Katiba mpya: Mambo yotenyawe ya muungano

Mkandara

JF-Expert Member
Mar 3, 2006
15,772
8,958
MAONI KUHUSU KATIBA MPYA

Kwa nini mambo yote yawe ya Muungano.
Kufuatia mgogoro uliopo baina ya pande mbili za kisiasa kushindwa kufikia muafaka juu ya muundo wa serikali ningependa kusema tatizo la nchi yetu lipo ndani zaidi ya swala la idadi ya serikali zetu iwe 1, 2 au 3 kwa sababu serikali huundwa kwa minajiri ya kugawana mamlaka ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo. Na ifahamike tu kwamba hakuna muundo maalum wa serikali ziwe ngapi ktk mfumo wa washirika ktk utawala wowote iwe ule wa Muungano (union), Shirikisho (federation), Jumuiya (Confederation/Community) kwa sababu ushirika haujengwi kwa idadi ya serikali bali hali halisi ya matakwa ya wananchi ktk ushirika wao kwa masharti na malengo walotaka kuyafikia ndio hujengwa serikali zake ili kuwafikia wananchi haraka na wepesi zaidi.

Mgogoro wa kisiasa
Sintojikita ktk mgogoro wa kisiasa ulofuatia bunge maalum la katiba kuvunjika kwa sababu huo ni mjadala mrefu sana pengine tutaugusia pale inapopaswa isipokuwa nitakwenda moja kwa moja katika kutoa maoni yangu kuhusiana na mapungufu ya kiutawala ndani ya katiba iliyopo ambayo wananchi walikusudia kufanywa na sio mgogoro juu ya Muungano wetu ama serikali ngapi zinafaa kwa sababu kati ya wananchi walochangia sana mjadala huu wa katiba na kuufuatilia kwa ukaribu sana toka mwaka 2002 hapa JF mimi nilikuwa mmoja wapo.

Kwa mtazamo wangu, baada ya kutazama kwa kina malalamiko ya pande zote mbili ambazo zingependa sana kuishi pamoja kwa amini na utulivu lakini wameshindwa kufikia muafaka wowote juu ya Mustakabali wa taifa hili ndani ya UTAIFA huu imetokana na wote kushindwa kuingia ndani zaidi kutazama kiini cha matakwa ya wananchi bali wametumia siasa zaidi kupanua wigo la hoja za Muungano wenyewe jambo ambalo wangeweza kuwakilisha hoja hiyo katika vikao vya bunge na kadhalika pasipo kuathiri uandishi wa katiba tuitakayo. Hivyo nimekuja na mapendekezo ambayo nina hakika yatagusa hisia za wananchi wa sehemu zote za JMT ikiwa ni kuanza na muundo wa UTAWALA na mamlaka yake.

Ni imani yangu kwamba kutokana na hoja za pande mbili zote ambazo zimejikita zaidi ktk Muungano na serikali ukiwasoma kwa undani utagundua kwamba wanahitilafiana zaidi ktk kugawana MAMLAKA ya utekelezaji wa shughuli za serikali hivyo matatizo hayapo ktk aidha Muungano wenyewe ama idadi ya serikali. Lakini hata utawala huu umejaribu sana kuongeza hesabu za mikoa, wialaya na hata majimbo lakini kwa vile mabadiliko hayo hayatoi mamlaka kamili kwa vyombo vya serikali hizo ili kutekeleza majukumu yao na kuwajibishwa na wananchi, mabadiliko hayo hayakuleta mafanikio zaidi ama kupunguza kero za wananchi.

Hivyo katiba yetu bado inapwaya sana ktk kutoa mamlaka kwa wananchi na serikali, serikali, halmashauri zao kwa sababu bado mfumo mzima wa utawala wa nchi hii upo bado ktk mageuzi (transition) ua Kisiasa na kiuchumi na ilitakiwa hatua kwa hatua kuweza kufikia mageuzi kamili ikiwa KATIBA ya nchi yetu hii itabadilishwa na kutoa mamlaka hayo kwa vyombo vinavyostahili kuleta mabadiliko yanayokusudiwa. Sheria mama ndiyo dira na mwongozo wa mabadiliko yote na sii kutegemea muundo wa washirika ama idadi ya serikali ndizo hupelekea kupata maendeleo.

