Kikwete jiwekee akiba | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kikwete jiwekee akiba

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Pdidy, Nov 26, 2009.

 1. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #1
  Nov 26, 2009
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,495
  Likes Received: 5,725
  Trophy Points: 280
  Kikwete jiwekee akiba
  NIMEPATA kueleza kwa zaidi ya mara mbili namna ninavyoguswa na ugumu wa kazi zinazomkabili Rais Jakaya Kikwete wakati anapotimiza wajibu wake kama mkuu wa nchi, Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama na Mwenyekiti wa taifa wa chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM).

  Sina sababu hata kidogo leo hii kuwachosha wasomaji wa safu yangu, nikirejea sababu hasa na za msingi za kumhurumia rais wangu ambaye kwa bahati mbaya sana, kikundi kidogo cha makachero wa nchi hii, ambao wao ndio hudhani kwa makosa kwamba, wanayo dhamana ya peke yao ya kumlinda, kumpigania na kumtetea.

  Ukweli kwamba Rais Kikwete anao wajibu mzito na mkubwa, si jambo la kubishana hata kidogo, hasa kwa mtu ambaye kwa moyo wake wote anakuwa amejitoa kwa dhati na pasipo unafiki kulitumikia taifa lake.

  Hata hivyo niseme mapema kwamba, pamoja na kutambua na kuheshimu uzito wa wajibu na majukumu aliyonayo rais wetu, bado tunao wajibu wetu kama wanahabari, kuhakikisha kwamba tunafanya kila linalowezekana kudadisi kwa nia njema, namna anavyojitoa kutimiza malengo ambayo Watanzania zaidi ya milioni 40 wanamtegemea.

  Ni kwa sababu hiyo na nyingine nyingi zinazofanana na hizo, ndiyo maana kila kukicha jina la Kikwete limekuwa likichambuliwa, na kwa hakika kwa njia na namna tofauti, wanazuoni, wanahabari, wanaharakati na wachambuzi wengine wa mambo, wamekuwa ama wakimpongeza kwa hatua madhubuti anazochukua akiwa rais au kumnyoshea kidole kutokana na hitilafu ambazo zinaonekana au kuhusishwa na yeye mwenyewe moja kwa moja.

  Safu hii ya Tuendako, kwa kadiri ilivyoweza, imefanya juhudi kubwa na wakati mwingine pasipo kufanikiwa kwa kiwango kinachotarajiwa, kupekua pekua mema ya kiwajibikaji ambayo rais wetu amekuwa akiyatenda wakati anapotimiza wajibu wake kama mkuu wa nchi, rais, amiri jeshi mkuu na mwenyekiti wa taifa wa CCM.

  Kwa mwelekeo huo, safu hii pia imekuwa ikifanya kila linalowezekana kumkosoa na wakati mwingine kumnyoshea kidole kiongozi huyo, hasa kwa mtazamo wangu, ninapotafakari, kuamini na kisha kujiridhisha kuwa katika mambo kadha wa kadha, mambo yanayoharibika katika maeneo mbalimbali upo mkono wa moja kwa moja au la wa Rais Kikwete mwenyewe kama kiongozi au mtu binafsi.

  Kwa mantiki hiyo basi, ndiyo maana wakati fulani tunaposoma katika maandishi au kuwasikia baadhi ya watu wakimsifu Kikwete kwa sifa za kila aina na wakati mwingine wakimbebesha taswira ya ushujaa unaotafutiwa maneno matamu, baadhi yetu hujikuta tukijiuliza mara mbili mbili iwapo kweli kiongozi wetu huyo anastahili wingi wa sifa anazomwagiwa.

  Kwa nyakati tofauti, nimepata kukutana na wasaidizi wa ngazi mbalimbali wa Rais Kikwete, hususan wale anaofanya nao kazi ama za dola akiwa Ikulu au wale wanaotokana na ofisi yake binafsi, ambao aghalab siku zote wamekuwa wakimmwagia sifa nyingi kiongozi wao huyo.

  Kama hiyo haitoshi, mbali ya kukutana nao, mara kadhaa nimepata kuwasikia au kusoma namna wasaidizi hao, wanavyotumia muda wao mwingi kumuelezea kwa maneno ya sifa njema kiongozi huyo mkuu, wakimtaja kuwa ni mtu mchapakazi asiyechoka, mzalendo wa kweli, mstahamilivu, mcheshi, mkarimu na kwa hakika kiongozi asiyependa makuu.

