Mundele Makusu
JF-Expert Member
- Sep 28, 2021
- 896
- 1,329
@
Nourhan pita hapa kuna madini mazuriiiiJirani yangu wa kule Goba hakuwa mtu wa kawaida - 06
Sikupoteza muda, nilijiandaa upesi nikaongozana na jirani mmoja wa kiume mpaka hospitali Mwananyamala tulipoambiwa kuwa ndipo alipo bwana Tarimo. Tulipofika huko, tulipokelewa na mke wa bwana huyo akiwa na uso ulioparama kwa majonzi.
Mwanamke huyo hakuwa anaweza kuongea hata maneno mawili kwa usahihi, kila alipotoa neno moja ni kama vile alitoneshwa upya kidonda akaishia kunyamaza akiufunika uso wake, alikuwa anatia huruma kwelikweli na alinifanya niamini kuwa hali haikuwa shwari huko ndani. Mama huyo pembeni yake alikuwa akifarijiwa na mmoja wa ndugu yake Tarimo, ndugu ambaye mimi sikuwa namfahamu kwani alikuwa mgeni machoni pangu.
Ndugu huyo, kwasababu angalau yeye alikuwa anajiweza, basi ndo’ akawa anaongea na sisi kutupatia taarifa ya kinachoendelea hapo, kwa maelezo yake bwana Tarimo alikuwa amevunjika miguu yote miwili, mkono mmoja, kiuno na taya pia! Kwa namna hiyo bwana Tarimo alikuwa anangojea tu rufaa apelekwe Muhimbili.
Baada ya muda kidogo wa kungoja nilipata nafasi ya kumwona bwana huyo, kwakweli hakuwa anatamanika, ajali ilimchakaza sana, lilikuwa ni jambo la kheri sana kumwona bado yu hai, pale niliamini kweli kama siku yako ya kwenda haijafika basi hautaenda hata iweje.
Tulikaa hapo kwa muda wa lisaa limoja hivi kabla hatujageuza kurejea nyumbani. Tulipanga siku ya kuja kumwona tena bwana Tarimo huku tukisihi maombi mengi yanahitajika bwana huyo apate kusimama kwa mara nyingine. Kuja kufika nyumbani, majira ya saa nane hivi ya usiku, sikufanya kitu kingine nikaoga na kupumzika usiku wake nikiwaza kumhusu bwana Tarimo.
Yale yote aliyotaka kuniambia yaligeuka mawe … kweli hamna mtu anayeijua kesho yake, niliwaza nikijigeuza huku na kule pale kitandani. Sasa kitu pekee ambacho bwana Tarimo alikuwa ameniachia kikawa ni mawazo makubwa kumhusu bwana BIGI, kwanini bwana huyo aliniambia tufanye kila linalowezekana ili BIGI ahame pale? Ni nini aliona mpaka akafikia hitimisho kama hilo? Kwakweli nilitamani sana kujua kama kuna mtu ameyaona zaidi ya yale ambayo mimi nimeyaona.
Nikiwa naendelea kuwaza, akili yangu ikipiga mbizi katika dimbwi hilo la mawazo, mara usingizi ukanibeba msobemsobe nisijue nimepotelea humo saa ngapi, ni baadae ndo’ nilikuja kugutuka baada ya kusikia ndoo ikianguka chini huko nje puuuh, nikaamka upesi kuangaza dirishani. Bila shaka ndoo ile ilikuwapo kibarazani ndo’ maana kuanguka kwake kukawa na kishindo.
Niliitazama ndoo ile ikiwa inazungukazunguka pale chini mpaka ikatulia kabisa. Kimya. Sikuona mtu wala kitu cha kutilia shaka. Nilitazama lile geti dogo, geti jipya, nalo nikaliona limefungwa basi nikarejea kitandani nikiamini ndoo ile iliangushwa na upepo wa huko nje.
Nilitazama saa kwenye simu yangu, ilikuwa ni saa tisa, nikajilaza kuutafuta usingizi tena lakini kabla sijapotelea kwenye njozi nilisikia tena ndoo ikipigwa, nikashtuka. Mlio niliousikia ni kana kwamba mtu ameipiga teke ndoo ile, taratibu nikafungua pazia la dirisha kutazama.
Niliona ndoo ile ikiwa karibu na geti dogo, hapo inazungukazunguka kwenda kushoto na kulia, kulia na kushoto, alafu ikatulia tuli.
Nilitazama kando na kando lakini sikumwona mtu, kulikuwa kimya na kumetulia sana, nikajiuliza ni masikio na macho yangu ndiyo yananidanganya ama? Au ni usingizi na sijapata muda wa kutosha kupumzika? Sikupata majibu … niliendelea kutazama ile ndoo na pande zingine zote kwa muda wa dakika tano hivi, nilipoona hamna kitu niliachia pazia nikajilaza, sikusikia tena kitu mpaka jua linakucha na ndo’ mimi nikalala kwa amani.
