Jenerali Ulimwengu ashangaa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Jenerali Ulimwengu ashangaa

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Shaycas, Jul 21, 2012.

 1. Shaycas

  Shaycas JF-Expert Member

  #1
  Jul 21, 2012
  Joined: Feb 13, 2009
  Messages: 899
  Likes Received: 34
  Trophy Points: 45
  NIMEKUWA nikisema kwamba tunahitaji kukua, na katika kukua tutende na
  tuenende kama watu wazima wasiohitaji ulezi wa karibu wa baba mkali wala
  uangalizi wa yaya.

  Nimejaribu kuonyesha kwamba ingawaje mwanzoni mwa maisha yetu kama Taifa tulihitaji baba mkali wa kutuelekeza katika hatua zetu za mwanzo za kukua,
  hivi sasa hatumhitaji tena. Tunatakiwa tujitegemee, tujielekeze kama jamii
  iliyokomaa na ambayo hainyonyi dole-gumba tena.

  Kwa bahati mbaya, bado tunazo dalili nyingi mno za jamii inayonyonya dole-gumba, jamii iliyoshindwa kukua na kukomaa, jamii changa ambayo uchanga
  wake ni wa tabia zisizofanana na wingi wa miaka ya umri wake. Katika mambo mengi ni jamii iliyovia.

  Kinachotia hofu zaidi, kwa mtazamo wangu, ni kwamba hata katika yale mambo ambayo kwayo tulikwisha kuonyesha kwamba tunaanza kukomaa, tumefanikiwa kupata mbinu za kuturudisha uchangani.

  Kwa mfano, miaka 50 ya Uhuru ni muda mrefu kwa jamii yo yote ile kuwa inatambua ni yapi matatizo yake yanayoisababishia unyonge, na ni nini inahitaji ili kujikomboa kutoka unyonge wa umasikini, ujinga na maradhi.

  Utambuzi wa aina hii ni jambo la msingi mno, hata kama ufumbuzi utachukua muda mrefu ujao. Utambuzi huo unasaidia kuweka misingi ya kimkakati na hatua za kwanza za mbinu za utekelezaji wa malengo hayo ya kimkakati.

  Tunajua kwamba misingi hiyo ilikwisha kujengwa na Baba wa Taifa, Mwalimu
  Julius Nyerere akisaidiwa na wazalendo wa kweli waliokabidhiwa majukumu wakati ule.

  Inawezekana kwamba wale vijana wasiopenda kuisoma nchi yao watakuwa hawajui hawa wazalendo ni akina nani waliomsaidia Nyerere kuweka misingi hiyo, lakini haiyumkiniki kwamba hata watu wa rika langu nao wanajifanya hawajui au hawakumbuki. Binafsi naamini kwamba hawataki, ama kwa sababu wanayo maslahi katika kutokumbuka au ni kutokana ule uvivu wa kufikiri tuliojijengea.

  Tungekubali kuzisumbua kumbukumbu zetu kidogo tu tungeweza kuwatambua akina Amir Jamal, Amon Nsekela, Dickson Nkembo, Clement G Kahama, Derek Bryceson, Obeid Katikaza, Gabrieli Mawala, Cleopa Msuya… na wengine kama hao, pamoja na wale waliokuwa vijana, akina Bakari Mwapachu, Omari Abebe, Basil Mramba, Mbaruk Mwandoro na kadhalika.

  Baadhi yao wamekwisha kututoka, na baadhi ya walio bado hai wanaweza kuonekana leo kama vile hawajawahi kuwa na thamani yo yote kwa sababu zama zao zimepita. Hata hivyo ni watu waliofanya kazi kubwa ya kuweka misingi fulani kama walivyoelekezwa na bosi wao, Nyerere.

  Kazi waliyoifanya wakati ule ilitakiwa iendelezwe na kizazi cha vijana wa leo,
  iboreshwe na ipelekwe kwenye viwango vya juu zaidi, lakini kwa sababu za upuuzi ambao nimekuwa nikiujadili, hilo halikufanyika, na wala sioni dalili
  kwamba watawala wetu wanalielewa hilo.

  Hali hii ya kutokuthamini urithi wetu imetufanya sasa tutafute walezi wengine
  badala ya baba yetu, na walezi hawa (ambao kwa hakika hawawezi kuwa na
  uchungu nasi) wanatuona kama “mazuzu” wa kutumiwa na watu wenye akili.

  Wanatuona kama punguani kwa jinsi tunavyoweza kuendelea kuwa “omba-omba” miaka 50 baada ya Uhuru wakati tunazo rasilimali ambazo wao wanazimezea mate.

