Ndugu Nafaka,
Kufunga, kuomba na kudai watu wamekuroga sio Kuokoka. Kabla sijaenda mbali naomba ninukuu maneno ya Kristo mwenyewe:
"Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu. - Mathayo 7:21-23
Hapo Yesu Kristo mwenyewe yuko wazi kuwa si kufunga tu, hata kutenda miujiza siyo kigezo kuwa mtu ameokoka. Labda tujiulize pamoja, tunaposema mtu ameokoka, maana yake nini?
Kuokoka kwa lugha ya kawaida ni kuepuka ajali au kitu kibaya kilichokuwa kikupate. Naomba kwa ufupi nikueleze tu juu ya kuokoka kwa muktadha wa Kikristo.
1. Mungu aliumba dunia kamilifu: Hakukuwa na maumivu, kuugua, uchawi wala kifo, mafuriko, matetemeko na kila mabaya tuyaonayo leo. Ukisoma kitabu cha Mwanzo sura ya 1 na 2 utaona Mungu anaumba dunia kamilifu kwa ajili ya Adam na mkewe kuishi.
2. Mwanadamu aliasi na kuleta uharibifu: Ukisoma sura ya 3 ya kitabu cha Mwanzo, Adamu hayupo mkewe katoka kupuyanga anakutana na shetani katika umbo la nyoka. Shetani anamjaribu na kumdanganya Hawa. Kwa tamaa yake anakula lile tunda ambalo Mungu aliwazuia wasile. Anamshawishi na mumewe wanakula. Uasi (dhambi) unaingia katika ulimwengu mkamilifu. Kwa sababu ya dhambi ulimwengu unaingia katika kufa. Magonjwa, miiba, kula kwa jasho, kuzaa kwa uchungu, uharibifu wa mazingira na mengine mabaya yanaingia ulimwenguni na kwa sababu hiyo maisha yanakuwa mabaya. Kifo kinaingia katika ulimwengu.
Kabla ya uasi huu, shetani alikuwa amekwisha kuasi na kusomewa hukumu yake. Muda wa kuitekeleza unakuwa bado na ndio maana alipata nafasi ya kumdanganya Hawa. Mwanadamu anaungana na shetani kwenye adhabu yake maana kosa lao lilikuwa ni moja, nalo ni uasi. Mwanadamu wa kwanza na uzao wake wakawa katika hatari ya wote kuishia Jehanamu ya mateso mengi sana. Hatari hii ni kw sababu mshahara wa uasi (dhambi) ni mauti. Rejea Warumi 6:23
3. Mungu anaahidi Ukombozi wa Wanadamu
Jehanamu haikutengenezwa kwa sababu ya wanadamu. Yesu anasema "Kisha atawaambia na wale walioko katika mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake" Mathayo 25:41. Wanadamu wanaenda Jehanamu kama kenge kwenye msafara wa mamba. Tumejiunganisha kwa kiherehere chetu tu.
Kwa sababu Mungu hakumuumba mwanadamu ili ateseke na kwa sababu alimpenda sana mwanadamu, alipanga kumuokoa toka kwenye janga la Jehanamu alilojitakia. Lakini tatizo ni kuwa Mungu ni Mtakatifu sana na wa haki. Kwa sababu hiyo, lazima ahakikishe kila dhambi inapata hukumu stahili. Dhambi dhidi ya Mungu asiye na mwanzo wala mwisho inadai hukumu isiyo na mwisho, ya milele. Kwa hiyo Mungu asingeweza kufumbia macho dhambi za mwanadamu awaye yeyote.
Lakini Upendo wake ulidai lazima afanye kitu kutusaidia wanadamu ambao tulishakuwa hopeless. Ndipo sasa akaamua aje mwenyewe katika mwili wa Mwanadamu, ili aishi maisha yasiyo na hatia, na kwa sababu hiyo hakupaswa kufa. Maana kifo ni matokeo ya dhambi. Akaishi bila kutenda dhambi.
Akajitoa afe, ili abebe hukumu ya dhambi za wanadamu. Dhambi dhidi ya Mungu asiye na mwisho zinadai hukumu ya Milele. Lakini Mungu wa milele, katika utu wa Kristo Yesu anaweza kulipia deni la milele ndani ya muda ule mfupi. Kwa hiyo Mungu muumbaji akaruhusu adhabu ya dhambi imuangukie, ili aweze kutusamehe dhambi bila kupungua kuwa Mwenye haki.
Ni kama ambavyo mahakama imewahukumu wale viongozi wa Chadema mil 350. Fikiria kwamba wasingekuwa na uwezo wa kulipa, wangeenda gerezani. Sasa fikiria baada ya hukumu, jaji angeamua kuwalipia mil 350 zote! Maana yake wangekuwa huru japo wamehukumiwa kuwa wamevunja sheria.