Nilikuja kuamka baadae majira ya mchana baada ya kusikia sauti za watoto huko nje wakiwa wanacheza na kukimbizana. Nilitoka nikaenda kuoga kisha nikaketi sebuleni pamoja na tarakilishi yangu kufanya kazi za hapa na pale, muda si mwingi alikuja jirani mmoja aliyegonga mlango na kuniambia kuna zoezi la kuchangia pesa kwaajili ya kuifariji familia ya Tarimo na mkasa uliowapata.
Jirani huyo alikuwa ameshikilia daftari, peni, noti na sarafu lukuki mkono wake wa kushoto ambazo bila shaka alikuwa ameziokoteza kwa majirani wengine. Aliniambia Tarimo ameshahamishwa kwenda Muhimbili kwaajili ya matibabu zaidi na hizo pesa wanazozichanga si kwamba wameombwa na familia ya wahanga, lah, bali ni jitihada za kuonyesha umoja wetu nyakati za matatizo, nikaona vema.
Nilitoa pesa akanipatia peni kuandika jina langu pamoja na sahihi, sikuona haja ya lile jambo lakini kwasababu nililazimika basi nikafanya hivyo, niliandika jina langu na kiasi nilichotoa, katika karatasi lile nikapata kuona majina matano hivi ya majirani wengine waliokwisha kutoa, sikuyatilia maanani majina hayo wala kiasi walichotoa, ila kitu kilichonishangaza ni wingi wa sarafu zile alizokuwa amezishikilia bwana mchangaji, sarafu nyingi mno za hamsini hamsini, nikamuuliza kwa utani,
“Ndugu yangu, umekuwa kondakta?”
Bwana yule alitabasamu kwanza alafu akaniambia sarafu zingine anazo mfukoni, kweli nilipotazama nikaona mfuko wake umenenepa haswa. Nilistaajabu, yeye akaongezea kutabasamu kabla hajaniambia kuna jirani amempatia sarafu hizo na kwa ujumla wake zilikuwa yapata alfu ishirini! … baada ya hapo alienda zake kuendelea na zoezi la kuchanga pesa na mimi nikaendelea na shughuli zangu nilizokuwa nafanya.
Majira ya mchana, kwasababu ya kuboreka kukaa nyumbani tangu asubuhi, niliona ni vema nikanyoosha miguu kwa kutembea hapa na pale. Nilifikiria nielekee wapi, mwishowe nikakata shauri kwenda ‘bar’ fulani hivi ambayo ni mashuhuri kwa kuuza mbege kwani ilikuwa ni muda mrefu sijapata kinywaji hicho na nilihisi kiu chake. Nilichukua chupa ya lita moja na kiasi fulani cha pesa kisha nikashika njia kuelekea huko.
Ukiwa unatumia njia ya lami ya Goba kwenda mwelekeo wa Mbezi Mwisho, kuna kituo kinaitwa kwa Ndambi, kituo cha nyuma yake na cha Kontena ambacho ndipo kina sisi wa Goba Mashuka huteremkia. Ukishukia hapo kwa Ndambi kuna njia kubwa ya vumbi mkono wa kushoto, njia hiyo ukiifuata moja kwa moja, kwa kama dakika sita hivi, mkono wa kushoto utaiona bar hiyo niliyokuwa naiendea, hapo wanauza vinywaji vyote lakini pia wameandika kibao ‘Mbege Ipo’.
Ili kuifikia Bar hiyo kwa sisi ambao tunatokea Goba kwa Mashuka unalazimika kutembea umbali mrefu kukwea kilima mpaka kituo cha Kontena alafu urudi kituo cha nyuma cha Kwa Ndambi, vinginevyo, kwa njia fupi zaidi ya miguu, unakatiza kwenye lile korongo kubwa kuibukia ng’ambo ambako huko ndo’ kwa Ndambi, yaani kwa Ndambi na hapo Mashuka pametenganishwa tu na korongo hilo, korongo ambalo si njia rasmi bali watu hulitumia tu kwaajili ya kupunguza umbali wa safari.
Korongo hilo majira ya usiku huwa na kiza totoro, bila ya kutembea na kurunzi huwezi kuona unapokanyaga na kwasababu hiyo watu hawapendi kutumia njia hiyo, hata majira hayo ya mchana ni watu wachache wachache wangependa kupita hapo.
