Juu ya udogo wake Zanzibar yaweza kustakimu na ikajikimu…

Calipso

JF-Expert Member
Mar 25, 2009
284
15
[h=1]Juu ya udogo wake Zanzibar yaweza kustakimu na ikajikimu…[/h]KWAME Nkrumah, baba wa uzalendo wa Kiafrika, alikuwa akipenda kusema kwamba Waafrika kwanza waunyakue uhuru wa kisiasa na mingine, kama vile uhuru wa kiuchumi, yatakuja baadaye. Zanzibar ya leo iko katika njia panda — ima ifuate njia itayoifikisha katika maendeleo na ustawi au ifuate njia itayozidi kuirejesha nyuma.

Lililo wazi ni kwamba haitoweza kujiendeleza bila ya kuwa huru.
Zanzibar haina cha kuhofia endapo itakuwa huru. Ukweli ni kwamba hivi sasa ikiwa ndani ya mfumo wa Muungano inajikimu yenyewe bila ya msaada wa Muungano. Imekuwa ikijiendesha kutokana na madukhuli yake ya karafuu na ya utalii.

Itapokuwa huru Zanzibar itapata ile fursa ya dhahabu — fursa nzuri ya kuweza kujiendeleza. Na itapokuwa inapata mapato kutokana na mafuta itakuwa na uwezo zaidi wa kujiendesha na kupata ufanisi.
Wala si mafuta peke yake yatayoiinua nchi hiyo. Itakuwa pia na uwezo wa kutumia vyema rasilimali zake nyingine na uwekezaji kutoka nje pamoja na mchango wa Wazanzibari wenyewe, walio Visiwani na ughaibuni.

Mustakbali wake utazidi kufana ikiwa itatimiza nia yake ya kuwa na mfumo wa uchumi na biashara ulio huru, usiotoza ushuru bidhaa zinazoingia nchini na ikiwa na serikali ya kidemokrasia yenye kuheshimu haki za kimsingi za kibinadamu, usawa na utawala unaofuata sheria.

Katika historia yake ya kiuchumi ya miaka 2000 iliyopita, siku zote Zanzibar imekuwa ikiweza kujikifu, ikiweza kuwa na utoshelevu. Hadi miongo ya hivi karibuni Visiwa hivyo havikuwa na ufukara. Kuna dhana isiyo na msingi kwamba Zanzibar haiwezi kusimama na kujiendesha yenyewe bila ya kufadhiliwa na Bara. Wenye kuivurumisha dhana hiyo mpaka sasa wameshindwa kueleza ni kwa njia gani hasa Zanzibar inafadhiliwa na Bara.

Mmoja kati ya wenye kutoa hoja hiyo ni Mheshimiwa Samuel Sitta, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, ambaye mapema mwezi uliopita aliliambia Bunge mjini Dodoma kwamba Serikali ya Muungano ndiyo inayoigharamia Zanzibar na kwamba nchi hiyo iliyoungana na Tanganyika haitoweza kujiendesha bila ya Muungano.
Hiyo ni hoja ya kuwatia hofu Wazanzibari wenye kutaka nafasi ya Zanzibar katika Muungano izingatiwe upya.

Tunapoujadili Muungano tunawajibika kuujadili kijituuzima. Tena inapasa tuwe na busara ili tuepushe hasara. Si jambo la busara, hasa kwa viongozi wa ngazi za juu, kutoa propaganda zisizo na msingi zenye lengo la kutia hofu ilimradi hali ya mambo iselelee kuwa kama ilivyo.
Wazanzibari wanawaona wenye kutoa propaganda hiyo kuwa ni watu wenye ajenda ya siri ya kutaka daima kuikalia kichwani nchi yao. Wanahisi kwamba wanaitia hofu Zanzibar ili isiweze kuzipigania haki zake za kihalali za kurejeshewa uhuru wake.