  Nimewasikia, kwa mshangao mkubwa, watawala wetu wakitamka kwamba hawajui ni kwa nini nchi yetu ni masikini baada ya miaka yote hii na ikiwa na rasilimali zote hizi. Huko kutotambua ndiyo sababu mojawapo kubwa ya hali tuliyo nayo.

  Haiyumkiniki kwamba mtu anaweza kugombea uongozi wa nchi au jamii, tena kwa juhudi kubwa na kwa kuahidi mambo lukuki, halafu baada ya kuwa ameingia madarakani akatangaza kwamba wakati wote huo alikuwa hajui matatizo ya jamii yake. Nini kilimsukuma kugombea?

  Pasipo na shaka akilini mwangu, sababu moja kubwa iliyotufanya tukwame kiasi
  hiki imekuwa ni upuuzi wa uongozi na udhaifu wa watawala, vikiambatana na uwezo na utashi mdogo mno wa raia kuwasaili viongozi watawala wao na kusaili kila kilichowazunguka.

  Tumefanikiwa kujenga jamii ya watu wasio na uwezo wa kusaili mambo ya msingi kabisa, na wasiotaka kuwasaili wale waliowakabidhi hatamu za uongozi, hata pale hao waliokabidhiwa hatamu hizo ni dhahiri kwamba wanazitumia vibaya; na matokeo yake ni kwamba wanawaumiza hao hao waliowaweka madarakani, na hao wanaoumizwa hawana la kufanya.

  Kukosekana kwa utamaduni wa kusaili mambo yanayotuzunguka ndiko kunatufanya tuendelee kuamini kwamba binadamu anaweza kupaa kwa ungo; mwili wa albino una nguvu za miujiza; mtu anaweza kugeuka fisi na fisi akageuka mtu; kumbaka mtoto mchanga kunatibu Ukimwi…na ujinga mwingine wa aina hiyo.

  Jamii isiyosaili mambo ni jamii ya wajinga, na wajinga wakisha kuwa wengi ndani ya jamii, hata weledi wachache ndani ya jamii hiyo hawafui dafu: watanyongwa.

  Ndiyo maana tunapiga kelele siku zote kuhusu elimu bora, na elimu bora si ile ya kumeza “maarifa” bali ni ile inayomwezesha mtu kusaili mambo yanayomzunguka, kuuliza maswali ili apate majibu na kuuliza maswali kuhusu majibu anayopewa, na siku zote kuendelea kusaili hata yale mambo aliyodhani kwamba aliyaelewa awali. Ndivyo wenzetu walivyoendelea, na ndiyo sababu wako waliko nasi tunaendelea kurejea tulikotoka.

  Bila shaka tunahitaji kuondokana na upuuzi na ujinga tulimozama iwapo tunataka kupiga hatua za kwenda mbele badala ya hizi za kurudi nyuma tunazozipiga kwa kasi leo hii (kwa sababu ni kweli tunarudi nyuma kwa kasi).

  Mahali pa kuanzia ni mwanzo, na mwanzo daima ni uongozi wa kisiasa. Siasa safi
  zitazaa mazingira safi ya watu kufanya kazi za kuleta maendeleo katika nyanja
  zote. Siasa hovyo zitajenga mazingira hovyo vivyo hivyo, ambayo yataendelea
  kutuzamisha katika upuuzi na ujuha.

  Siasa zetu hazina budi kuwa na misingi ya usaili wa masuala yote yanayotuzunguka, na ziachane na unafiki wa wale wanaodhani kwamba kutosaili jambo au mtu ndio uaminifu na nidhamu.

  Tukumbuke, wale wanaodhani viungo vya mwili wa albino vinaleta utajiri, au
  kwamba ungo ni helikopta, msingi wao mkuu ni kushindwa kusaili mambo na watu.

  Katika siasa kushindwa kuwasaili wale waliokabidhiwa madaraka ya kuendesha
  jamii, au kushindwa kusaili miundo, mifumo na michakato inayoendesha jamii, ni ushirikina mwingine ambao matokeo yake ni kuidumaza jamii yetu. Htuna budi
  kupambana na dalili zo zote zinazotusukuma kutokomoea zaidi katika nakisi ya usaili.

  Ndiyo maana napingana moja kwa moja na baadhi ya mambo yanayotamkwa na kufanywa na baadhi ya wakuu wa asasi za utawala nchini, ikiwa ni pamoja na wakuu wa shughuli za Bunge.

