Jirani yangu wa kule Goba hakuwa mtu wa kawaida

Jirani yangu wa kule Goba hakuwa mtu wa kawaida - 04

Kikao kilikwisha kwa pande zote mbili kuelewana, mwenye nyumba alisema baada ya siku tatu mafundi watakuja kwaajili ya kuanza ujenzi lakini pia hapohapo kabla kikao hakijaisha akasisitizia kuhusu kodi yake, hili nililijua tu litakuja, alisema na yeye atapata nguvu zaidi ya kuboresha miundombinu endapo sisi tutatoa pesa zake kwa wakati, baada ya kikao kuisha aliaga na kwenda zake na kila mtu akaendelea na shughuli zake, angalau sasa na mimi nikapumzika na macho ya yule shemeji, macho ambayo sikuelewa yanamaanisha nini zaidi ya kunitisha.

Zikapita siku mbili, mafundi hawakuja kama tulivyoambiwa, ikapita siku ya tatu na ya nne, hola, mpaka wiki nzima iliyoyoma si fundi wala mhandisi aliyekuja, mwenye nyumba anatupiga tu kalenda.

Siku moja nikiwa niko nyumbani, sikumbuki haswa zilipita siku ngapi tangu tufanye kile kikao, katika majira ya saa saba usiku nikasikia mtu anafungua mlango wake, sikujua ni nani maana mimi nilikuwa ndani sebuleni lakini ni bayana alikuwa ni jirani mmojawapo katika milango ile miwili, kidogo mlango wa grill ulifunguliwa kakaaa-kakaaaa kisha kukawa kimya, nami nikawa kimya nikiwaza huenda mtu anaenda maliwatoni hivyo nikaendelea na mambo yangu ya kutazama runinga.

Nilikaa kama nusu saa lakini sikusikia mlango ule wa grill ukifungwa, na kwa namna yoyote ile mlango ule usingeweza kufungwa bila kutoa sauti, hapo nikapata shaka. Nilitoka sebuleni nikaenda chumbani ili nipate kuchungulia nje kuna nini kinaendelea, nilipofungua pazia la dirisha kwanza nikatazama pikipiki yangu, nikaona kuna usalama, nikaangaza huku na kule lakini sikumwona mtu, nje kulikuwa kimya sana.

Nilitulia kusikiliza labda kuna mtu bafuni, napo sikusikia kitu, kila pembe ilikuwa kimya sana. Hapo nikapata wasiwasi. Niliufungua mlango nikaenda nje kutazama maana ule mlango wa grill kuwa wazi kwa muda wote huo haikuwa salama kabisa ukizingatia tulinusurika kupigwa tukio mara ya mwisho, huko nje nikatazama upande wa magharibi, hamna mtu, nikatazama upande wa mashariki nao hamna mtu, kabla ya kurudi ndani nikaenda kule bafuni, bafu zote zilikuwa zimezimwa taa hivyo nikahitimisha hamna mtu humo, basi nikarejea mlangoni na kuurejeshea ule mlango wa grill pasipo kuufunga na ufunguo ili kama kuna mtu huko nje basi ataingia na kuufunga mwenyewe, mimi nikareja sebuleni nikaendelea kutazama televisheni.

Nilitazama mpaka nilipohisi naelemewa na usingizi ndipo nikaenda zangu chumbani, huko nikajilaza na kuskilizia lakini muda wote huo sikusikia mlango wa grill ukifunguliwa, kulikuwa ni kimya tu kama hapo awali, nikajiuliza nini kinaendelea au ni mimi ndo' mwenye matatizo? Mpaka napitiwa na usingizi sikupata kusikia kitu, asubuhi palipokucha wakati naenda kuoga niende kazini, pale bombani, nilikutana na jirani yangu wa mlango mwingine ndani ya ile nyumba kubwa, mwanamke huyo alikuwa anafua nguo zake hapo nje, wanawake hawa huwa wana utaratibu wa kuamka mapema kufua kwaajili ya kuwahi kamba, baada ya kunisalimu aliniuliza,

"Shemeji, ni wewe ndo' uliacha mlango wa grill ukiwa wazi jana usiku?"

