Kesi ya Agnes Doris Liundi - Nini hasa kilitokea...? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kesi ya Agnes Doris Liundi - Nini hasa kilitokea...?

Discussion in 'Jukwaa la Sheria (The Law Forum)' started by Mtambuzi, May 11, 2012.

 1. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #1
  May 11, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280

  court.png

  Mahakama_Kuu_2.JPG


  Tukio lenyewe lilitokea hapo majira ya asubuhi mnamo Februari 21, 1978. Ni baada ya kuambiwa mumewe wakati anaenda kazini kwamba akirudi asimkute hapo nyumbani, na kama akimkuta, atamtoa hapo nyumbani kwake uchi. Alikuwa na watoto wao wanne hapo nyumbani. Baada ya mumewe kuondoka, na yeye aliondoka na gari kuelekea mjini ambapo alinunua chupa kadhaa za sumu ya kuulia wadudu.


  Alipofika nyumbani kwake, aliwaita watoto wake wote wanne chumbani kwake na kujifungia nao ndani, kisha akawaambia "tunaondoka" watoto wale walimuuliza, "tunakwenda wapi?" yeye akawajibu, "tunasafiri, lakini huko tunakokwenda hatupajui." Aliwabusu watoto wale na wao wakambusu mama yao na kisha wakapeana mikono kama ishara ya kutakiana safari njema. Baada ya tukio hilo, aliwapa kila mmoja kikombe chenye mchanganyiko wa ile sumu na Orange Squash na yeye akachukua mchanganyiko huo uliokuwa kwenye kikombe na kunywa. Baada ya kunywa mchanganyiko huo wote walianza kutapika, kutokana na kutapika huko, aliamua kunywa Iodine. Pia alikunywa vipande vya chupa zilizosagwa na kujifungia katika chumba kingine.

  Mfanya kazi wake wa hapo nyumbani aitwae Ramadhan na mtu mwingne aliyetajwa kwa jina la Bibie waliwasikia watoto wakilia huko chumbani. Baadae kidogo alifungua mlango na kumwambia Bibie amuoshe mmoja wa watoto wale ambaye alikuwa ni mdogo kwa wenzie kwani alikuwa anatapika na kuharisha kisha akarudi ndani na kujifungia katika chumba hicho peke yake.

  Aliombwa na Ramadhan pamoja na Bibie watumie simu ya pale nyumbani kumjulisha mumewe juu ya tatizo lile lakini alikataa.

  Wale watoto wengine watatu nao walianza kutapika na kuharisha na hali zao zilibadilika na kuwa mbaya. Ramadhan aliwajulisha majirani na walipofika, yeye alikwenda hadi chumba cha pili alipokuwa amejifungia na kumuuliza kama ni kitu gani kimewatokea wale watoto. Alimwambia, "Ramadhan, naomba uniache nife na watoto wangu, kwa sababu baba Taji (yaani Mumewe) hanipendi."

  Wote walikimbizwa hospitalini na watoto watatu waliripotiwa kufariki lakini yeye na mwanaye mkubwa madaktari walifanikiwa kuyanusuru maisha yao.

  Taarifa ya kitabibu ilithibitisha kwamba wale watoto watatu walifariki kutokana na kunywa sumu, ambayo walinywesha na mama yao.

  Kesi hii ni ya mwaka 1979 ya Agnes Doris Liundi, alishitakiwa na Jamhuri kwa kosa la kuwauwa watoto wake watatu kwa kuwanywesha sumu hapo mnamo tarehe 21 Februari 1978 nyumbani kwake. Kosa hilo la Kuua kwa kukusudia (Murder) limeainishwa kwenye kanuni ya adhabu (Penal Code) kifungu cha 196.

  Kwa mujibu wa maelezo yaliyosomwa pale mahakamani wakati wa kusikilizwa kwa kesi hii ilielezwa kwamba, Agnes Doris Liundi aliolewa na George Liundi mnamo Februari 1967.

