Jinsi Nyerere alivyomtia hofu Karume

abdulahsaf

JF-Expert Member
Aug 31, 2010
858
130
[h=1][/h]
Ahmed Rajab


KUFIKIA mwanzoni mwa mwezi wa Aprili mwaka 1964, kama miezi mitatu baada ya Mapinduzi ya Zanzibar, mambo Visiwani humo yalikuwa shwari. Hali ya kisiasa ilikuwa thabiti na hivyo mazingira ya kijamii nayo yalikuwa mazuri.
Mandhari ya kisiasa ya wakati huo yalikuwa ya kimapinduzi. Hata steshini ya Redio ya Serikali iliacha kupiga nyimbo za taarab zilizokuwa na maudhui ya kimapenzi. Badala yake ikipiga nyimbo kuwaenzi wakwezi na wakulima na nyingine kuhusu Mapinduzi ya Januari 12, 1964.
Serikali ya Mapinduzi, ikiongozwa na Sheikh Abeid Amani Karume, ilikuwa Serikali iliyokuwa na umoja. Wakati huo ilikwishaanza kuchukua hatua mbalimbali zilizokuwa na lengo la kuleta usawa katika jamii.
Hatua hizo, zikiwa pamoja na kutoa huduma bure za afya na elimu bure kwa watoto wote na kutaifisha ardhi, ziliwavutia wananchi wengi wa kawaida katika nchi nyingine za Afrika ya Mashariki.
Iwapo kuna wataosema kwamba hatua hizo hazikufanikiwa, ni swali jingine. Ukweli ni kwamba hatua hizo zilizitia homa serikali fulani. Haikustaajabisha kwamba mara baada ya Mapinduzi ya Januari 12 wanajeshi waliasi nchini Tanganyika (Januari 20), Uganda (Januari 23) na Kenya (Januari 24). Uasi huo haukushangaza kwa vile serikali za nchi hizo hazikuonyesha ari ya kuchukua hatua kama zile za Zanzibar ambazo zingewanyanyua watu wao.
Lakini labda waliotishika zaidi walikuwa wakubwa wa serikali za Kimagharibi. Pamoja na mengine walitishika na jina jipya la ‘Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.’ Nchi hiyo haikuwa Jamhuri tu ya kawaida baada ya kuondoshwa usultani lakini ilijitambulisha rasmi kuwa ni ‘Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.’
Kulikuwa tofauti kubwa kiitikadi kati ya nchi iliyokuwa ikijiita ‘Jamhuri’ na ile iliyokuwa ikijinata kuwa ni ‘Jamhuri ya Watu.’
Isimu hiyo ya pili ikitumiwa na serikali zilizokuwa zikijigamba kwamba zinatawala kwa maslahi ya wengi wa watu wao. Kinyume na Zanzibar lakini nyingi ya serikali hizo zikifuata itikadi ya kisiasa ya Kimarx na Kilenin au ya Kikomunisti.
Kufikia mwanzoni mwa Aprili 1964 wengi wa Wazanzibari walikuwa wamekwishayakubali Mapinduzi kuwa ni kudura ya Mungu. Watu wakiendelea na shughuli zao kama kawaida.
Vituko vya watu kufukuzwa kazini kwa sababu za kikabila au za kisiasa vilizuka baadaye pamoja na visa vya kamatakamata na misiba ya mauaji.
Serikali ikiwapeleka nchi za nje kwa masomo ya juu wanafunzi wa kila kabila na ikiendesha shughuli zake kwa nidhamu. Hakukuwa na segemnege katika uendeshaji wa vyombo vya dola.
Ingawa mazingara yalikuwa tofauti na yale ya serikali iliyopinduliwa, watumishi wakuu wa serikali waliiendesha nchi kwa mujibu wa sheria zilizokuwapo na mpya zilizotungwa na Baraza la Mapinduzi.
Hali hiyo iliyodumu kwa muda mfupi iliwafanya wengi wawe na matumaini na mustakbali wa taifa lao jipya. Leo tukikaa na kuipima hali ya mambo ilivyokuwa hatuoni ushahidi kwamba utawala wa Karume ulikabiliwa na kitisho kikubwa cha kutaka kuuangusha.