Hivyo kwa kuwa naamini kwamba mgogoro mkubwa wananchi wa pande zote mbili unahusiana na maslahi ya nchi hizo inaonyesha wazi kwamba katiba iliyopo ina mapungufu ambayo hayakomei ktk washirika wa muungano wa nchi hizi mbili bali mgogoro huo unashuka hadi ktk tawala za mikoa, wilaya na miji yake kwa madai ya kutopewa huduma bora kulingana na mahitaji yao. Mapungufu haya ya muda mrefu yamezua kero nyingi sana toka Halmashauri za mitaa, miji, wilaya, mikoa, serikali 2 hadi imefikia watu kutokuwa na imani na viongozi ama serikali zao kwa sababu ya muundo mzima wa Utawala wa nchi yetu ulijengwa ktk misingi ya Kijamaa.

Chama tawala kilikuwa na mamlaka yote ya kiutawala toka uchaguzi wa wajumbe wa nyumba kumi, viongozi wa halmashauri, wabunge, mawaziri, baraza kuu la Mawaziri (executive council), mahakimu, uteuzi wa viongozi wote wa taasisi serikali, mashirika ya umma, vyoombo vya serikali, vyama vya ushirika, uteuzi wa watendaji wakuu wa ngazi zote za serikali, nafasi za kazi kwa waajiriwa na kadhalika. Chama tawala pia kilikuwa ndicho chombo pekee kilichomiliki njia kuu za uchumi ambazo ni pamoja na Ardhi, maji, madini, misitu, mafuta, nguvu za umeme, usafiri, njia za habari, bishara za nje, mabenki, bima, viwanda vya chuma, silaha, simenti, mbolea, viwanda, ugawaji na mambo mengi makubwa ambayo kwa wakati ule ndio ilikuwa msingi mkubwa wa ujenzi wa UTAIFA wetu.

Haya yote ni mambo yalokuwa ktk siasa ya Ujamaa na Kujitegemea chini nya chama kimoja na haya hayawezi kuondoka kwa kubadilisha ushirika wetu iwe kwa kuvunja muungano ama kujadili idadi ya serikali zetu, ititiri wa vyama vya siasa na mahitaji yao bali yanahitaji mabadiliko makubwa ya katiba yetu ili Mamlaka hayo yote yapelekwe katika sehemu zinazohusika ili kurahisisha utekelezaji wa shughuli zote za serikali, taasisi na na vyombo vya kijamii ambavyo ndivyo pekee leo hii vinavyotakiwa kuwajibika ktk kushiriki katika kutoa huduma, haki na usawa wa jamii hii. Hatuwezi kuendelea na mfumo ule ule tukitegema kubadilika kwa serikali ndio muarobaini wa mapungufu makubwa ya kikatiba uwajibikaji na mamlaka ya vyombo vya utekelezaji.

Ni Imani yangu kwamba Watanzania wengi wameitaka katiba mpya ambayo italenga kuondoa mapungufu ya katiba yetu ya mwaka 1977. Wananchi wanaitaka katiba ambayo inayojitosheleza ktk maswala yote UTAWALA, KISIASA, KIJAMII na KIUCHUMI kulingana na mazingira ya dunia tuishiyo, hivyo basi

Napendekeza MUUNGANO na sio SHIRIKISHO uendelee kuwepo isipokuwa ktk sehemu ya kwanza ibara ya 4 (3) ya katiba ya JMT ya mwaka 1977 pamoja na rasimu ya katiba ya tume ya Warioba ziyaweke MAMBO YOTE YAWE YA MUUNGANO isipokuwa Ushuru wa bidhaa na mapato yasokuwa ya kodi kama liseni na sheria. kwa kufanya hivo Serikali zetu, Manispaa, Mashirika ya Umma, na vyombo vya serikali kama TISS, NEC, na kadhalika yote yapewe mamlaka kamili ya kupanga Utekelezaji wa shughuli zao kama itakavyo ainishwa pasipo kuvunja masharti ya katiba na hivyo kuwajibika moja kwa moja na sheria mama ilotungwa kwa manufaa ya wananchi ili kukuza amani na utulivu.

Mambo yote yakiwa ya Muungano yataweza vipi kuondoa mapungufu na kufuta kero za wananchi? Hili nitalizungumzia baada ya kujibu hoja za wanabodi ambao watakuwa na haja ya kulizungumzia hili.

  • Nawakilisha
 
Inaendelea.

Wanabodi, hatua ilotakiwa kufuata katika sehemu hii ya pili, ilikuwa kuelezea mambo yote yawe ni ya muungano itakuwa na malengo gani muhimu na msingi ktk mwelekeo wa utekelezaji mzuri wa shughuli za serikali. Lakini kutokana na kutoelewa kwa nini nimependekeza hivyo, kwa sababu hizi itanibidi nirudi nyuma kidogo kuzungumzia kwanza sababu za mfarakano huu uliopo na ulodumu kwa miaka 30 pasipo kupatiwa ufumbuzi, halafu ndipo nitarudi kuelezea zaidi Mambo yote yakiwa ya Muungano yatawezaje kuondosha mapungufu ya katiba iliyopo na pia kufuta kero za wananchi wa pande zote mbili.