  Baada ya miaka miwili ya maisha yao ya ndoa iliyokuwa na furaha na amani, ghafla kukazuka kutoelewana na ugomvi usiyoisha kati ya wanandoa hao. Sababu iliyoelezwa kusababisha kutokuelewana huko ni hofu aliyokuwa nayo mume kuwa huenda mkewe siyo muaminifu kwake.

  Kutokana na ugomvi huo, mtuhumiwa alifukuzwa hapo nyumbani kwao na mumewe.

  Kama wiki moja hivi kabla ya kutekeleza mauaaji hayo, Mtuhumiwa na mumewe walihudhuria sherehe fulani. Wakiwa hapo kwenye hiyo sherehe ndipo mumewe alipomuona mwanaume mmoja ambaye alimtuhumu kwamba alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mkewe na ndipo ule uhasama wao ukaibuka upya na kukazuka ugomvi mkubwa kati yao, yaani mtuhumiwa na mumewe, na ndio ukapelekea mtuhumiwa kutekeleza mauaji hayo siku ya tarehe 21, Februari 1978.

  Ilielezwa pale mahakamni kwamba, kabla ya kutekeleza mauaji hayo, mtuhumiwa aliandika barua nne na zote zilikuwa na tarehe hiyo ya 21 Februari 1978, na barua hizo ziligunduliwa na Polisi na zilifikishwa pale mahakamani kama kidhibiti. Barua tatu zilikuwa zimendikwa kichwa cha habari kisemacho, "kwa yeyote anayehusika," na moja ilikuwa inamuhusu mtu mmoja aliyetajwa kwa jina la mama Gaudensia ambaye ni rafiki wa mtuhumiwa.

  Barua moja kati ya zile tatu zilizoandikwa kichwa cha habari kisemacho "Kwa yeyote anayehusika" ilisomwa pale mahakamani kama ifuatavyo:

  c/o Box 9050
  DAR ES SALAAM

  21/2/1978


  KWA YEYOTE ANAYEHUSIKA


  Uamuzi niliouchukuwa ni wa mwisho. George mume wangu naomba asisumbuliwe au kuteswa au kulazimishwa kwa namna yoyote kwa sababu nilikuwa nampenda.

  Nimewachukuwa wanangu kwa sababu sitaki wateseke kama nilivyoteseka katika upweke wa kutisha. George mume wangu, hukujua ni kiasi gani nilikupenda nilipokuwa hai. Lakini sasa unaelewa.

  KWA AFISA WA POLISI

  Tafadhali msimchukulie mume wangu hatua yoyote kwa sababu hana hatia.

  Kwa mujibu wa maelezo yake aliyoandikisha Polisi hapo mnamo 3 April 3, 1978, ikiwa ni miezi miwili baada ya tukio hilo la mauaji, mtuhumiwa alieleza historia ya maisha yake tangu utotoni. Alieleza jinsi alivyoishi maisha ya tabu na mashaka baada ya mama yake kufariki ambapo alililelewa kwa mateso na upweke na mama yake wa kambo.

  Mtuhumiwa alielezea maisha yao ya ndoa na mumewe yalivyokuwa na furaha na amani kwa kipindi cha miaka miwili tangu waoane, na jinsi maisha yalivyobadilika na ndoa yake kukumbwa na misukosuko isiyoisha.

  Alisema kwamba, matatizo yalianza baada ya yeye kudai kwamba aliwahi kubakwa na kaka wa mmoja wa marafiki zake, na kutokana na kitendo hicho alimuambukiza mumewe maradhi ya zinaa. Hakuthubutu kumweleza mumewe kuhusu tukio hilo la kubakwa kwa muda mrefu alitunza siri hiyo, lakini baadae aliaamua kumweleza mumewe, jambo ambalo lilimletea matatizo makubwa katika ndoa yake mpaka kupelekea tukio hilo la tarehe 21 Februari 1978.

  Wakati mumewe anaondoa hapo nyumbani siku hiyo ya tarehe 21 Februari 1978, mtuhumiwa alichanganyikiwa na alianza kukumbuka maisha yake ya utotoni jinsi yalivyokuwa ya mateso na kujikuta akiwa hana pa kwenda. Alimuona mumewe kama mama yake, baba yake, kaka yake na dada yake na maisha yake yote alikuwa akimtegemea mume wake huyo.

