Kigoda cha Nyerere na ‘utakatifu’ wake | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kigoda cha Nyerere na ‘utakatifu’ wake

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Ngongo, Mar 26, 2009.

 1. Ngongo

  Ngongo JF-Expert Member

  #1
  Mar 26, 2009
  Joined: Sep 20, 2008
  Messages: 12,155
  Likes Received: 3,632
  Trophy Points: 280
  KIGODA cha marehemu Mwalimu Nyerere, kilichozinduliwa mwaka jana kwenye Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam, na kukaliwa na Profesa Issa Shivji, mwaka huu kitashuhudia ugeni mkubwa wa kusherehekea kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mwalimu.

  Sherehe hizo, zitakazoanza mwezi ujao - Aprili 13 hadi Aprili 17 na kutengeneza kitu kijulikanacho kama Wiki ya Tamasha la Mwalimu; zitapambwa na mihadhara ya kisomi, majadiliano na kuelimishana juu ya mawazo ya Mwalimu, matendo yake na hasa juu ya mapenzi yake kuhusu Umoja wa Afrika.

  Kaulimbiu ya tamasha hilo itakuwa: Binadamu wote ni sawa, Afrika ni moja na Afrika ni lazima iungane.

  Katika tamasha hilo, Chuo Kikuu cha Dar es salaam kitazindua Mhadhara wa Mwalimu wa kila mwaka. Na mwaka huu mhadhara huo utatolewa na mwandishi maarufu wa vitabu wa Afrika, Wole Soyinka. Atachambua na kuchochea majadiliano juu ya Ubeberu Mamboleo.

  Tumemsoma sana Wole Soyinka enzi za kale, na leo hii watoto na wajukuu wetu bado wanasoma mawazo ya Wole Soyinka. Itakuwa ni heshima ya pekee kumsikiliza akizungumza juu ya Mwalimu Nyerere, kuuchambua Ubeberu Mamboleo na kukitukuza Kiswahili, lugha anayoamini inaweza kuliunganisha bara la Afrika.

  Mbali na Wole Soyinka, kwenye tamasha hilo kutakuwepo pia wageni wengine kama vile mtoto wa marehemu Kwame Nkrumah anayeitwa Gamal Nkrumah na mtoto wa Franzt Fanon anayeitwa Olivier Fanon. Wageni wengine watatoka Ghana, Kenya, Uganda na Afrika ya Kusini.

  Mbali na kumbuku ya Mwalimu, Kidoga cha Mwalimu kina malengo ya kufufua chemichemi ya mawazo iliyokuwa kwenye Chuo Kikuu cha Dar es salaam miaka ya sabini. Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam kinafikiri tamasha hili la Mwalimu litakuwa tukio kubwa litakalo wavutia pia Watanzania wengi wasomi na wale wa kawaida.

  Ninaandika makala hii kuwaunga mkono waandaaji wa tamasha hili na Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Nawaunga mkono kwa kuwashawishi na kuwaomba wasomaji wangu na wale wote wenye mapenzi mema na taifa letu, kukusanyika kwa wingi pale Chuo Kikuu cha Dar es salaam ili tusherehekee siku ya Mwalimu na kujifunza mengi kutoka kwa wachambuzi mbalimbali na watu mashuhuri kama Wole Soyinka.

  Lakini pia ninaandika kuwashawishi wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, waruhusu watu kujadili mada mbalimbali juu ya Mwalimu. Wasikalie mada za kisomi peke yake. Kuruhusu mijadala mbalimbali kutawavutia watu wengi kufika kusikiliza na kuchangia.

  Kuna haja ya kutafuta na kuunda mifumo ya kuwavutia watu kupenda mihadhara ya kisomi na majadiliano. Mfano ni mchakato wa Kanisa Katoliki wa kutaka kumtangaza Mwalimu kuwa ni mwenye heri na hatimaye kumtangaza mtakatifu, ni jambo ambalo linahitaji mjadala wa wazi, bila shinikizo, bila upendeleo na bila ya ushawishi wowote ule.

  Ni bahati mbaya au ni uzembe wetu kwamba baada ya miaka 100 ya ukristu hapa Tanzania, hatujatunukiwa mtakatifu Mtanzania au yule aliyefanya kazi hapa Tanzania. Wengine wana mawazo kwamba watakatifu wanadondoka kutoka mbinguni au si watu kama sisi.

  Kama mpango wa kumtangaza Mwalimu Nyerere ukifanikiwa, itasaidia kuonyesha kwamba watakatifu ni watu kama sisi na wanazaliwa na kuishi miongoni mwetu. Wanakuwa na mapungufu kama sote tulivyo, lakini wanajiweka mikononi mwa Mungu, na kukubali kuongozwa naye!

