Jambo hili lilikuwa na busara huko mwanzoni , likionekana kuweka msawaziko wa udini hasa kwenye nchi changa iliyoanza kujitawala kama yetu yaani msingi wa "check and balance!"
Ukiangalia wenzetu wa Kenya, bado wana matatizo ya udini, tangu nchi yao ipate Uhuru mwaka 1963 haijawahi kutawaliwa/kuongozwa na Rais muislam (japo sio lazima) lakini kwenye nchi yenye mchanganyiko wa dini kuu mbili lazima kigezo hicho kitaleta manung'uniko. Na tayari watu wa ukanda wa pwani hasa maeneo ya Mombasa na Lamu wameshaanza kulalamika hata kudai kuundwa kwa "Mombasa Republic".
Mwl Nyerere aliona mbali na alikuwa na mantiki nzuri kufanya hivyo, sio kwenye dini tu Bali hata ukabila , ukanda na bara na visiwani, kwamba Rais akitokea Bara basi makamu wake Lazima atokee visiwani, na waziri mkuu atoke kanda Fulani tofauti na anayotoka Rais au makamu wake, inaleta picha nzuri kwamba nchi nzima imejumuhishwa kwenye utawala / serikali.
Japo ni kweli jambo hili likizidi sana linaweza kuja kuleta mshikeli au malalamiko huko mbeleni kwa wengine kuona kama haki yao imepokwa kwakuto kupewa mtu/kiongozi wa imani yao, maana mazoea mabaya na wanasema "kawaida ni kama sheria!"
Japo hilo sio takwa la sheria au katiba yetu kwamba lazima Marais wafuate mbadilishano wa dini au kanda.
Pia sio tu kwamba inaweza kuleta malalamiko ya udini lakini hata udhehebu, kwani tangu nchi hii imepata Uhuru wake mwaka 1961 inaongozwa na maraisi kutoka dhehebu moja tu la Roman Catholic, hili pia tuliona likileta malalamiko kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 pale mzee Edward Lowassa alipowaambia waumini kanisani kwamba "sasa ni zamu ya walutheri!". Japo hili pia sio jambo la kikatiba lakini tayari linalalamikiwa sana kwa baadhi ya wakristo wa madhehebu ya kiprotestanti wakisema tunaongozwa na mfumo Katoliki.
Sikubaliani na hoja hizo kwa maana katiba yetu haina mwongozo wa dini, dhehebu wala kabila, japo naunga mkono hekima na busara ya kuangalia " check & balance" ili kuondoa malalamiko yasiyo na msingi ambayo yanaweza kuja kuathiri umoja wetu na mshikamano uliojengwa kwa miaka mingi na waasisi wa taifa hili.
Mungu ibariki Tanzania.