  Aliamua kwenda kununua sumu na kurudi nayo nyumbani, alijaribu kulala lakini hakupata lepe la usingizi na hakupata suluhu, nini cha kufanya kuhusiana na jambo hilo, na ndipo alipoamua kunywa hiyo sumu.

  Kwa maelezo yake mwenyewe alisema:

  "Nilikuwa na hasira na wasiwasi kuhusiana na matatizo kati yangu na mume wangu. Nilijiuliza, ina maana matatizo haya yamefikia hatua ya kutisha kiasi cha mume wangu kufikia hatua ya kunifukuza. Nilijiwa na wazo kwamba, acha nijimalize (Kujiuwa) mwenyewe niwaache wanangu wakiwa hai. Lakini baadae nilianza kukumbuka maisha yangu ya utotoni jinsi yalivyokuwa ya mateso na upweke, na nilijiuliza kwamba huenda na wanangu nao wataishi maisha kama yangu kwa kuishi na mama wa kambo. Kwa kuwa mume wangu aliniambia nitakapoondoka nihakikishe siwaachi wanangu nyuma, niliamua kuwachukuwa na kuingia nao chumbani na kufunga mlango. kisha nikawaambia "tunaondoka" wakaniuliza, "tunakwenda wapi?" nikawajibu, "tunasafiri, lakini huko tunakokwenda hatupajui." Kisha nikawabusu na wao wakanibusu, wakapeana mikono kama ishara ya kutakiana safari njema. niliwapa kila mmoja kikombe chenye mchanganyiko wa ile sumu na Orange Squash na mimi nikachukua mchanganyiko huo uliokuwa kwenye glasi na kunywa. Baada ya kunywa mchanganyiko huo wote tulianza kutapika, kutokana na kutapika huko, aliamua kunywa Iodine. Pia nilikunywa vipande vya chupa zilizosagwa na kujifungia katika chumba kingine. Kutoka muda huo, nilipoteza fahamu na sikuweza kutambua kilichotokea baada ya hapo"

  Wakati alipokamatwa mtuhumiwa alikuwa chini ya uangalizi wa daktari aliyejulikana kwa jina la Dk. Haule, huyu ni mtaalamu wa magonjwa ya akili aliyekuwa akifanya kazi katika Hospitali ya Muhimbili.

  Aliwasilisha ripoti yake pale mahakamani na pia alitoa ushahidi wake pale mahakamani. Kwa kifupi katika maoni yake Dk. Haule alisema kwamba, wakati akitekeleza tukio hilo la mauaji, mtuhumiwa alikuwa anajua ni nini anachokifanya, alikuwa anajua kwamba anawauwa watoto wake kwa kuwalisha sumu, lakini hakujua kwamba kufanya kitendo hicho ni kosa.

  Kwa mujibu wa vifungu vya 12 na 13 vya sheria ya kanuni ya adhabu ambavyo vinahusika na swala hili la uwendawazimu vinaeleza kama ifuatavyo:

  Kifungu cha 12. Sheria inamchukulia mtu yeyote kuwa ni mwenye akili timamu kwa wakati wowote mpaka pale itakapoamuliwa vinginevyo.

  Kifungu cha 13. Mtu yeyote hawezi kuchukuliwa kuwa ametenda kosa kama kutenda kwake au kutokutenda kwake na katika muda wa kutenda au kutokutenda alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa na akili na hivyo kumfanya kutokutambua alichokuwa anakifanya.

  Dk. Haule katika ushahidi wake kwenye ripoti yake aliainisha vidokezo vifuatavyo,

  Kwa mara ya kwanza alipomuona mtuhumiwa muda mfupi baada ya tukio hilo la mauaji, mtuhumiwa hakuwa katika hali ya kawaida na hakuonekana kujali. "nilikuwa kama vile naongea na mti." Alisema Dk. Haule. Kwa maoni yake Dk. Haule alisema, inawezekana kwamba mtuhumiwa alikuwa katika hali ya isiyo ya kawaida kwa majuma mawili au zaidi kabla ya tukio hilo, na kwamba, mtuhumiwa alikuwa anajua ni nini anachokifanya wakati alipokuwa akiwanywesha sumu wanae, lakini hakujua kwamba kitendo hicho ni kosa.

