Jinsi mabasi ya wanafunzi yalivyotafunwa na wajanja

tpaul

JF-Expert Member
Feb 3, 2008
21,835
18,248
Tatizo la usafiri kwa wanafunzi jijini Dar es Salaam ni tete kuliko tunavyoweza kudhani na halipaswi kufumbiwa macho hata kidogo. Ni muda mrefu sasa tumeshuhudia watoto wetu wakiteseka na kunyanyaswa na utingo wa mabasi ya binafsi huku mamlaka zinazohusika zikiwa kimya. Kila siku wanafunzi huchelewa kufika shule na kurejea majumbani mwao na hufika wakiwa hoi kufuatia kadhia wanayokutana nayo njiani wakati wanaenda na kurudi shule. Hali hii huwaathiri sana kimwili, kisaikolojia na kitaaluma.

Ni mara nyingi tumeshuhudia wanafunzi wakizuiwa kupanda kwenye mabasi na wakati mwingine kushushwa chini na utingo wakorofi. Misukosuko waipatayo wanafunzi katika usafiri wa kwenda na kurudi shule huwafanya washindwe kufuatilia masomo kikamilifu, hivyo kuathiri maendeleo yao ya kitaaluma. Ni vigumu sana mpango wa ‘Matokeo Makubwa Sasa’ kuzaa matunda yanayotarajiwa endapo tatizo la usafiri kwa wanafunzi halitapatiwa ufumbuzi mwanana. Suluhisho la usafiri wenye staha kwa watoto wetu ni lazima litafututwe ikiwa kweli tunataka kuboresha kiwango cha ufaulu. Hatuwezi kuwa wanafunzi ambao kila saa wanawaza jinsi ya kwenda na kurudi shule halafu tukategemea ufaulu mzuri kutoka kwao.

Siku za nyuma kulikuwa na mabasi ya wanafunzi ambayo yaliishia kutafunwa na mafisadi wachache huku serikali ikiwa inawachekea badala ya kuwachukulia hatua kali za kisheria. Aidha, kuna mabasi kadhaa ya wanafunzi yalitolewa na benki ya CRDB ambayo nayo yaliishia mifukoni mwa mafisadi haohao na wananchi wamemekaa kimya kana kwamba hakuna tatizo lolote lililotokea. Hapa ndipo hawa wachumia tumbo walipotufikisha na tunazidi kuangamia zaidi kwa sababu ya kutojali kwetu.

Wakati umefika serikali iamke kutoka usingizini na kutafuta jawabu la usafiri kwa wanafunzi hawa wanaotaabika bila huruma. Na wale mafisadi waliokula mabasi ya watoto wa shule wafikishwe kwenye vyombo vya sheria ili sheria ichukue mkondo wake. Hatuwezi kuwa tunaimba wimbo ule ule kila siku bila kuchukua hatua maridhawa na madhubuti dhidi ya wendawazimu wanaorudisha nyuma maendeleo ya elimu. Matokeo yake ni kwamba wananchi wanajenga chuki kwa serikali yao kwa sababu ya watu wachache wanaopenda kujinufaisha wao wenyewe bila kuzingatia adha wanayosababisha kwa wengine.


mabasi ya crdb.jpg

Mabasi yaliyotolewa na CRDB yakizinduliwa kwa mbwembwe

pinda akizindua mabasi.jpg

Bw Pinda akizindua mabasi ya wanafunzi yaliyokabidhiwa na CRDB
 
Back
Top Bottom