Kesi ya wapinga Muungano kusikilizwa Juni 6

Kakke

JF-Expert Member
Dec 4, 2010
1,883
1,482
← PreviousPosted on May 7, 2012 by zanzibaryetu
Kiongozi wa kikundi kinachopigania kuwepo kura ya maoni kuhusu Muungano, Rashid Salum Adiy akiwatuliwa wafuasi wake ambao hawapo pichani, nyuma ni afisa wa jeshi la polisi akimtaka awatulize wafuasi wake kabla ya kukamatwa mwezi uliopita

KESI inayowakabili watu 12 walioshitakiwa kwa kosa la kubeba mabango ya kupinga Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ushahidi wake umekamilika na inatarajiwa kusikilizwa Juni 6 mwaka huu. Mwendesha Mashitaka Said Ahmed Mohammed, aliieleza Mahakama ya Mwanakwerekwe mbele ya hakimu Omar Mcha Hamza jana kuwa upelelezi umekamilika wakati kesi hiyo ilipofikishwa kwa kutajwa mahakamani hapo.
Mwendesha Mashitaka huyo kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar (DPP), aliiomba mahakama hiyo kuiahirisha kesi hiyo na kuipangia tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa.
Kwa upande wake Hakimu Omar Mcha Hamza alikubaliana na hoja zilizotolewa na kuiahirisha kesi hiyo hadi Juni 6 mwaka huu kwa kusikilizwa.
Hakimu Hamza aliutaka upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku ya kesi hiyo katika mahakama siku ya hiyo ya kesi kusikilizwa.
Kabla ya kuahirisha kwa kesi, watuhumiwa wa kesi hiyo, waliiomba mahakama imtaje mlalamikaji wa kesi hiyo ambaye amepelekea kushitakiwa kwa watu 12 katika mahakama hiyo ya Mwanakwerekwe.
Mbali na ombi hilo la watuhumiwa hao wote kwa pamoja wameiomba mahakama hiyo iwapatie hati ya mashitaka, pamoja na kutoa muda mrefu ili waweze kutafuta Wakili wa kuweza kuwasimamia na kuwatetea katika kesi inayowakabili watuhumiwa hao 12 ambao wamshitakiwa pamoja na Kiongozi wao Rashid Salum Adiy.
Akijibu kuhusiana na ombi la upande wa washitakiwa, Mwendesha Mashtaka alisema pamoja na kuwapatia hati hiyo ya mashitaka, washitakiwa hao wanapaswa kufahamu kwamba makosa yote ya jinai yanalalamikiwa na serikali kupitia Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), ambaye ndiye mwenye maamuzi ya kuyafungulia mashitaka mahakamani kwa mujibu wa sheria za Zanzibar.
Jumla ya watuhumiwa wa kesi hiyo ni 12 walishitakiwa kwa pamoja baada ya kukusanyika katika viwanja vya baraza la wawakilishi mwezi uliopota akiwemo kiongozi wa kikundi hicho, Rashid Salum Adiy (48) mkaazi wa Kikwajuni, Khamis Hassan Hamadi (51) mkaazi wa Jang’ombe na Hashim Juma Issa (54) mkaazi wa Mbweni
Wengine ni Ali Omar Omar (54) mkaazi wa Bububu,Masoud Faki Masoud (31) mkaazi wa Kilimahewa, Rammy Mbaraka Ahmed (48) mkaazi wa Michenzani na Salum Masoud Juma (38) mkaazi wa Rahaleo.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mussa Omar Kombo (67) mkaazi wa Mpendae, Omar Kombo Is-hak (21) mkaazi wa Magogoni, Haji Sheha Hamadi (49) mkaazi wa Chumbuni, Rashid Ali Rashid (21) mkaazi wa Mombasa, Suleiman Mustafa Suleiman (31) mkaazi wa Mombasa wote hao ni wakaazi wa Zanzibar.
Washitakiwa hao wote kwa pamoja wameshitakiwa kwa makosa ya kufanya mkusanyiko usio halali, kuendelea kukusanyika baada ya kutangazwa kutawanyika na ofisa wa jeshi la polisi na shitaka la uhuni na uzururaji na kubeba mabango yenye kupinga Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mwendesha Mashitaka wa mahakama hiyo, Said Ahmed Mohammed, aliwasilisha mashtaka hayo mbele ya mahakama hiyo ambayo ilijaa watu ndani na nje waliofika kusikiliza kesi hiyo.
Mapema mahakamani hapo, Mwanasheria huyo wa serikali aliwasomea watuhumiwa hao shitaka la kufanya mkusanyiko usio halali kinyume na vifungu vya 55 (1) (2) (3) na 56 vya kanuni ya adhabu sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.
Katika shitaka hilo aliifahamisha mahakama kwa kudai kuwa, Aprili 20 mwaka huu, majira ya saa 2:30 za asubuhi, huko Mbweni wilaya ya Magharibi Unguja, kwa pamoja na bila ya halali walijikusanya katika barabara ya Baraza la Wawakilishi huko Mbweni Zanzibar.
Alidai kuwa, mkusanyiko huo uliwafanya majirani na watu waliokuwa wanakwenda kwenye Baraza kupata khofu, kuwa wangeliweza kusababisha uvunjifu wa amani wakati hawakuwa na sababu za msingi za kukusanyika nje ya viwanja hivyo.
Mwanasheria hiyo alidai mahakamani hapo kuwa shitaka jengine ni kuendelea kukusanyika baada ya kutangazwa kutawanyika na ofisa wa polisi, ambapo washitakiwa hao walitakiwa kutawanyika kwa amani baada ya tangazo polisi, lakini waliendelea kukusanyika kinyume cha sheria.
Kwa mujibu wa Mwanasheria huyo, kitendo hicho cha kukataa amri hiyo halali ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 60 cha kanuni ya adhabu sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.
Aidha aliieleza mahakama hiyo kwamba shitaka la mwisho linalowakabili watuhumiwa hao 12 ni la uhuni na uzururaji, ambapo mahakama ilifahamishwa kuwa siku hiyo walipatikana wakiwa wamejikusanya kwenye barabara hiyo ya Baraza la Wawakilishi, wakiwa na mabango yenye maneno yanayopinga Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Ilielezwa mahakamani hapo kwamba kitendo hicho cha kukusanyika na kukamata mabango ni kosa chini ya kifungu cha 182 (d) cha sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar, ambacho walidaiwa kukifanya katika wakati na mazingira yanayoonesha kuwa hawakuwa na madhumuni halali.
Watuhumiwa wote 12 wapo nje kwa dhamana ya fedha taslimu shilingi 500,000 kila mmoja, pamoja na wadhamini wawili wenye vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, na mdhamini mmoja kati ya wadhamini hao wawili awe ni mfanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
 
Back
Top Bottom