  Alielezea juu ya kipindi kigumu cha maisha ya ndoa ya mtuhumiwa alichopitia, jinsi maisha yake ya ndoa yalivyokumbwa na misukosuko ya kutoelewana na mumewe. Nafasi aliyokuwa nayo, maisha aliyopitia utotoni na jinsi alivyokuwa akimtegemea na kumtii mumewe. Dk. Haule, alikuwa na maoni kwamba, kitendo cha mtuhumiwa kuamua kujiuwa na kuwaua wanae, aliamini kwamba, alikuwa amemriwa na mumewe afanye hivyo. Alisema kwamba, alisoma barua zilizokuwa zimeandikwa na mtuhumiwa kabla ya kutekeleza mauaji hayo lakini barua hizo hazikuweza kubadili maoni yake juu ya jambo hilo.

  Wakati fulani Dk Haule alidai kwamba mtuhumiwa hakuwa na tatizo la kurukwa na akili lakini baadae alisema kwamba mtuhumiwa alikuwa na tatizo hilo.

  Kwaq mamneno yake mwenyewe Dk. Haule alisema. "Alikuwa amerukwa na akili, na aliona kitendo alichokifanya kilikuwa kinakubalika."

  Dk. Haule alisema kwamba, mwaka mmoja baada ya tukio hilo hali ya mtuhumiwa iliimarika, kiasi cha kujua kwamba, kitendo alichokifanya kilikuwa ni kosa, lakini bado alikuwa kwenye matibabu.

  Katika kesi hii mwanasheria aliyekuwa akimtetea mtuhumiwa alikuwa ameegemea kwenye utetezi wa uwendawazimu.

  Akitoa utetezi wake wakili Jadeda alisema kwamba, wakati mtuhumiwa akitekeleza mauaji hayo, hakuwa akijua kwamba kitendo anachokifanya ni kosa. Wakili huyo alirejea maoni ya Dk. Haule.

  Wakili huyo alisema kwamba, mtu yeyote aliyerukwa na akili anaweza kupanga hatua kwa hatua kutekeleza mauaji kama aliavyofanya mtuhumiwa na asijue kama kitendo alichokifanya ni kosa.
  Wakili Jadeda alikuwa akipinga maoni ya upande wa mashitaka kwamba, mtuhumiwa alikuwa kijua kitendo anachokifanya ni kosa.

  Akisoma hukumu Mheshimiwa Jaji Makame alikubaliana na swala la mtuhumiwa kuwa na dhamira ovu (Malice aforethought), hasa kwa kuangalia vitendo vya mtuhumiwa tangu maandalizi, dhamira na akiwa na utambuzi kwamba, akiwanywesha wanae sumu itawasababishia kifo, na hiyo inadhihirisha kwamba mtuhumiwa alikuwa anajua ni nini anachokifanya, na si lazima ajue kwamba kufanya hivyo ni kosa.

  Hata hivyo Mheshimiwa Jaji Makame alikuwa ameshawishika kuamini hivyo kutokana na barua nne alizoziandika mtuhumiwa kabla ya kutekeleza mauaji hayo, ambazo aliziandika sambamba na tendo alilofanya tarehe 21 Februari 1978. Barua hizo kwa uwazi zilionyesha kabisa kwamba mtuhumiwa alikuwa anajua anachokifanya ni kosa.

  Kwa maneno yake Mwenyewe Mheshimiwa Jaji Makame alisema, "Katika barua ambayo ilisomwa hapa mahakamani wakati wa shauri hili, mtuhumiwa alisema wazi kwamba mumewe asije akaadhibiwa au kuteswa kwa kitendo alichokifanya yeye mtuhumiwa. Pia kulikuwa na ombi la mtuhumiwa kwa Polisi kwamba, wasije wakamchukulia hatua mumewe kwa sababu hana hatia."

