Je, Rushwa imewahi kukuumiza au inakuumiza kwa namna gani?

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
617
1,801
Ufisadi Rushwa.jpg


Watu wanaonufaika na rushwa na ufisadi wanaonekana kujivunia kwani wanapata pesa nyingi kwa muda mfupi tena bila hata kutokwa na jasho. Ubaya zaidi ni kwamba wanaojihusisha navyo wanaweza kupandishwa vyeo na kupata fursa nzuri zaidi kuliko wengine. Hali hii inanaendelea kuaminisha wengi kwamba kujihusisha na vitendo hivyo ni namna bora ya kurahisisha maisha yao.

Hata hivyo, athari za vitendo hivyo havimuachi yoyote salama. Hapa chini ni baadhi tu ya athari za rushwa na ufisadi:

Ukosefu wa Huduma Bora: Katika mfumo wenye rushwa, hakuna ubora wa huduma, na ili kupata ubora mtu anahitajika kutoa kitu kidogo ili apate kitu ambacho anastahili. Katika mazingira hayo, stahiki yoyote inapaswa kulipiwa. Je, unakumbuka wakati wowote ambao ilibidi kulipia stahiki yako?

Ukosefu wa Haki: Rushwa katika mfumo wa mahakama husababisha kukosekana kwa haki na wanaostahili kupata haki wanaikosa huku wasiostahili wakiipata kwa kuinunua. Pia, kutokana na rushwa katika mfumo wa polisi, mchakato wa uchunguzi unaweza kuchukua miongo kadhaa kukamilika na kukwamisha upatikanaji wa haki kwa wanaostahili. Hii huwaruhusu wahalifu kuzurura na hata kutekeleza uhalifu zaidi. Je, umewahi kununua haki yako?

Ukosefu wa Ajira: Hii tunaweza kuona kwa mfano wa Taasisi za elimu na mafunzo binafsi ambazo hupewa vibali vya kuanza kutoa elimu. Kibali hiki kinatolewa kwa kuzingatia miundombinu na uajiri wa kutosha wa wafanyakazi wanaostahiki. Taasisi au uongozi wa chuo hujaribu kuwahonga wakaguzi wa ubora ili kupata vibali. Ingawa hakuna wafanyakazi wa kutosha wanaostahiki, taasisi hizi hupata idhini kutoka kwa wakaguzi unaosababisha ukosefu wa ajira. Badala ya vitivo 10, kwa mfano, chuo kinaendeshwa na vitivo 5. Kwa hivyo, hata waliohitimu vizuri wakitamani kupata kazi huko, hawatapata. Pasingekuwa na rushwa imehusika, basi kungekuwa na nafasi zaidi za ajira. Je, unadhani rushwa imewahi kukunyima ajira?

Afya Duni: Katika nchi zilizo na rushwa, mtu anaweza kugundua shida zaidi za kiafya miongoni mwa watu. Hakutakuwa na maji safi ya kunywa, barabara zinazofaa, miundombinu ya afya, huduma bora za afya n.k. Huduma hizi zisizokidhi viwango mara nyingi huwa ni matokeo ya kuokoa pesa ambazo zinaingia katika mifuko ya maafisa wanaohusika. Kwa hivyo haya yote yanaweza kuchangia afya mbaya ya watu katika jamii. Je, umewahi kupata madhara ya kiafya baada ya miradi fulani kutekelezwa kwa viwango duni?

Uharibifu wa Mazingira: Rushwa serikalini inaweza kuruhusu viwanda kutoa taka hatarishi na kuzielekeza kwenye vyanzo vya maji vinavyotumiwa na jamii fulani bila hata kuwajibishwa. Watu pia wanaweza kutoa rushwa ili kuvuna bidhaa za misitu au kufanya biashara haramu ya wanyamapori bila kuguswa na mkono wa sheria. Ikiwa hakuna rushwa, kunaweza kuwa na uchunguzi wa haki na hatua stahiki zinaweza kuchukuliwa. Kwa hiyo tunaweza kusema kuwa rushwa ni miongoni mwa vyanzo vikuu cha uchafuzi na uharibifu wa mazingira. Ni kwa vipi mazingira yako yameathirika kwa sababu ya rushwa?