Sisemi kwamba hakujakuwako watu waliokuwa wakiiapiza serikali yake na waliokuwa wakiomba isambaratike au ipinduliwe moja kwa moja. Walikuwepo. Lakini nguvu zao za kuandaa mapinduzi ya kuyapinga Mapinduzi ya Januari 12 zilikuwa dhaifu. Hakuna mpinga Mapinduzi aliyethubutu kufurukuta wakati huo.
Tarehe Aprili 13 Karume alimwambia Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Salim Rashid, kwamba Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Tanganyika, alimpigia simu akimtaka ende Dar es Salaam. Siku ya pili yake Karume na Salim Rashid wakafunga safari kwenda kwa Mwalimu.
Walipofika Ikulu, Dar es Salaam, Mwalimu huku akimuangalia Salim Rashid aliwaambia wasaidizi wake: ‘Mpeni gari (Salim) akanyoe ndevu.’
Ni wazi kuwa Nyerere hakutaka Katibu wa Baraza la Mapinduzi asikie aliyokuwa amepanga kumwambia Karume. Ndipo Salim Rashid akashika njia kwenda kwa kinyozi akimuacha Karume na Mwalimu. Mbali ya Marais hao wawili hakuna mtu anayejuwa kwa uhakika nini hasa kilijiri kati yao sebleni Ikulu.
Kuna wanaoshikilia kwamba Nyerere alimtisha Karume kwa kumwambia kulikuwa na njama za kumpindua na kwamba muungano wa nchi zao utampa himaya.
Na kuna wasemao kwamba wakati huohuo Nyerere alisema atawarejesha kwao askari polisi 300 Wakitanganyika waliokuwa na silaha na waliopelekwa Zanzibar kusaidia kuzuia fujo.
Miaka michache kabla ya hapo Karume aliwahi kutaja nia yake ya kuiunganisha Zanzibar na Tanganyika na kuifanya iwe jamhuri. Kauli hiyo, aliyoitoa uwanja wa ndege wa Dar es Salaam na iliyoripotiwa kwenye gazeti la Mwongozo la chama cha Zanzibar Nationalist Party (maarufu kwa jina la Hizbu), ilimchongea baadaye amuangukie na kumtaka radhi sultani wa wakati huo Seyyid Khalifa bin Haroub.
Ingawa tangu hapo Karume alikuwa na ndoto ya Muungano wa Zanzibar na Tangayika hatujui akitaka uundwe kwa masharti gani au uwe wa aina gani. Tunachoweza kufikiria ni kwamba matamshi ya Nyerere ya Aprili 14 yalimtia hawafu kubwa Karume kiasi cha kumfanya ampe mwenzake aliyemzidi akili uhuru kamili wa kuziunganisha nchi zao.
Aliporejea Zanzibar Karume aliwaficha memba wenzake wa Baraza la Mapinduzi alichokubaliana na Nyerere. Siri ya Muungano ilikuwa yake peke yake Zanzibar. Hakulishauri Baraza la Mapinduzi, hakuishauri serikali wala hajakishauri chama cha Afro-Shirazi Party (ASP).
Wadadisi na wataalamu wengi wenye kuitalii kwa kina historia ya Muungano wanaamini kwamba ingawa Nyerere alikuwa mtetezi wa umoja wa Afrika na ingawa Karume alikwishadokeza kwamba angependelea Zanzibar na Tanganyika ziungane, Muungano ulioundwa Aprili 26 mwaka 1964 uliandaliwa ili kuliridhia matakwa ya dharura ya Marekani.
Wakati huo Marekani kwa kweli ilikuwa hamnazo, majununi kabisa, kuifikiria Zanzibar kuwa ngome ya ukomunisti upande wa Afrika ya Mashariki na kitisho kwa maslahi yake. Marekani ikawa mbioni kutafuta njia au mamba wa kuyameza Mapinduzi ya Zanzibar.
Siku tatu au nne baada ya huo mkutano wa siri wa Marais wawili Karume alipelekewa Hati za Muungano kutoka Dar es Salaam. Hati hizo alikabidhiwa Ikulu ya Zanzibar na aliyekuwa waziri mdogo wa mambo ya kigeni wa Tanganyika.
Hii leo mustakbali wa Zanzibar uko njia panda kama ulivyokuwa pale Karume na Nyerere walipoziunganisha nchi zao. Lakini hali halisi za Aprili 1964 na za leo zimebadilika sana. Hii ni kwa sababu kwanza hali ya ndani ya Zanzibar kwenyewe imebadilika; pili, mahusiano yake na nchi zilizo ngeni kwake yamebadilika na tatu, mazingara ya ulimwengu pia yamebadilika.