  Muheshimiwa Jaji Makame aliendelea kusema kwamba, wazo la kutokuwa na hatia na kutompa mumewe adhabu katika barua alizoandika mtuhumiwa, linadhihirisha wazi kwamba mtuhumiwa alikuwa anajua kwamba kitendo anachokifanya ni kosa na alitaka kuweka wazi kuwa mumewe hahusiki kwa namna yoyote na kitendo alichokifanya yeye mtuhumiwa. Alijua kama mumewe akihusishwa na kitendo alichokifanya yeye mtuhumiwa, ataadhibiwa kwa kosa hilo.

  Mheshimiwa Jaji Makame aliendelea kusema,

  "Ni kweli Dk. Haule alisema kwamba, ukiachana na barua hizo alizoziandika mtuhumiwa, lakini yeye alikuwa na maoni kwamba, mtuhumiwa hakuwa anajua anachokifanya kuwa ni kosa. Alisema, barua zilimuonesha kwamba, mtuhumiwa alikuwa akimtegemea mumewe kwa kiasi kikubwa na hasa katika mahusiano yao. Kama tunamuelewa Dk. Hauli vizuri, alikuwa huenda anamaanisha kwamba, hizo barua zilikuwa na uhusiano na imani aliyokuwa nayo mtuhumiwa kwamba, alikuwa ameshurutishwa kujiuwa na kuwauwa watoto wake na mumewe. Kwa bahati mbaya barua haijaeleza kuwa mtuhumiwa alikuwa na imani ile. Ilikuwa ni ahuweni aliyoiweka Dk Hauli. Japokuwa barua ilieleza kuwa mtuhumiwa alikuwa anamtegemea sana mumewe, lakini bado zilikuwa zinathibitisha kwamba mtuhumiwa alikuwa anajua kitendo anachokifanya ni kosa.
  Pia nashindwa kuunganisha maelezo ya barua hizo na maoni ya kurukwa na akili yaliyotolewa na Dk. Haule, aliposema kwamba, mtuhumiwa aliamini kuwa ameamriwa na mumewe ajiuwe na kuwauwa watoto wake."

  Mheshimiwa Jaji aliendelea kusema,

  "Kwangu mimi, namuona Dr. Hauli kama mtaalamu mwenye uzoefu na ujuzi mkubwa wa magonjwa ya akili, pamoja na mambo mengine, pia ni mwanachama Royal College of Psychiatrists na anayo Diploma ya Psychiatric Medicine aliyoipata nchini Uingereza. Naheshimu sana maoni yake kulingana na utaalamu wake na ninashindwa kupinga ushahidi wake. Pia ninakubaliana na ukweli kwamba hata kama mtuhumiwa ataonyesha kurukwa lakini hiyo itakubalika iwapo kutakuwa na kipimo chenye uwelekeo (Balance of Probability).

  Mtuhumiwa lazima aoneshe ushahidi wote; kwamba kutokuwa na akili timamu ni zaidi ya kuwa timamu. Ingawa inawezekana ikawa chini ya tunachodhamiria. Katika kuliweka sawa hili mamlaka ya kuthibitisha inafananishwa na kesi ya Nyinge Siwato Vs Jamhuri 1959 East Africa 974 ikifuatiwa mara nyingi sana ikihusishwa na MbekuleV-R. 1971, East Africa 479. Jaji Enzi zake alielezea katika kesi ya Siwato "Mahakama haifungwi kukubaliana na ushahidi wa hospitalini (Medical Testimony) kama/endapo kuna sababu madhubuti ya kutofanya hivyo. mwisho wa siku ni kazi ya mahakama kutafuta ushahidi na viambatanisho katika kufanya hivyo, ni wajibu wangu kuangalia na kulipima na ushahidi uliotolewa kabla na ikiwemo utaalam wa Daktari."