Viongozi Kupoteza Heshima: Viongozi hupoteza heshima miongoni mwa wananchi endapo watakuwa wasioaminika katika nafasi zao. Watu huenda kupiga kura wakati wa uchaguzi kwa nia ya kuboresha hali zao za maisha, hivyo wanasiasa hao wakihusishwa na ufisadi/rushwa, watu wakijua hilo watapoteza heshima kwao na hawatapenda kuwapigia kura wanasiasa wa aina hiyo. Umewahi kupoteza heshima dhidi ya kiongozi yoyote mla rushwa?

Kupungua kwa Uwekezaji: Mara nyingi tumeona wawekezaji wa kigeni ambao walikuwa tayari kuja katika nchi zinazoendelea wakirudi nyuma kutokana na ufisadi/rushwa kubwa katika mashirika na taasisi za serikali. Kukosekana kwa uwekezaji huu kunasababisha kupotea kwa fursa nyingi za ajira kwa wananchi na mapato kwa serikali husika. Je, unamfahamu mwekezaji yeyote aliyekimbia kwa woga wa rushwa nchini? Ilikuathiri vipi?

Kuchelewesha Maendeleo: Kutokana na nia ya kutengeneza pesa na manufaa mengine kinyume cha sheria, ofisa anayehitaji kupitisha vibali vya miradi au viwanda anachelewesha mchakato huo. Kazi ambayo inaweza kufanywa kwa siku chache inaweza kufanywa kwa mwezi au zaidi. Hii inasababisha kuchelewa kwa uwekezaji, kuanza kwa viwanda au fursa nyingine zinazopaswa kuwanufaisha wananchi. Uwepo wa rushwa unaweza kukwamisha watu kupata miundombinu bora au huduma za kijamii kwa wakati. Je, katika eneo unaloishi kuna miradi inayochelewa kutekelezwa kwa sababu ya uwepo wa rushwa?

Kuzuia Maendeleo: Viwanda au miradi mingi mipya iliyo tayari kuanza katika eneo fulani hubadilisha mipango yao ikiwa eneo hilo halifai. Ikiwa hakuna barabara zinazofaa, maji, na umeme, kampuni na mashirika husita kuanzisha miradi yao huko. Hii inazuia maendeleo ya kiuchumi ya eneo hilo. Je, kuna fursa yoyote ambayo umeikosa kutokana na rushwa kuathiri miradi fulani?

Tofauti Katika Uwiano wa Biashara: Baadhi ya nchi zina taasisi legelege za udhibiti wa viwango. Au kwa maneno mengine, taasisi hizi za udhibiti wa viwango zinanuka rushwa na zinaweza kuidhinisha bidhaa za ubora wa chini kuuzwa katika nchi yao. Nchi hizi pia zinaweza kutengeneza bidhaa za bei nafuu lakini haziwezi kuziingiza katika nchi zilizo na taasisi thabiti za udhibiti wa viwango. Wanaweza kufanya hivyo tu katika nchi zilizo na maafisa wala rushwa wasiojali udhibiti wa viwango. Mfano mmoja ni bidhaa ambazo haziwezi kuingizwa Ulaya na Marekani lakini zinaweza kuingizwa katika masoko ya nchi nyingine zenye mifumo mibovu ya uagizaji na ukaguzi wa ubora.

Hitimisho
Athari za rushwa na ufisadi kwa maisha ya watu ni kubwa sana. Zinaweza kuharibu uchumi, afya, na ubora wa maisha. Pamoja na hayo, bado inaonekana kwamba matatizo hayo yanazidi kuongezeka na hayawezi kukomeshwa. Je, rushwa imewahi kukuumiza au inaendelea kukuumiza kwa namna gani?
 
  • Thanks
Reactions: Auz
Rushwa ni mbaya sana, inanyima haki kwa watu wanaostahili kupata,

Nakumbuka kuna siku nilimpeleka mzazi kujifungua kwenye hospital ya Serikali kufika pale hospital wale wahudumu wakawa hawajali wagonjwa hata awakihitaji msaada wanawaangalia tu hadi wawape rushwa vinginevyo utagalagala chini na kujifungua mwenyewe sakafuni wala hawakupi msaada.

