Jarida lathibitisha: Vikosi maalumu vya Marekani vinapigana bega kwa bega na Wazayuni katika vita vya Gaza
Oct 29, 2023 03:00 UTCKwa mujibu wa shirika la habari la ISNA, Military Watch Magazine, limefichua katika makala yake kwamba kuna ripoti zinazoonyesha kuwa Marekani imetuma vikosi vyake vya operesheni maalumu huko Ukanda wa Gaza kwa ajili ya kuanzisha mashambulizi ya pamoja na jeshi la Israel dhidi ya Harakati ya Hamas katika eneo hilo.
Jarida hilo limemnukuu Douglas McGregor, kanali mstaafu wa Jeshi la Marekani na kutangaza kuwa katika muda wa saa 24 zilizopita, idadi kubwa ya vikosi maalumu vya Marekani na Israel vimeingia huko Gaza ili kufanya upelelezi kwa lengo la kupanga mikakati ya mahali vinakotaka kushambulia kwa ajili ya kuwakomboa mateka na kuleta mabadiliko katika eneo hilo.
Afisa huyo wa Marekani ameendelea kufichua kwa kwa kusema, "kwa mujibu wa taarifa nilizonazo, vikosi hivyo vimeshambuliwa na kutiwa hasara kubwa".
Kwa kuzingatia kuwa Marekani ni muungaji mkono mkuu na wa bila masharti yoyote wa utawala wa Kizayuni, inataka kusiwepo na kizuizi wala mpaka wowote katika hatua inazochukua Israel dhidi ya Wapalestina na makundi ya Muqawama.
John Kirby, msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa la Ikulu ya White House amesema mapema leo: "sisi hatuiwekei Israel mistari myekundu. Tunaendelea kuunga mkono mahitaji yao ya kiusalama".
Hivi sasa utawala haramu wa Kizayuni ambao unapata uungaji mkono kamili wa Washington inayoukingia kifua dhidi ya azimio lolote la kukwamisha hatua zake za kijinai dhidi ya Wapalestina, unaendeleza mauaji ya kikatili na kinyama dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Ukanda wa Gaza.