  Kuna wamisionari wengi waliofanya kazi hapa Tanzania na kuzikwa hapa au nchi jirani kama Rwanda. Hawa walifanya kazi kubwa. Kutowatangaza watakatifu ni kuisaliti kazi yao yote waliyoifanya.

  Askofu Hirth (kwa mfano) alianzia Kagera akieneza dini na maendeleo ya binadamu hadi akafika Rwanda. Alikufa na kuzikwa nchini Rwanda. Huyu, kama kungekuwa na jitihada za pekee za Askofu wa Bukoba, basi naye angekuwa katika mchakato wa kutangazwa Mtakatifu. Wanahistoria wengi akiwemo Askofu Methodius Kilaini, ambaye anaonyesha uelewa mkubwa na kipaji cha hali ya juu cha kuyachambua matukio mbalimbali ya kihistoria, wameandika mengi kuhusiana na maisha ya Askofu Hirth. Lakini inashanaza kuona hadi leo hakuna jitihada zilizofanyika kufuatilia maisha na kazi za Askofu Hirth.

  Wako na walei wengi waliojitolea kufanya kazi za kueneza Injili na kuchangia kukua kwa maendeleo ya binadamu. Mzee Kazigo, aliyetoka Bukoba kwenda Karagwe, ni mtu aliyeacha historia ya imani, mapendo na uvumilivu. Mtu kama huyu, ni muhimu katika historia ya Kanisa. Lakini pia wapo walei wengine waliokataa kuipokea imani, ila wakalazimishwa kuipokea ili wapate huduma za kijamii kama shule, matibabu na ustaarabu wa kigeni, lakini kwa kufanya hivyo wamekuwa chanzo na kichocheo cha imani na maendeleo.

  Hawa walipata nafasi ya kuwapeleka watoto wao mashuleni ambao sasa hivi ni madaktari, maprofesa, wanasheria, mapadri, masista nk. Waliipokea imani kwa uchungu, walifanyishwa kazi na kulazimika kutembea mwendo mrefu na wakati mwingine kuyapoteza maisha yao. Hawa wote wakifanyiwa utafiti wanaweza kupata heshima ya utakatifu.

  Tuna mama zetu wanaopigwa hadi kufa wakizitetea ndoa zao. Wanavumilia mateso, hadi kufa ili kulinda sakramenti ya ndoa. Ipo mifano mingi ya akina mama waliokatwakatwa au kupigwa risasi au kwa mauaji ya aina nyingine. Wanawake hawa wanakufa wakitetea imani yao. Hivyo si haki kabisa akina mama kama hawa kuwanyima nafasi ya kukumbukwa katika Kanisa na katika jamii nzima.

  Mwanamke daktari wa Italia alifanywa mtakatifu kwa vile alichagua kufa kuliko kuitoa mimba yake. Alikuwa na nafasi ya kuendelea kuishi kama angekubali kuitoa mimba. Hapa Tanzania tunao akina mama wengi ambao wanapoteza maisha kwa kukataa kutoa mimba.

  Ni lazima tumpongeze Marehemu Askofu Samba, aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma, kwa juhudi alizozianzisha za kufanya utaratibu wa kumtangaza Mwalimu Nyerere kuwa mwenye heri na hatimaye kutangazwa mtakatifu. Kitu muhimu ni miujiza inayojitokeza ili kuonyesha kwamba kweli marehemu ni mtakatifu.

  Miujiza hiyo ni kama vile umoja wetu Watanzania, amani yetu, na hata watawala kukubali kufuata mifano ya Mwalimu ya kuachia madaraka. Hizi ni kazi alizozifanya Mwalimu. Kama tuna amani, ni kwa vile Mwalimu alijenga misingi ya amani. Kama tuna umoja ni kwa vile Mwalimu alijenga misingi ya umoja. Kama viongozi wanakubali kuachia madaraka ni kwa vile Mwalimu alijenga misingi imara ya kupokezana uongozi!

  Mwalimu alishiriki kikamilifu kuzikomboa nchi za Afrika. Huu ni muujiza mkubwa. Pia Mwalimu alianzisha mazungumzo ya Burundi. Leo hii Burundi ina serikali iliyochaguliwa na wananchi wenyewe. Huu pia ni muujiza mkubwa.

  Miujiza ya Mwalimu ni mingi kiasi kwamba kama ikifanyiwa kazi kwa makini, haitachukua muda bila ya kumtamgaza Mwalimu Nyerere kuwa ni mwenye heri na hatimaye mtakatifu.

  Mwalimu Nyerere alisimamia umoja wa Afrika, lakini pia alisimamia umoja wa nchi yake ya Tanganyika. Alitaka Watanzania kujitambua kwanza kama Watanzania wenye maadili fulani mema, ambayo mtu akitenda kinyume, wenzake wamsute na kusema kwamba huu si Utanzania!