  Ni kama vile wakuu hawa wa Bunge, pamoja na Spika na wasaidizi wake, wamo bungeni kuhakikisha watawala hawasailiwi, hawadadisiwi na hawakosolewi.

  Niliangalia kwa mshangao mkubwa ubishi kati ya Spika na mbunge aliyesema kwamba, pamoja na uzembe na upuuzi wa asasi nyingine, alibaini pia “udhaifu wa Rais,” na hili likawa ni tatizo kubwa lililositisha shughuli za Bunge kwa muda na likawa ni chanzo cha gumzo nchini.

  Mimi najiuliza, iwapo mbunge wa upinzani atazuiwa kusema kwamba Rais, ambaye ni kiongozi wa chama tawala (ndiyo kusema chama anachokipinga mbunge huyo) ni dhaifu sasa aseme nini? Amsifu Rais kwa umahiri, ukakamavu na ushujaa? Apendekeze kwamba Rais abakie madarakani maisha, na chama chake kisipingwe? Kazi ya mbunge wa upinzani ni nini hasa?

  Nadhani ni kutokana na ukali wa Spika kuhusu “udhaifu” wa Rais ndiyo ofisa
  mwandamizi serikalini akasimama bungeni kwa ukali kumshambulia mbunge aliyesema kwamba baadhi ya majaji hawafai na kwamba uteuzi wao ulikuwa wa kutiliwa shaka.

  Ndipo nikatambua kwamba tunalo tatizo la msingi kuliko nilivyodhani mwanzo.

  Tatizo hilo ni la kifalsafa katika mfumo ambao msingi wake wa kidhana ni kwamba mkubwa hatiliwi shaka, na mambo yalivyo ndivyo yalivyo, na hakuna bora zaidi ya yalivyo.

  Inaitwa falsafa ya Pangloss, ambayo nitaijadili wiki ijayo.

  Chanzo: Raia mwema, toleo 250 la tarehe 18 Julai 2012
   
 2. Q

  QARBU Member

  #2
  Jul 21, 2012
  Joined: Jul 4, 2012
  Messages: 14
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 3
  sehemu kubwa(watu) ya nchi yetu inayohusika na kusaili watawala ni rahisi kudanganyika na watawala wetu huutumia huo mwanya kama mtaji wao badala kuuziba ili tusiendelee kurudi nyuma na badala yake tuende mbele
   
 3. B

  Bulesi JF-Expert Member

  #3
  Jul 21, 2012
  Joined: May 14, 2008
  Messages: 6,447
  Likes Received: 414
  Trophy Points: 180
  CCm ya leo tofauti na ile ya Nyerere imejaa wanafiki kwasababu siku hizi FITINA SIO MWIKO TENA na ndio maana wanachama wa ccm hawawezi tena kuwasaili viongozi wao ambao ndio watawala wetu na hivyo nchi kudumaa kimaendeleo!!CCm ya leo haina bahati ya kuwa na wakina Rajab Diwani na Masudi Mtandika; wanachama waliokuwa na ujasiri wakuwakabili viongozi wa chama pale walipoona wanakwenda kinyume na maadili ya chama; leo wanachama wanaiba mali za nchi na kuzificha ughaibuni na bado wanazawadiwa kuwa viongozi wa kamati nyeti za chama!!Je katika hali kama hiyo nchi itaendelea?
   
 4. GodfreyTajiri

  GodfreyTajiri JF-Expert Member

  #4
  Jul 21, 2012
  Joined: Sep 26, 2010
  Messages: 846
  Likes Received: 229
  Trophy Points: 60
  natumaini jenerali ulimwengu atapata nafasi ya kuyakusanya yote anayoandika na kuweka katika
  chapisho (kitabu) moja au kadhaa ili viwe kumbukumbu nzuri kwa vizazi vijavyo kwamba walikuwepo
  watu makini.
   
 5. MAMA POROJO

  MAMA POROJO JF-Expert Member

  #5
  Jul 21, 2012
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 4,966
  Likes Received: 27
  Trophy Points: 135
  gazeti la Raia mwema halielewiki liko upande gani siku hizi linachoma kotekote.
   
 6. Emmanuel J. Buyamba

  Emmanuel J. Buyamba Verified User

  #6
  Oct 21, 2017
  Joined: May 24, 2013
  Messages: 642
  Likes Received: 206
  Trophy Points: 60
  Mkuu,unaweza nisaidia kuipata habari ya mwendelezo wa hii makala inapozungumzi nadharia ya Pangloss!?