Mnamo Aprili 1964 mustakbali wa Zanzibar uliamuliwa kwa njama zilizoandaliwa na Marekani pamoja na madola mengine ya Kimagharibi, ambayo tunaweza kuyabandika lakabu ya ‘wapishi wa kimataifa’. Mpishi mwengine alikuwa jirani Tanganyika.
Kama inavyokumbushwa mara kwa mara Muungano uliopo leo sio ule ulioelezwa na Hati za Muungano, zilizokuwa na mambo 11 tu ya Muungano. Kwa muda wa miongo kadhaa Zanzibar ikiachiwa ijiendeshe yenyewe.
Kwa mfano, ilikuwa na uhuru kamili wa kisiasa toka 1964 hadi 1972 alipouliwa Sheikh Karume.
Kwa upande wa uchumi serikali za Zanzibar ziliendelea kuwa na uhuru kamili mpaka ilipoingia ile ya awamu ya tano ya Rais (Mstaafu) Salmin Amour. Serikali hiyo ilishindwa nguvu na shinikizo za Bara. Ikabidi isalimu amri na kuchanganya sera yake ya fedha pamoja na kodi na ushuru na ile ya Bara (yaani ya serikali ya Muungano).
Tukiuzingatia umoja walio nao Wazanzibari na matarajio yao kwa Serikali yao ya Umoja wa Kitaifa, halitokuwa la ajabu iwapo mchakato utaopelekea kupatikana kwa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania utayathibitisha matakwa yao.
Matakwa hayo yatabainika watapotoa maoni yao kwenye Tume ya Katiba na yataonyesha kuwa wengi wao watataka pawepo Muungano wa Mkataba na si wa Katiba.
Ushahidi kwamba hali ya mahusiano ya Zanzibar na Muungano ni tofauti na ilivyokuwa zamani ni ile migogoro isiyokwisha kati ya pande hizo mbili. Shtuma zilizoko Visiwani ni kuwa Serikali ya Muungano yenyewe ndiyo inayoianzisha migogoro hiyo, kama kwa mfano kwa kuandikiana mikataba na jumuiya za kimataifa kwa niaba ya Zanzibar au kwa kuwa na makubaliano ya kibalozi kwa niaba ya Zanzibar na madola ya nje, mfano Norway.
Serikali ya Tanzania haina haki ya kufanya hivyo hata ikiwa sekta zote zinazohusika za utawala ziko chini ya mamlaka yake. Na hivyo sivyo ilivyo. Tena haina haki hiyo kwa sababu mfumo wa Muungano uliopo sasa si wa kudumu kwa vile kuna huu mchakato wa kuamua kuhusu majaaliwa ya Muungano wenyewe pamoja na mfumo wake na katiba yake.
Wakuu wa Bara watapata taabu Zanzibar na huenda hata wakahatarisha usalama endapo watajaribu kushikilia kwamba mfumo uliopo sasa wa Muungano uendelezwe kama ulivyo.
Hatimaye tukumbuke kuwa ulimwengu nao pia umebadilika. Tujuavyo, tena kwa uhakika, ni kuwa kinyume na mwanzoni mwa 1964 hii leo nchi kadhaa za Kimagharibi ziko tayari kuiunga mkono Zanzibar ikiwa itadai mamlaka yake kamili kutoka Serikali ya Muungano. Tumeyadaka haya faraghani yakidondoka kutoka ndimi za wanabalozi wa nchi fulani wasiotaka kutajwa.

www.mzalendo.net
 
Island Syndrome!

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ilikiwa siri ya Nyerere na Karume Snr.

Maridhiano yaliyozaa SUK ni SIRI ya Karume Jnr na Maalimu Seif. Si JK wala Prof.
Lipumba wanaofahamu hiyo Siri (wanyeviti wa vyama vya CCM na CUF).

Inaelekea Wazenji mnapenda sana SIRI! TAFAKARI
 
Kama muungano ulikuja kwa matakwa ya nchi za magharibi, si ajabu kwani hata mipaka ya nchi za Africa ilichorwa kwa matakwa ya nchi za magharibi pia. Hata Pemba na Unguja ziliunganishwa kwa matakwa ya Sultani kutoka Oman.
 
Back
Top Bottom