Yule mzazi niliyempeleka alpoona hali yake imekuwa mbaya ikabidi atoe pesa ndipo wakamuingiza chumba cha kujifungulia akajifungua, ila hali ni mbaya sana.

Kuna mazingira ya rushwa yanatengenezwa kwa kuchelewesha huduma ili watu watoe hela kupata huduma, eneo lingine ni RITA, hao watu wanataka rushwa sana ili kutoa vyeti vya kuzaliwa, utaomba cheti utakaa miezi 7 hujapata ili uwape pesa wakutengenezee chap chap.
 
Rushwa bado ni janga kwa taifa letu.

Binafsi nimeiona zaidi barabarani wa Askari wa usalama. Kwa upande wa kuniathiri kwakweli ni kwenye foleni hospitali. Sikumbuki tarehe lakini nakumbuka nilipoenda hospitali fulani niliwahi mapema ili nipate huduma kwa haraka.

Nikashangaa watu wapya wanauja na kuhudumiwa fasta na kusepa nikawa naduwaa. Kumbe bwana walikuwa wanawashikisha wauguzi pesa kidogo ili wasikae kwenye foleni.

Kimsingi rushwa imekuwa janga kubwa kwenye sehemu nyingi za kutolea huduma. Watu wepesi kutoa pesa wananufaika kwa kupata huduma bora na haraka.
 
Mifumo ya Tz Haina udhibiti yaani in uholela mwingi na kujuana.

Ukienda polisi asubuhi utatoka mchana Kama huna kitu, mwenye nacho hakai benchi.

Unaomba leseni miezi miwili hujaipata mwenye nacho anapata siku hiyohiyo.

Umeomba uhamisho eti mpk miezi 6 wakati mwenye nacho siku mbili 2 ashahama.

Mifano ni mingi huko mahakamani ndio kabisa nguvu ya pesa inaongea na mahakimu .
 
Kwenye hitimisho, athari katika maeneo uliyotaja na maisha kwa ujumla sio "zinaweza" bali tayari zimekuwa zikiathiri maisha ya kila siku ya kila mtu na zinaendelea kuathiri haya maisha.

Zaidi ni kukosekana kwa furaha ya maisha, kwani hakuna mwenye uhakika wa haya maisha hasa ikizingatiwa mifumo yetu haijisimamii, haijiendeshi bila ya rushwa!

Utatenga kiasi gani cha pesa, utalala kingono na wangapi ili kukidhi rushwa iliyotamalaki katika jamii yetu?
 
Rushwa ipo kila sehemu. Binafsi nilikuwa na shida ya majina kwenye vyeti vyangu vya shule, na cheti cha kuzaliwa. Kutokana na usumbufu wa kutengeneza affidavity kila muda ninapotaka kutumia vyeti vyangu ilibidi nifanye mchakato wa kubadili cheti cha kuzaliwa.

Kibaya zaidi nilitaka kusafiri mapema, mama aliyekuwa anahudumia akaniambia itachukua wiki 2 lakini kama nitajiongeza, naweza kupata ndani ya siku 1.

Ilibidi nilipie kiasi fulani cha pesa kupata cheti, na hauwezi amini nilikipata siku kesho yake kikiwa tayari.

Too bad!
 
Sijajua upande wangu ila mi rushwa imenisaidia sana hususani nikiwa na shida ninayojua itachkua mda mrefu kuitatua mi huwa narahisisha tu so kiupande wangu ni hivyo kuhusu wengine kuathirika is none of my business.
Dunia haikuumbwa kwa ajili ya usawa
 
Nina machungu yasioisha mpaka nafukiwa kaburini, nilinyimwa haki yangu ya msingi ambayo niliisotea miaka na miaka kwa jasho na damu lakini siku Moja kukata kutoo rushwa ilisababisha nikose haki yangu. Rushwa rushwa rushwa nakuchukia rushwa na waomba rushwaa.

Nimesoma miaka mitatu chuo lakini nimenyimwa cheti. Nimehangaika saana kutafuta haki yangu kihalali lakini imeshindikana nimenyoosha mikono. NIMEMWACHIA MUNGU.
 
Back
Top Bottom