Awali ya yote, nawaomba wasomaji wenzangu tujikumbushe na turudi nyuma kujiuliza ni mapungufu gani yalosababisha wananchi kudai katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Nadhani hili ndilo swala la msingi pamoja na kwamba yapo mengi sana isipokuwa tutazame kiini cha kuitaka katiba mpya maana kama pasingekuwa na Mapungufu basi hapakuwa na sababu wala haja ya kuandika katiba Mpya bali tungeomba katiba iliyopo ifanyiwe marekebisho ama kuandika au kufuta baadhi ya vipengele vya sheria.

Na kama wananchi wa pande zote mbili walikuwa hawautaki Muungano basi pia wasingeomba katiba mpya bali wangeomba taratibu za upigaji kura ili kuvunja muungano huu. Hizi ndizo taratibu zinazokubalika kisheria na sii vinginevyo. Hivyo ni basi tujiulize ni malalamiko gani haswa yaliyosababisha wananchi kutoridhika na katiba ya mwaka 1977.

Wananchi wa Tanzania visiwani (Zanzibar)

Wananchi wa Zanzibar wamedai kwa muda mrefu sana juu ya Muungano huu kutokana na Tanzania bara kutumia mamlaka ya serikali ya Muungano kujinufaisha haswa katika mambo yote ya muungano na yasokuwa na Muungano wakati fursa kama hiyo Zanzibar hawana. Hili ni swala ambalo halikuanza jana bali toka wakati wa hayati marehemu Sheikh Abeid Karume aliwahi kuulizwa na akasema hivi "Muungano ni sawa na koti, unalivaa unapolihitaji na unalivua likikubana" haya ni maneno mazito sana na yanavuta uradi mkubwa (Meditation) na ukiyatafakari kwa kina utayaona ambayo hayakuonekana wakati ule. Hivyo kuna watu walitia shaka muungano huu na kutaka kujua kama unaweza kuvunjwa ikiwa hatutafikia maridhiano.

Haya leo hii yasemekana Tanzania bara tumelivaa koti la Muungano na limetupendeza hivyo kulivua imekuwa kazi kubwa kwa sababu ya fursa tulizopata kutokana na mamlaka tulonayo. Na ukweli ni kwamba nani atakayekubali kulivua koti linalompa fursa kubwa japo linambana? Waasisi wetu hawakuyaona haya na hivyo mapungufu yalojitokeza ni FURSA SAWA kwa nchi washirika. Na hili limetokana na ukweli kwamba toka nchi yetu itoke ktk mfumo wa Ujamaa kuingia Utandawazi na soko huria, hii katiba iliyopo haija ainisha wazi ikaeleweka mipaka na mamlaka ya Serikali ya Muungano katika mambo ya Muungano, na ile yale ya Tanzania Bara yaani mambo yasiyokuwa ya Muungano. Swala hili ni miongoni mwa malalamiko ya Wazanzibar na ndio sababu kubwa inayotumiwa na bara kujipatia fursa zitokanazo na kutoeleweka huko.

Wazanzibar wanadai pia kuwepo kwa uchakachuaji kuhusiana na uchangiaji wa gharama za uendeshaji shughuli za mambo ya Muunganobaina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ikifuatiwa na ugawanaji wa mapato. Hapa inaonekana tunakwenda kiholela tu hakuna mfumo kamili unaoeleweka na wazi kwa kila mshirika kufahamu kinachoendelea.
Wananchi wa Zanzibar wameendelea kuweka madai mengine ya kwamba Rais wao aliondolewa katika nafasi ya utawala kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Pia swala la ongezeko la mambo ya Muungano iliyoongezwa kutoka mambo 11 mwaka 1964 mpaka kufikia 22 mwaka 1992 haya yote yamepunguza uhuru wa Zanzibar kwa mambo yake yasiyokuwa ya muungano.

Wananchi wa Tanzania Bara (Tanganyika)
Wananchi wa Tanzania Bara, wao wanasema kuwepo kwa Muungano wa Serikali mbili ndio umepoteza utambulisho wa kihistoria wa Tanganyika (Identity) na fursa ya watu wa upande wa Tanzania Bara kutetea maslahi yao ndani ya Muungano kiasi kwamba wakitazama upande wa pili, Zanzibar sasa imekuwa nchi huru, ina serikali yake, ina bunge lake ina mahakama zake ina bendera yake, wimbo wake wa taifa ili mradi wao hawakumezwa na muundo huu basi matokeo yake ilomezwa ni Tanganyika.

