Kesi ya Sumry High Class, kesi ya manji, na mafunzo kwa vijana wanaofungua

Bashir Yakub

Member
May 27, 2013
84
1,562
KESI YA SUMRY HIGH CLASS, KESI YA MANJI, NA MAFUNZO KWA VIJANA WANAOFUNGUAMAKAMPUNI.

Na Bashir Yakub.
+255 784 482 959.

Moja ya faida kubwa ambayo huwavutia wengi kuacha kufanya biashara kama mtu binafsi na kuamua kufanya biashara kwa kutumia kampuni ni hii ya kuwa kampuni na mmiliki ni vitu viwili tofauti na hivyo kosa la kampuni halimhusu mmiliki na kosa la mmiliki haliihusu kampuni.

Maana yake hata ukikopa kwa kutumia kampuni na ukashindwa kulipa basi mali zako binafsi haziguswi isipokuwa za kampuni tu. Kadhalika makosa mengine yatahesabika kutendwa na kampuni na itashitakiwa kampuni na si wewe mmiliki. Hili huwavutia wengi,yumkini tupate funzo kutoka kesi hizo hapo juu tukianza na hii ya Sumry.

Katika mahakama kuu ya biashara kanda ya Dar es salaam Mwaka 2012 kulifunguliwa maombi ya biashara (Misc.Commercial Cause No. 20/2012) kati ya MUSSA SHAIBU MSANGI vs SUMRY HIGH CLASS LIMITED.

Mlalamikaji/mleta maombi Mussa Shaibu Msangi alikuwa akiiomba mahakama kumkamata na kumfunga jela mmiliki/mkurugenzi Hamoud Muhammed Sumry kwa kushindwa kumlipa deni lake linalofikia Tshs 179,379,980 lililolimbikizwa kwa zaidi ya mwaka mmoja japokuwa mahakama ilishaamua alipwe.

Katika utetezi wake ndugu Sumry alisema kuwa inayodaiwa ni kampuni na hivyo ni kosa kisheria kutaka kumpeleka jela kwa kutolipa kwakuwa kisheria kuna tofauti kati ya kampuni na mmiliki wake, na hivyo kosa la kampuni ni kampuni ihusike, na kosa la mmiliki ni mmiliki ahusike.

Katika hukumu yake Jaji Songoro, alisema kuwa ni lazima Hamoud Muhammad Sumry yeye kama yeye mmiliki na mkurugenzi alipe deni hilo hata kama mkataba ulikuwa kati ya Mussa Shaibu na kampuni, kwasababu yeye kama mkurugenzi ameshindwa na inaonekana anaifanya kampuni ikwepe kumlipa mlalamikaji kwa zaidi ya mwaka.

Mahakama ikasema kuwa pale inapoonekana kampuni inakwepa kutekeleza majukumu yake ya kisheria kama kumlipa mlalamikaji, basi ukuta unaotenganisha kampuni na mmiliki unaondolewa na hapo wamiliki wanawajibika moja kwa moja kwa makosa ya kampuni. Hivyo ndugu Hamoud Muhammad Sumry akapewa siku 30 kuwa amemlipa ndugu Mussa Shaibu laa sivyo aenda jela yeye kama yeye.

Mwaka 2002 Yusuf Manji alikata rufaa katika CIVIL APPEAL No. 78/2002 kati ya YUSUF MANJI dhidi ya EDWARD MASANJA NA ABDALLAH JUMA.

Kupitia wakili wake Ndugu Mpaya Kamara alikuwa akiilalamikia mahakama kuu kwa kumuamuru awalipe overtime,hela ya usafiri na posho ya pango Edward Masanja na Abdallah ambao walikuwa walinzi kwenye kampuni yake ya Metro Investment Limited.

Hoja mojawapo kati ya hoja alizokuwa nazo ni kuwa kwanini mahakama kuu imtake alipe yeye kama yeye wakati walinzi wana mkataba na kampuni na sio yeye, na kuwa kwa mujibu wa sheria yeye na kampuni ni vitu viwili tofauti.

Mahakama ya rufaa chini ya majaji watatu ilisema kwamba, kwa kuwa kumbukumbu zinaonesha kuwa Manji amekuwa akificha mali za kampuni ili zisiweze kukamatwa ili kuwalipa walalamikaji basi ni sahihi kukamatwa yeye kama yeye ili kulipa, na akishindwa aende jela hata kama mkataba ulikuwa kati ya walinzi na kampuni.

Katika kesi hizi mbili sisi wajasiriamali tunaofungua makampuni tunapata kujifunza kuwa kanuni ya kisheria ya kumtenganisha mmiliki wa kampuni na kampuni haiwezi kutumika kuvunja sheria ukiamini kuwa hautaguswa kwakuwa kampuni ndiyo imetenda.

Kanuni hii ina ukomo na mipaka yake, na moja ya mpaka ni pale kampuni inapotumika kuvunja au kukwepa taratibu za kisheria. Kwa hivyo ni muhimu kulijua hili na ukajihadhari.
 
Lifting Corporate Veil....Salomon v Salomon hahahaha lile desa la Wakenya la Corporate Law lilikua na madini ya kutosha sana aiseee.....
 
Back
Top Bottom