Kakke
JF-Expert Member
- Dec 4, 2010
- 1,883
- 1,483
MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, ameleezea shaka yake kuhusu kuwapo kwa juhudi za kupotosha kwa makusudi uharamia aliofanyiwa wa kutobolewa jicho, kukatwa kidole na kuumizwa maeneo mengine ya mwili, na watu ambao hadi sasa hawajulikani, akisema ukweli wa tukio hilo hauwezi kufichwa daima.
Kwa mujibu wa Kibanda ambaye alikuwa akizungumza katika kipindi cha televisheni katika Kituo cha Televisheni cha Channel-10, kinachorushwa hewani kila Jumatatu na kuongozwa na mwanahabari nguli, Jenerali Ulimwengu, makundi mbalimbali na baadhi ya watu binafsi wamekuwa katika jitihada za kupotosha ukweli kwa sababu wanazozijua, lakini hawataweza kuficha ukweli huo wakati wote.
Akisimulia zaidi kuhusu mwenendo wa matibabu yake nchini Afrika Kusini alikolazwa kwa miezi zaidi ya mitatu, kutokana na kuumizwa nje ya uzio wa nyumbani kwake Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, Kibanda alisema waliompiga na kumuumiza walikuwa na malengo maalumu na kwamba ni watu waliokuwa na utaalamu wa kutesa.
"Walikuwa watalaamu wa kupiga na kuumiza. Madaktari waliokuwa wakinitibu walinieleza suala hilo. Kuna rafiki yangu mmoja katika taasisi nyeti nchini (hakuitaja) aliwahi kuniambia kabla ya tukio hilo, kwamba nichukue hadhari hasa ninapokaribia nyumbani, kwa mfano nje ya geti," alisema Kibanda ambaye pia aliumizwa nje ya lango kuu la kuingia nyumbani kwake.
Kibanda ambaye alilazwa katika Hospitali ya Millpark nchini Afrika Kusini, katika kujibu maswali ya mwongoza kipindi, Jenerali Ulimwengu, aliendelea kusema; "Magenge ya utesaji (kama aliofanyiwa) yanaweza kutengenezwa na vyama vya siasa au baadhi ya watendaji wa vyombo vya dola."
Katika kuonyesha wasiwasi wake kuhusu mwenendo wa baadhi ya watu wenye utajiri nchini ambao maadili yao yana shaka, Kibanda alisema; "Labda wapo wenye nguvu (fedha) lakini wameajiri watu wa kutenda uhalifu, kuna jitihada za kupotosha ukweli katika tukio lililonikuta.
Lakini kimsingi, nimeikubali hali hii (ya kupewa ulemavu, sambamba na mateso makali), sitakuwa tena na kigugumizi kwa sababu sina cha kupoteza. Nilikuwa mwoga sana kabla sijapata madhara haya, nawatia moyo wanahabari wenzangu. Lakini kwa sasa tahadhari yangu ni kwamba tukio hilo dhidi yangu linachunguzwa na vyombo vya dola vinaendelea kufanya mawasiliano nami kwa kila hatua inayofikiwa."
Raia Mwema - Kibanda ahofia upotoshaji