  Moja ya mifano ya namna hii, ni mahojiano niliyokutana nayo wiki iliyopita aliyofanyiwa Januari Makamba, mmoja wa wasaidizi wa karibu wa Rais Kikwete, ambaye hakuna shaka ni mmoja wa vijana ambao akili zao zinafanya kazi barabara na wenye sifa zote za kumsaidia kiongozi huyo mkuu wa nchi, si kwa sababu yoyote nyingine, bali kwa kuwa tu na fursa ya kufahamu mapito ya kuelekea Ikulu aliyopita bwana mkubwa huyo katika miaka ya mwisho ya kuelekea mwaka 2005.

  Katika mahojiano hayo, Januari ambaye ni mtoto wa Katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba, amekaririwa akimtaja Kikwete kuwa mmoja wa viongozi wa taifa hili ambao anawachukulia kuwa ndio walimu wake (mentors) wa masuala ya uongozi, akitumia vigezo mbalimbali kama ustahamilivu wake, hekima, subira na uwezo mkubwa wa kuona mambo alionao.

  Ingawa ni wazi kwamba lingekuwa ni jambo la kushangaza iwapo Januari angetoa maelezo tofauti na hayo aliyoyatoa dhidi ya mkuu wake wa karibu kikazi, lakini tafakuri yangu binafsi inanieleza pia kwamba, iwapo kijana huyo angekuwa hakiamini kwa dhati kile alichokizungumza katika mahojiano hayo, angeweza kukaa kimya pasipo kueleza lolote jema au baya dhidi ya kiongozi wake kama njia ya kukwepa lawama.

  Ni kutokana na ukweli huo basi, ndiyo maana nilipoyasoma maneno haya ya Januari, kwanza nilikataa katakata kuyapuuza na kuyaona kuwa ni tuzo asizostahili, bali nilijikuta nikijiuliza mara kadhaa iwapo sifa nyingi ambazo alimmwagia Kikwete kama kiongozi na ‘mentor’ wake, zilikuwa zikifanana na za mtu ambaye wengi wetu tunamfahamu japo si kwa uhakika, kwani fursa pekee ya kumpima tuliyonayo ni ile ya kuangalia aina na ubora wa matunda anayozaa akiwa rais wetu na mkuu wa nchi.

  Mbali ya hilo, sifa hizo ambazo Januari alimmwagia Kikwete, zilisababisha nianze kumuangalia kiongozi huyo na mwenendo wake mzima wa kiuongozi aliouonyesha kwa vitendo, tangu aliposhika madaraka makubwa ya nchi, kuanzia siku alipoapishwa Desemba 21, mwaka 2005.

  Hoja hizo za Januari zilinifanya nijikute nikifadhaishwa na namna Rais Kikwete alivyoamua kwa makusudi au kwa sababu yoyote nyingine aijuayo yeye mwenyewe, aiweke kando kaulimbiu aliyoingia nayo madarakani ya Kasi, Mpya, Ari Mpya na Nguvu Mpya, iliyodumu kwa takriban mwaka mmoja tu tangu alipoingia madarakani.

  Kwa mwelekeo huo huo, hoja hizo za Januari Makamba zilinifanya nijiulize mara mbili mbili, ni kitu gani hasa kitakuwa kimemfika rais wangu ambaye aliingia madarakani kwa mbwembwe nyingi za kiuongozi akianza na mkwara wa semina elekezi za viongozi takriban wote wakuu wa kisiasa walio chini ya mamlaka yake, mkwara ambao leo hakuna kigezo chochote cha utendaji kinachoeleza mafanikio ya hatua hiyo iliyoanzia Ngurdoto kabla ya kusambaa katika kanda mbalimbali hapa nchini.

  Katika mantiki hiyo hiyo, nilijikuta nikijiuliza ni kwa namna gani, kiongozi madhubuti anayemwagiwa sifa lukuki ashindwe kuunda baraza la mawaziri madhubuti na lenye mwelekeo unaoeleweka na rekodi ya kutukuka wakati ikijulikana bayana kwamba, CCM pamoja na kukabiliwa na kila aina ya uchafu ndani, inayo hazina ya kutosha ya makada wenye uwezo mkubwa wa kazi na maamuzi thabiti ambao si mawaziri, wakuu wa mikoa au wa wilaya.

