Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 20,788
- 30,086
KABURI LA BI. TITI MOHAMED, KISUTU
Siku tatu hizi zimekuwa ngumu sana kwangu na naamini na kwa wenzangu wengi tuliokulia Dar es Salaam kwa kuondokewa na wapenzi wetu.
Juzi nikiwa nimesimama pembeni mwa kaburi tukimzika mmoja wa wapendwa wetu jicho langu lilivutiwa na kaburi lililokuwa pembeni kwa jinsi majani ya kijani yalivyokuwa yameota kama vile kuna mtu ananyeshea majani yale maji kila siku na kupalilia.
Kaburi hili ni kaburi la Bi. Titi Mohamed mmoja wa wapigania uhuru wa Tanganyika.
Bi. Titi alipata kuniambia nyumbani kwake nilipokwenda kutaka kufanya mahojianonae ya historia ya maisha yake wakati nafanya utafiti wa kitabu cha Abdul Sykes.
Alinambia, ''Bwana Mohamed una lipi wewe la kuandika kuhusu mimi ambalo bado halijaandikwa?''
Hakika sikuwa na jipya ambalo halikuwa limeandikwa kuhusu Bi. Titi lakini pia nilikuwa na mengine ambayo yeye hakuyasema kuhusu maisha yake na wengi hawayajui lakini wale waliokuwapo wakati wa kupigania uhuru walinieleza.
Abbas Sykes na Tewa Said Tewa walipata kunieleza mengi kuhusu Bi. Titi na uwezo wake katika kuhamasisha umma wakati wa kupambana na Waingereza.
Nitalieleza moja.
Abbas Sykes anasema, ''Tuko chini ya jukwaa tunasubiri kuanza mkutano Mnazi Mmoja.
Nyerere anataka kupanda jukwaani lakini anatuambia kuwa nachoka na hana jipya la kusema.
Nyerere hakika amechoka basi atamwendea Bi. Titi, ''Titi hebu anza wewe kuzungumza,'' Mwalimu atamwambia Bi. Titi.''
Bi. Titi atapanda jukwaani akisindikizwa na nyimbo mashuhuri ya TANU iliyokuwa ikiimbwa na Bi. Hawa Maftah na kundi lake la akina mama:''Muheshimiwa nakupenda sana wallah sina mwinginewe, In Shaa Allah Mungu yuko Tanganyika tutajitawala.''
Bi. Titi atakapoanza kuzungumza uwanja utalipuka kwa vimondo ambavyo Bi. Titi anavirusha.
Bi. Titi anawauliza Waingereza, '' Hivi nyie hamna kwenu? Kwa nini mnatung'ng'ania hivi ondokeni nendeni kwenu. Nyie watu gani msiojua kukataliwa?''
Vifijo vinazizima uwanja mzima.
Mwalimu Abbas Sykes akanambia kuwa kutokana na hotuba ile ya Bi. Titi Nyerere atakuwa kapata ''cue'' na atakapopanda jukwaani Nyerere atapita mle mle alimopita Bi. Titi lakini kwa namna nyingine ya kuhutubia.
Allah mrehemu mama yetu na lifanye kaburi lake kuwa moja ya mabustani ya peponi.
Sent using Jamii Forums mobile app