Ndio maana katika kitabu cha 1 Petro 3:18 Biblia inasema
"Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; akauawa kimwili, lakini akahuishwa kiroho"
Kwa hiyo Yesu alikuja ili kutuokoa na hatari ya Jehanamu. Sasa nitamalizia na mambo mawili ya msingi: Ni vipi mtu anaokolewa/anaokoka na mwisho ushuhuda wa mtu aliyeokolewa.
4. Namna Gani Tunaokolewa?
Waefeso 2:8-9 inasema "Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu"
Kwa maana rahisi, wokovu ni zawadi au kipawa. Zawadi hauifanyii kazi au itakuwa ni ijara na si zawadi. Mungu ametulipia dhambi zote bure. Lakini Mungu hamlazimishi mtu kuipokea zawadi kama hataki. Kama ilivyo kwa zawadi zote, lazima inapotolewa ipokelewe. Kama watu wanakufa kwa njaa, halafu akajitokeza mtu na kutoa zawadi bure ya chakula lakini watu wakaikataa basi watakufa. si kwa sababu hakukuwa na chakula, bali kwa sababu wahusika wameikataa. Vivyo hivyo na zawadi ya Mungu ya uzima wa milele.
Kuokoka ni rahisi sana na Biblia iko wazi kuwa:
"Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. 19 Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu" Yohana 3:16 - 20
"Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika" Warumi 10:9-11
"Na iwapo mtu yeyote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto" Ufunuo 20:15
Kwa hiyo wokovu unakuja kwa kumwamini Yesu Kristo kuwa ni Bwana Mungu, aliyekuja katika mwili ili afe kwa ajili ya dhambi zako. Unapaswa kutubu (Kugeuka na kuziacha njia zako za awali) na kumlilia Kristo kwa ajili ya msamaha wa dhambi. Baada ya hapo Bwana atakusamehe na kukupa moyo mpya wenye nia mpya, ambayo ni kuyafanya mapenzi ya Mungu.
5. Utamtambua vipi mtu aliyeokolewa?
2 Wakorintho 5:15-17 inatufundisha kuwa "tena alikufa kwa ajili ya wote, ili walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa akafufuka kwa ajili yao. Hata imekuwa, sisi tangu sasa hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya mwili. Ingawa sisi tumemtambua Kristo kwa jinsi ya mwili, lakini sasa hatumtambui hivi tena. Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita, tazama! Yamekuwa mapya"
"Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wakiwa wamevaa mavazi ya kondoo, lakini kwa ndani ni mbwamwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri. Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni. Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua" Mathayo 7:15-20
Kwa hiyo ishara ya mtu aliyeokoka kwanza ni kubadilika. Anakuwa mtu tofauti na uliyemjua. Anakuwa obsessed na yule aliyemuokoa na anamtumikia kwa bidii. Kumbuka aliyemuokoa ni Yesu na sio nabii so and so au mchungaji nanilihii au paroko whoever. Mambo mabaya anayaacha, na anakuwa anatamani kufanya yale yanayompendeza Mungu. Marafiki wabaya, lazima ataachana nao. Note hapa sio kujitenga na watu. Kama alikuwa mwizi kwa mfano, kampani yake ya wezi atajitenga nayo kwa sababu atakuwa ha fit tena. Lakini hatawachukia na kuwaona mashetani. Hii ni kwa sababu anajua alikuwa mwovu kama wao na ni Neema ya Mungu tu imemuokoa. Atawapenda na kuwaombea na kwenye mazingira yanayofaa atataka akae nao awaeleze habari za Yesu anayeweza kuwaokoa toka kwenye utumwa wa dhambi.
Atajitahidi kukaa karibu na ndugu na kuwashirikisha upendo wa Mungu na sio kujitenga. Ataungana na wenzake katika ibada na mafundisho. Lakini atarudi kwao na kwa walio wake (ndugu jamaa na marafiki) apate kuwahubiria habari njema. Maana Yesu aliposema enendeni ulimwenguni mkaihubiri injili hakumaanisha kwa waliokwisha kuokoka, bala ambao bado wanahitaji nuru ya wokovu.
Kuwapenda na kuwahubiria watu ndio msingi hasa wa mtu aliyeokoka. Nimejaribu kujibu kwa kifupi sana. Kama utapenda nipe anuani yako au namna naweza kukutumia kijitabu kidogo cha kukusaidia kuelewa zaidi, bure. Hii ni ofa kwa yeyote anayependa. Nitumie details inbox nitakutumia kaba mwezi huu haujaisha, Mungu akitupa uhai!
Mungu akubariki!