Nilikatiza korongoni nikipiga mahesabu ya kwenda na kuwahi kurudi kabla ya giza halijawa kubwa kwani sikutaka kutumia njia ndefu zaidi ya ile. Nilipomaliza korongo hilo, nilitumia kama dakika sita tu kufika katika ile bar, hapo nilikuta mziki mtamu na laini ukipiga kuburudisha wateja, tena ule muziki usiokuwa na fujo wala purukushani, nikaona ni vema sana nikipumzika hapo. Watu wachache na muziki usiokuwa na fujo ni moja ya mandhari zangu pendwa kabisa.
Nilitafuta sehemu palipokuwa pweke, nikakaa hapo, muda mchache tu mhudumu akaja kunikirimu. Mhudumu huyo ndiye aliyekuwa mmiliki wa ile biashara hivyo alikuwa anafanya kazi kwa moyo wake wote.
“Karibu, kaka.”
“Ahsante,” nilimwitikia nikampatia chupa yangu na kumwambia: “nahitaji mbege lita moja.”
Mara akaufinyanga uso wake kwa kuhuzunika.
“Daah pole, mbege imeisha muda si mrefu. Hapa ni mpaka kesho tena!”
Basi kwasababu hiyo nililazimika kuagiza bia mbili za baridi ili safari yangu yote isiwe bure, nikawa nakunywa taratibu huku naperuzi simu yangu nikiingia hapa na kutokea pale, nikiingia pale na kutokea hapa, kwa mbali muziki ukiniburudisha vilivyo.
Niliagiza bia tena na tena, kwa namna nilivyokuwa ‘busy’ na simu sikuwa natambua hata bia zile zilikua zinaenda wapi, nilijikuta nakunywa chupa na chupa hata nisijali. Baadae nilipata ‘kampani’ ya bwana mmoja ambaye naye alikuwa mpenzi wa nyimbo zile zilizokuwa zinapigwa basi nikajikuta nazidi kulowea hapo, tunaongea hiki na kile, kuja kupata ufahamu ni saa mbili usiku, kinyume kabisa na muda niliopanga kuondoka!
Nilinyanyuka upesi nikalipia bili yangu kisha nikaanza kiguu na njia, mwelekeo ni uleule wa korongoni kwani sikuwa radhi kuzunguka na njia ndefu ya kule barabarani, baada ya dakika chache nikafika korongoni, nilipotazama humo nikahamaki kwa kiza chake, aisee, kulikuwa ni kweusi tiii! Ile miti ambayo inapeperuka kwa upepo nyakati za mchana iligeuka kuwa mavitu meusi marefu ambayo yanatisha kwelikweli, ilitaka moyo sana kupita humo.
Niliwaza kurudi nyuma lakini nilipofikiria umbali wa safari ile, mmmh, nikajipa moyo, nitapita humohumo, siwezi kurudi nyuma wakati mataa ya nyumbani nayaona yalee kwa macho yangu, basi nikaingia korongoni huku nikitumia mwanga wa tochi ya simu yangu.
Nilitembea taratibu nikiwa naangaza ninapokanyaga, ndani ya korongo hilo kupo kimya, cha zaidi unachosikia ni matawi ya miti pale upepo unapopuliza. Nikiwa katikati ya korongo hilo, mara nilisikia sauti ya kitu kinachotembea … kabla sijafanya jambo lolote, mara nikasikia kitu hicho kikimbia! Niligeuka kuangaza kwa macho na tochi ya simu yangu nikamwona paka mmoja akiwa anakimbia kama mwehu, ni kana kwamba paka huyo alishambuliwa na mtu ama aliona kitu cha hatari.
Nilimtazama namna anavyokimbia nikajikuta napatwa na hofu nisijue ni ya kitu gani. Paka yule alipoishia katika macho yangu, upande uleule alokuwa anakimbilia, nikapata kuona viroba vitatu vikiwa vimepangana … sikujua ni nini lakini viroba hivyo vilinikumbusha taswira ya bwana BIGI upesi mno!
Vipi kama vile viroba ndo’ vile anavyovibeba nyakati za usiku wa manane? Nilijiuliza.
Nilivitazama kwa sekunde kadhaa, nafsi yangu ikawa inanituma niende nikavitazame viroba hivyo vina nini ndani yake. Baada ya muda mchache wa kujiuliza nilikata shauri kwenda kutazama, nikakwea kingo ya korongo na kuvuta kiroba kimojawapo mpaka chini miguuni mwangu. Kiroba hicho kilikuwa cheupe na kimefungwa mdomo kwa kamba ya katani, niliposogeza uso wangu karibu na kiroba hicho nilihisi harufu kali ya kuoza, na harufu hiyo ikawa inaongezeka kadiri nilivyokuwa najaribu kufungua kamba ile kuona kilichomo ndani.
***
Muendelezo soma Jirani yangu wa Kule Goba hakuwa mtu wa kawaida