JK: Kwenye vijiwe tusemane lakini maendeleo tushiriki

Mtu wa Pwani

JF-Expert Member
Dec 26, 2006
4,184
671
JK: Kwenye vijiwe tusemane lakini maendeleo tushiriki

*Asema katika maendeleo hakuna itikadi

Na Maura Mwingira, Mafia

RAIS Jakaya Kikwete amewasihi wanasiasa wenzake kuhimiza wanachama wao kushiriki katika shughuli za maendeleo kwa faida ya Watanzania wote.

Amesema katika jambo lolote linalohusu maendeleo, wananchi washirikiane bila kujali wako chama gani cha siasa, kwa sababu maendeleo hayana itikadi.

“Ikijengwa zahanati haitamhudumia mwana CCM tu ni ya kila mtu, vilevile kwa upande wa shule, barabara, miradi ya maji na mengine mengi...wanasiasa wenzangu tuendelee kusemana kwenye vijiwe vyetu, wewe hufai, mimi nafaa, wewe uko vile huyu yuko vile, lakini tutakapofika kwenye maendeleo yetu, haya ni maendeleo kwa manufaa yetu sote,” alisema.

Alikuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika wilaya ya Mafia akiwa katika ziara ya kukagua na kuhimiza shughuli za maendeleo mkoani Pwani.

“Tumeunda vyama vya siasa kwa sababu tunataka kuwaletea watu maendeleo, tunataka watu wapate barabara, wapate maji safi na salama, wapate huduma za afya kwa karibu na wapate elimu. Sasa pale tunapoendelea kushughulikia haya naomba sana sote tuungane kuyafanikisha,” alisihi.

Alieleza kuwa anayevutia upande mwingine hana maslahi ya maendeleo ya watu, bali anatawaliwa na ubinafsi wake. “Tuondoe ubinafsi wetu ndugu zangu tujenge maendeleo yetu,” alisema.

Aliongeza kuwa tofauti za kisiasa miongoni mwa Watanzania kunawapa fursa ya kuchagua sera bora zaidi, akiona CCM inamfaa zaidi basi atakwenda huko na akiona CUF inamfaa zaidi atakwenda huko.

“Lakini tusiichukulie fursa hiyo kuwa chanzo cha mifarakano katika jamii, ninachohimiza ni kujenga umoja na mshikamano wa kimataifa na kuwaletea wananchi maendeleo," alisema.

Alisisitiza kuwa chama chochote cha siasa kinachopinga wanachama wao kushirikiana na wenzao kujiletea maendeleo yao, basi ni bora chama hicho kisiwepo kabisa.

Katika mikutano yake mbalimbali aliyoifanya hapa, Rais Kikwete mara kwa mara aliwasisitiza wananchi kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kushirikiana katika kujiletea maendeleo.

Alitahadharisha kuwa kuendekeza malumbano ya kisiasa, na kukatazana kuchangia miradi mbalimbali ya maendeleo si tu kunawachelewesha wao wenyewe katika kujiletea maendeleo yao kwa kasi, lakini wataachwa nyuma na Watanzania wenzao katika maeneo mengine ya nchi.

Rais aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule ya sekondari ya kata ya Belen na kutoa sh. milioni moja kuchangia nguvu za wananchi katika ujenzi wa shule hiyo inayotarajiwa kuchukua wanafunzi wa kidato cha kwanza mwakani. Hadi kukamilika kwake itagharimu sh. milioni 200.

Rais pia aligawa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya sh. milioni 51 ambavyo vilitolewa na Serikali ya Japani kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii wa Japani(JSDF).
Vikundi sita kati ya hivyo ni vya wanawake wafanyabiashara ya kukaanga samaki, migahawa na vya uvuvi, kilimo cha miwa na ukaushaji/uhifadhi wa samaki.

Vifaa vilivyotolewa kwa vikundi hivyo ni injini saba za kupachika, nyavu 14 za kuvulia, masanduku 102 ya kuhifadhia samaki, friji kubwa mbili na ndogo moja, vikaango vikubwa vitatu vya samaki, meza nne za kuchakatia samaki, viti 14, makasha 152 na oven moja ya mkaa.

Baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Rais Kikwete aliwataka wajasiriamali hao kuvitumia vizuri ili viwasaidie katika kuboresha maisha yao, lakini pia utunzaji huu uwawezeshe kupata vifaa vingine kutoka kwa wahisani mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Rais Kikwete aliwataka wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri, kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo imelenga katika kuwainua kimaisha na kuwaongezea kipato.

Rais alisema haipendezi na wala haifurahishi Mkuu wa Mkoa au wa Wilaya na hata Mkurugenzi anaposhindwa kujua nini kinachofanyika katika eneo lake kuwasaidia wananchi wake ili wajipatie maisha bora.

“Hivi kwa nini mnababaika pale ninapowauliza niambieni ni miradi gani munayoitekeleza ya kuwaondolea umaskini wananchi iwe mmoja mmoja au katika vikundi mnababaika, yaani mnasoma tu kilichoandikwa kwenye taarifa zenu, lakini nikihoji tu, mnachanganyikiwa, acheni kutoa taarifa za kwenye makaratasi, miradi inayohusu wananchi lazima muifahamu kwa kichwa,” alisema Rais.

Alisisitiza kuwa maisha bora kwa kila Mtanzania hayawezi kuja kwa kuwapatia fedha, bali ni kwa kuwaibulia miradi na kuwawezesha waiendeshe kwa ufanisi, wajipatie kipato chao na hapo ndipo maisha bora yanapoanzia, sasa ninyi kazi yenu nini?” alihoji Rais.

Kauli hiyo ya Rais ilifuatia baada ya Mkuu wa Wilaya ya Mafia kushindwa kubainisha kwa uwazi ni miradi gani ambayo wameiandaa kwa ajili ya wananchi wake, hata alipoulizwa, Mkurugenzi wa Halmashauri naye alibabaika, mpaka pale Mbunge wa Mafia, Bw. Abdulkarim Shah alipofafanua.

source majira
 
Back
Top Bottom