Watanzania bara wanadai tena ya kwamba Zanzibar imebadilisha Katiba yake mwaka 2010 pasipo ridhaa ya serikali ya Muungano na kujitambulisha kama nchi na kuchukua madaraka kinyume cha katiba ya JMT. Aidha Sheria zinazotungwa na Bunge la Muungano lazima zipelekwe kama muswada kwenye Baraza lao la Wawakilishi kuidhinishwa ili zipate kutumika Zanzibar.

Kuna swala la Ardhi ambalo wananchi wa Tanzania Bara wanalalamika kutokuwa na haki ya kumiliki ardhi Zanzibar wakati wenzao wanayo haki hiyo huku Bara. Vile vile kuna sitoelewa kuhusu jinsi ya uchangiaji gharama za uendeshaji wa shughuli za mambo ya Muungano pamoja na ugawajiwa mapato ndani ya muundo wa serikali mbili.

Haya ndiyo maswala muhimu sana yalochangia kuleta mgogoro mkubwa baina ya wananchi wa Tanzania bara na visiwani kiasi kwamba uandikaji wa katiba mpya umekwama kutokana na kutoelewana juu ya muundo gani wa ushirika unaweza kuyaondoa mapungufu hayo, ndipo maoni yakaanza kukusanywa kupitia tume ya Warioba ambao wameleta rasimu yenye mapendekezo ya kubadilisha muundo wa serikali mbili kwanza ili kuzipa utambulisho nchi zote mbili washirika na kisha kugawana tena mambo ya Muungano ili serikali ya JMT isiwe na mamlaka nayo.

Navyoamini mimi ni kwamba bado tunazunguka mbuyu kutafuta muundo wa serikali kwa sababu Tanzania inaweza kuwa muundo wowote ule ili mradi tu kunakuwa na Mamlaka ya kutosha, uwazi na katika masuala ya Muungano ili kuiweka nchi pamoja na kuwa na Taifa imara mbele ya mataifa. Na n muundo gani wa Utawala unaotufaa sisi leo hii ni uamuzi wetu wenyewe. Hata hivyo uamuzi huo ni lazima ujibu maswali ya wananchi katika malalamiko yao ili vigezo vitakavyo tumika vimelenga kuondosha mapungufu yaloainishwa

Je, Muundo ulopendekezwa kweli utajibu hofu ya baadhi ya watu Muungano kuvunjika? maana swala la serikali tatu limetazama mahitaji ya kwanza ya watanzania bara na hapo ndipo tulipokwama wakati hoja na malalamiko ni mengi. Mimi naamini pia ya kwamba idadi ya Serikali haina uhusiano wowote na kiini cha malalamiko ya wananchi kwa sababu ukisoma kwa makini malalamiko hayo mengi yamehusiana na MAMBO YA MUUNGANO. Na ndipo nilipokuja na mapendekezo haya nikiacha yale ambayo yanaweza kupatiwa ufumbuzi kwa kuzingatia kwamba sasa hivi hatupo tena katika Ujamaa ambao rais wa jamhuri alikuwa na mamlaka yote juu ya utekelezaji wa shughuli za serikali chini ya itikadi moja.

Ikumbukwe ilivunja hata Jumuiya ya EAC baada ya mkutano wa Uganda ambao nchi husika zilikubaliana zote kuhusu kugawa fursa sawa lakini Kenya walokuwa wamevaa koti la Jumuiya walikataa na ikafikia kikomo cha EAC. Tusirudie makosa hayo tena katika Muungano huu wala huo wa Jumuiya ya EAC ambao hadi sasa haujafikia hatua tulokuwa kabla ya kuvunjika kwake. Ningetegemea sana sisi Watanzania kujifunza kutokana na makosa yalofanywa wakati ule japo washirika wa Jumuiya hizo walikuwa na serikali zao zenye mamlaka kamili lakini utengano ukatokea ktk mapungufu ya uchangiaji na ugawanaji wa MAMBO YA JUMUIYA.

Mambo yote yakiwa ya Muungano yataweza vipi kuondoa mapungufu na kufuta kero za wananchi? Hili nitalizungumzia baada ya kujibu hoja za wanabodi ambao watakuwa na haja ya kulizungumzia hili.
 
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom