Karume: Washindi kura ya maoni ni wananchi wote

X-PASTER

JF-Expert Member
Feb 12, 2007
11,610
1,810
Karume: Washindi kura ya maoni ni wananchi wote

Salma Said, Zanzibar


VIONGOZI wa CUF na wanachama wao walipiga kelele kushangilia matokeo ya kura za maoni juu ya serikali ya umoja wa kitaifa wakati yakitangazwa juzi, lakini Rais Amani Abeid Karume amesema hakuna mshindi kati ya waliopiga kura ya kukataa au kukubali.


Katika kura hizo za maoni zilizopigwa Julai 31, waliopiga kura za ndio walishinda kwa asilimia 66.4, matokeo ambayo yanavifanya visiwa hivyo visiepuka kuunda serikali ya mseto mara baada ya uchaguzi wa Oktoba 31.

“Washindi ni wananchi wote wa Zanzibar,” alisema Rais Karume katika salamu zake za kuwapongeza wananchi baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo wakati alipoongea na waandishi jana Ikulu.

“Bado tuna wajibu wa kuthibitisha kuwa mshindi wa zoezi hili ni Zanzibar na Wazanzibari wote, kwa kuhakikisha kwamba sote kwa pamoja tunaendesha uchaguzi mkuu ujao katika hali ya amani, salama na utulivu.”


Rais Karume alisema Wazanzibari watathibitisha hilo wakati watakapopiga kura za kuchagua viongozi wao kwenye uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 31, akisema kuwa ni wajibu wa kila mmoja kudumisha utulivu na ushirikiano uliopo hivi sasa.


“Kwa vile nchi yetu ni ya kidemokrasia na inafuata misingi hiyo, na kwa kuwa uamuzi wa wengi umeshafanywa na kauli ya wachache imesikika, sasa ni wajibu wetu sote kushirikiana kuendeleza gurudumu la maendeleo ya demokrasia chini ya mfumo mpya nchini mwetu,” alisema Rais Karume ambaye ni mtoto wa muasisi wa taifa la Zanzibar, Abeid Amani Karume.


“Katika hili (matokeo ya kura ya maoni), hakuna mtu aliyeshinda wala aliyeshindwa ila mshindi ni Zanzibar yenye amani, umoja na mshikamano. Washindi ni wananchi wenyewe kutaka kukuza umoja, demokrasia, utawala bora, amani na maendeleo kwa pamoja. Huo ndio msingi hasa wa Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964,” alisema rais Karume.


Alisema baada ya kura hiyo ya maoni, wajibu uliobaki ni kwa Baraza la Wawakilishi ambalo linatarajiwa kukutana hivi karibuni kufanya marekebisho ya msingi katika katiba ya Zanzibar ya 1984.


“Sisi Zanzibar tutakuwa ni nchi ya kutolea mfano kwa chaguzi zitakazokuwa za amani na utulivu ikitiliwa maanani namna ya zoezi la upigaji kura ya maoni ilivyokwenda. Ni matarajio yetu sote kuwa waheshimiwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa umoja wao wataheshimu uamuzi wa wananchi wa Zanzibar na kufanya wajibu wao kwa faida ya kila mmoja wetu,” alisema.


Rais Karume alisema zoezi hilo la kupiga kura ya maoni ili kufanya uamuzi wa mabadiliko makubwa ya mfumo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuliachia Baraza la Wawakilishi kupitisha muswada wa mabadiliko ya katiba, litaingia katika historia ya maendeleo ya demorasia visiwani hapa na Afrika nzima kwa jumla.


Alisema mara nyingi nchi za Afrika zinakumbana na majanga na mizozo kwenye harakati za uchaguzi na kwamba hali hiyo haipaswi kupuuzwa.

Kwa msingi huo, alisema wananchi wa Zanzibar wameamua kubadilisha sura hiyo kwa kuweka mfano mzuri wa kuigwa na nchi nyingine ili demokrasi iendelezwe kwa kuendesha chaguzi kwa amani na kuwashirikisha wananchi wote katika utawala wa nchi yao.

“Baada ya hapo tutaingia, Inshaallah, katika kipindi kipya cha kuleta maendeleo makubwa katika nchi yetu katika hali ya umoja na mshikamano. Matokeo yatakuwa ya manufaa kwa wananchi wote na tutakuwa tumejenga Zanzibar mpya yenye umoja na mshikamano tukiwa sote ni Wazanzibari,” alisema Rais Karume katika hutuba yake ambayo ilisheheni shukurani kwa wananchi na wafadhili wa ndani na nje.


Pia aliwashukuru na kuwapongeza wananchi wote wa visiwa vya Unguja na Pemba walioshiriki kupiga kura ya maoni na kutumia haki yao ya kidemokrasia kutoa maamuzi au mapendekezo yao juu ya mfumo wa serikali.


Rais Karume alisema bila ya kujali walipiga kura ya ndio au hapana, wananchi wote walioshiriki wamethibitisha kupevuka kwa demokrasia na utawala bora nchini na kwamba zoezi hilo ni la kihistoria ambalo limewapa wananchi wa Zanzibar haki ya kushiriki moja kwa moja katika maamuzi mazito yanayowahusu.


Chanzo:gazeti la mwananchi
 
Back
Top Bottom