  Mheshimiwa Jaji Makame akihitimisha hukumu hiyo alisema:

  "Inawezekana hasa kwamba sheria yetu katika swala la kurukwa na akili imepitwa na wakati na ni ya zamani sana, Dk. Haule katika ushahidi alieleza kuwa katika utaalamu wa sasa, utofauti kati ya kurukwa na akili na kutojitambua katika utenedaji vinapingana. Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa hekima linaweza kulifanyia marekebisho hili sambamba na sheria ndogo ndogo na kulileta katika utandawazi wa kitabibu. Mipaka ya kimahakama, ikiwemo ya Afrika Mashariki wamefanya hivyo."

  Mtuhumiwa katika kesi hii alihukumiwa kunyongwa.
   
 2. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #2
  May 11, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Haya ni Ijumaa nyingine tena wasomaji wa JF, nimekuja na kesi hii iliyowahi kutokea hapa hapa nchini miaka ya mwishoni mwa 1970. Leo sina maneno mengi, nawaachie wenyewe msome na kuweka maoani yenu...........
   
 3. Smile

  Smile JF-Expert Member

  #3
  May 11, 2012
  Joined: Jul 18, 2011
  Messages: 15,427
  Likes Received: 194
  Trophy Points: 160
  daaah mimi kuzaliwa ilikuwa bado sana mtambuzi....
  ila dah .... am speechless kwa kweli..
  nitarudi
   
 4. Limbani

  Limbani JF-Expert Member

  #4
  May 11, 2012
  Joined: Apr 24, 2008
  Messages: 1,438
  Likes Received: 91
  Trophy Points: 145
  Duh, huyu Taji mtoto aliyebaki ndio huyu mtangazaji Taji Liundi?
   
 5. Smile

  Smile JF-Expert Member

  #5
  May 11, 2012
  Joined: Jul 18, 2011
  Messages: 15,427
  Likes Received: 194
  Trophy Points: 160
  huyo mama alinyongwa kweli Mtambuzi
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 6. mtotowamjini

  mtotowamjini JF-Expert Member

  #6
  May 11, 2012
  Joined: Apr 23, 2012
  Messages: 4,540
  Likes Received: 10
  Trophy Points: 0
  aisee story ndefu sana nimeshindwa kuisoma yote...so kwa walioisoma yote huyo mama alifanywa nini na mahakama??
   
 7. SALOK

  SALOK JF-Expert Member

  #7
  May 11, 2012
  Joined: Sep 20, 2011
  Messages: 2,677
  Likes Received: 867
  Trophy Points: 280
  Ahsante sana Mtambuzi kwa kuendelea kutuhabarisha kile kinacho.../kilichopata kutokea mahakamani, mungu azidi kukuimarisha kwa afya na siha njema kabisa! labda ningependa kujua kama hiyo adhabu ilitekelezwa ama la! Historia ya maisha ya huyo mama yanasikitisha kwakweli!
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 8. Bishanga

  Bishanga JF-Expert Member

  #8
  May 11, 2012
  Joined: Jun 29, 2008
  Messages: 15,347
  Likes Received: 47
  Trophy Points: 0
  Kwanza wali commute to life sentence,kisha Mwalimu akamuachia after seven years,she is alive and well,yuko hapa dar maeneo ya keko.
   
 9. M

  MAHEPE Member

  #9
  May 11, 2012
  Joined: Mar 10, 2011
  Messages: 84
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 15
  NASIKIA NDIO HUYU HUYU TAJI LIUNDI MTANGAZAJI NA BABA YAKE NDIO YULE ALIKUWA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA... kama nimekosea mnaojua mnisahihishe
   
 10. Bishanga

  Bishanga JF-Expert Member

  #10
  May 11, 2012
  Joined: Jun 29, 2008
  Messages: 15,347
  Likes Received: 47
  Trophy Points: 0
  Mkuu Mtambuzi,mmmhhhh haya bana.........
   