  Nimeitafuta kule Raia Mwema nikakutana na maneno ya kuondolewa sababu ya sijui robot gani!!
   
 7. maonomakuu

  maonomakuu JF-Expert Member

  #7
  Oct 21, 2017
  Joined: Jul 24, 2015
  Messages: 2,511
  Likes Received: 967
  Trophy Points: 280
  Tatizo hilo ni la kifalsafa katika mfumo ambao msingi wake wa kidhana ni kwamba mkubwa hatiliwi shaka, na mambo yalivyo ndivyo yalivyo, na hakuna bora zaidi ya yalivyo.
   
 8. Allen Kilewella

  Allen Kilewella Verified User

  #8
  Oct 21, 2017
  Joined: Sep 30, 2011
  Messages: 7,376
  Likes Received: 10,375
  Trophy Points: 280
  Andiko lililojaa maarifa yaliyotukuka!
   
 9. zipompa

  zipompa JF-Expert Member

  #9
  Oct 21, 2017
  Joined: Aug 19, 2014
  Messages: 3,066
  Likes Received: 4,556
  Trophy Points: 280
  uoga, unafiki, umaskini wa fikra, wa jamii yetu ndio chanzo cha yote haya na kuwa na viongozi wabovu.

  yaani mtu ananunua dumu/dramu la pombe tayari imekuwa tiketi ya kupata kura.
   
 10. l

  lufungulo k JF-Expert Member

  #10
  Oct 21, 2017
  Joined: Apr 19, 2012
  Messages: 1,267
  Likes Received: 451
  Trophy Points: 180
  Kalamu ya Jenerali huwa ni hatari, point point tupu ,
  Uwezo wa kusaili ,kuuliza swali ili apate majibu na kuuliza maswali juu ya majibu anayopewa.

  Mfano swali hili na jibu lake "mkuu pembejeoooo, jibu pembejeoo mikono yako"
   
 11. Super Handsome

  Super Handsome JF-Expert Member

  #11
  Oct 21, 2017
  Joined: Jul 16, 2013
  Messages: 2,862
  Likes Received: 2,723
  Trophy Points: 280
  Boonge moja la makala ..ni ya 2012 lakini kama ameandika Jana asubuhi!
   
 12. Tetty

  Tetty JF-Expert Member

  #12
  Oct 21, 2017
  Joined: Jan 6, 2012
  Messages: 25,560
  Likes Received: 16,530
  Trophy Points: 280
  Ni ajabu kwa vijana kumuamini mtu anauesema alisukumiziwa tu kwa maana kwamba hakujiandaa
   
 13. I

  Isa khamisi JF-Expert Member

  #13
  Oct 21, 2017
  Joined: Mar 9, 2017
  Messages: 326
  Likes Received: 299
  Trophy Points: 80
  Ndivyo gazeti linavyotakiwa liwe
   
 14. Lambardi

  Lambardi JF-Expert Member

  #14
  Oct 21, 2017
  Joined: Feb 7, 2008
  Messages: 10,313
  Likes Received: 5,605
  Trophy Points: 280
  Jenerali ana akili mingi sana....kumfuata inabidi uwe nguli sana ili uweze kumuelewa , la sivyo utaishia kumshangaa kama yeye anavyoshangaa watanzania walio wengi na watawala wetu
   
 15. A

  August JF-Expert Member

  #15
  Oct 21, 2017
  Joined: Jun 18, 2007
  Messages: 4,506
  Likes Received: 723
  Trophy Points: 280
  Hili toleo si zilipendwa? Au aliliandika Jana
   
 16. x

  xaracter JF-Expert Member

  #16
  Oct 21, 2017
  Joined: Jul 28, 2015
  Messages: 849
  Likes Received: 460
  Trophy Points: 80
  Kama taifa tulipotea tangu mwanzo,Mwalimu alitupoteza kinachoendelea hivi sasa tunazidi kutokomea kusikojulikana ,tulipotea kwenye ujamaa na kujitegemea,yule alikuja na ruksa,akafuata wa ukweli na uwazi ,yule wa maisha bora kwa kila mtanzania na huyu sasa wa nchi ya viwanda na kuisoma namba,mwingine atakuja na yake.Kinachotakiwa ni kuanza upya wakati huu ambao jamii ina uelewa mpana kuliko ilivyokuwa awali .Turudishe tanganyika na Zanzibar kila mtu aanze kujipanga upya kisha tuone tunafanyaje.Vingine vyo tunazidi kutokomea kusikojulikana!
   
Loading...