Nikamweleza namna mambo yalivyotokea kuwa mimi sikuuacha wazi bali niliurejeshea tu baada ya kusikia mtu alitoka, ajabu akaniambia kuwa mumewe asubuhi ya mapema sana alipotoka aliukuta mlango ukiwa wazi kabisa, umeachama kama mdomo! Nikastaajabu kusikia hayo, nilijiuliza ni muda gani mlango ulifunguliwa lakini sikupata majibu, nikaenda zangu kuoga nikilenga kuwa siku n'takayokutana na BIGI nimuulize kuhusu jambo hilo, sikuwa najua ni lini ila nilitumai ndani ya wiki hiyo basi nitambahatisha.

Ikapita siku mbili, sikumwona BIGI wala mkewe, siku ya tatu yake nikiwa sebuleni majira yangu ya usiku mtulivu, siku hiyo sikuwa natazama televisheni bali namalizia kazi fulani kwenye laptop, nikasikia mtu akiufungua mlango na kisha akaufungua mlango wa grill kakakaaa-kaaakaa, nikakaa tenge, mara hiyo sikutaka kupuuzia nilinyanyuka upesi nikaenda chumbani kutazama, ile kufungua tu pazia nikamwona mtu akiishia kwa kulifunga geti dogo, sikumjua mtu huyo ni nani kwani nilichoambulia kukiona ni mkono tu tena kwa muda mchache mno, basi nikabaki hapo nikiendelea kutazama pengine nitaona kitu.

Ngoja lakini wapi! Nilitumia kama nusu saa hapo lakini sikuona kitu nami nilikuwa nina hamu sana ya kumwona mtu huyo kwani niliamini yeye ndiye yule aliyeacha geti wazi siku ile, nilitamani kujua anafanya nini muda huo na kwanini anaacha geti wazi?

Nilikaa hapo dirishani kwa muda mrefu pasipo kuona kitu nikakata shauri kwenda nje, nilipoufungua mlango wangu kudaka korido nilisikia sauti ya watu wakizungumza, nikasita nikiskiliza. Sauti hiyo ilikuwa inatokea kwenye chumba cha BIGI na nilipoisikiliza kwa kitambo kidogo tu nilibaini sauti hiyo haikuwa ngeni masikioni mwangu, nilishawahi kuisikia mahali, ila ni wapi?

Kidogo kuwaza nikaikumbuka, sauti hii ilikuwa ni ileile niliyoisikia siku ile kwenye mlango huuhuu nikajua ni ya televisheni, ina maana imejirudia au ni masikio yangu? Nilistaajabu, lakini kadiri nilivyoisikia sauti hiyo tena na tena, tena kwa umakini, nikaamini kabisa haikuwa sauti ya televisheni, sauti hiyo ilikuwa ya watu wanaozoza na kunong'ona kitu ambacho sikuwasikia vema nikaelewa.

Nikiwa naendelea kuskiza hapo, mara nikasikia kishindo cha hatua za mtu kibarazani alafu mlango wa grill ukafunguliwa kakaaa kaakaaa! Nikashtuka kweli kweli, ni kama vile moyo wangu uliruka pigo moja kwa fujo!

Upesi nilirejea karibu na mlango wangu nikayatupa macho kule langoni, punde nikamshuhudia BIGI akiingia ndani huku amebebelea kiroba kitupu mkononi, huku juu amevalia 'vest' yake ileile aliyokuja nayo wakati mke wake anaumwa, aliponiona alisimama akan'tazama, nahisi na yeye alishtushwa na uwepo wangu pale, alinitazama pasipo kusema kitu chochote ila mimi nikamsalimu, hakujibu, alisimama tu akiendelea kun'tazama, sijui alikuwa anawaza kitu gani, mapigo yangu ya moyo yalikuwa yanapiga kwa kasi sana, niliona ni busara kuingia ndani kwangu upesi nikaufunga mlango kwa funguo kisha nikasimama hapo kusikiliza, kimya, nlidhani nitasikia vishindo vya miguu vikijongea lakini sikusikia chochote zaidi ya sauti ya mlango ukifungwa kisha kukawa kimya tena.

Nilizima kila kitu changu nikaenda chumbani moja kwa moja mpaka dirishani. Nilitazama pale kibarazani nikaona mlango wa grill ukiwa wazi. Nilitamani kwenda kuufunga lakini nikawaza vipi kama bwana yule akawa bado hajamaliza shughuli zake? Nikaona ni stara nikitulia lakini niendelee kungoja kama atatoka tena.

