Kikwete avicharukia vyombo vya habari | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kikwete avicharukia vyombo vya habari

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by BAK, Jan 14, 2009.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Jan 14, 2009
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,449
  Likes Received: 81,504
  Trophy Points: 280
  Kikwete avicharukia vyombo vya habari

  na Mwandishi Wetu
  Tanzania Daima~ya Watu​

  RAIS Jakaya Kikwete, amevionya vyombo vya habari kuwa, serikali yake haitavivumilia iwapo vitajiingiza katika uandishi wa habari unaolenga kuchochea watu kwa misingi ya dini au ukabila.

  Amesema pamoja na kulea uhuru wa vyombo vya habari, serikali anayoiongoza, haitavumilia vyombo vya habari vyenye malengo ya kuyumbisha nchi pamoja na misingi yake.

  Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kurugenzi ya mawasiliano Ikulu jana, rais Kikwete aliyasema hayo wakati akizungumza na balozi wa Marekani hapa nchini anayemaliza muda wake, Mark Green, ambaye alifika Ikulu kumuaga.

  Taarifa hiyo inaeleza kuwa rais Kikwete amevikumbusha vyombo vya habari kutimiza majukumu yake inavyopaswa na kuonya kuwa Watanzania wanapaswa kukumbuka kuwa nchi za kiafrika hazijakomaa kiasi cha kutosha kuruhusu uandishi ama vyombo vya habari vinavyochochea mifarakano na migongano.

  "Kweli tunaruhusu uhuru wa kuandika, kusema na kutangaza, lakini hatuwezi kuruhusu uhuru wa kuvunja misingi ya amani na usalama wa taifa letu.

  "Hatuwezi kuruhusu uhuru wa watu wetu kuchochewa kwa misingi ya dini au kabila, hatuwezi kuruhusu uhuru ambao unalenga kuyumbisha nchi yetu," inasomeka taarifa hiyo ya Ikulu ikimnukuu rais Kikwete.


  Katika taarifa hiyo, rais Kikwete aliwataka Watanzania kukumbuka matukio yaliyotokea nchini Rwanda ambapo redio moja ilitosha kuchochea mauaji ya Kimbari jambo aliloeleza kuwa haliwezi kukubalika.

  Naye Balozi Green, alimpongeza Rais Kikwete na utawala wake kwa kufanikisha mapambano dhidi ya rushwa.

  Green alimpongeza rais Kikwete, kwa kulea uhuru wa vyombo vya habari nchini alivyovieleza kuwa vimefanya kazi kubwa katika mapambano dhidi ya rushwa.

  "Tunakushukuru na tunakupongeza kwa hatua zako katika mapambano dhidi ya rushwa. Umeonyesha kiwango cha juu kabisa cha uongozi. Dunia inasikia na dunia inaangalia…..".

  "Tunakushukuru hasa kwa mashtaka ya karibuni katika kesi ya ulaji rushwa mkubwa. Ni matarajio yetu kuwa mashtaka haya yatasimamiwa hadi mwisho, na kuona wale wote ambao wanahusika na rushwa wanawajibishwa bila kujali nafasi zao," alisema Balozi Green.

  Kwa maelezo ya balozi huyo, imekuwa ni heshima ya pekee katika taaluma yake kupata nafasi ya kufanya kazi hapa nchini, na kufanya kazi katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne.

  " Imekuwa miezi 16 ya shughuli nyingi ambazo nitazikumbuka maishani mwangu," alisema na kuongeza kuwa, "Hata hili la uhuru wa vyombo vya habari, tunakushukuru kwa kuonyesha uongozi na uvumilivu mkubwa katika kulea uhuru wa habari nchini."

  Alimhakikishia Kikwete kuwa misaada yote ambayo Marekani imekubali kuitoa kwa Tanzania wakati akiwa balozi, pamoja na programu zote za misaada za sasa, zitaendelea kama ilivyokubaliwa kati ya nchi hizo mbili.

  Naye rais Kikwete kwa upande wake alimwambia balozi huyo kuwa, amekuwa hodari na bora, amekuwa muwazi na mkweli na amesaidia katika mambo mengi.

  "Umechangia misaada ya Marekani kwa Tanzania katika MCC, katika elimu, PEPFAR, kuhusu malaria na ulifanikisha sana ziara ya Rais Bush hapa nchini. Tunakushukuru sana," alisema rais Kikwete.
   
 2. J

  Jamco_Za JF-Expert Member

  #2
  Jan 14, 2009
  Joined: Jul 14, 2007
  Messages: 1,315
  Likes Received: 24
  Trophy Points: 135
  No Comment nasubiri mhandike kwanza maana salamu kwa watu furani
   
Loading...