Tukiiangalia historia ya Zanzibar ya kama karne moja iliyopita, tutaona kwamba wakati wa utawala wa ukoloni wa Waingereza, Visiwa hivyo vikijiendesha vyenyewe na katu havikuwa vikihitaji kufadhiliwa na serikali ya kikoloni. Hali hiyo imeendelea hata baada ya kuundwa Muungano.
Wenzetu wa Bara wenye kudai kwamba Zanzibar ni mzigo kwao ama hawaujui ukweli ulivyo au wanaupuuza kwa makusudi. Pia hawatambui kwamba Zanzibar ina uwezo wa kutumia rasilimali zake ili iweze kuwa na maendeleo ya haraka.
Hivi kweli lau pasingalikuwako Muungano Zanzibar ingeanguka kiuchumi, kisiasa na kijamii? Inaingilia akilini kwamba bila ya Muungano Zanzibar isingeliweza kuwa nchi, tena yenye maendeleo?

Nimesema mwanzo kwamba Zanzibar iko kwenye njia panda kwa sababu ina njia mbili za kufuata. Ima iendelee kuwa ndani ya mfumo wa Muungano na Tanganyika na izidi kurudi nyuma kimaendeleo au ijitoe ili iweze kuendesha shughuli zake zote za utawala na za kiuchumi bila ya kuingiliwa na hivyo kupata ufanisi.

Kipindi cha karibu nusu karne cha kuwa ndani ya Muungano hakikuiwezesha Zanzibar kupata maendeleo. Sababu kubwa ya kuzuka hali hiyo ni kuwa nchi hiyo ilipokonywa nguvu zake za kiuchumi kwa kisingizio kwamba nguvu hizo sasa ni miongoni mwa yale yanayoitwa ‘mambo ya Muungano’. Na hadi hivi karibuni tu nchi hiyo haikuwa ikiruhusiwa kutafuta misaada ya kigeni au uwekezaji kutoka nje.

Ushahidi uko wazi kwamba kila sekta ya uchumi wake imeanguka katika kipindi cha miaka 47 tangu uundwe Muungano. Matokeo yake ni kwamba nchi hiyo ambayo zamani ikisifika kwa maendeleo, ikipitwa na Afrika ya Kusini tu, hivi sasa imegeuka na kuwa moja ya visiwa vilivyo nyuma kabisa duniani.
Wengi wetu tunakumbuka, kwa mfano, siku ambapo Zanzibar ilikuwa na mfumo bora wa elimu, mifumo bora ya afya na huduma za kijamii na mfumo bora wa miundombinu kwa wakati ule. Ubora wa mifumo hiyo ulitoweka baada ya Muungano.
Hebu tuilinganishe Zanzibar na Mauritius. Nchi zote hizo mbili ni mkusanyiko wa visiwa na vina ukubwa usiopitana sana. Wakati wa uhuru Zanzibar ilikuwa na uchumi ulioendelea kuushinda ule wa Mauritius.

Leo hii hali imegeuka. Mauritius iliyosalia kuwa huru imeipita pakubwa Zanzibar iliyopoteza mwingi wa uhuru wake.
Mafaniko ya Mauritius pia yanaivunja nguvu ile hoja ya kwamba kwa vile Zanzibar ni nchi ndogo haitoweza kujimudu kiuchumi. Tukiiacha Mauritius kuna nchi kadhaa nyingine ambazo pia ni visiwa na vinavyojiendesha vyenyewe kwa mafanikio makubwa.
Inazidi kuuma kuona kwamba serikali ya Muungano, kama nilivyowahi kuandika kabla, haikuanzisha hata mradi mmoja wa maana Visiwani Zanzibar uwe wa kiuchumi au wa kijamii. Na wakubwa wa Serikali ya Muungano wanashindwa kutambua kwamba wana dhamana sawa kwa Watanzania wa Bara na Wazanzibari.
Kwa hivyo kudai kwamba Zanzibar imeendelea ikiwa ndani ya Muungano au kwamba mahusiano yake na Tanganyika katika mfumo wa sasa yamewanufaisha Wazanzibari ni uzushi mtupu.

Tukiangalia misaada ya kigeni tu iliyopata Tanzania tunaona kwamba Zanzibar haikupewa fungu lake inalostahiki hata katika mambo yasiyo ya Muungano kama vile yale ya sekta za kilimo na afya. Serikali ya Muungano imekuwa ikipokea misaada ya kigeni kutoka kwa wafadhili kwa niaba ya Zanzibar na Tanganyika, lakini Zanzibar imekuwa ikipunjwa.
Hakuna nchi barani Afrika iliyopata misaada mingi ya kigeni kuliko Tanzania. Lau Serikali ya Muungano ingelitoa kijisehemu kidogo tu cha misaada hiyo kwa maendeleo ya Zanzibar basi hali ya mambo ingekuwa tofauti kabisa hii leo. Uchumi wa Zanzibar ungezinduka, skuli zingekuwa na madeski na hospitali zingekuwa na madawa.

Aidha wenye kuyakuza mahusiano ya kiuchumi ya Zanzibar na Tanzania Bara wanatia sana chumvi na kukoroga mambo kwani ukweli ni kwamba Zanzibar inategemea sana juu ya kuagiza na kusafirisha bidhaa zake nje ya Tanzania Bara kuliko inavyoitegemea Bara.
Hivyo ni wazi kwamba Zanzibar inaweza kuwa na sera yake yenyewe ya kiuchumi iliyo huru bila ya kuhofia kwamba kukosekana soko la Bara kutakuwa na athari mbaya kwa uchumi wake.

Nikisema haya sikusidii kwamba Zanzibar haitaki kuwa na mahusiano ya kiuchumi na jirani zake. Ninachosema ni kwamba uchumi wa Zanzibar umeathiriwa vibaya na Mambo ya Muungano kama vile masuala ya sarafu, biashara, utozaji wa kodi na ushuru, sera na kanuni za hazina ya serikali, utoaji wa leseni za viwanda na nyinginezo, uhamiaji, biashara ya nje na uwezo wa serikali yake wa kukopa.
Zanzibar ina rasilimali ya kutosha na siku hizi ina jina zuri kwa wafadhili na wawekezaji wa kimataifa wanaotiwa moyo na Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Na hata ikiwa haitopata mafuta katika muda wa miaka kadhaa ijayo bado Zanzibar itakuwa na uwezo wa kujiendesha.

Lau serikali ya Muungano ingekuwa na sera za maana kuhusu Zanzibar, mifumo ya uchumi, afya na ya kijamii Visiwani ingekuwa ya hali ya juu.
Ndiyo maana baadhi ya Wazanzibari wanaamini kwamba taathira za Muungano kwa hali zao za kiuchumi na za kijamii hazikuwa njema hata chembe. Hii ndiyo sababu kuu inayowafanya wengi wao wauchukie Muungano.

Wakuu wa serikali ya Muungano wanapenda sana kutaja ile asilimia 4.5 ya faida ya Benki Kuu ya Tanzania ambayo hupewa Zanzibar. Wanasema kwamba Zanzibar inafadhiliwa kwa kima hicho.
Wanachosahau ni kwamba Zanzibar ni mshirika katika kuundwa kwa Benki Kuu ya Tanzania na kwamba iliwekeza asilimia 11 katika hisa za benki hiyo. Benki Kuu ya Tanzania ikila hasara Zanzibar huondokea patupu. Ikipata faida ndipo Zanzibar inapogaiwa hiyo asilimia 4.5 lakini hiyo asilimia 4.5 ni kasoro ya fungu lake la faida inalostahiki kupata. Na wala kima hicho hakitoshelezi kukidhia haja zote za kuipatia maedeleo.
Kwa hiyo tunaona kwamba hata katika hili ambalo ni la wazi watawala wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hawatendi mambo kiungwana kwani wanainyima Zanzibar fungu lake la haki.

Wazanzibari hawawachukii Watanganyika na wala wengi wao hawalipingi wazo la kuwa na umoja au muungano wa nchi za Kiafrika. Wanachochukia ni uonevu wa kupokonywa haki na uwezo wa kujiamulia mambo yao
 
Back
Top Bottom