Nilingoja hapo kitandani kwangu mpaka usingizi ukanibeba, sikusikia kitu abadani. Kesho yake niliporejea tu kazini nikaelezwa kulitokea mjadala mkubwa hapo nyumbani juu ya swala la mlango wa grill kuachwa wazi kwa mara nyingine tena usiku ulopita, siku hiyo majira ya saa tatu hivi usiku kama sijakosea, nilikutana na jirani yangu yule wa dukani tukaongea mambo kadhaa kuhusu hapo nyumbani, moja kuhusu swala la ujenzi wa uzio na namna ambavyo mwenye nyumba haeleweki, na pili kuhusu swala la mlango wa grill kuachwa wazi nyakati za usiku. Bwana huyo alikuwa ndo' mtu wa kwanza kutoka asubuhi hivyo yeye ndiye aliyekuwa anaukuta mlango huo ukiwa wazi.

Kwa upande wangu nilimweleza yale niliyoyajua ya kuwa bwana BIGI ndiye anayeacha mlango huo wazi na basi kwa pamoja tukaazimia kumwambia endapo yeyote akipata nafasi hiyo. Siku zikapita, sijui kama yeye alifanikiwa kuonana na jamaa lakini mimi sikufanikiwa na uzuri mlango haukuachwa wazi tena.

Nakumbuka siku ambayo mafundi walikuja kwaajili ya ujenzi ndo siku ambayo nilipata kumwona bwana BIGI. Siku hiyo ilikuwa ni usiku kama wa saa nane hivi kama niko sawa, nilikuwa sebuleni kama kawaida yangu kabla ya kwenda kulala, televisheni inaongea lakini akili yangu yote ipo kwenye simu naperuzi mitandaoni, naingia instagram, whatsapp na JamiiForums.

Nilisikia mlango unafunguliwa na kisha mlango wa grill, nikanyanyuka kwenda kutazama dirishani. Hapo nilimwona BIGI akiwa amebebelea kiroba begani mwake anatoka kwenda geti dogo.

Kwasababu za ujenzi, geti hilo lilikuwa wazi tena limeegeshwa pembeni kabisa hivyo unaweza kuona mpaka nje. Nikamwona mtu huyo akitokomea huko mpaka kiza kikammeza!

Niliendelea kukaa hapo kwa muda kidogo lakini sikumwona akirudi, nikajua ni kama kawaida sitamshuhudia mpaka nitakapolala, lakini siku hiyo hali ilikuwa tofauti, baada ya kurudi kule sebuleni na kukaa kwa dakika kadhaa nilisikia kishindo cha mtu akikatiza koridoni alafu sauti ya mlango ikaita, nikawaza moja kwa moja atakuwa BIGI ndo amerejea lakini kwanini haufungi mlango wa grill? Nikaazimia ningoje kidogo hapo na nikiona kimya basi nitatoka nikaufunge mlango huo mwenyewe.

Kweli nilikaa hapo kwa kama nusu saa hivi, kimya, nilienda chumbani kutazama dirishani, hali ilikuwa shwari, nikauendea mlango wangu kuufungua lakini nilipotekenya tu funguo nikasikia mlango mwingine unafunguliwa, nikatulia kuskiza.

Vishindo vilipita koridoni nikahisi na kuamini kabisa alikuwa ni BIGI, vishindo hivyo vilipofifia nikaufungua mlango na kuchungulia nje, kweli alikuwa BIGI, nilimwona anatoka nje ya uzio akiwa na kiroba chake begani. Sikujua alikuwa anabebelea kitu gani humo lakini kilichonitatiza zaidi ni kwanini alikuwa anafanya zoezi hilo usiku wa manane?

Nilitoka nikatembea kwa upesi lakini pia kwa uangalifu mpaka kwenye geti dogo. Hapo nilirusha macho yangu kule kutazama, kwa mbali kwa msaada wa mataa mengine ya kule nje, nikamwona BIGI akiwa anayoyomea kuelekea kule korongoni, kule ambapo ndiyo wezi wanapokimbilia. Mwendo wake ulikuwa wa haraka sana na kwasababu ya uweusi wake basi kiroba ndo kilikuwa kinaonekana kikikata upepo, kile kinapepea, kilee kinapepea!

Niliijikuta nina hamu ya kwenda zaidi kutazama.


***
Duh! Mpaka hapa kazi uliyokua unaifanya ni zaidi ya CCTV camera
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom