Je, unayo sababu ya wewe kufanikiwa? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Je, unayo sababu ya wewe kufanikiwa?

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by eRRy, Nov 2, 2009.

 1. eRRy

  eRRy JF-Expert Member

  #1
  Nov 2, 2009
  Joined: Jun 12, 2009
  Messages: 1,080
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  Kama kuna kitu napenda kufanya katika maisha yangu ni kutia watu moyo, nafurahia sana kufanya jambo hili. Hakuna tukio naweza kusema huwa linanipa furaha kama kumwona mwanadamu anabadilika kutoka hatua moja kwenda nyingine, anaacha kulia na kuanza kufurahi, huzuni zinaondoka na tumaini linarejea! Kwangu mimi huu ni aina nyingine ya uwekezaji, kuwekeza katika watu, uwekezaji wenye uhakika kabisa ambao mtu huwezi kupoteza, hakuna mtu hata mmoja ambaye amewahi kuwekeza katika watu mwisho wa siku akapoteza.

  Nalifanya jambo hili kwa sababu hata hapa nilipofika kuna mtu fulani huko nyuma aliwahi kunitia moyo, alifanya jambo la muhimu sana katika maisha yangu, ndio maana na mimi najisikia kudaiwa, kwamba ni lazima katika maisha yangu niwasaidie watu wengine wengi kusimama! Nikiamini katika sheria moja isemayo; If you help someone smile, some else will make you smile and if you help someone stand up someone will help you standup, sheria hii inaamanisha mtu yeyote kutabasamu na wewe kuna mtu atakusaidia utabasamu na ukimsaidia mtu kusimama na wewe kuna mtu atakusaidia kusimama.

  Nimejifunza katika maisha yangu kama ninataka kufurahi basi niache kuwa mchoyo, niache kujifikiria mwenyewe katika kila kitu bali niwafikirie watu wengine kwanza kabla sijajifikiria mwenyewe, kwa kufanya hivyo mwisho wa siku nitaishia kuwa mtu mwenye furaha zaidi! Popote ulipo msomaji wa makala hii lazima ulielewe jambo hili, jishughulishe sana na furaha ya watu wengine kabla hujajishughulisha na furaha yako, watie watu moyo, lazima na wewe kuna mtu atakutia moyo.

  Msaidie huyo jirani yako kusimama, mfanyakazi mwenzako, mjane mwenzako, mgonjwa mwenzako, mwanafunzi mwenzako aweze kusimama! Kwa kufanya hivyo utakuwa unawekeza katika watu, uwekezaji mkubwa kabisa ambao mwanadamu amewahi kufanya katika historia.

  Miaka kama minane hivi iliyopita nilipata taarifa za msichana mmoja aitwaye Ng’endelaki Charles, mkazi wa Kigogo jijini Dar es Salaam. Msichana huyu alikuwa mgonjwa, kwa muda mrefu alilala ndani bila msaada wowote, zaidi ya kuwa mgonjwa alikuwa yatima aliyekuwa akilea wadogo zake wanne!

  Mimi na wafanyakazi wenzangu, Soud Kivea na Makongoro Oging tulikwenda kumtembelea binti huyo nyumbani kwao, hali niliyoikuta ilinisikitisha sana, alikuwa amelala kitandani tumbo likiwa limevimba, mwili wake ulikuwa umekondeana kupita kiasi! Katika maongezi yangu na yeye aliniambia alikuwa amekata tamaa kabisa, alichokuwa akisubiri ni kifo sababu kwa muda mrefu ilikuwa imeamriwa apelekwe nchini India kwa upasuaji wa Moyo lakini ilishindikana.

  “Umasikini ndio unaonifanya nife, ningekuwa na fedha hakika ningekuwa nimekwishapona, ili niendelee kuwatunza wadogo zangu nilioachiwa,” alisema binti huyo akilia.

  Niliumia sana, alinikumbusha maisha yangu ya nyuma, hasira yangu dhidi ya umasikini ikazidi kuongezeka! Najua kwa muda mrefu binti huyo alikuwa akimwomba Mungu atume malaika wake ili aokoe maisha yake, ndani ya moyo wangu niliamini huyo Malaika aliyekuwa akimsubiri, bila shaka alikuwa Eric Shigongo na siku ya kupona kwake ilikuwa ni hiyo.

  Nilisikia sauti ndani yangu ikiniambia “Eric, msichana huyu hatakufa bali ataishi!”, nilimtia moyo nikamwambia asingekufa bali angepona! Nikamjaza matumaini na kumwambia Mungu angefanya kila kinachowezekana aweze kupona! Wakati nayasema hayo sikujua nini kingetokea, niliamini tu Mungu angetenda muujiza.

  Niliporudi ofisini siku hiyo nilikuwa na huzuni sana, msukumo wa ajabu ulikuwemo ndani yangu kwamba ni lazima Ng’endelaki apone, hivyo basi nilichokifanya ni kuanza kuandika habari za msichana huyo kwenye gazeti la UWAZI nikiwaomba Watanzania wamsaidie kupata fedha ambazo zingemwezesha kwenda India kwa matibabu. Nikifanya hilo tulimchukua kutoka nyumbani na kumpeleka hospitali ambako madaktari walithibitisha kwamba kama akifanyiwa tu upasuaji na kubadilishwa Valvu za moyo wake zilizoharibika, angekuwa mzima.

  Hii ilinitia moyo wa kuendelea kuandika zaidi habari zake, sikuamini jinsi watu walivyoguswa na habari hiyo, zaidi ya shilingi milioni kumi na nne zikachangwa na Watanzania wenye moyo wa huruma na Ng’endelaki akasafiri kwenda India ambako alifanyiwa upasuaji na kurudi nchini akiwa msichana mrembo! Nilipomwona baada ya kurejea, alipokuja ofisini kunileta ua la shukurani, kidogo machozi yanitoke lakini nilimshukuru Mungu kwa muujiza wake. Mwaka mmoja baadaye Ng’endelaki alifunga ndoa na hivi ninavyoandika ana mtoto wa kiume!

  Hii ni historia ambayo haiwezi kubadilika, mtoto wa Ng’endelaki atazaa watoto wengine zaidi na pengine siku moja ndiye akaja kuwa Rais wa nchi yetu, nafurahi sana kuwa sehemu ya historia hii na ninaamini ukimsaidia mtu kusimama Mungu atakusaidia wewe kusimama. Hivyo msomaji wangu popote ulipo jaribu kumsaidia mtu aliye jiraniyako, ukifanya hivyo utashangaa jinsi maisha yako yatakavyobadilika, hii ni siri nyingine ya mafanikio ambayo watu wengi hawaijui.

  Huu ni waraka wangu kwako msomaji, lengo langu ni kukusaidia uweze kutambua uwezo mkubwa ulionao ndani, ambao kwa muda mrefu umebaki humo umeduwaa kwa sababu ya wewe kuamini huwezi kufanya jambo lolote maishani mwako! Nakuandikia waraka huu kukusisimua, ili sasa uanze kutafuta ni kitu gani ambacho Mungu amekuwekea ndani, kumbuka hakuna mwanadamu hata mmoja aliyezaliwa bila sababu, ipo sababu ya wewe kuwa duniani, ni lazima uitafute, usipofanya hivyo hakika utakufa ukijua ulimaanishwa kuwa ombaomba kumbe ulikuwa mwanamuziki au tajiri mkubwa, vyote hivyo utakwenda navyo kaburini.

  Ni wakati wewe kuchukua hatua na kubadili maisha yako, inawezekana! Hata kama kila mtu anakuambia huwezi, mimi nakueleza leo kwamba unaweza, hata kama huna senti tano, mimi nakueleza wazi kwamba unaweza kuanza bila kitu na ukamaliza maisha yako na kila kitu! Achana na maneno ya watu, achana na wavunja moyo, amini kile ambacho Mungu alikiweka ndani yako, mbegu ya ushindi, Mungu anataka kukunyanyua ili na wewe uweze kuwanyanyua wengine.

