uhusiano wowote na yeye kuwa ndiye mwenye chama. "Huyu bwana alisaidia kama walivyosaidia wengine. Msaada wake haukuwa na maana kwamba yeye ndiye alikuwa mwenye chama," alisema.

Taarifa zinasema Sitta na wenzake waliamua kuanzisha CCJ kwa hofu kwamba Kamati ya wazee iliyoundwa na chama hicho kutafuta chanzo cha mpasuko ndani ya Bunge na katika chama ingeshindwa kupata suluhu.
Gazeti toleo na. 242Kikwete ndani ya CCJ


Na Saed Kubenea - Imechapwa 18 May 2011
 
Back
Top Bottom