Return Of Undertaker
JF-Expert Member
- Jun 12, 2012
- 4,572
- 26,868
Kwa ufupi
Mpaka sasa maofisa 20 wa Kitengo cha Usalama wa Taifa (NIA) ama wako mahakamani au wanakabiliwa na mashtaka kuhusiana na kifo cha mwanaharakati ambaye alikamatwa wakati wa maandamano.
Banjul, Gambia. Katika utawala wa Rais Yahya Jammeh ilikuwa kawaida kusikia mwanaharakati au mwanahabari au kiongozi fulani wa siasa kauawa na watu wasiojulikana na haukufanyika msako wala uchunguzi.
Mambo yamebadilika, wale watu ambao walikuwa wanadaiwa ‘wasiojulikana’ sasa wanasakwa na wanajulikana. Jumatatu polisi walimkamata ofisa mwandamizi wa intelijensia akihusishwa na mauaji ya mwanaharakati Solo Sandeng Aprili 2016.
Kifo cha mwanaharakati huyo akiwa mahabusu kilichochea vuguvugu la kisiasa ambalo hatimaye lilifanikisha kuuangusha utawala wa miaka 22 wa Jammeh.
Kuteswa na hatimaye kuuawa kwa mwanaharakati huyo aliyekuwa akiongoza chama cha United Democratic Party (UDP) kuliibua maandamano yasiyo ya kawaida ambayo yalihamasisha kambi dhaifu ya upinzani na iliyogawika kuungana dhidi ya utawala wa kidikteta.
Mpaka sasa maofisa 20 wa Kitengo cha Usalama wa Taifa (NIA) ama wako mahakamani au wanakabiliwa na mashtaka kuhusiana na kifo cha mwanaharakati huyo ambaye alikamatwa wakati wa maandamano.
Msemaji wa polisi David Kujabie alisema Jumatatu kwamba Mkuu wa Usalama wa Taifa, James Mendy alikamatwa na polisi na akawekwa kizuizini kwa mahojiano “kuhusiana na kuuawa kwa Solo Sandeng”.
Maofisa wengine tisa wa NIA, akiwemo kiongozi wa zamani, Yankuba Badjie wamefunguliwa mashtaka yanayohusu ushiriki wao katika kifo cha Sandeng. Mchakato unakwenda taratibu: mashahidi 13 wameitwa.
Maofisa wengine wa zamani wa NIA, Ngora Njie na Shiekh Tijan Camara walikubali wiki iliyopita kwamba watakuwa mashahidi upande wa mashtaka.