  Kwa muda mrefu nimeongea juu ya kutoruhusu mtu mwingine yeyote akuchagulie maisha yako ya baadaye, sasa nianze kusema na wewe juu ya njia kumi muhimu sana ambazo mtu yeyote aliyeamua kutafuta mafanikio ni lazima azipitie, njia hizi tutaziongelea kwa urefu wake, zitatutibu na kutuonyesha wapi yalipo matatizo yetu, utagundua kabisa ni kitu gani kinachokukwamisha wewe kutoka kwenye umasikini ambacho kama ukifanikiwa kukiondoa, basi kesho yako itakuwa ni yenye mafanikio makubwa.
  Njia hizi kumi ni:

  1. Sababu
  2. Lengo.
  3. Mpango
  4. Utekelezaji.

  5. Uvumilivu.
  6. Nidhamu,
  7. Chagua marafiki.

  8. Uwe na watu unaotamani kuwa kama wao.
  9. Kiu ya kupata taarifa.
  10. Kumbuka ulikotoka.

  Mambo haya kumi ndio niliyoyapitia mimi mpaka kufika hapa nilipo leo, najua sijafika mwisho wa safari yangu, kila siku naota ndoto mpya na ninajaribu kuzitafuta kwa nguvu zangu zote, nikiwa tayari kukosea, kuonekana mjinga na hata kupoteza! Unayesoma waraka huu leo kama kweli umechoshwa na hali uliyonayo na unataka kubadili maisha yako ni lazima uyatambue mambo haya kumi na uwe tayari kuyapitia moja baada ya lingine, sasa nitakueleza kwa undani wake jinsi mambo haya kumi yalivyofanya kazi katika maisha yangu;

  1.SABABU
  Mara nyingi ninapoelezea historia yangu ya maisha ya nyuma huwa naongelea taabu nyingi nilizozipata nikiwa mtoto, baadhi ya watu hufikia mpaka hatua ya kunionea huruma na kulia machozi! Lakini mimi huwa sitazami maisha yangu ya nyuma kwa huzuni tena, hiyo kwangu ni historia, sipendi iendelee kunitesa mpaka leo.

  Ninapoiongelea jana yangu huiongelea kwa tabasamu si kwa machozi tena, nililia sana nilipokuwa mtoto sihitaji kuendelea kulia tena leo.

  Zaidi sana huwa naitazama historia yangu kwa shukurani, nikimshukuru Mungu kwa kunipitisha katika maisha hayo, pengine ndio sababu leo hii naweza kuandika haya ninayoandika ili niweze kumsaidia mtu mwingine atoke kwenye dhiki! Kwa sababu naelewa kulala na njaa ni kitu gani, ndio maana naweza kumhurumia mtu aliyelala na njaa.

  Naelewa umasikini ni nini ndiyo maana nauchukia na kujaribu kuwasaidia watu wengine ambao bado wako kwenye hali hiyo ili watoke, pengine ningezaliwa Ikulu ya Dar es Salaam, nisingekuwa nafanya mambo haya kila siku! Hivyo basi naamini Mungu alikuwa na makusudi yake kuruhusu mimi nipite huko ili haya ninayoyafanya yaweze kutimia.

  Ndugu zangu,
  Taabu na shida si kitu kibaya, kinaweza kuwa kibaya tu pale mtu aliyepo katika taabu anaporidhika na kusema; “Haya ndiyo maisha yangu” “Mimi ni wa hivi hivi”, lakini kwa mtu mwenye malengo, shida si kitu kibaya, kimemaanishwa kuwa darasa kwa maisha yetu! Kukomaza miili na akili zetu, tukitayarishwa kwa ajili ya utukufu na heshima zijazo.

  Hebu ufikirie mti wa Mbuyu, ambao hauna mtu wa kuumwagilia maji na pia uufikirie mti wa Mpapai ambao kila siku una mtu wa kuumwagilia na wakati mwingine kuuwekea mbolea, upi ni imara kati ya miti hiyo miwili? Bila shaka ni Mbuyu ambao ni mnene wala hauyumbi unapokuja upepo mkali, lakini Mpapai huyumba kutoka upande mmoja hadi mwingine kwa sababu ni mwembamba na mrefu.

  Inaendelea wiki ijayo, usikose kunisoma.
  Nimeanzisha mradi wa Jikomboe ili kuzalisha mamilionea wengi Tanzania, wasiliana nami kwa warakapepe, warakawashigongo@yahoo.com au tuma barua kwa anuani, S.L.B 7534, Dar.
  source:http://www.globalpublisherstz.com/2009/11/02/je_unayo_sababu_ya_wewe_kufanikiwa.html

  [​IMG]
   
Loading...