  Sifa hizo alizomwagiwa na mdogo wangu ninayemheshimu, zilinifanya nijiulize mara mbili mbili, ni kwa namna gani, rais aliyepewa kila aina ya madaraka makubwa kikatiba, ajikute akiwa mateka wa hoja za kishabiki, kinazi na zisizo na maslahi kwa taifa kama zile zinazohusu kashfa ya Richmond ambayo hakuna shaka udhaifu wake binafsi kama kiongozi mkuu wa nchi, ndiyo unaosababisha mpaka leo hii mwangwi wake uendelee kulitafuna taifa, huku wahuni wachache wa ndani ya CCM na nje wakiutumia kulihujumu taifa.

  Niseme bayana kwamba, sifa hizi anazomwagiwa Kikwete leo na akina Januari na maelfu ya wana CCM wengine, ambao baadhi yao wanafanya hivyo kwa unafiki, wakimpongeza hadharani na kumponda gizani, ndizo ambazo zinaweza zikawa sababu kubwa ya kumpofusha fikra rais wetu kwa kiwango cha kubebwa na upuuzi unaoratibiwa hivi sasa na makachero waliofikia hatua ya kutunga uongo, kusingizia watu, kuwasafisha wengine kwa sababu tu ya kutaka waonekane wakifanya kazi yao, kwa gharama za kuliyumbisha taifa.

  Ni wazi kwamba, nyuma ya sifa nyingine ambazo naweza kusema wazi baadhi yake, Kikwete hastahili kuwa nazo, ndizo zilizosababisha yeye mwenyewe na serikali yake waanze kubeba lawama zote za ama kuchochea, kuziundia mkakati au kushindwa kuzimaliza baadhi ya tuhuma zinazoelekezwa kwa baadhi ya viongozi wastaafu na makada maarufu wa CCM.

  Katika hili niseme mapema kwamba, ni jambo la kusikitisha sana unapowasikia hadharani au kwa faragha viongozi mbalimbali wanaoshutumiwa au kutuhumiwa kwa kashfa na makosa mbalimbali ya kiutendaji au kimaamuzi, kama walivyo Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, Edward Lowassa, Rostam Aziz, Andrew Chenge, Nazir Karamagi, Sophia Simba, Samuel Sitta na wengine wakivinyoshea vidole vyombo vya habari na wakati mwingine watu wengine, na wakawa mstari wa mbele kumuacha Kikwete akibakia jabali Ikulu, ilhali ukweli ukijulikana kuwa yeye ndiye anayestahili kubebeshwa kila aina ya lawama.

  Kwa watu wanaofikiri sawasawa na ambao hawajapofushwa macho na rushwa ya mamilioni ya fedha zinazomwagwa na matajiri waliogawanyika katika makundi tofauti, kila mmoja akitetea maslahi yake, wanapaswa kutafakari upya na kukubaliana nami, kwamba yule mdudu maarufu anayetafuna dhana nzima ya uongozi wetu ajulikanaye kwa jina la ‘Bwana Ombwe’ (Sir Vacuum) ametua na kuweka makao yake kwenye eneo yalipo makazi ya rais: Ikulu.

  Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, Watanzania bado hatujalibaini tatizo hili kubwa linalotutatiza, na hata wale ambao kwa bahati tunaliona na kulikiri, hatuna uwezo (japo kwa sasa) kulihamasisha taifa kukabiliana na tatizo hili kwa njia ya sanduku la kura, kwani kama tungelikuwa tumejizatiti, maamuzi dhidi ya ombwe tulilonalo leo yangekuwa yameshafanyika kabla ya Desemba 2005.

  Pamoja na udhaifu huo mkubwa tulionao kama taifa, Rais Kikwete na wasaidizi wake wakuu na baadhi ya makachero wanaopika taarifa za majungu kwa lengo la ‘kumlinda na kumfurahisha mkubwa’, wanapaswa kujua kuwa, muhula wa kiongozi huyo kukaa Ikulu hatimaye utafikia mwisho, iwe ni mwakani au hata mwaka 2015 na kwamba, hatua thabiti zisipochukuliwa (leo) atajikuta akiishi maisha ya ustaafu ya kusakamwa yanayoweza kuwa machungu kuliko yale anayokabiliana nayo Mkapa leo.

  Nikiwa miongoni mwa wananchi wanaomtakia mema Kikwete na taifa hili, ninajiona ninao wajibu wa kumuasa kiongozi huyo kuzitafakari upya njia zake, na kupima katika misingi ya haki na kweli iwapo ushabiki unaokarabatiwa na makachero wanaotaka kulinda kitumbua chao leo hii, kwa sababu tu ya kumfanya aendelee kuhodhi mamlaka makubwa aliyonayo, utamjengea heshima ya kudumu huko tuendako. Anapaswa kuanza kujiwekea akiba sasa.


  juu
   
Loading...