 11. PetCash

  PetCash JF-Expert Member

  #11
  May 11, 2012
  Joined: Mar 20, 2012
  Messages: 1,679
  Likes Received: 170
  Trophy Points: 160
  Duh! kweli tembea uone na kusikia!...Ila sasa Jaji Makame alivyomhukumu kifo si ndio katekeleza alichokua anataka Agness?
  Insecurities za huyo mumewe is one thing( Probably hurts ) but seeing your children die and your wife hanged? Probably anajilaumu hadi sasa if at all he is alive. Guys we have to try to understand our women- its not that hard! Sio unakurupuka tu eti nisikukute home, mke mwenyewe hujamkuta red handed!
   
 12. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #12
  May 11, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Smile ....habari ambazo sijazithibitisha ni kwamba adhabu haikutekelezwa, alipata msamaha wa rais..........................
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 13. Smile

  Smile JF-Expert Member

  #13
  May 11, 2012
  Joined: Jul 18, 2011
  Messages: 15,427
  Likes Received: 194
  Trophy Points: 160
  dah Bishanga kwa kunusa...loh
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 14. Lukolo

  Lukolo JF-Expert Member

  #14
  May 11, 2012
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 5,137
  Likes Received: 76
  Trophy Points: 145
  Duh, haya maisha haya ni safari ndefu sana. Hiki kisa ni kigumu kupindukia na cha hatari sana. Huyu mama alikuwa na moyo wa ajabu sana. Hakuona huruma pale anapoanza kuwalisha sumu watoto wake? Kwanini asingejiua mwenyewe tu awaache watoto wahangaike wanavyoweza? Najiuliza pia mmewe aliathirika kiasi gani kisaikolojia kutokana na hili. Na kwa upande wetu tunajifunza nini? Tuvumilie kuishi na wale wasiotufaa kwa vile tu resulting outcomes zake ni za hatari au tuchukue hatua bila kujali consequences.
   
 15. FirstLady1

  FirstLady1 JF-Expert Member

  #15
  May 11, 2012
  Joined: Jul 29, 2009
  Messages: 16,575
  Likes Received: 541
  Trophy Points: 280
  Mtambuzi mbona umenipiga kamba kule ..aaaaaaaaaagh asante sana uwe na Ijumaa njema kama kawaida namba ya M-pesa ni ile ile sijabadili
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 16. Bishanga

  Bishanga JF-Expert Member

  #16
  May 11, 2012
  Joined: Jun 29, 2008
  Messages: 15,347
  Likes Received: 47
  Trophy Points: 0
  Kusema kweli najisikia vibaya kusoma hii story, hata huyo mama aliyewabeba watoto kuwapeleka watoto muhimbili na wakamfia mkononi namjua,sipendi kukumbuka kabisa.
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 17. Amyner

  Amyner JF-Expert Member

  #17
  May 11, 2012
  Joined: Jul 13, 2011
  Messages: 2,404
  Likes Received: 54
  Trophy Points: 145
  Mtambuzi you always make my fridays good kwa hizi habari za kusisimua. Nilishawahi isikia hii story ya kusikitisha ya familia ya liundi. Ila eti nilisikia Mwl nyerere aliamuru kuachiwa huyu mama sababu kuua wanae ilikua ni torment tosha katika maisha yake? Au maneno ya watu tu!
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 18. FirstLady1

  FirstLady1 JF-Expert Member

  #18
  May 11, 2012
  Joined: Jul 29, 2009
  Messages: 16,575
  Likes Received: 541
  Trophy Points: 280
  Oooops kuna matukio ya kutisha utabaki na picha gani kichwani baada ya kuua wanao namna ile
  inasikitisha sana
   
 19. Amyner

  Amyner JF-Expert Member

  #19
  May 11, 2012
  Joined: Jul 13, 2011
  Messages: 2,404
  Likes Received: 54
  Trophy Points: 145
  Pole sana bishanga.
   
 20. J

  JOJEETA Senior Member

  #20
  May 11, 2012
  Joined: Mar 27, 2012
  Messages: 163
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  well said petcash,wanaume muache kuongozwa na hisia.ni vizuri kuthibitisha jambo kabla ya kutoa maamuzi.swali la kizushi hivi mtambuzi wewe mwanasheria?
   
Loading...