  “Hoja lazima ijengwe kwamba hatimaye kinga madhubuti ya haki za raia, uhuru wa raia, na mambo yote wanayoyathamini, hatimaye yatahifadhiwa na maadili ya kitaifa. Taifa linapokuwa halina maadili yanayowezesha Serikali kusema: ‘ Hatuwezi kufanya hivi, huu si U-Tanganyika.’

  Iwapo watu hawana maadili ya aina hiyo, haisaidii sana hata kama wangekuwa na Katiba iliyoandikwa vizuri sana. Bado raia wanaweza kukandamizwa….

  Tunachopaswa kukifanya ni kujenga maadili ya taifa hili, kila mara kuimarisha maadili ya taifa hili, maadili yatakayomfanya rais yeyote yule kusema, ‘Ninayo madaraka ya kufanya jambo hili chini ya Katiba, lakini sitalifanya, maana huu si u-Tanganyika.

  Au kwa watu wa Tanganyika, iwapo wamekosea na kumchagua mwenda wazimu kuwa rais, mwenye madaraka ndani ya katiba na kufanya XYZ, akijaribu kufanya hivyo, watu wa Tanganyika waseme, ‘Hatukubali hili lifanyike, hata alitake rais au rais maradufu, hatulikubali, maana huu si U-Tanganyika’."

  Hayo ni maneno ya Mwalimu aliyoyatamka Juni 28, 1962 wakati akiwasilisha bungeni muswada wa kuifanya iliyokuwa Tanganyika kuwa jamhuri. Kwa hakika, maneno hayo ni kipimo cha vyama, viongozi na Watanzania wanaojigamba kwamba wao ni “Watanzania”.

  Tujiulize, u-Tanzania unanyesha kama mvua? Inatosha kuzaliwa Tanzania mtu akatenda na kuishi ya u-Tanzania? Mtanzania hawezi kuisaliti nchi yake, hawezi kuipora nchi yake. Mtanzania wa kweli ni mzalendo. Mtanzania wa kweli analitanguliza taifa bila kuangalia kwanza maslahi yake binafsi, analitanguliza taifa bila kutanguliza tumbo lake. Huyu yuko tayari kuyapoteza maisha yake kwa kutetea uhai wa taifa lake.

  Ili kuujenga u-Tanzania, Mwalimu Nyerere alibuni mbinu na mifumo mbalimbali kama vile lugha moja, siasa ya ujamaa na kujitegemea, vijiji vya ujamaa, kuwasambaza watoto kwenye shule za mikoa mbalimbali, jeshi la kujenga taifa, mwenge wa uhuru nk.

  Leo hii, lugha yetu tunaipiga vita. Tunataka kutumia lugha za kigeni! Ujamaa tumeuweka kaburini. Vijiji vya ujamaa havisikiki tena. Jeshi la kujenga taifa lilokuwa linawakutanisha vijana waliomaliza kidato cha sita, sasa ni historia! Mwenge wa huru umetaifishwa na CCM. Badala ya kujenga umoja wa kitaifa unatumika kukipigia debe chama tawala.

  Tuna mbinu gani za kujenga u-Tanzania? Ni nani mwenye sera ya wazi ya kuujenga u-Tanzania? Tusijidanganye na kuamini kwamba jambo hili linaweza kunyesha kama mvua. Ni jambo la kufanyia kazi.

  Na mwenye nafasi ya kufanya jambo hili hawezi kupata nafasi ya kujilimbikizia mali, nafasi ya kuwa na viwanja na kujenga nyumba kila mkoa. Mwalimu Nyerere alikuwa na nyumba ngapi? Je, nyuma yake ameacha vitabu vingapi vyenye sera, visheni, falsafa na mambo mengine mengi ya kuujenga u-Tanzania na ubinadamu?

  Alitumia muda wake kufikiri, kusoma, kupanga na kuandika. Kujenga u-Tanzania kunahitaji umakini. Huwezi kushinda na kulala kwenye pombe, kufukuzia dogodogo, kujenga nyumba ndogo, kugombania viwanja, kufukuzia asilimia kumi kwa kila mradi upitao, ukapata muda na uwezo wa kujenga visheni.

  Hivyo Kigoda cha Mwalimu kijitanue na kusambaa kwa lengo la kuambukiza moyo wa Mwalimu Nyerere kwa Watanzania wote. Tukipokee kigoda hiki na kukitumia. Kigoda hiki kiwe kama nuru ya kutuongoza kuendeleza mapinduzi ya kifikra ya Watanzania na Afrika nzima.

  Source:Raia Mwema
   
Loading...